Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Kiongozi Muadhamu Aonana na Mkuu na Maafisa wa Ngazi za Juu wa Chombo cha Mahakama Chapa
22/06/2014
Supreme Leader Meets with Judiciary OfficialsAyatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, leo asubuhi (Jumapili) ameonana na mkuu na maafisa wa ngazi za juu wa Chombo cha Mahakama na vile vile viongozi wakuu wa mahakama na idara za sheria za makao makuu ya mikoa ya Iran.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amebainisha vipaumbele sita vikuu vya kipindi kipya cha miaka mitano cha uongozi wa Ayatullah Amoli Larijani katika Chombo cha Mahakama cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusema kuwa, ushirikiano, kupendana na kuwa na sauti moja wakuu wa Mihimili Mitatu Mikuu ya dola (Mahakama, Serikali na Bunge) katika masuala makuu ya nchi na katika kulinda maslahi ya umma ni jambo la dharura sana.
Vile vile ameashiria matukio ya hivi sasa ya Iraq na kusisitiza kuwa, nyuma ya pazia la fitna na mauaji yanayofanyika Iraq sasa hivi, kuna madola ya kibeberu ya Magharibi yakiongozwa na utawala wa Marekani na kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sambamba na kupinga vikali uingiliaji wa aina yoyote ile wa Marekani katika masuala ya ndani ya Iraq, inaamini kuwa, wananchi na serikali ya Iraq pamoja na maraji'i wa kidini wa nchi hiyo wanaweza kwa pamoja kukomesha mauaji na kuzima moto uliowashwa nchini humo.
Katika mkutano huo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewaenzi na kuwakumbuka kwa wema mashahidi wa Tir 7 (1360 Hijria Shamsia sawa na Juni 28, 1981 wakati genge la wanafiki la MKO lilipofanya shambulio la bomu katika Makao Makuu ya chama cha Jamhuri ya Kiislamu mjini Tehran na kupelekea kuuawa shahidi Ayatullah Beheshti na wafuasi 72 wa Mapinduzi ya Kiislamu) na hususan shahid Ayatullah Beheshti kama ambavyo pia amemuenzi shahid Ayatullah Quddusi.
Aidha ameitaja sifa ya kipekee ya Chombo cha Mahakama ikilinganishwa na vyombo vingine kuwa ni kudhamini kwake ufanikishaji wa kusimamishwa haki na uadilifu katika taasisi zote za mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu.
Ameongeza kuwa: Ni kwa sababu hiyo ndio maana matarajio yaliyopo kwa Chombo cha Mahakama yakawa makubwa na kwamba kwa kuzingatia uwezo na ustahiki mkubwa wa mkuu wa chombo hicho ambaye ni mwanachuoni mkubwa, mujtahidi, aliyeshikamana vilivyo na dini, mwenye fikra pana, mwanamapinduzi, shujaa na mweledi wa mambo, kunaufanya uwezekano wa kufanikishwa matumaini ya kufikiwa malengo yaliyokusudiwa uwe mkubwa sana.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu vile vile amemshukuru mkuu wa Chombo cha Mahakama cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na maafisa wa ngazi za juu wa chombo hicho kwa juhudi zao kubwa za kufanikisha malengo yaliyokusudiwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita na kubainisha vipaumbe sita vya chombo hicho katika kipindi kipya cha miaka mitano ijayo.
Kuwa na ratiba na mipangilio maalumu na iliyo wazi kwa ajili ya kutekeleza sera na siasa za chomo hicho, ni kipaumbele cha kwanza kilichoashiriwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi katika mkutano huo.
Amesema: Inabidi iweko mipangilio na ratiba maalumu na za wazi kwa ajili ya kusimamia utekelezaji wa siasa zinazohusiana na Chombo cha Mahakama na kuzifanya sera hizo zote kuwa ratiba zinazotekelezeka kivitendo.
Ayatullah Udhma Khamenei ametaja kipaumbele cha pili kikuu cha Chombo cha Mahakama kuwa ni kuweko usimamiaji wa utendaji wa kazi zote iwe za majaji na pia za viongozi na wakuu wa chombo hicho.
Amesisitiza kuwa: Usimamiaji huo ni lazima upewe uzito wa hali ya juu na uwe mpana kiasi kwamba uweze kukifanya kiwango cha matatizo na malalamiko kuhusiana na utendaji wa maafisa wa chombo hicho kuwa cha chini kabisa kadiri inavyowezekana.
Vile vile amelitaja suala la kutocheleweshwa utekelezaji wa hukumu zinazotolewa kuwa ni kipaumbele cha tatu cha Chombo cha Mahakama cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Ameongeza kuwa: Baadhi ya ucheleweshaji wa muda mrefu wa utekelezaji wa hukumu zinazotolewa na mahakama unatokana na baadhi ya mapungufu yaliyopo hivyo inabidi mapungufu hayo yatafutwe na yaondolewe.
