Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Atembelea Makumbusho ya Mashahidi ya Mashariki mwa Kārun Chapa
26/03/2014
Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, leo asubuhi (Jumatano) ametembelea makumbusho ya mashahidi huko mashariki mwa Kārun (magharibi mwa Iran) na kuzungumza kwa karibu na maelfu ya wafanya ziara katika maeneo vilikopiganwa vita vya kujihami kutakatifu (vita vya miaka minane vilivyoanzishwa na utawala wa zamani wa Iraq dhidi ya Iran). Mkutano huo umefanyika katika eneo la umma la operesheni za kuvunja mzingiro wa Abadan, mashariki mwa Kārun.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitizia udharura wa kutumika vizuri fursa ya misafara inayofanya ziara katika maeneo kulikofanyika operesheni za kijeshi wakati wa vita vya kujihami kutakatifu na kusema kuwa kuna wajibu wa kuzibakisha hai kumbukumbu za jitihada kubwa na kujitolea katika njia ya haki zilikofanywa na mashahidi wa vita hivyo kwenye maeneo tofauti ya operesheni za kijeshi za wakati wa vita vya kujihami kutakatifu na kuwakumbuka kwa wema wakati wote wanamapambano na shakhsia wakubwa waliotoa mchango wao katika vita hivyo.
Ameongeza kuwa: Somo kubwa zaidi linalopatikana kutoka katika vita vya kujihami kutakatifu ni kwamba vita hivyo vimeonesha kuwa, wakati taifa linapokuwa chini ya kivuli cha umoja, imani thabiti kuhusu Mwenyezi Mungu pamoja na kuwa na itikadi madhubuti kuhusiana na ahadi za Mwenyezi Mungu, taifa hilo linaweza kuvuuka kishujaa kwenye vigingi na vizuizi vyote vizito na pia kumshinda na kumlazimisha adui kurudi nyuma, kwa kusimama imara taifa hilo mbele ya adui huyo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameitaja hatua ya watu wa matabaka mbali mbali ya kufanya ziara katika maeneo kulikofanyika operesheni za kijeshi wakati wa vita vya kujihami kutakatifu katika siku hizi za mapumziko ya mwaka mpya (wa Kiirani wa 1393 Hijria Shamsia) na vile vile katika kipindi chote cha mwaka, kuwa ni hatua nzuri, sahihi na ya kimantiki kabisa na kuongeza kwamba: Maeneo yote kulikofanyika operesheni za vita vya kujihami kutakatifu yakiwemo maeneo ya Khuzestan, yalikuwa ni medani bora kabisa za kujitolea muhanga katika njia ya haki, kupigana jihadi na kujitolea kwa ajili ya kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu.
Ayatullah Udhma Khamenei amekumbushia amri ya Imam Khomeini (quddisa sirruh) kuhusu kuvunjwa mzingiro wa Abadan na namna operesheni ya kijeshi ya "Thaminul Aimma" ilivyobuniwa, kupangiliwa vyema na kutekelezwa kwa ufanisi mkubwa mwezi Mehr 1360 (Septemba 1981) katika eneo la mashariki mwa Kārun na kusisitiza kwamba: Ushindi walioupata wanamapambano wa Kiislamu katika operesheni hiyo, ulikuwa mwanzo wa mlolongo wa operesheni za baada yake yaani za Tariqul Quds, Fat'hul Mubin na Ilaa Baytil Muqaddas ambazo zingeliweza kumaliza vita hivyo katika miaka ile ile ya mwanzoni mwa vita hivyo vya kutwishwa na kulazimishwa.
Hata hivyo ameongeza kuwa: Kambi ya maadui wa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, yaani madola ya Ulaya na dola la Marekani yaliupa utawala wa Baath wa Iraq silaha mpya na za kisasa kabisa na kumshawishi Saddam aendeleze vita hivyo na jambo hilo ndilo lililopelekea vita hivyo vya kutwishwa, vidumu kwa muda wa miaka minane.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia shabaha na lengo la kambi ya kiistikbari la kutaka kuhakikisha kuwa taifa la Iran halitoki kifua mbele katika vita hivyo na kujaribu kuonesha kuwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ni dhaifu katika kupambana na adui wa Kibaath aliyekuwa anaungwa mkono kikamilifu na mabeberu hao na kusisitiza kwamba: Hata hivyo Mwenyezi Mungu Mtukufu alionesha uwezo Wake na nguvu isiyoshindika ya sunna ya Mwenyezi Mungu ilitoa pigo kubwa kwa maadui wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuzirambisha mchanga pua zao.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Kutokana na kwamba mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu nchini Iran ulikuwa imejizatiti kwa imani thabiti na hisia na mapenzi ya wananchi, ulisimama kidete kupambana kiume katika kipindi cha miaka minane ya kujihami kutakatifu na kuonesha kuwa inawezekana taifa kujilinda mbele ya madola yote makubwa kimaada ya dunia na vile vile inawezekana kuulazimisha upande huo wa pili ukiri kushindwa.
