Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Kiongozi Muadhamu Aonana na Mkuu, Wakurugenzi na Watafiti wa Taasisi ya Jihadi ya Vyuo Vikuu Chapa
09/06/2014
Kiongozi Muadhamu Aonana na Mkuu, Wakurugenzi na Watafiti wa Taasisi ya Jihadi ya Vyuo VikuuAyatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, leo asubuhi (Jumatatu) ameonana na mkuu, wakurugenzi, wahakiki na watatifi wa taasisi ya Jihadi ya Vyuo Vikuu na kusisitiza kuwa, jambo la lazima katika kuendelea kwa njia sahihi na kwa kasi kubwa na harakati ya kielimu ya Iran ni kufanya kazi kwa bidii na kuwa na uongozi na usimamiaji wa kijihadi na vile vile kutia nguvu moyo wa "Sisi tunaweza" sambamba na kulinda misimamo na mielekeo ya kimapinduzi na Kiislamu na kuwa na ramani ya kina kuhusiana na hadhi, nafasi na majukumu taasisi hiyo chini ya mwavuli wa ramani kuu wa kielimu ya Iran.
Amesisitiza kuwa: Malengo makuu ya harakati ya kielimu nchini Iran yanapaswa yawe ni kuongeza elimu ya kimataifa kupitia kuzalisha elimu na teknolojia mpya na zisizotambulika za mwanadamu sambamba na kuchunga matukufu ya kibinadamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametumia fursa hiyo pia kutoa mkono wa baraka kwa mnasaba wa maadhimisho ya "Siku ya Kijana" nchini Iran (inayoadhimishwa kwa mnasaba wa maadhimisho ya siku ya kuzaliwa mmoja wa wana watukufu wa Imam Husain AS na mmoja wa mashujaa watukufu wa mapambano ya Karbala yaani Ali Akbar AS).
Kiongozi Muadhamu amesema, moja ya sifa za kipekee kabisa za Jihadi ya Vyuo Vikuu ni kuwa na nguvu kazi ya vijana wasomi na wataalamu ambao wana fikra za kijihadi.
Ameongeza kuwa: Jihadi ya Vyuo Vikuu ni taasisi muhimu sana kwani ina uhusiano na Vyuo Vikuu ikiwa ni ngao kubwa ya kielimu na kituo muhimu cha maendeleo ya kielimu nchini Iran na vile vile inafanya kazi zake kijihadi na haitetereshwi na vizuizi na kero inazokumbana nazo katika harakati zake.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza pia kwamba, kutakasa nafsi, kuwa na imani thabiti ya Mwenyezi Mungu na kutawakali na kumtegemea Mwenyezi Mungu Mtukufu ni miongoni mwa mambo ya lazima katika harakati ya kijihadi na kuongeza kwamba: Kuwa na tafakuri na moyo wa namna hiyo katika kazi za kielimu, husababisha kupatikana msaada wa Mwenyezi Mungu na kufunguka njia za kuelekea kwenye maendeleo ya kielimu.
Hapo hapo ameashiria shubha na suala moja lenye utata akisema: Inawezekana baadhi ya watu wakajiuliza swali kwamba kama kuwa na taqwa kwa Mwenyezi Mungu huandaa mazingira ya kupatikana maendeleo ya kielimu, sasa ni vipi tunaona kwamba baadhi ya wasomi na wataalamu hawana taqwa bali wengine hata hawamwamini kabisa Mwenyezi Mungu lakini pamoja na hayo wameweza kupata maendeleo ya kielimu?
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amejibu swali hilo kwa kuashiria ahadi za Mwenyezi Mungu zilizomo ndani ya Qur'ani Tukufu za kwamba mtu yeyote anayefanya jitihada na kufanya kazi kwa bidii atapata matunda yake na atafanikisha shabaha na malengo ya juhudi zake na kuongeza kwa kusema: Lakini ubora na aina ya matunda na maendeleo yanayopatikana kupitia kazi na jihadi zilizo na imani ya Mwenyezi Mungu unatofautiana sana na aina ya matunda na maendeleo yanayopatikana kupitia njia zisizo na imani ya Mwenyezi Mungu ndani yake.
Ayatullah Udhma Khamenei ametoa ufafanuzi zaidi kuhusiana na tofauti hiyo akisema: Leo hii ni licha ya kuweko maendeleo makubwa ya kielimu duniani katika sekta na nyuga tofauti, lakini kuna pia hatari nyingi, madhara mengi na maporomoko makubwa ya kimaadili na vita vya madaraka ambavyo vinahatarisha sana usalama wa duniani na wa mwanadamu na kwamba madhara hayo makubwa yamemsababishia matatizo na mateso makubwa mwanadamu.
