Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Walimu Waonana na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Chapa
07/05/2014
Walimu Waonana na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya KiislamuAyatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, leo asubuhi (Jumatano) ameonana na maelfu ya walimu na kuitaja kazi ya kutoa elimu na kufundisha fikra na kufunza mienendo mizuri na maadili bora ni mambo matatu makuu yaliyomo ndani ya taaluma tukufu na yenye fakhari kubwa ya ualimu na huku akisisitizia wajibu wa kuweko mipango mizuri inayotekelezeka kivitendo kwa ajili ya kutekeleza hati ya mabadiliko makubwa katika Wizara ya Elimu na Malezi ya Iran ameongeza kuwa: Kuungwa mkono kikamilifu chombo hicho adhimu, ni uwekezaji wenye taathira kubwa na nzuri kwa ajili ya mustakbali unaong'ara wa wana wa taifa hili na kwa ajili ya maendeleo yenye kasi, ya kimaada na kimaanawi ya Iran azizi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha amelitaja lengo kuu la kuonana kwake na walimu kuwa ni kuonesha shukrani zake nyingi kwa jamii ya walimu nchini Iran na kuonesha heshima zake kwa nafasi na umuhimu mkubwa wa taaluma ya ualimu na malezi.
Amesisitiza kuwa, sote tuna deni kubwa kwa walimu, hivyo kuna ulazima wa kuitukuza na kuiheshimu taaluma ya ualimu inabidi na kuhakikisha kuwa suala hilo linakuwa ni jambo la watu wote katika jamii na ifikie kiwango ambacho kila mtu aone fakhari kumsalimia na kuonesha heshima zake kubwa kwa mwalimu.
Aidha amewataja watoto wa watu kuwa ni amana wanayopewa walimu kuitunza na huku akitoa ufafanuzi kuhusu vipengee vikuu vya taaluma ya ualimu amesema: Kutoa elimu na maarifa, ni jukumu muhimu sana, lakini jambo lililo muhimu zaidi ya hilo, ni kuwapa elimu ya tafakuri watoto na vijana wadogo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja suala la kuwa na fikra hafifu na kuwa na kiwango cha chini cha utaalamu katika utoaji elimu, kuwa hupelekea mambo kukwama katika jamii na kuongeza kwamba: Iwapo mtoto atajifunza moyo wa kutafakari na kama atajifunza njia sahihi za kufikiri kutoka kwa mwalimu wake, basi mustakbali wa nchi nao utasimama juu ya msingi wa tafakuri na mantiki, hivyo walimu wetu azizi wana jukumu zito sana katika uwanja huo.
Ayatullah Udhma Khamenei amekutaja kutoa elimu za kivitendo za maadili bora na mienendo mizuri kuwa ni upeo wa tatu wa taaluma iliyojaa fakhari ya ualimu na kusisitiza kuwa: Ili kufanikisha shabaha na malengo matukufu na makuu ya taifa, kuna haja ya kuwa na watu wenye subira, wenye akili, walioshikamana na dini, wabunifu, wenye huruma, mashujaa, wanaojiweka mbali na maovu, wenye heshima na wachapa kazi mahiri wasiochoka na kwamba walimu wana jukumu la juu kabisa na athari kubwa na zenye kubakia milele katika kulea watu wa namna hiyo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia nukta nyingine muhimu katika uwanja hao na kuwasisitizia walimu kuhusu nukta hiyo nayo ni kwamba elimu ya akhlaki na mtindo mzuri wa maisha haufundishwi tu kwa kutumia vitabu, bali msomeshaji mwenyewe anatakiwa ajipambe kwa mienendo mizuri ya kimaadili na kiakhlaki.
Ayatullah Udhma Khamenei vile vile amebainisha nukta nyingine kadhaa kuhusiana na usimamiaji na uendeshaji wa mambo na kuwataka maafisa na viongozi wa chombo hicho adhimu kuipa uzito mkubwa hati ya mageuzi katika Wizara ya Elimu na Malezi na kuongeza kuwa: Utekelezaji wa hati hiyo muhimu sana na ya kimsingi unahitajia kuwa na muongozo, ramani ya njia na mipango inayotekelezeka kivitendo na kwamba kuna ulazima wa kutungwa mikakati mizuri na kusimamiwa mambo hayo kwa kushauriwa Baraza Kuu la Mapinduzi ya Kiutamaduni na kutekelezwa hatua kwa hatua.
Vile vile amelitaja suala la nguvu kazi kuwa ni jambo jingine muhimu katika majukumu ya Wizara ya Elimu na Malezi na kuongeza kuwa: Chombo hicho kinaainisha kwa njia ya moja kwa moja mustakbali wa taifa na kina uhusiano na makumi ya mamilioni ya watu, hivyo viongozi na maafisa wa ngazi za juu wa chombo hicho, wana wajibu wa kujipamba kwa sifa maalumu za kipekee za kuwawezesha kutekeleza vizuri majukumu yao.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia amesisitiza kuwa: Nguvu kazi ya vijana wanamapinduzi, walioshikamana na dini, wenye hamasa, wenye misukumo inayotakiwa na wanaopenda kazi zao, ndiyo inayopaswa kupewa kipaumbele na uzito wa hali ya juu na pia amewataka viongozi na maafisa wa chombo hicho kuhakikisha kuwa, shabaha yao kuu inakuwa ni kufanikisha malengo ya chombo hicho yaani Wizara ya Elimu na Malezi.