Amesema, moja ya malengo ya maadui wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika vita hivyo vya kulazimishwa vya miaka minane ni kujaribu kuonesha kuwa hakuna yeyote yule anayeweza kusimama kidete na akasalimika mbele ya nguvu za madola hayo makubwa ya kimaada duniani. Hata hivyo amesema: Taifa fulani linaweza kushindwa pale taifa hilo linapoamini kuwa haliwezi kufanya lolote, lakini taifa la Iran liliwathibitishia kinyume chake walimwengu katika vita hivyo vya kujihami kutakatifu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Sababu kuu ya kuliletea heshima na utukufu taifa moja kati ya mataifa mengine na pia katika kipindi chote cha historia, ni kufanya juhudi na jitihada kubwa taifa hilo katika nyuga tofauti za kielimu, kiuchumi, ushirikiano wa kijamii na muhimu kuliko yote katika uwanja wa kujiandaa vilivyo kwa ajili ya kujitolea muhanga katika kufanikisha malengo.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Somo kubwa zaidi lililotolewa na Mapinduzi ya Kiislamu kwa taifa la Iran ni kwamba, mapinduzi hayo matukufu yameonesha kuwa, njia ya kuweza kufikia malengo makuu matukufu ni kufanya jitihada kubwa, kujitolea muhanga katika kufanikisha malengo hayo na kusimama kidete katika kuyalinda na kuyahami malengo hayo.
Vile vile amekitaja kipindi cha vita vya miaka minane vya kujihami kutakatifu ambavyo vimejaa mambo mengi sana yasiyo ya kawaida kuwa ni mfano wa wazi wa kusimama kidete taifa la Iran na vijana wa nchi hii katika kuyalinda na kuyahami malengo yao matukufu mbele ya kambi ya kufru na uistikbari na kuongeza kuwa: Kuna wajibu wa kubakishwa hai daima kipindi cha vita hivyo vya kujihami kutakatifu.
Aidha Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Wale wanaolitakia mabaya taifa la Iran wanafanya njama za kufuta kumbukumbu za watu waliojitolea muhanga roho na nafsi zao katika kipindi cha kujihami kutakatifu na shakhsia waliotoa mchango mkubwa katika vita hivyo na ni kwa sababu hiyo ndio maana watu hao wanajaribu kupotosha mambo na kukana kujitolea muhanga wanamapambano wa Kiislamu katika vita vya kujihami kutakatifu, na miongozo pamoja na njia zilizokuwa zinaoneshwa na mja wa Mwenyezi Mungu mwingi wa busara na hekima ambaye alikuwa akiona mbali, Imam Khomeini (quddisa sirruh).
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza pia kuwa: Hatua kwa hatua matukio ya vita vya kujihami kutakatifu yamekuwa si kitu kinachoweza kusahauliwa tena na taifa la Iran na kwamba kujihami huko kutakatifu kuna taathira zake kubwa nzuri katika njia ya harakati ya taifa hili kuelekea kwenye ufanikishaji wa malengo yake mkuu matakatifu.
Mwishoni mwa hotuba yake, Ayatullah Udhma Khamenei amewashukuru wananchi ambao kupitia misafara mbali mbali wanakwenda kufanya ziara katika maeneo zilikofanyika operesheni za kijeshi wakati wa vita vya kujihami kutakatifu na kuongeza kuwa: Akiba na matunda ya safari hiyo ya kimaanawi yawe ni kupata tajiriba na uzoefu, muono wa mbali na nuru ya Mwenyezi Mungu.
Mara baada ya kuingia kwenye eneo hilo la umma la operesheni ya kuvunja mzingiro wa Abadan, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekwenda moja kwa moja kwenye makumbusho ya mashahidi watukufu 9 waliopotea wa vita vya kujihami kutakatifu na kuwasomea Faatiha pamoja na kuwaombea dua kwa Mwenyezi Mungu ili awapandishe daraja za juu ya utukufu.
 
< Nyuma   Mbele >

^