Ameongeza kuwa: Kama jitihada na harakati za kielimu zitafanyika chini ya kalibu na mwavuli wa kumuogopa Mwenyezi Mungu, bila ya shaka yoyote matunda yake yatakuwa ni kumwepushia mbali madhara mwanadamu na kumletea faida na manufaa makubwa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Ni kwa kuwa na mtazamo huo ndipo tutakapoona kuwa, mafanikio iliyoyapata majimui ya Vyuo Vikuu na taasisi za utafiti nchini Iran katika kipindi cha miaka 35 iliyopita bila ya shaka yoyote ni makubwa zaidi na ni bora zaidi ikilinganishwa na yale yaliyopatikana bila ya kuwa na moyo wa kijihadi.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Ni kwa sababu hiyo ndio maana kama harakati hii ya kielimu itaendelea kwa miaka 150 mingine, maendeleo na mafanikio ya kielimu ya taifa la Iran yatakuwa makubwa zaidi ikilinganishwa na yale ya harakati za kielimu za nchi kama vile Marekani za kipindi cha miaka 150 iliyopita.
Vile vile ameashiria namna ulimwengu wa Magharibi unavyozidi kuziacha mbali kielimu nchi za Mashariki na za Asia na kusisisitiza kuwa, harakati ya kijihadi inahitajika kuweza kujaza pengo hilo kubwa la kielimu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameitaja nia yenye ikhlasi, mfungamano wa karibu na Mwenyezi Mungu, unyenyekevu mbele ya Allah na kutojitenga na malengo matukufu ya Mwenyezi Mungu kuwa ni misingi mikuu ya harakati na uongozi wa kijihadi na kuongeza kwamba: Iwapo moyo huo utakuwepo, basi Mwenyezi Mungu atatoa msaada Wake katika medani zote iwe za uongozi wa nchi, uendeshaji wa masuala ya kielimu, kisiasa, kijamii au miamala ya kimataifa na atawafungulia njia waja Wake wema.
Ayatullah Udhma Khamenei amelitaja suala la kutia nguvu moyo wa kujiamini na wa "sisi tunaweza" kuwa ni moja ya mambo ya dharura katika harakati ya kijihadi na kuongeza kuwa: Inasikitisha kuona kwamba kulifanyika njama za miaka mingi za kuwalazimisha Wairani waamini kuwa hawawezi kufanya chochote lakini baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Imam mtukufu (Imam Khomeini - quddisa sirruh) aliingiza moyo wa "sisi tunaweza" katika msamiati wa kisiasa na kimapinduzi wa Iran na matokeo yake ni kuwa nguvu za taifa la Iran sasa zinaonekana katika nyuga tofauti.
Amesisitiza kuwa: Pamoja na kupulizwa roho na moyo wa kujiamini kwa taifa la Iran katika miaka ya baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, lakini pamoja na hayo bado mzizi wa utamaduni ghalati na pofotu wa "sisi hatuwezi" haujang'olewa kikamilifu na inasikitisha kuona kuwa kuna baadhi ya watu katika medani tofauti wanawakodolea macho ya tamaa watu baki wakitarajia kuwa watawasaidia kupata maendeleo ya kielimu, kisiasa, kijeshi pamoja na masuala ya kimaada na kidunia.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekumbushia pia nukta nyingine hapo akisema: Kaulimbiu ya "Sisi tunaweza" haina maana ya kukana na kukataa kujifunza elimu na maarifa kutoka kwa wengine na kutoka kwa watu waliopiga hatua kubwa kielimu, hapana, bali maana yake ni kuzingatia na kutilia maanani kwamba kinachotakiwa ni kujifunza elimu na sio kuchukua elimu pamoja na mambo maovu na misimamo ghalati ya pande zenye elimu hiyo.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kuwa: Katika kadhia ya maendeleo ya kielimu, jambo la wajibu ambalo linaangaliwa kwa jicho la lengo na shabaha kuu ni kuongeza kitu katika elimu kimataifa na kuzalisha teknolojia mpya na kuziingiza elimu na maarifa ya wanadamu.
Amesema: Sisi leo hii kupitia maendeleo ya kielimu yaliyopo nchini, tunaweza kuzalisha teknolojia tata na za kisasa kabisa duniani jambo ambalo kwa kweli ni kitu cha kujivunia kabisa. Hata hivyo teknolojia hizo ni zile ambazo tayari zimeshavumbuliwa na wataalamu wa nchi nyinginezo; hivyo tunachotakiwa kufanya ni kuzalisha elimu na teknolojia mpya ambazo hadi hivi sasa hakuna mwanadamu yeyote aliyeweza kuzizalisha na kuwa nazo, teknolojia ambazo hazitakuwa na madhara kwa mwanadamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu hapo hapo pia amezungumzia teknolojia ya nyuklia ikiwa ni moja ya maendeleo muhimu na tata ya kielimu ya mwanadamu na kusema: Teknolojia hiyo licha ya kwamba ina umuhimu mkubwa, lakini pia imeandaa mazingira ya kutenengezwa silaha angamizi na haribifu sana za atomiki ambazo ni dhidi ya mwanadamu mia kwa mia na zina madhara makubwa sana kwa dunia.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Katika jitihada zetu za kujiimarisha kielimu, tunapaswa tutafute na tuvumbue elimu zisizojulikana kabisa ambazo zitakuwa na manufaa kwa maisha ya mwanadamu na ambazo zitanyanyua thamani za mwanadamu na wakati huo huo hazitakuwa na madhara wala uharibifu kwa kiumbe huyo.
