Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Aonana na Kundi la Wasoma Kasida za Ahlul Bayt AS Chapa
19/04/2014
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Aonana na Kundi la Wasoma Kasida za Ahlul Bayt ASHusainia ya Imam Khomieni (quddisa sirruhu) mjini Tehran imehinikiza manukato ya umaanawi wa Fatimatuz Zahra AS, katika maadhimisho ya siku ya kuzaliwa kulikojaa baraka kwa Bibi huyo mteule wa Mwenyezi Mungu katika "dunia mbili," binti wa Bwana Mtume Muhammad SAW, Swiddiqatul Kubra Salamullahi Alayha.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei ameonana na majimui ya wasoma kasida na mashairi ya Ahlul Bayt wa Mtume wa Mwenyezi Mungu SAW kwa mnasaba wa maadhimisho hayo na huku akitoa mkono wa baraka na fanaka kwa mnasaba wa maadhimisho ya siku ya kuzaliwa Bibi Fatimatuz Zahra, Salamullahi Alayha na kuadhimisha pia siku ya kuzaliwa Imam Khomeini (quddisa sirruh) ambayo imesadifiana na maadhimisho hayo, amesema kuwa, somo kubwa inalopata jamii ya mwanadamu kutoka katika maisha ya Fatimatuz Zahra Salamullahi Alayha ni kufanya jitihada, idili na kuishi maisha ya waja wasafi wa Mwenyezi Mungu.
Ameongeza kuwa: Mikusanyiko ya kidini ni fursa ya kipekee ya kuweza kubainisha mafunzo na masomo muhimu ya kimaisha ya nyota zinazong'ara za dini na inabidi mafundisho matukufu ya nyota hizo yafikishwe kwa watu kwa ustadi wa hali ya juu, kwa weledi wa aina yake, kwa sura ya muamko na kutia matumaini katika nyoyo za watu pamoja na kuleta umoja na mshikamano miongoni mwao na kuchunga kikamilifu mipaka ya kidini na kisheria katika mikutaniko hiyo ya kidini ili kwa njia hiyo iwezekane kutumiwa vizuri fursa hiyo katika kupambana na njama tata za maadui wa Uislamu sambamba na kufanikisha malengo ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameitaja mikusanyiko ya kidini ya kuwazungumzia maimamu watoharifu katika mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ni fursa muhimu sana na ni moja ya neema kubwa za Mwenyezi Mungu na kuongeza kwamba: Ijapokuwa akili iliyofungwa kila upande ya mwanadamu haiwezi kujua kiundani vipengee vya shakhsia za nyota zinazong'aa za mbinguni kama Bibi Fatimatuz Zahra Salamullahi Alayha, lakini pamoja na hayo mienendo na sira za viongozi hao wakubwa wa kimaanawi inatupa ruwaza na vigezo vya kuweza kumfikisha mwanadamu kwenye malengo makubwa ya kijamii.
Vile vile ameyataja maisha bora ya Kiislamu na kujenga jamii iliyo stawi, iliyo huru, inayojitegemea na nyenye maadili matukufu, iliyoshikamana na yenye umoja pamoja na kuunda jamii ya watu wenye taqwa na wacha Mungu, ni mifano katika malengo na shabaha za jamii ya Kiislamu na kusisitiza kuwa: Haiwezekani kufikia kwenye jamii kama hiyo isipokuwa tu kwa idili na jitihada zisizochoka na kujiweka mbali na ugoigoi, utepetevu na uvivu pamoja na kujiepusha na kukata tamaa na kuvunjika moyo.
Aidha Ayatullah Udhma Khamenei amelitaja suala la kueneza hadi mashinani sunna ya kuwapenda na kuwaenzi watu wa nyumba ya Bwana Mtume Muhammad SAW nchini Iran kunakofanywa na mamia ya malenga na majimbi wa tungo za Ahlul Bayt AS kuwa ni fursa nzuri sana na kuongeza kwamba: Fursa hiyo sambamba na suhula nyingi zilizopo nchini Iran, zinayafanya majukumu ya watu kuwa makubwa zaidi na kwamba jambo hilo linaweza kuleta mapinduzi makubwa nchini.
