Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Aonana na Wabunge wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu Chapa
25/05/2014
Supreme Leader Meets with Members of MajlisAyatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu leo asubuhi (Jumapili) ameonana na Spika na wabunge wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) na kuitaja njia pekee ya kukabiliana na kambi iliyo dhidi ya ubinadamu ya kiistikbari kuwa ni kuendelea na fikra ya "mapambano" na huku akiashiria ulazima wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu na Serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kulipa uzito wa hali ya juu suala la kutunga mpango wa sita wa maendeleo amesisitizia udharura wa kuyapa uzito mkubwa masuala matatu makuu ambayo ni "uchumi wa kusimama kidete," "utamaduni wa kimapinduzi na kidini" na kuendelea na mwenendo wenye kasi kubwa wa "maendeleo ya kielimu" akisema kuwa, njia ya kuweza kutatua matatizo ya kiuchumi na kisiasa nchini haiwezekani kuipata nje ya mipaka ya nchi, bali utatuzi wa kweli wa matatizo hayo umo ndani na umo katika kutegemea uwezo na nguvu za ndani ya nchi.
Katika mkutano huo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha ametoa mkono wa pole kwa mnasaba wa kumbukumbu za siku aliyouawa shahidi Imam Musa al Kadhim (Alayhis Salaam). Vile vile amegusia namna mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ulivyoundwa na jinsi ulivyoweza kudumu na kuimarika kutokana na kushikamana na "fikra ya mapambano" na kusisitiza kwamba: Maendeleo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuvuuka kwa mafanikio mfumo wa Kiislamu katika vipindi muhimu mno kwenye kipindi chote hiki cha miaka 35 iliyopita kunatokana na ukakamavu na mapambano ya kweli na yenye busara nyingi ya taifa la Iran na kwamba fikra hiyo inabidi ilindwe na sifa zake za kipekee ziendelezwe.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza pia kuwa, bila ya kuendelea na fikra ya kupambana na kambi ya kiistikbari na kibeberu, haiwezekani hata kupata picha tu ya kuyafikia malengo makuu matukufu ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na kuongeza kuwa: Sababu inayotufanya tusisitizie suala la kuendelea na mapambano, si kwa kuwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu unapenda vita, bali akili na busara inahukumu kuwa, mtu anayepita kwenye eneo lililojaa maharamia, anapaswa ajiandae vilivyo na awe na uwezo wa kutosha wa kujilinda mbele ya mashambulizi ya maharamia hao.
Amesisitiza kuwa: Dunia ya leo imejaa wezi na waporaji wa heshima, utamulisho na maadili ya kibinadamu ambao wamejiimarisha kielimu, kiutajiri na kwa nguvu za aina mbali mbali na wanafanya jinai kiurahisi sana duniani huku wakijidhihirisha kwa sura ya kupenda ubinadamu lakini kumbe ni wasaliti wa malengo matakatifu ya kibinadamu na wanaeneza vita katika nukta mbali mbali za dunia.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia amesema, katika hali na mazingira kama haya hatuna njia nyingine isipokuwa kuendelea na mapambano na kuhakikisha kuwa fikra ya mapambano inatawala katika masuala yote ya nchi yetu, iwe ni katika masuala ya ndani au masuala ya nje ya nchi.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria pia namna baadhi ya watu wanavyojaribu kupandikiza fikra ya mapatano na kusalimu amri mbele ya mabeberu na kusema kuwa: Watu ambao wanataka kueneza fikra ya mapatano na kusalimu amri mbele ya mabeberu na ambao wanautuhumu mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu kuwa eti unapenda vita, wajue kuwa kitendo chao hicho ni sawa na usaliti.
Ameongeza kuwa, mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ni mfumo wa kibinadamu unaolinda heshima na kutukuza utukufu wa mwanadamu na ni mfumo unaopenda amani na mambo ya kheri.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza pia kuwa: Viongozi wote nchini Iran na katika sekta mbali mbali iwe sekta za kiuchumi, au za kielimu au za kiutamaduni na sekta zinazohusiana na mazungumzo ya kimataifa, wanapaswa kujua kuwa wako katika mapambano na kwamba wamo katika njia ya kuendeleza mapambano kwa ajili ya kuujenga na kuudumisha mfumo wa Kiislamu.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Suala hilo inabidi liwe mithili ya fikra pana sana iliyotawala katika masuala yote ya nchi na inabidi tujiimarishe na tusimame imara katika kukabiliana na kambi ya kiistikbari.
Akiendelea na kuchambua suala hilo Ayatullah Udhma Khamenei ameuliza swali akisema: Mapambano haya yataendelea hadi lini?
