Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Atembelea Kundi la Viwanda la Mapna Chapa
30/04/2014
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Atembelea Kundi la Viwanda la MapnaIkiwa ni katika kukaribia siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, leo asubuhi (Jumatano) amekagua kundi la viwanda la Mapna lililoko katika eneo la Fardis Karaj, magharibi mwa Tehran na kutembelea maonyesho yaliyoandaliwa maalumu kwa ajili ya kuonesha uwezo wa wataalamu, wasomi na wafanyakazi wa Iran katika kundi hilo la viwanda katika mambo mbali mbali kama vile kubuni na kutengeneza zana na vifaa vya viwandani, pamoja na uwezo wao katika sekta za mafuta, gesi, petrokemikali na ufundi wa masuala ya reli.
Baada ya kutembelea maonyesha hayo amewahutubia wafanyakazi, viongozi, wabunifu na wapangaji wa mipango ya kazi za kundi hilo la viwanda la Mapna pamoja na mamia ya wafanyakazi wa sehemu nyingine mbali mbali za uzalishaji na kusema kuwa, kuenziwa, kuzingatiwa na kuheshimiwa jamii ya wafanyakazi na watu wote wenye michango yao katika sekta ya uzalishaji ni jambo la dharura sana na limesisitiziwa mno na mafundisho ya dini tukufu ya Kiislamu. Vile vile ameashiria namna taifa la Iran lilivyo na vipaji na welewa wa kupigiwa mfano wa mambo na kusisitiza kwamba: Azma ya kweli na uongozi wa kijihadi si tu ni kaulimbiu ya mwaka huu (wa Kiirani wa 1393 Hijria Shamsia) bali ni nara na kaulimbiu yetu na daima na ni dhihirisho la utambulisho, heshima na mustakbali unaong'ara wa nchi hii.
Wakati alipokuwa akikagua maonyesho hayo ya kundi la Mapna katika wakati huu wa kukaribia kuingia mwezi mtukufu wa Rajab na maadhimisho ya kuzaliwa Imam Muhammad Baqir Alayhis Salaam, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameona kupitia video kuanza kufanya kazi kituo cha umeme cha Najaf tukufu cha nchini Iraq kilichobuniwa na kutengenezwa na wataalamu wa kundi la viwanda la Mapna.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu vile vile ametembelea maonyesho hayo yanayoonyesha uwezo wa wataalamu wa Kiirani wa kundi la viwanda la Mapna kwa muda wa saa moja na nusu na kuona kwa karibu mafanikio na hatua mbali mbali zilizopigwa na wataalamu hao. Katika maonyesho hayo kumeonyeshwa mafanikio na uwezo wa wasomi na wataalamu wa Kiirani katika kutengeneza na kufunga tabo (injini za maji/mvuke/hewa/gesi), na vinu vya upepo, uundaji wa aina kwa aina za mabwela na vifaa vya kuchemshia vitu vya viwandani, kuunda na kukarabati aina kwa aina ya tabo na majenereta, kuunda kompresa za viwandani, kutengeneza mifumo ya kudhibiti na kuendeshea vitu mbali mbali, kutengeneza anuwai kwa anuwai za vipuri vya visima vya mafuta na pampu za kila namna, kutengeneza minara na milingoti ya baharini, kubuni na kuzalisha vifaa vya kubadilisha maji ya chumvi kuwa matamu, kubuni na kutengeneza vichwa vya magarimoshi pamoja na kuboresha na kukarabati reli na mchakato mzima wa utafiti na upanuzi wa kila kitu katika kundi la viwanda la Mapna.
Baada ya kutembelea maonyesho hayo ya mafanikio ya majimui na kundi hilo la uzalishaji viwandani na masuala ya uchumi, amehutubia hadhara ya maelfu ya wafanyakazi na watu wengine wanaohusika katika masuala ya uchapaji kazi na huku akiashiria kukaribia kuingia mwezi uliojaa baraka na wenye mvuto wa aina yake wa Rajab, ameutaja mwezi huo kuwa ni mwezi wa ibada, kunyenyekea kwa Mwenyezi Mungu na kumdhukuru Allah sana na ameelezea matumaini yake kwamba taifa la Iran chini ya kivuli cha auni na uongofu wa Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema, litafanikiwa kupiga hatua kubwa zaidi ya lilizopiga hivi sasa.