Vile vile ameashiria namna maadui wa Mapinduzi ya Kiislamu wanavyofanya njama kubwa za kuharibu itikadi na imani za kidini za wananchi wa Iran na kujaribu kuingiza mambo ya kipotofu katika njia ya harakati ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na katika harakati ya taifa lililojaa fakhari la Iran kwa kutumia nyenzo tata sana za mawasiliano na za kielektroniki na kusisitiza kuwa: Lengo la adui ni kuushinda na kuupigisha magoti Uislamu na kuzuia jamii ya Waislamu wa Kishia na mafundisho ya Kishia yasiweze kuwa kigezo na ruwaza njema kwa mataifa mengine.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu una suhula na uwezo wa kipekee wa kuweza kupambana na njama na hila hizo tata mno za adui ambapo mikusanyiko na mikutaniko ya kidini na kuzungumza na watu moja kwa moja na uso kwa uso kupitia mimbari na usomaji wa kasida na mashairi ya Ahlul Bayt AS ni miongoni mwa suhula na uwezo huo wa kipekee ulio nao mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu.
Pia amekutaja kutumiwa vibaya fursa hiyo yenye thamani kubwa na ya kipekee kuwa ni kukufuru neema ya Mwenyezi Mungu na huku akibainisha baadhi ya vielelezo vinavyoonesha kupotea bure fursa ya mimbari na usomaji wa kasida za Ahlul Bayt AS, amesema kuwa: Kama matokeo ya mimbari na usomaji wa kasida za Ahlul Bayt yatakuwa ni kuwavunja moyo na kuwakatisha tamaa watu kuhusu mustakbali wao, au kama fursa hiyo itashindwa kuleta mwamko kwa watu katika jamii na kuwafanya watekeleze ipasavyo majukumu yao, basi ni wazi kuwa fursa hiyo itakuwa imepotezwa bure na itakuwa imetumiwa vibaya.
Ayatullah Udhma Khamenei amelitaja suala la kuleta madhara kwenye juhudi za kuimarisha umoja na mshikamano na kuzusha mizozo kati ya Waislamu wa Kishia na Kisuni kuwa ni mfano mwingine wa wazi wa kukufuru neema za Mwenyezi Mungu na kuongeza kwa kusema: Nimesisitiza mara nyingi kuwa mikusanyiko ya kidini haipaswi kuwa sehemu ya kueneza chuki za kimadhehebu kwani ni jambo lililo wazi kabisa kwamba, kueneza chuki na mizozo kati ya Waislamu ni mfano wa kuwapa upanga maadui wa Uislamu wawapige vita Waislamu na kufanikisha malengo yao ya kiuadui.
Aidha amegusia nasaha za viongozi wakubwa wa ulimwengu wa Kiislamu kuhusiana na umuhimu wa kudumishwa umoja na mshikamano kati ya Waislamu na kusema kuwa: Sisi tunaona fakhari kwa kuwa kwetu wafuasi wa Imam Ali AS na tunaona fakhari pia kuona kwamba, Imam wetu mtukufu (Imam Khomeini - quddisa sirruh) ni mbeba bendera ya "Wilaya" na amekuwa sababu ya kupata fakhari ulimwengu mzima wa Kiislamu, uwe wa Kishia au wa Kisunni hivyo si sahihi hata kidogo kunoa upanga wa kueneza chuki na mizozo kati ya Waislamu kupitia maneno na vitendo visivyostahiki vya baadhi ya watu.
Nasaha nyingine zilizotolewa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa jamii ya wasoma kasida za Ahlul Bayt AS ni udharura wa kuchunga kina, mipaka na usuli za kisheria na kidini katika maeneo kunakofanyika mikutaniko ya kidini.
Amesema, maeneo zinakofanyika sanaa za kidini na kusoma kasida, kiasili ni maeneo safi na yaliyotakasika na kila aina ya uchafu wa kimaadili na kusisitiza kwamba: Maeneo hayo na mazingira yake inabidi yaendelee kuwa masafi na ya staha na haipasi kuruhusu kuingia katika ulimwengu wa sanaa ya Kiislamu na kidini, mambo yasiyochunga mipaka na hududi za kisheria.
Mwishoni mwa hotuba yake, Ayatullah Udhma Khamenei amelitaja suala la kuteua kwa umakini wa hali ya juu, maudhui na maelezo yenye mafunzo na yenye kuleta mwamko kuwa ni jambo jingine la dharura linalopaswa kuwemo kwenye sanaa zinazowahusu Ahlul Bayt wa Bwana Mtume Mtukufu SAW na kuongeza kuwa: Mashairi na kasida za maombolezo zenye kuleta mwamko na kuamsha watu zilizokuwa zikisikika zikisomwa kote nchni Iran katika ule wakati wa hamasa, msisimko na shauku za Mapinduzi ya Kiislamu zilitoa mchango mkubwa sana katika kupatikana ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran.
Mwanzoni mwa mkutano huo, washairi na wasoma kasida wanane wamesoma mashairi na kasida zao zilizozungumzia adhama na utukufu wa binti wa Bwana Mtume Muhammad SAW, Bibi Fatimatuz Zahra SA.
 
< Nyuma   Mbele >

^