Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Aonana na Maafisa wa Jumuiya ya Wakunga Chapa
05/05/2014
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Aonana na Maafisa wa Jumuiya ya Wakunga Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, leo (Jumatatu) ameonana na maafisa kadhaa wa Jumuiya ya Wakunga ya Iran sambamba na maadhimisho ya Siku ya Wakunga Duniani na kusisitiza kuwa, umuhimu na nafasi ya tabaka hilo la wananchi katika kudhamini usalama wa kiafya wa jamii na vile vile katika kusaidia kubakia kizazi cha mwanadamu ni muhimu mno na ni yenye thamani kubwa sana. Vile vile amesisitizia umuhimu wa kujengwa tabia na utamaduni wa watu wote wa kustafidi vizuri na huduma zinazotolewa na wakunga kwa ajili ya kuzitia katika utekelezaji wa kivitendo siasa kuu za nchi za kuongeza idadi ya watu na kuongeza kuwa: Suala la kuongeza idadi ya watu na kuzuia kupungua idadi ya vijana nchini, ni suala muhimu mno na inabidi lifuatiliwe kwa uzito wa hali ya juu.
Ayatullah Udhma Khamenei amewashukukru wakunga wa nchini kutokana na kukubali kubeba tabu nyingi na kuwahudumia watu kwa moyo mkunjufu kabisa akisema, wakunga nchini Iran wanatumia subira, elimu, uzoefu, kuheshimu majukumu na kufanya kazi kwa idili na bidii kubwa na kwamba jamii hiyo ya wanchi wa Iran inatoa mchango mkubwa na muhimu zaidi katika kulinda usalama wa mama na mtoto na kuongeza kwamba: Ni kwa msingi huo ndio maana watu wote, wanaume kwa wanawake, wana deni mbele ya wakunga na ndio maana pia miaka yote jamii ya wakunga katika jamii imekuwa ikiheshimiwa na kutukuzwa sana na watu.
Aidha amelitaja suala la kujenga utamaduni na tabia ya kuwaheshimu na kuwapa nafasi muhimu zaidi wakunga kuwa ni jambo muhimu na la kimsingi katika kuishajiisha na kuihamasisha jamii ya wanawake kutumia huduma zinazotolewa na wakunga na vile vile kushajiisha watu kuzaa kwa kawaida (si kwa upasuaji) na kuongeza kuwa: Wataalamu wa masuala ya tiba wanapaswa kuielimisha jamii mara kwa mara na kutumia vizuri vyombo vya habari katika kuwaelimisha watu juu ya umuhimu na faida nyingi za kuzaa kwa kawaida, ikiwa ni katika kulinda usalama wa kiafya wa mama na mtoto.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia umuhimu mkubwa wa kuzaa watoto wengi na kuongeza idadi ya watu na nafasi muhimu sana ya kuzaa kwa njia za kawaida na huduma zinazotolewa na wakunga katika suala hilo muhimu akisisitiza kuwa: Kuongezeka idadi ya vijana ni moja ya mambo mazuri kwa nchi na iwapo siasa na hatua zisizo sahihi zitaendelea kuchukuliwa na hivyo kupelekea kupungua vibaya idadi ya vijana nchini katika miaka ijayo, basi Iran itapata pigo kubwa sana linalojulikana kwa jina la kuwa na jamii kubwa ya vizee.
Ameongeza kwamba: Nchi isipokuwa na vijana ina maana ya kwamba ni nchi isiyo na ubunifu wala maendeleo na wala hamasa na uchangamfu. Hivyo mipango hii muhimu sana ya kuongeza idadi ya watu inabidi ifuatiliwe vilivyo na itekelezwe kwa uzito wa hali ya juu kabisa.
Ayatullah Udhma Khamenei vile vile amesisitizia udharura wa kutatuliwa matatizo ya jamii ya wakunga nchini na kuongeza kuwa, viongozi katika vyombo vya serikali wanapaswa kutia nia ya kweli ya kufidia mapungufu na nakisi zilizopo katika suala hilo.
Mwanzoni mwa mkutano huo, Dk Bi Masoumeh Aabad, Mkuu wa Jumuiya ya Wakunga ya Iran amesema kuwa, kuna wahitimu 50 elfu waliomaliza mafunzo ya ukunga nchini Iran na huku akiashiria nafasi ya ukunga katika suala zima la ustawi na kuongezeka idadi ya watu ameongeza kuwa: Leo hii karibu asilimia 50 ya watoto wanaozaliwa nchini Iran wanazaliwa kwa njia ya upasuaji na kwamba kujifungua kwa namna hiyo ambako mara nyingine linakuwa si jambo la dharura, ni kizuizi kikuu katika kuendelea kubeba ujauzito wazazi na kuongezeka idadi ya watu nchini.
Aidha amelitaja suala la kuongezewa nguvu huduma za ukunga na vile vile kuweko mipango mizuri ya kutoa elimu kwa wasichana kuhusu suala hilo katika vituo vya elimu, kuwa ni miongoni mwa kazi zinazofanywa na jumuiya hiyo katika juhudi za kurekebisha utamaduni wa watu na mtazamo wao kuhusiana na huduma zinazotolewa na wakunga.
 
< Nyuma   Mbele >

^