Amesema siku zote mikutano yake na wafanyakazi inakuwa na mvuto wa aina yake na huwa ya kuvutia sana na kuongeza kwamba, furaha aliyoipata leo imeongezeka maradufu baada ya kutembelea maonyesho hayo na kuona kwa macho yake mafanikio makubwa yaliyopatikana.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa mara nyingine tena amesisitizia imani yake thabiti kuhusiana na udharura wa kuenziwa na kupewa heshima yao wafanyakazi katika utamaduni wa watu wote kwenye jamii na kuongeza kuwa: "Asili ya kazi na kufanya jitihada" katika Uislamu ni suala ambalo linaheshimiwa sana na kwamba kitendo cha Uislamu cha kuzingatia sana haki na nafasi ya wafanyakazi na watu wote wanaohusika katika masuala ya uzalishaji, nacho kinatokana na mtazamo huo huo uliotukuka na usiotetereka wa dini tukufu ya Kiislamu kwa jambo hilo.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa, aidiolojia za Kimaksi na Kimagharibi zinakuwa na msimamo mmoja linapofika suala la kuhakikisha kuna mitazamo inayokinzana na inayogongana baina ya mfanyakazi na mwajiri na kusema kuwa, mtazamo huo kwa hakika ni ghalati na ni makosa. Amesema, dini tukufu ya Kiislamu lakini inalihesabu suala la kuheshimiana, kuvumiliana na kushirikiana katika kazi baina ya mfanyakazi na mwajiri kuwa ni jambo la msingi sana, na kwamba hilo halihusiana na mwajiri na mfanyakazi tu, bali linahusu nyuga na nyanja zote na inabidi suala hilo liwe msingi mkuu katika medani zote zikiwemo za kijamii na za kiuchumi.
Nukta ya pili iliyosisitiziwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika hotuba yake ya leo mbele ya wafanyakazi na viongozi wa kundi la viwanda la Mapna na majimui nyingine za uzalishaji nchini Iran ni kuchapa kazi kwa idili na jitihada zote kwa kutegemea elimu, utambuzi, welewa, ubunifu, bidii kubwa pamoja na nia na azma ya kweli.
Amesisitiza kuwa: Uhakika huu wa kuvutia ambao baadhi yake tumeuona leo wakati tulipotembelea maonyesho ya kundi la viwanda la Mapna unaonesha kwamba azma ya kitaifa na uongozi na usimamiaji wa kijihadi si tu kwamba ni kaulimbiu ya mwaka huu tu (wa Kiirani wa 1393 Hijria Shamsia), bali ni kaulimbiui ya daima na ni nembo ya utambulisho na heshima na mustakbali bora wa nchi yetu.
Amesema, kuweko ustawi wa kiuchumi bila ya kuweko ustawi wa kiutamaduni ni jambo lisiloyumkinika bali ni suala lisilo na faida kabisa na kuongeza kuwa: Ni kwa sababu hiyo ndio maana kaulimbiu yetu ya mwaka huu ikawa ni kaulimbiu ya maisha na ikawa ndiyo nara yetu ya milele.