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amejibu swali hilo kwa kusisitiza kuwa: Mapambano na jihadi si kitu kinachoweza kumalizika kwani shetani na kambi yake ni vitu vilivyopo wakati wote, ingawa inawezekana mbinu na aina za mapambano na jihadi zikatofautiana kulingana na mazingira na nyakati tofauti.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Mapambano hayo yatamalizika wakati jamii ya mwanadamu itakapofanikiwa kujikomboa kutoka katika shari ya kambi ya kibeberu inayoongozwa na Marekani ambayo imeshindilia makucha yake ndani ya mwili na roho na fikra ya mwanadamu na kwamba jambo hilo nalo linahitajia kuweko mapambano magumu, mazito na ya muda mrefu pamoja na wajibu wa kupigwa hatua kubwa za kivitendo katika suala hilo.
Amelitaja suala la kuundwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu nchini Iran kuwa ni hatua kubwa iliyopigwa katika njia ya mapambano hayo na kuongeza kuwa: Kuundwa mabunge ya vipindi tofauti mfululizo katika kipindi cha miaka 35 iliyopita na kushiriki wabunge katika mabunge hayo wakiwa ni dhihirisho la kuimarika demokrasia ya kidini nchini Iran, nako ni aina mojawapo ya mapambano ambayo inabidi tujue thamani yake na tuyaendeleze.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia pia sababu ya kutiliwa mkazo maneno "uongozi wa kijihadi" katika kaulimbiu ya mwaka huu (wa Kiirani wa 1393 Hijria Shamsia) na kuongeza kuwa, uongozi wa kijihadi haumalizikii tu katika masuala ya serikali bali bunge nalo kama litatekeleza kazi zake za kutunga sheria na kuzisimamia kwa lengo moja tu la kuwatumikia wananchi, basi litakuwa limefanya kazi moja kubwa sana ya kijihadi.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Njia pekee ya kuweza kutatua matatizo ya nchi ni kushikamana na uchumi wa kimuqawama na wa kusimama kidete na kuacha kukodolea macho na kuwa na tamaa na msaada kutoka nje ya mipaka ya nchi.
Ameongeza kuwa: Mimi ninawaunga mkono kwa moyo wa dhati na kikweli kweli watu wote wanaofanya jitihada zao katika nyuga tofauti za ubunifu lakini pia ninaamini kuwa, utatuzi wa matatizo yaliyopo umo ndani ya nchi, hauko nje ya mipaka ya nchi yetu.
Amesema: Inabidi kuzielewa njia sahihi za kutatua matatizo yaliyopo na kufuata njia hizo kwa ushujaa na ujasiri ambapo moja ya hatua muhimu katika suala hilo ni kushikamana na uchumi wa kusimama kidete.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu vile vile ameashiria uungaji mkono na kusifiwa kwa maneno uchumi wa kusimama kidete kulikoshuhudiwa katika miezi ya hivi karibuni nchini na kusisitiza kuwa: Kusifia kwa maneno tu hakutoshi katika utekelezaji wa uchumi wa kimuqawama bali inabidi hatua za kivitendo zichukuliwe katika suala hilo.
Ayatullah Udhma Khamenei aidha ameishukuru Serikali na Bunge kutokana na harakati zao za kutekeleza siasa za uchumi wa kusimama kidete akisema: Bunge linapaswa kulipa uzito wa hali ya juu suala la kulindwa hatua zilizochukuliwa hadi hivi sasa katika upande wa kutunga sheria na kusimamia utekelezaji wake.
Amesema, miongoni mwa majukumu makuu ya bunge ni kutunga sheria nzuri na sahihi kwa ajili ya uchumi wa kusimama kidete na kuondoa sheria zinazoleta usumbufu au zile zinazokwamisha mambo pamoja na kusimamia utendaji wa serikali na kuongeza kuwa: Bunge halipaswi kutegemea tu mipango iliyopo katika kutunga sheria zinazohusiana na uchumi wa kusimama kidete, bali serikali nayo inapaswa iwasilishe bungeni miswada mizuri ya kufanikisha uchumi huo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu vile vile ameashiria namna Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu linavyojiandaa kwa ajili ya kutunga mpango wa sita wa miaka mitano wa maendeleo na kusisitiza kuwa, mambo matatu inabidi yapewe kipaumbele kikuu katika mpango huo nayo ni uchumi wa kusimama kidete, utamaduni na elimu.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema kuhusu utamaduni kwamba: Makusudio yetu kuhusu utamaduni, ni utamaduni wa kimapinduzi na kidini na kuleta harakati ya kiutamaduni chini ya misingi ya Uislamu na matukufu ya Kiislamu na kutia nguvu itikadi, ada, desturi na maadili ya Kiislamu katika jamii.