Kuhusiana na uakhirishaji wa uchunguzi na upelelezi wa kesi, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekumbushia nukta moja muhimu akisema: Kupunguza kiwango cha wastani cha muda wa uchunguzi na upelelezi ni jambo zuri lakini vile vile inabidi kuzingatia ni kesi na mafaili mangapi katika kipindi cha muda wa juu kabisa uliotengwa kwa kazi hiyo, yanafanyiwa uchunguzi, na kama wastani wa muda wa kiwango hicho uko juu, basi upunguzwe.
Kuandaa wafanyakazi na kukabidhiana nyadhifa ni kipaumbele cha nne alichokiashiria Ayatullah Udhma Khamenei katika mkutano huo.
Kipaumbele cha tano amekitaja kuwa ni kuzuia kutokea uhalifu.
Amesema kuhusu kipaumbele hicho kwamba: Kuzuia kutokea uhalifu ni suala ambalo halikihusu tu Chombo cha Mahakama, hivyo katika kuzuia kutokea uhalifu, chombo hicho kina wajibu wa kuwa na uhusiano na ushirikiano mkubwa na wa karibu na vyombo vingine husika, na kuimarisha mambo yanayovikutanisha vyombo hivyo katika masuala hayo.
Amesema: Kuzuia kutokea uhalifu ni suala ambalo pia ni la kielimu kikamilifu na ndio maana inabidi kushirikiana na wasomi, wataalamu na wanafikra wa masuala hayo katika kutambua sababu za kutokea uhalifu na madhara yake.
Kipaumbele cha sita na cha mwisho kilichobainishwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika mkutano huo ni kuongezwa kiwango cha ushirikiano baina ya mihimili mitatu mikuu ya dola (Serikali, Bunge na Mahakama).
Ayatullah Udhma Khamenei amesema: Jambo ambalo nimekuwa nikilisisitizia wakati wote ni kwa wakuu wa Mihimili Mitatu Mikuu ya dola ni kuongeza ushirikiano baina yao na kwamba ushirikiano huo unahusu pande mbili, unahusiana na masuala ya ndani ya chombo husika na masuala makuu ya nchi yanayoviunganisha vyombo na taasisi zote.
Amesisitiza kuwa: Kiujumla ni kwamba, mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu unataka kusikia kauli moja kutoka kwa wakuu wa mihimili mikuu ya dola katika masuala tofauti ya nchi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia misimamo muhimu mno, makini sana, iliyojengeka kihoja na ya kimantiki ya Ayatullah Amoli Larijani (Mkuu wa Chombo cha Mahakama cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran) katika masuala tofauti na kusema kuwa: Kushirikiana na kuwa na fikra za pamoja wakuu wa Mihimili Mitatu Mikuu ya dola inaweza kuisaidia serikali katika kazi zake kama misimamo hiyo itaenea na kushuhudiwa kwenye sekta na kada tofauti.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza pia kuwa masuala ya kitaifa ya nchi ni muhimu zaidi kuliko masuala mengine yote na kuongeza kuwa: Wakuu wa Mihimili Mitatu Mikuu ya dola wanapaswa kuongeza vikao vyao vya pamoja kwani kukutana kwao huko kunatoa msaada mkubwa katika utatuzi wa matatizo mbali mbali na kunaleta maendeleo katika mambo tofauti na husaidia kuondoka malalamiko yanayojitokeza.
Amma kuhusiana na masuala muhimu ya nchi amesisitiza kuwa: Matatizo yaliyopo nchini na hata yale ambayo baadhi ya watu wanadhani kuwa nayo ni matatizo ijapokuwa si matatizo, yote yanaweza kupatiwa ufumbuzi kwa sharti kwamba tuweze kujitegemea wenyewe na kutumia uwezo wetu wa ndani kuyatatua.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Moja ya changamoto kubwa za nchi yetu ni uadui na upinzani mkubwa wa madola ya kibeberu ya Magharibi kwa mfumo wetu wa Kiislamu na inabidi uhakika huo ueleweke na utambuliwe vyema.
Ameongeza kuwa kusema: Kama tutashindwa kuuzingatia uadui wa madola ya kibeberu dhidi ya nchi yetu, basi tutafanya makosa katika kuchanganua masuala ya taifa letu.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Watu ambao hawako tayari kuuona uadui wa kambi ya adui dhidi ya nchi yetu, ndio wale wale watu ambao wameelekeza matumaini yao kwa adui.
Amesema, sababu kuu inayowafanya mabeberu waifanyie uadui Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni aidiolojia mpya iliyoletwa na mfumo wa utawala wa Kiislamu na kuyumba misingi ya mfumo wa kibeberu.