Ayatullah Udhma Khamenei amelitaja suala la kufikia katika vilele vya juu vya uchumi na utamaduni wa nchi kuwa linahitajia kuweko nia na azma ya kweli ya kitaifa na uongozi na usimamiaji wa kijihadi na kuongeza kwamba: Iwapo lengo hilo litafikiwa, basi hakuna mtu yeyote atakayethubutu kulidhalilisha taifa hili.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia jinsi taifa la Iran lilivyokuwa linadunishwa katika kipindi cha kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu na kuongeza kuwa: Katika zama ambazo Ulaya na Magharibi zilikuwa ndani ya ujahili mutlaki, Iran ilikuwa ni taifa lililostaarabika na kuwa na fakhari nyingi, likikuwa ni taifa lililokuwa linaitunuku jamii ya mwanadamu shahksia adhimu wa kielimu na kiutamaduni, lakini hao hao Wamagharibi waporaji walitumia vibaya uduni waliokuwa nao watawala mataghuti waliokuweko madarakani kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu na kudhibiti masuala ya kiuchumi, kisiasa na mambo ya kijamii ya Iran na kwamba tukio hilo chungu lilikuwa ni udhalilishaji mkubwa kwa taifa kama la Iran ambalo lina ustaarabu mkongwe na lenye turathi zenye thamani kubwa za kiutamaduni.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria pia kumalizika kipindi cha kudhalilishwa na kufanywa duni taifa la Iran baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kusisitiza kuwa: Kama taifa la Iran linataka kufikia kwenye daraja na hadhi yake ya juu linayostahiki kuwa nayo katika upande wa kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiutamaduni duniani, na kugeuka kuwa marejeo ya maendeleo ya kielimu ya mwanadamu, linapaswa kuhakikisha lina nguvu za kielimu, utambuzi, nguvu za harakati, nguvu za ubunifu na nia na azma ya kweli katika nyuga zote.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria kudhihiri athari nzuri na zilizojaa baraka za kujiamini katika sekta mbali mbali za jamii ya Iran na kuongeza kuwa: Matukio hayo yenye kutia shauku yanazidi kuthibitisha kuwa nara na kaulimbiuu kuu ya Imam Khomeini (quddisa sirruh) ya kwamba "tunaweza" si kaulimbiu ya maneno tu bali ni shaari na nara inayoweza kufanikishwa kivitendo.
Vile vile ameashiria wasiwasi, hatihati na hofu wanayo kuwa nayo baadhi ya watu kuhusu nguvu na uwezo wa vijana wa Iran na kuongeza kuwa: Kushika Iran nafasi ya sita kati ya watengenezaji wakuu wa vinu vya gesi duniani ni moja na mifano midogo tu ya uwezo adhimu wa nguvu kazi ya Iran ambayo yaliwekewa misingi yake na vijana wa Iran katika kipindi kigumu cha vita na mashinikizo makubwa ya kila upande na hivi sasa juhudi hizo zimeanza kuzaa matunda.
Ayatullah Udhma Khamenei amewakhutubu watu wanaojihusisha na masuala mbali mbali akisisitiza kuwa, matarajio yenu yaongezeni sana na yawe ni kwa ajili ya kujiletea maendeleo mara kumi zaidi ya maendeleo yaliyopo leo na ni jambo lililo wazi kabisa kwamba hilo linawezekana.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika sehemu nyingine ya hotuba yake ameyataja mafanikio yaliyopatikana kwenye kundi la viwanda la Mapna kuwa yameiletea fakhari nchi na wafanyakazi na watu wote wanaohusika na kundi hilo la viwanda. Ameongeza kuwa, sekta mbali mbali za Serikali zinapaswa kusaidia na kuunga mkono majimui kama hizo za uzalishaji.
Vile vile amelitaja suala la kuunga mkono uzalishaji wa ndani kuwa ni miongoni mwa nguzo za uchumi wa kusimama kidete na kuongeza kuwa: Chini ya kivuli cha siasa hizo, vyombo mbali mbali vya serikali ni lazima sambamba na kuwaunga mkono wazalishaji, vizitafutie masoko bidhaa na mazalisho ya wazalishaji hao wa ndani na kuangalia kwa kina matatizo na dosari zilizomo katika bidhaa kama hizo zinazotoka nje ya nchi.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria pia nguzo nyingine muhimu ya uchumi wa kimuqawama na wa kusimama kidete yaani kujizalisha ndani kwa ndani na kuwa na nafasi nje akiongeza kuwa: Inabidi tuwe na ustawi na tujiimarishe vizuri ndani lakini wakati huo huo tujiimarishe na tuwe na nafasi muhimu pia katika masoko ya kimataifa.
Vile vile amekutaja kujiamini na kuwa na imani ya kuweza kufanya jambo na vile vile kutawakali kwa Mwenyezi Mungu na kutegemea misaada Yake kuwa ni miongoni mwa masuala muhimu sana katika kusimamia na kuongoza mambo kijihadi.