Amesisitiza pia kuwa: Si sahihi kudhani kuwa madhali umejitokeza na kuenea wenzo fulani tu wa kiutamaduni katika jamii basi jamii hiyo imeshapiga hatua za kimaendeleo katika masuala ya utamaduni, hapana, bali maendeleo ya kiutamaduni ya jamii hupatikana pale utamaduni wa kidini na kimapinduzi unapoenea katika jamii hiyo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Ninachokitarajia mimi kutoka kwa wajumbe wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ambao ni walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, ni kuunga mkono na kupigania kuenea utamaduni wa kimapinduzi na Kiislamu katika jamii.
Amma kuhusiana na elimu ambacho ni kipaumbele cha tatu katika kutunga mpango wa sita wa maendeleo, Ayatullah Udhma Khamenei amesema, harakati yenye kasi kubwa ya maendeleo ya kielimu ambayo ilianza nchini miaka 12 iliyopita, haipaswi kuachiwa ipungue kwa hali yoyote ile, bali inabidi jitihada ziongezwe kuhakikisha kasi ya harakati hiyo inaongezeka na kuwa kubwa zaidi.
Amesema, suala la elimu kwa nchi yetu ni muhimu mno na kusisitiza kuwa: Sehemu kubwa ya fakhari za kitaifa, heshima ya kitaifa na utajiri wa taifa hupatikana kupitia elimu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameendelea ya hotuba yake kwa kusema kuwa, jukumu jingine kubwa la Bunge katika usimamiaji, ni kupambana vilivyo na ufisadi na kusisitiza kwamba: Katika suala la kupambana na ufisadi, inabidi kuzingatia kwamba, haipasi - tangu mwanzoni kabisa mwa mapambano hayo - kuruhusu na kutoa mwanya wa kuundika maeneo machafu kwani kama jambo hilo litaruhusiwa, basi imma kupambana na maeneo hayo itakuwa haiwezekani kabisa au kupambana nayo litakuwa ni jambo zito sana.
Ayatullah Udhma Khamenei vile vile amegusia hatua ya kuwasilishwa Siasa Kuu kuhusiana na wajibu wa kuongezwa idadi ya watu nchini na vile vile amesifu mpango wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu wa kuongeza kiwango cha watu kuzaa na kuzuia kupungua idadi ya watu nchini akisema kuwa: Kuhusu suala la idadi ya watu inabidi tuchukuwe tahadhari na kutoruhusu kujirudia makosa ya huko nyuma, kwani hali bora kwa adui, ni kuona Iran ina idadi ndogo ya watu, au ina idadi kubwa ya watu wenye umri mkubwa.
Amesisitiza pia kuwa: Kuna wajibu wa kuwa na mipango mizuri, sahihi, ya kimantiki na ya kiutaalamu kwa ajili ya kufanikisha suala la kuongeza idadi ya watu.
Kabla ya miongozo hiyo ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Dk Ali Larijani, Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (bunge la Iran) ametoa hotuba fupi na sambamba na kutoa mkono wa pole kwa mnasaba wa kukumbuka siku aliyouawa shahidi Imam Musa al Kadhim Alayhis Salaam na vile vile kutoa mkono wa Baraka kwa mnasaba wa maadhimisho ya hamasa ya ukombozi wa mji wa Khorramshahr (wa kusini magharibi mwa Iran) na sikukuu ya kusherehekea siku ya kubaathiwa na kupewa Utume Mtume Muhammad SAW amesema: Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu siku zote ikichukua misimamo imara katika masuala kama Palestina, Syria na kadhia ya nyuklia.
Dk Larijani pia ameashiria namna kulivyotolewa mipango na miswada 450 katika kipindi cha miaka miwili iliyopita ya Bunge la Tano na kuongeza kuwa: Katika miaka miwili iliyopita, kumetungwa sheria 80 kutokana na mipango na miswada iliyowasilishwa bungeni, na ametoa mifano ya sheria hizo.
Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu pia amesema, msimamo na mwelekeo mkuu wa chombo hicho cha kutunga sheria ni kutia nguvu anga za uchapaji kazi na kutafuta rizki za halali, kufuatilia siasa za uchumi wa kusimama kidete na kuimarisha wigo wa usimamiaji unaofanywa na bunge kupitia kamisheni mbali mbali husika au kupitia kuwauliza maswali viongozi wa serikali na kufanya uchumi, utafiti na kupitia kitengo cha udhibiti wa mahesabu.
 
< Nyuma   Mbele >

^