Vile vile ameashiria matukio ya hivi sasa ya nchini Iraq na kusema kuwa: Katika kadhia ya Iraq, madola ya kibeberu ya Magharibi na hasa hasa utawala wa Marekani, yamekusudia kutumia vibaya ujinga na taasubu za baadhi ya watu kwa manufaa yao.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Lengo kuu katika masuala ya hivi sasa ya Iraq ni kuwanyima wananchi wa nchi hiyo matunda ya mfumo wao wa utawala wa kidemokrasia waliojiamulia wenyewe licha ya Marekani kuingilia masuala yao ya ndani.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza pia kuwa: Marekani haifurahishwi na hali ya mambo ilivyo hivi sasa nchini Iraq yaani kufanyika uchaguzi na kushiriki vizuri wananchi ndani yake ambao wametumia haki yao ya kidemorasia kuchagua viongozi wanaowapenda kwani inachotaka Marekani ni kuona Iraq inatawaliwa na watawala vibaraka ambao watakuwa wanatii tu amri zitokazo Marekani.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria pia matamshi ya viongozi wa Marekani wanaofanya njama za kuyaonesha matukio ya Iraq kuwa ni vita vya kimadhehebu baina ya Waislamu wa Kisunni na Kishia na kuongeza kuwa: Kinachotokea nchini Iraq hivi sasa si vita baina ya Mashia na Masunni bali madola ya kibeberu yanatumia mabaki ya utawala uliopita wa Saddam kama silaha yao kuu na yanayatumia makundi ya kitakfiri kama askari wa kutembea kwa miguu kufanya njama za kuvuruga utulivu na maelewano nchini Iraq na kuhatarisha umoja wa ardhi ya nchi hiyo.
Ameongeza kuwa: Wahusika wakuu wa fitna inayoendelea nchini Iraq hivi sasa wanawafanyia Waislamu wa Kisunni wenye imani thabiti na wanaopigania ukombozi wa kweli wa Iraq, uadui ule ule wanaowafanyia Waislamu wa Kishia.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza pia kuwa, ugomvi mkubwa ulioko Iraq hivi sasa ni baina ya watu wanaotaka Iraq iingie kwenye kambi ya Marekani na watu ambao wanataka uhuru kamili wa nchi yao bila ya kuwepo uingiliaji wa aina yoyote ile wa Marekani.
Ayatullah Udhma Khamenei pia amesisitiza kwamba Wairaq wenyewe wanao uwezo wa kuuzima moto uliowashwa nchini mwao na kuongeza kuwa: Sisi tunapinga vikali uingiliaji wa Wamarekani na madola mengine katika masuala ya ndani ya Iraq na kamwe hatuwezi kuunga mkono jambo hilo kwani tunaamini kuwa serikali na taifa la Iraq na maraji'i wa kidini wa nchi hiyo wanao uwezo wa kukomesha fitna hiyo na Inshaallah fitna hiyo itaisha kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu.
Mwanzoni mwa mkutano huo, Ayatullah Amoli Larijani, Mkuu wa Chombo cha Mahakama cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa ripoti fupi kuhusu kazi za chombo hicho katika kipindi cha miaka mitano iliyopita na kusema kuwa: Kuongeza kiidadi na kiubora nguvu kazi, kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wa chombo hicho kabla kuajiriwa, wakati wa kuajiriwa na baada ya kuajiriwa, kupandisha kiwango cha kielimu ndani ya chombo hicho kupitia kuanzisha vituo viwili vya utafiti wa kiutaalamu katika miji ya Qum na Tehran, kuimarisha njia na namna ya usimamiaji wa utendaji wa wafanyakazi wa chombo hicho wakiwemo majaji, wafanyakazi wa Mahakama Kuu na kitengo cha kuhifadhi na kukusanya taarifa cha Chombo cha Mahakama, kutumia teknolojia mpya na kuongeza huduma za kielektroniki, kurekebisha miundo na taasisi pamoja na kubuni miswada muhimu kuhusiana na kazi zinazohitajika katika masuala ya mahakama, kama vile muswada wa polisi wa mahakama na muswada mkuu wa uwakili, ni miongoni mwa hatua muhimu zilizochukuliwa na chombo hicho katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Ayatullah Amoli Larijani vile vile amesema kuhusu kupunguza muda wa uchunguzi na kufuatilia kesi kuwa, wastani wa kufuatilia kesi nchini Iran unakubalika kulingana na hali ilivyo katika nchi nyingine duniani.
Aidha amesisitizia udharura wa kushirikiana vizuri Mihimili Mitatu Mikuu ya dola na kuongeza kuwa: tunajitahidi kuhakikisha kuwa Chombo cha Mahakama cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kinashirikiana vizuri na mihimili mingine ya dola yaani Serikali na Bunge sambamba na kulinda uhuru wake.
 
< Nyuma   Mbele >

^