Ameongeza kuwa, kutawakali kwa Mwenyezi Mungu na kuomba msaada Wake huleta rehema na auni ya Mwenyezi Mungu hata katika masuala ambayo kwa mahesabu ya kawaida inakuwa haiwezekani hata kuyatabiri na kufikiria kuwa yanaweza kutokea.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekutaja kuyategemea mashirika na makundi ya elimu za kimsingi kuwa ni nguzo nyingine ya uchumi wa kusimama kidete na huku akiashiria udharura wa serikali wa kuunga mkono majimui hizo ameongeza kuwa: Maendeleo anayoyapata mtu hayapaswi kumfanya abweteke na kutosheka na alipofikia bali inabidi yampe shauku na mori wa kupiga hatua kubwa zaidi za maendeleo na kuvuuka kwa mafanikio kwenye njia ambazo hajawahi kuzivuuka.
Sisitizo kwa udharura wa kufanya utafiti na kuleta ustawi mkubwa zaidi katika majimui za uzalishaji na za kiuchumi na kuunganishwa pamoja nguvu za sehemu zote zilizoko nchini ikiwa ni pamoja na nguvu za maeneo ya viwandani na Vyuo Vikuu ni nukta nyingine mbili ambazo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezitaja kuwa ni mambo ya lazima na ya dharura.
Ameutaja uwezo wa kila sekta nchini kuwa unao uwezo wa kuvilazimisha vikwazo viondoke vyenyewe kutaka na kukataa na kuongeza kuwa: Kila tunavyopata maendeleo katika sekta yoyote ile, ndivyo upande wa pili unavyozidi kutambua kuwa vikwazo vyake dhidi yetu ni upuuzi na ujinga mtupu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa mfano kuhusu uhakika huo akisema: Wakati tulipohisi kuwa hatukuwa na haja ya kuzalisha urani iliyorutubishwa kwa asilimia 20 kwa ajili ya kituo cha utafiti wa nyuklia cha Tehran na kwa ajili ya kuzalisha dawa za mionzi zinazohitajiwa na wananchi wetu kwa vile tulihisi tunaweza tu kununua urani tunayoihitajia, tulikuwa tayari kununua urani hiyo, lakini madola ya kibeberu duniani yakiongozwa na Marekani yalifanya kila hila ili kutuzuia tusiweze kuinunua.
Ameongeza kuwa: Hapo Jamhuri ya Kiislamu ikaamua kujizalishia yenyewe urani iliyorutubishwa kwa asilimia 20, jambo ambalo maadui wa taifa la Iran hata hawakuwa wakifikiria kuwa taifa letu linao uwezo na utaalamu wa kurutubisha urani, lakini baada ya kuona kuwa wanasayansi wetu vijana wameonesha kivitendo uwezo wao na kudhihirisha vipaji vyao vikubwa chini ya kivuli cha usimamiaji na uongozi mzuri wa kusimamia teknolojia hiyo na kuweza hata kutengeneza fito na sahani zinazohitajika katika kazi hiyo, madola yote ya kibeberu hivi sasa yanasema, tuko tayari sasa kukuzieni urani mnayoitaka, na acheni kujizalishia wenyewe urani hiyo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema katika sehemu nyingine ya hotuba yake hiyo kuwa dunia hivi sasa inateseka kutokana na tabia mbaya na michezo miovu ya kisiasa ya madola makubwa na kusisitiza kuwa: Vitendo visivyo vya kimantiki vya madola ya kibeberu duniani kuhusiana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vinategemea nguvu na udhaifu wetu. Wakati wowote tunaposimama imara na kuwa na nguvu katika jambo fulani, madola hayo hulazimika kuamiliana nasi kwa heshima na kimantiki. Amesema utatuzi wa masuala yote ya Iran ni kuzingatia uhakika huo.
Katika mkutano huo, Bw. Rabei, Waziri wa Ushirika, Kazi na Ustawi wa Kijamii wa Iran ametoa hotuba fupi na huku akiashiria umuhimu wa kuweko harakati ya nchi nzima ya kuimarisha uzalishaji wa elimu za kimsingi amesema: Wafanyakazi, ndio nguvu ya uchumi wa kusimama kidete na kwamba leo hii wafanyakazi wa Iran mhimili wao mkuu umekuwa ni elimu na maarifa.
