Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Aonana na Akina Mama Bora wa Iran Chapa
19/04/2014
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Aonana na Akina Mama Bora wa IranAyatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu leo asubuhi (Jumamosi) ameonana na mamia ya akina mama bora walioteuliwa kutoka kona mbali mbali za Iran na kulitaja suala la kuanzisha kituo kikuu kitakachofanya kazi hadi nje ya mihimili mikuu ya dola kwa ajili ya kutunga mikakati sahihi kuhusiana na kadhia muhimu ya mwanamke na familia, kuwa ni jambo la dharura na kuongeza kwamba: Kuweza kupata mkakati huo wa pande zote na unaoweza kutekelezeka kunahitajia masuala matatu makuu ambayo ni: kujiepusha kikamilifu na kuzifanya fikra ghalati, potofu na zilizopitwa na wakati za Magharibi kuwa marejeo katika masuala ya wanawake; kutegemea mafundisho na miongozo safi na ya asili ya Uislamu na vile vile kushughulikia masuala ambayo kwa hakika ni masuala muhimu na makuu ya wanawake.
Aidha ametoa mkono wa baraka na fanaka kwa mnasaba wa maadhimisho ya siku ya kuzaliwa Bibi Fatimatuz Zahra (Salamullahi Alayha) na kusema kuwa, kuoana siku za maadhimisho haya na maadhimisho ya wiki ya wanawake na siku ya kumuenzi mama nchini Iran ni fursa nzuri ya kuweza kupata somo la kimaisha kutoka kwa bibi bora wa "dunia mbili" Siddiqatul Kubra (SA).
Kiongozi Muadhalmu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria namna Bibi Fatimatuz Zahra (Alayhas Salaam) alivyokuwa maasumu na alivyopambika kwa sifa bora za ukamilifu wa mwanadamu na jinsi mtukufu huyo alivyokuwa mbora wa wanawake wote licha ya umri wake kuwa mdogo na kuongeza kuwa: Inabidi kuangalia tena na tena na kwa umakini wa hali ya juu zaidi maisha ya bibi huyo bora kuliko wanawake wote duniani ili tupate kujifunza sifa zake bora kama taqwa, staha, usafi, jihadi, namna ya kuishi na mume, namna ya kulea watoto, siasa zenye welewa na muono mpana na kushiriki kwenye nyuga muhimu kabisa za maisha ya mtu na kumfanya kuwa ruwaza na kigezo chema kwa maana halisi ya neno.
Ayatullah Udhma Khamenei amelitaja suala la Iran ya Kiislamu kuwa na akina mama bora na wasomi, wanafikra na wenye muono mpana, kuwa ni neema za Mwenyezi Mungu kwa nchi hii na moja na ni fakhari kubwa za Jamhuri ya Kiislamu.
Ameongeza kuwa: Uhakika huo ambao haujawahi kushuhudiwa mfano wake katika kipindi chote cha historia ya Iran unatokana na miongozo na mafundisho yaliyojaa baraka ya dini tukufu ya Uislamu na fikra na mitazamo iliyojaa hekima na busara ya Imam Khomeini (quddisa sirruh).
Vile vile amekutaja kujitokeza kwa sura ya wazi kabisa na iliyotukuka shakhsia huru ya mwanamke wa Kiirani katika medani za vita vya miaka minane vya kujihami kutakatifu kuwa ni nukta nyingine inayong'ara katika historia ya wanawake wa Iran na amewapongeza na kuwashukuru sana mama na wake wa mashahidi na majeruhi wa vita kutoka na subira, uvumilivu na kujitolea kwao kwa namna ya kupigiwa mfano.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, kadhia ya mwanamke katika pande zake tofauti inahitajia kufanyiwa kazi za kifikra, utafiti na ufuatiliaji wa wanadamu wote, na hapo amegusia nukta tatu muhimu katika kadhia hiyo ambazo ni:
Mosi: Namna gani itaweza kutumiwa kwa njia sahihi na salama, nafasi na uwezo adhimu walio nao wanawake.
Pili: Kuangalia namna gani linaweza kutumiwa vizuri suala nyeti na muhimu mno la jinsia ya kike ya wanawake katika kustawishwa na kutiwa nguvu ubora wa wanawake na sio kutumiwa suala hilo kuwaporomosha wanawake katika sifa na heshima zao.
Na Tatu: Kuangalia ni miamala ya namna gani inapaswa kuweko baina ya mwanamke na mwanamme hasa kwa kuzingatia tofauti zao za kimaumbile ili kwa njia hiyo iwezekane kupambana na dhulma na unyanyasaji dhidi ya wanawake katika familia na kwenye jamii.