Vile vile amebainisha udharura wa Wizara ya Elimu na Malezi ya Iran kutegemea nguvu kazi za watu wana mapinduzi na walioshikamana vizuri na dini na kuongeza kuwa: Lengo na shabaha kuu ya taifa na viongozi nchini ni kuhakikisha kuwa, kwa baraka za Uislamu na Qur'ani Tukufu, kunapatikana jamii ambayo itakuwa ni kigezo cha maendeleo ya pande zote, ya kimaada, kimaanawi na kimaadili na kwamba ili kuweza kufanikiwa katika safari ndefu na nzito ya kufanikisha lengo hilo muhimu, kunahitajika kulelewa kizazi cha watu makini, wenye fikra nzuri na walio imara katika Wizara ya Elimu na Malezi na suala hilo nalo ni kazi ya viongozi na nguvu kazi ya watu walioshikamana vilivyo na dini na wana mapinduzi.
Ayatullah Udhma Khamenei pia amelitaja suala la kuangalia mambo kwa kuzingatia misimamo ya mirengo ya kisiasa, kivyama na kimakundi kuwa ni sumu kwa Wizara ya Elimu na Malezi na kuongeza kuwa: Ni jambo la kusikitisha kuona kwamba kuna wakati jambo hilo liliiteka wizara hiyo na kulisababishia taifa hasara kubwa.
Vile vile amesema ni jambo la dharura mno kuungwa mkono kikamilifu Wizara ya Elimu na Malezi na vyombo vyote nchini hususan vyombo vinavyohusiana na sekta ya bajeti ya serikali na kusisitiza kuwa: Kadiri itakavyowekezwa na kutengwa fedha nyingi zaidi za kuiimarisha Wizara ya Elimu na Malezi ndivyo matunda mazuri yatakavyoweza kupatikana, kwani chombo hicho ni mzizi na msingi wa maendeleo yote ya hivi sasa na ya siku za usoni ya taifa.
Aidha amesisititizia sana wajibu wa kuchunga na kuwa makini katika mambo na kuangalia sana aina ya vitabu vinavyosomeshwa na kusema: Masuala yaliyomo katika vitabu ni lazima yawe ya kina, makini na ya maana na kuna wajibu wa kujiepusha na kuingiza jambo lolote la upotofu na lisilo na uzito unaotakiwa katika vitabu hivyo, iwe ni suala la kisiasa, au la kidini au jambo lolote lile lisiloakisi ukweli wa jambo, hivyo maafisa wanaohusika na kutunga na kuratibu vitabu vya kufundishia wanapaswa kutekeleza vilivyo majukumu yao na kuwa makini mno na kuheshimu inavyotakiwa amana waliyo pewa.
Mwishoni mwa hotuba yake, Ayatullah Udhma Khamenei amewakumbusha viongozi na maafisa wa Wizara ya Elimu na Malezi nukta nyingine mbili muhimu. Ya kwanza ni kukizingatia na kukipa umuhimu sana Chuo Kikuu cha walimu nchini kwani hiyo ni sehemu inayolea nguvu kazi inayohitajika na pili ni kutoghafilika na kusahau umuhimu na nafasi yenye taathira kubwa ya kitengo cha malezi katika masuala ya kiwizara, uongozi na uendeshaji wa mambo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu vile vile amewausia walimu kustafidi vizuri na baraka za mwezi huu mtukufu wa Rajab ambao unatoa fursa ya kujiimarisha kiibada na kuilea vizuri nafsi na pia amemkumbuka na kumtaja kwa wema mwalimu, shahidi Ayatullah Mutahhari na kuongeza kuwa: Mwanafikra na mwalimu huyo mkubwa mpigania jihadi, alitumia njia ya fikra na itikadi za Kiislamu na kupitia fakhari ya kuuawa kwake shahidi, akafanikiwa kupata shahada ya ufaulu wa jitihada zake za muda mrefu kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Vile vile amewataja mashahidi Rajai na Bahonar kuwa nao walikuwa walimu wapigania jihadi wakubwa na wenye ikhlasi ambao umri wao wote waliutumia katika kutumikia ufundishaji na kufanya juhudi za kulea kizazi cha watu bora.
Mwanzoni mwa mkutano huo, Waziri wa Elimu na Malezi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa ripoti fupi na huku akiashiria jamii wa walimu milioni moja wa Iran amesema: Wizara ya Elimu na Malezi ndicho chombo kikubwa zaidi nchini Iran katika masuala ya utamaduni ambacho kinatoa huduma kwa wanafunzi milioni 12 wa shule za msingi nchini.
Dk Ali Asghar Fani amesema, miongoni mwa mikakati muhimu sana ya wizara yake ni kuongeza ubora wa elimu na malezi na kubainisha kuwa: Kubadilisha mfumo wa kuhifadhi mambo kwa moyo kuwa mfumo wa kuonesha vipaji na kubuni mambo, kutia nguvu ustaarabu wa kusoma vitabu, kuimarisha moyo wa kuuliza maswali, kustawisha utamaduni wa Hijab na kujisitiri vizuri, kuwa na mfungamano wa karibu na Qur'ani na Ahlul Bayt Alayhimus Salaam na kuweka misingi ya mtindo wa maisha ya Kiislamu Kiirani, ni miongoni mwa mipango inayopewa umuhimu na Wizara ya Elimu na Malezi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
 
< Nyuma   Mbele >

^