Vile vile ameashiria hatua ya kuitwa mwaka huu (wa Kiirani wa 1393 Hijria Shamsia) kuwa mwaka wa uchumi na tamaduni wenye azma na nia ya kitaifa na uongozi na usimamiaji wa kijihadi na kukumbushia nafasi ya wafanyakazi katika medani na nyuga tofauti za Mapinduzi ya Kiislamu na kuongeza kuwa: Hatuna njia nyingine isipokuwa kutekeleza siasa zetu zote za kiuchumi, kiutamaduni na kijamii kwa msingi na kwa kuzingatia uchumi wa kimuqawama na wa kusimama kidete.
Bw. Rabei pia amelitaja suala la kusimamisha uadilifu wa kijamii kuwa ni miongoni mwa malengo makuu na ya kimsingi ya Mapinduzi ya Kiislamu na kuongeza kuwa: Leo hii kunashuhudiwa uhusiano mzuri mno baina ya Serikali kwa upande mmoja na makundi na asasi mbali mbali za wafanyakazi, kwa upande wa pili.
Mwanzoni mwa mkutano huo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameonana kwa karibu na viongozi na wataalamu kadhaa wa kundi la viwanda la Mapna ambapo katika mkutano huo Muhandisi Hamid Chitchian, Waziri wa Nishati wa Iran ametoa ripoti fupi kuhusu uwezo mbali mbali wa kundi la viwanda la Mapna katika nyuga tofauti.
Waziri wa Nishati wa iran amesema: Zaidi ya thuluthi moja na vinu na vituo vya nishati nchini Iran na ambavyo vina uwezo wa kuzalisha megawati 24 elfu za umeme, vimetengenezwa na viwanda vya shirika la Mapna.
Bw. Hamid Chitchian ameitaja hatua ya kuasisiwa shirika hilo mwaka 1992 na uwezo mkubwa na wa kila namna lilio nao sasa hivi, kuwa ni ushahidi wa kivitendo wa kuweko uongozi na usimamiaji wa kijihadi katika shirika hilo na kuongeza kuwa: Kutumia teknolojia za kisasa na kunyanyua kiwango cha teknolojia hizo pamoja na kupanua wigo wa kazi za utafiti na uhakiki, kutumia nishati zenye uwezo wa kujadidishwa na kuzalishwa upya na kuingia katika hatua ya kutengeneza vizazi vipya vya vinu vya kila nui ni miongoni mwa hatua, jitihada na kazi zinazofanywa na kundi hilo la viwanda.
Naye Muhandisi Ali Abadi, Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Viwanda la Mapna ametoa ripoti fupi kuhusu shirika hilo na huku akiashiria kuhodhiwa utengenezaji wa vinu mbali mbali na baadhi ya nchi duniani kama vile Marekani na nchi chache za Ulaya amesema kuwa, shirika la Mapna kwa kutumia uwezo wa wataalamu na wasomi ya ndani ya Iran, limeweza hivi sasa kushika nafasi ya sita duniani katika utengenezaji wa zana, vifaa na vinu vya kila namna.
Aidha ameashiria utafiti, upanuzi na ustawi mbali mbali unaofanyika ndani ya shirika hilo kwa kutumia teknolojia za kisasa na kuongeza kuwa: Shirika la Mapna sasa limeingia katika sekta mbali mbali za umeme, mafuta, gesi, uchukuzi, vifaa vya kuzalisha maji matamu na katika eneo la nishati jadidifu na limepiga hatua kubwa sana katika nyuga hizo.
Ayatullah Udhma Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu naye kwa upande wake ametoa hotuba fupi mbele na wataalamu na viongozi wa shirika hilo na kumesema kuwa, kuundwa shirika la viwanda la Mapna na mafanikio makubwa na uwezo wa kupigiwa mfano lilio nao hivi sasa shirika hilo ni matunda ya kushikamana na vitu vitatu vikuu, "elimu, azma ya kweli na sanaa." Amesisitiza kuwa, inabidi mambo hayo matatu yalindwe na kuhifadhiwa vyema.
 
< Nyuma   Mbele >

^