Pia amesema kuwa, mwanamke na familia ni masuala mawili ambayo ni muhali kuyatenganisha na kusisitiza kuwa: Mtu yeyote yule anayezungumzia suala la mwanamke na kuamua kulitenganisha na suala la familia bila ya shaka yoyote atafanya makosa pia katika kulielewa na kulitatua suala la wanawake.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia amesema, ni jambo la dharua kuwa na kituo cha utafiti na utendaji kazi kwa ajili ya kuyapatia majibu maswali yanayoulizwa na kulifanyia utafiti wa kina na wa pande zote suala la wanawake na kuongeza kuwa: Kituo hicho ambacho inabidi kifanye kazi zake hadi nje ya mihimili mikuu ya dola kinapaswa kibebe jukumu la kutunga mkakati na stratijia sahihi inayokusanya mambo yote kuhusu mwanamke na kusimamia kikamilifu utekelezaji wa kivitendo wa mikakati hiyo.
Amelitaja suala la kutunga mkakati huo na kufanyia utafiti kadhia ya mwanamke katika asasi au chombo chochote kile kunahitajia kushikamana vilivyo na mambo ya lazima katika kadhia hiyo.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Kutokana na sababu mbali mbali, Wamagharibi wameielewa vibaya kadhia ya mwanamke lakini pamoja na hayo welewa wao huo huo ghalati na potofu ndio walioulazimisha kuwa marejeo ya watu duniani na hawatoi hata mwanya wa kusikika fikra, misimamo na mawazo ya watu wa mataifa mengine na ya wapinzani wa mtazamo wao huo potofu.
Ameongeza kwa kusema: Tab'an ni jambo lililo wazi kwamba inabidi kuwa na welewa wa kina kuhusu mitazamo ya Wamagharibi kuhusiana na pande mbali mbali za kadhia ya mwanamke, lakini pia inabidi kusimama imara kukabiliana na suala la kuzifanya fikra hizo kuwa marejeo, na kujiepusha na kudanganywa na fikra hizo chakavu za Wamagharibi ambazo wanajaribu kuzionesha ni za kisasa, fikra hizo za kusaliti haki ya wanawake ambazo lakini zinajionesha kuwa zinawaonea uchungu wanawake; kwani fikra hizo kamwe haziwezi kuiongoza vizuri wala kuiletea saada na ufanisi jamii ya mwanadamu.
Ayatullah Udhma Khamenei ameutaja mtazamo walio nao Wamagharibi wa kuiangalia dunia na mambo yote kwa mtazamo wa kimaada na kutoyapa nafasi masuala ya kiroho na kidini, kuwa ndio uliowapelekea Wamagharibi kufanya kosa kubwa katika kuliangalia suala la mwanamke na kuongeza kwamba: Kumwangalia mwanamke kama bidhaa na kutumiwa vibaya wanawake katika masuala ya uchumi na kazi na kudhalilishwa mwanamke kwa kugeuzwa chombo tu cha kuwastarehesha wanaume na kukidhi ghariza za kijinsia za wanaume, ni msingi mwingine ambao fikra za Magharibi zimejengewa juu yake kuhusu mwanamke, msingi ambao kwa hakika unatokana na fikra finyu na ni dhulma kubwa sana wanayofanyiwa wanawake huko Magharibi.
Vile vile ametoa ushahidi kutoka katika makala na vitabu mbali mbali ambavyo vimeandikwa na kusambazwa kuhusu hali halisi ya wanawake huko Magharibi na kuongeza kwamba: Kama tutataka kuufanya mtazamo wetu kuhusu kadhia ya mwanamke uwe salama, wa kimantiki, wa kina na wa hekima na busara, hatuna njia nyingine isipokuwa kuhakikisha tunajiweka mbali na mitazamo ya Wamagharibi kuhusu masuala kama vile kazi na usawa wa kijinsia baina ya mwanamke na mwanamme.
Amesema "usawa wa kijinsia baina ya mwanamke na mwanamme" ni moja ya mambo ghalati na ya upotofu mkubwa waliyo nayo Wamagharibi.
Ameongeza kuwa: Usawa hauna maana kuwa siku zote ni uadilifu. Uadilifu siku zote ni haki, lakini usawa baadhi ya wakati ni haki na baadhi ya wakati ni batili.
Hapo hapo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amehoji na kuuliza swali akisema, kuna mantiki gani kulazimisha kumuingiza mwanamke katika nyuga na sehemu ambazo zinamsumbua na kumtesa tofauti kabisa na ambavyo Mwenyezi Mungu amemuumba na kumtofautisha na mwanamme kimaumbile, kijinsia na kihisia na kumuweka katika sehemu yake bora na maalumu katika maisha?
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitizia mtazamo wa kibinadamu wa dini tukufu ya Kiislamu kwa kadhia ya mwanamke na kuongeza kwa kusema: Katika maeneo mengine ikiwa ni pamoja na katika utukufu wa kimaanawi, hakuna tofauti yoyote kati ya mwanamke na mwanamme lakini wanatofautiana katika kalibu na fremu zake na kwamba uhakika huo pamoja na kuwepo nyuga za pamoja, unapelekea kuwepo pia nyuga zinazowajibisha kuwepo tofauti baina ya mwanamke na mwanamme.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekosoa vikali misingi ya kifikra ya vyommbo vingi vya kimataifa duniani na kusema kuwa: Kung'ang'ania Wamagharibi kutekelezwa misingi hiyo ghalati na potofu kunaipotosha jamii ya mwanadamu na ndio maana tukasema kuwa, inabidi tuchukue tahadhari kubwa katika juhudi zetu za kuwa na mtazamo sahihi na wa kimantiki kuhusiana na kadhia ya mwanamke.