Akiendelea na hotuba yake, Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria kuundika na kuanza kufanya kazi Jihadi ya Vyuo Vikuu nchini Iran kwa tafakuri ya kimapinduzi na kuongeza kuwa: Inabidi msimamo na njia ya kimapinduzi ya Jihadi ya Vyuo Vikuu ilindwe na kuhifadhiwa na haipasi kuruhusu kituo hicho muhimu cha kielimu kikumbwe na matatizo yatokanayo na songombingo za kisiasa na misimamo ghalati ya kulia na kushoto ya wanasiasa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametaja moja ya madhara ya songombingo zinazoshuhudiwa katika nyuga za kisiasa kuwa ni kubadilika badilika kama kinyonga baadhi ya wanasiasa na kuongeza kwamba: Kuna baadhi ya watu wakati fulani walikuwa na misimamo na misukumo mikubwa sana ya kimapinduzi, lakini hivi sasa wamebadilika kwa daraja 180 kiasi kwamba wanajifanya kutoelewa hata masuala ya wazi kabisa ya Mapinduzi ya Kiislamu. Hivyo kuna wajibu wa kuchukua tahadhari, yasije mambo kama hayo yakaingia katika taasisi ya Jihadi ya Vyuo Vikuu.
Ayatullah Udhma Khamenei amewataka viongozi wa taasisi ya Jihadi ya Vyuo Vikuu kuwatumia vizuri vijana wanamapinduzi na kukiimarisha na kukitia nguvu kizazi cha vijana wanamapinduzi katika Vyuo Vikuu kupitia harakati ya kielimu akisisitiza kuwa: Mfano mmoja wa watu waumini, wanamapinduzi na ambaye ametoa mchango mkubwa wa kielimu nchini Iran ni marhum Dk Kazemi ambaye kwa imani na ikhlasi yake alileta maendeleo na mabadiliko makubwa katika taasisi ya Royan na kulea na kusomesha wasomi wakubwa sana.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia amesisitizia wajibu wa kutungwa na kubuniwa malengo ya muda mfupi na muda mrefu ya taasisi ya Jihadi ya Vyuo Vikuu kwa kuzingatia nafasi na majukumu ya taasisi hiyo katika ramani kuu ya kielimu ya Iran na kuongeza kuwa: Viongozi na maafisa wa taasisi ya Jihadi ya Vyuo Vikuu wanapaswa kufanya kazi ya kimsingi ya kielimu na kutoa maana sahihi ya namna ya kuamiliana na Vyuo Vikuu tofauti na kusimamia na kuongoza vizuri muamala huo ili kupitia lengo na shabaha moja kuu na ya kina iweze kujichorea vyumba vyake maalumu katika jedwali kuu la ramani ya kielimu nchini Iran.
Mwishoni mwa hotuba yake, Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kuwa: Taasisi ya Jihadi ya Vyuo Vikuu inapaswa kujiepusha na kazi ndogo ndogo na kujihusisha na kazi kubwa kubwa, za kimsingi na zenye taathira pana na za kudumu.
Mwanzoni mwa mkutano huo, Dk Hamid Reza Tayebi, Mkuu wa Taasisi ya Jihadi ya Vyuo Vikuu ya Iran ametoa ripoti fupi ambayo ndani yake mlikuwa na ufafanuzi kuhusu shabaha, malengo ya muda mrefu na mfupi na mipango ya baadaye ya taasisi hiyo na kusema: Kwa msaada wa ngao ya kimaanawi, kidini, rasilimali ya binadamu na nguvukazi zetu za kijihadi, tumeweza kupata moyo na azma ya kweli ya kulinda fikra za Mapinduzi ya Kiislamu na kuingiza katika medani ya Vyuo Vikuu utamaduni wa kufanya jitihada kimapinduzi.
Amesema kwamba; kuwa na moyo wa kuamini uwezo na nguvu za ndani na kuimarisha vipaji na ubunifu pamoja na kulinda sifa za ndani ya taifa, kutunga na kubuni miundo ya kielimu na kiutafiti, kuleta anga ya kazi kwa ajili ya wanafunzi wa Vyuo Vikuu, kuunda na kubuni vifaa na mifumo muhimu ya kiviwanda, kupata teknolojia ya seli shina, kutia nguvu moyo wa kujiamini ndani ya nyoyo za watu wanaofanya utafiti, kutunga mpango wa tano wa Jihadi ya Vyuo Vikuu unaokubaliana na uchumi wa kimuqawama na kusimama kidete na kuanzisha mashirika ya elimu msingi; ni miongoni mwa mipango na ratiba za taasisi ya Jihadi ya Vyuo Vikuu ya Iran na kusema kuwa, taasisi hiyo ya kimapinduzi iko tayari wakati wote kutoa mchango wake mpya wa kitaifa wakati wowote itakapotakiwa kufanya hivyo.
 
< Nyuma   Mbele >

^