Ayatullah Udhma Khamenei pia amesisitizia udharura wa kutegemea mafundisho na miongozo ya dini tukufu ya Kiislamu kama jambo la pili la lazima katika jitihada za kupata mkakati na stratijia sahihi kuhusu suala la mwanamke.
Ameongeza kuwa: Katika juhudi za kuwa na mkakati sahihi wa kulifanyia kazi suala la mwanamke, hatupaswi kukubali kila kitu tu tunachokisikia kwa watu kuhusiana na msimamo wa dini kuhusu mwanamke. Hata hivyo lakini tunapaswa kuifanya misingi iliyoiimarishwa na kupata ustahiki kwa kutumiwa mbinu sahihi za kufutu mas'ala kutoka katika "Qur'ani, sunna na hadithi" kuwa marejeo yetu makuu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameutaja wajibu wa kujiepusha na masuala ya pembeni na kuzingatia masuala ya kimsingi kuwa ni jambo la tatu la lazima la kuweza kupata mkakati na stratijia sahihi kuhusu kadhia ya mwanamke na kuongeza kuwa: Suala la familia na hasa hasa "usalama, amani na utulivu wa mwanamke katika familia" ni suala la msingi ambalo inabidi lizingatiwe sana.
Amesisitiza kwamba: Inabidi ufanyike uchunguzi wa kugundua mambo yanayomuondolea utuvu na utulivu wa roho mwanamke katika familia na kupambana na mambo hayo kwa kutumia mbinu mbali mbali kama vile kuweka sheria na kufanya tablighi na kuwaelimisha watu kwa njia sahihi.
Ayatullah Udhma Khamenei vile vile ameelezea kusikitishwa kwake na namna fikra za zamani na za sasa zinavyomwangalia mwanamke kuwa ni kiumbe wa daraja la pili ambaye ana wajibu na jukumu la kumtumikia mwanamme tu na kuongeza kuwa: Suala hili ni kinyume kabisa na mtazamo wa fiqhi iliyostawi ya Kiislamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kwa kusema: Inasikitisha kuona kuna baadhi ya watu wanachukua kitu katika Uislamu lakini kwa vile wanaogopa kuwakasirisha Wamagharibi wanaongeza kitu kingine kwenye kitu hicho, jambo ambalo kwa kweli halikubaliki kabisa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja suala la kupewa haki yake mwanamke, ya kusoma na kujiendeleza kielimu kuwa ni jambo la dharura sana na kuongeza kwamba: Tofauti na baadhi ya mitazamo, kufanya kazi nje ya nyumba si katika masuala ya kimsingi ya mwanamke ingawa hata hivyo kufanya kazi nje ya nyuma na kusimamia mambo ya kijamii hakuna tatizo lolote kwa sharti kwamba kufanya hivyo kusiharibu jukumu kuu na la kimsingi ya mwanamke yaani kuisimamia na kuitunza familia yake.
Vile vile ameashiria masuala yaliyopo kuhusu kutoingia wanawake katika baadhi ya elimu na kozi za masomo katika Vyuo Vikuu akisema: Hata kama tutakubali kuwa jambo hilo lipo na kuna tofauti baina ya wanawake na wanaume katika baadhi ya masomo, suala hilo halitakuwa ni kinyume na uadilifu kwani hatupaswi kumbebesha mwanamke masomo na kazi ambazo hazioani na maumbile yake ya kike.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Kama inasemwa kwamba wanawake wasifanye baadhi ya kazi, jambo hilo si kuwanyanyasa wanawake na wala ni kosa, bali kosa ni kumbebesha kazi mwanamke ambazo hazioani na maumbile yake ya kike ambayo Mola wake amemuumba nayo.
Mwishoni mwa hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewataja wanawake wasomi, weledi wa mambo na wenye welewa mpana na bora kuwa ndio watu mwafaka zaidi wa kuweza kufuatilia kwa njia sahihi masuala ya wanawake na ametoa mwito kwao wa kujitokeza kwa wingi na kulipa uzito mkubwa suala hilo.
Baada ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Bi Shahindokht Molaverdi, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika masuala ya wanawake na familia ametoa ripoti fupi kuhusu masuala yanayohusiana na wanawake na kusema kama ninavyomnukuu: Wanawake wa Iran tuna hali nzuri mno katika eneo la Mashariki ya Kati kwa kuzingatia vigezo vya usalama wa kiafya na ushiriki katika jamii, na kwamba wanawake katika jamii ya Iran tuna nafasi yenye taathira kubwa na isiyo na mbadala katika kufanikisha kaulimbiu ya "Uchumi na Utamaduni wenye Azma ya Kitaifa na Uongozi na Usiamamiaji wa Kijihadi" (ya mwaka huu mpya wa Kiirani wa 1393 Hijria Shamsia).
 
< Nyuma   Mbele >

^