Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Kiongozi Muadhamu Aonana na Familia za Mashahidi wa Tir Saba na Familia za Mashahidi wa Tehran Chapa
28/06/2014
Supreme Leader Meets with Families of Martyrs of the 7th of TirAyatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu leo asubuhi (Jumamosi) ameonana na familia za mashahidi wa Tir 7 (Juni 28) na familia kadhaa za mashahidi na majeruhi wa vita wa mji wa Tehran na huku akisisitizia haja kubwa ya Iran ya kuelewa na kutekeleza kivitendo risala na ujumbe wa mashahidi, amelitaja suala la taifa la Iran kuwendeleza njia iliyojaa nuru na matukufu mengi ya mashahidi kuwa linaanda uwanja wa kuendelea kuzishinda njama za mabeberu. Vile vile ameashiria matukio mbali mbali ya eneo la Mashariki ya Kati kama vile Iraq na kuongeza kuwa: Kile kinachoendelea hivi sasa nchini Iraq ni vita baina ya magaidi na vibaraka wa nchi za Magharibi kwa upande mmoja na wapigania uhuru na ukombozi wa mataifa ya dunia kwa upande wa pili.
Mwanzoni mwa hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria kukaribia mwezi mtukufu uliojaa baraka wa Ramadhani na kusema kuwa mwezi huu adhimu ni mwezi wa kumzingatia Mwenyezi Mungu kwa ikhlasi, na kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu kwa unyofu, shauku na dhati ya nafsi. Aidha amewataka wananchi kuitumia vizuri fursa ya mwezi mtukufu wa Ramadhani kuomba taufiki, rehema na maghufira ya Mwenyezi Mungu.
Pia ameitaja Tir 7, 1360 (Hijria Shamsia sawa na Juni 28, 1981 siku genge la wanafiki la MKO lilipofanya shambulio la bomu katika Makao Makuu ya chama cha Jamhuri ya Kiislamu mjini Tehran na kupelekea kuuawa shahidi Ayatullah Beheshti na wafuasi 72 wa Mapinduzi ya Kiislamu) kuwa ni siku ya kihistoria isiyosahaulika na kuongeza kuwa: Mashahidi hawana haja kwetu sisi lakini sisi tunahitajia mno risala na ujumbe wao wa kila aina kama ambavyo tunahitajia sana kuelewa malengo yao na kufuata njia yao iliyojaa saada na ufanisi.
Ayatullah Udhma Khamenei ametoa ushahidi ndani ya Qur'ani Tukufu kwa kunukuu aya za Kitabu hicho Kitakatifu zinazowabashiria mashahidi wa jamii ya Kiislamu kwamba watakuwa mbali na hofu, huzuni na majuto na kuongeza kuwa, tunapaswa kuuelewa vizuri ujumbe huo na kuongeza jitihada zetu za kuendeelea na njia iliyojaa nuru ya kufanikisha malengo ya Mapinduzi ya Kiislamu kwa shahuku, unyofu na hamasa kubwa.
Vile vile amezishukuru na kuzisifu familia za mashahidi na za majeruhi wa vita kutokana na kuwa pamoja na jamaa zao hao kwa subira na kuona fakhari kuwa katika familia hizo akilitaja tukio la Tir 7 (Juni 28) lililopelekea kuuawa shahidi makumi ya wafuasi wa Imam Khomeini (quddisa sirruh) na wafuasi wa Mapinduzi ya Kiislamu wakiongozwa na shahksia mkubwa wa kifikra, kielimu, kisiasa na kidini yaani Ayatullah Beheshti kuwa ni tukio linalopaswa kufanyiwa utafiti wa kina na kutathmini miamala ya taifa la Iran kwa upande mmoja na miamala ya maadui wa taifa hilo kwa upande wa pili.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Tunapoifanyia utafiti wa kina na kutaamali kuhusu jinai kubwa ya Tir Saba (Juni 28) tutaona kuwa, kambi ya dhulma duniani ambayo ilihisi kuwa dhaifu na kushindwa mbele ya mantiki ya Jamhuri ya Kiislamu na tafakuri na ustaarabu wa taifa la Iran iliamua kutumia vibaraka wake kufanya jinai hiyo kubwa na pia kuwaunga mkono vibaraka wao hao waliowaua kigaidi karibu viongozi na wananchi 17 elfu wa nchi hii katika matukio tofauti ya kigaidi.
Ayatullah Udhma Khamenei ameitaja tarehe 7 Tir kwamba lilikuwa ni tukio jingine lililowafedhehesha kikamilifu wale wanaodai kutetea haki za binadamu duniani na kuongeza kwamba: Waliofanya jinai hizo na wale wote waliofanya mauaji ya kigaidi dhidi ya maelfu ya Wairani wanakumbatiwa na madola ya Magharibi tangu wakati huo hadi hivi sasa kiasi kwamba hadi leo hii mabunge na taasisi za kiserikali za Marekani na za nchi za Magharibi zinawakaribisha magaidi hao.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Wakati madola ya Magharibi yakijinadi kuwa ni watetezi wakuu wa haki za binadamu na wakati huo huo yakiwakumbatia na kuwapa hifhadhi ya kila namna waliofanya mauaji ya kigaidi na mashambulio ya umwagaji wa damu dhidi ya Wairani; madola hayo yanapata uthubutu wa kujitokeza hadharani na kuituhumu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa inaunga mkono ugaidi wakati yenyewe ni muhanga mkubwa wa vitendo vya kigaidi na kwa hakika hicho ni kielelezo kizuri cha kuitathmini na kuitambua vizuri misimamo ya Wamagharibi na madai yao.
Ayatullah Udhma Khamenei vile vile ameashiria namna utawala wa Saddam (utawala wa zamani wa Iraq) ulivyowashambulia kwa silaha za kemikali wananchi tarehe 7 Tir 1366 (Hijria Shamsia sawa na Juni 28, 1987 Milaadia) na kuongeza kuwa: Licha ya utawala wa Baath (wa wakati huo wa nchini Iraq) kuwashambulia kwa silaha (zilizopigwa marufuku) za kemikali wananchi wa Sardasht na wananchi wa Halabcheh, lakini Marekani na nchi za Ulaya ziliendelea kuusaidia kwa kila namna utawala huo kwa miaka mingi na waliendelea kuunga mkono kadiri walivyoweza vitendo vya Saddam hadi pale walipokuwa hawana haja naye tena. Hadi wakati yalipokuwa na haja na Saddam, madola hayo hayakupinga kitendo chake chochote kile ambapo hiki nacho ni kielelezo kingine kinachobainisha uhakika wa madai ya Wamagharibi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelipongeza taifa la Iran kwa kusimama imara mbele ya maadui na kuongeza kuwa: Taifa hili limeshinda katika vita vyake vya kupambana na maadui kwa kuwa na msimamo imara, kukubali kutoa gharama na kutumia mantiki katika mambo yake kiasi kwamba kila mtu anayetumia akili na mantiki leo hii duniani anaihesabu Jamhuri ya Kiislamu na taifa la Iran kuwa limedhulumiwa lakini wakati huo huo liko imara, liko huru na linazidi kupiga hatua mbele za kimaendeleo. Amesema, njia hiyo inazidi kupiga hatua mbele na kwa kasi kubwa kwa baraka za msaada wa Mwenyezi Mungu na kwa baraka za kushikamana wananchi wa Iran na njia ya mashahidi.
Aidha amekutaja kufeli mara kwa mara njama za maadui wa taifa la Iran katika kipindi hiki cha miongo mitatu iliyopita kuwa kumepelekea kuongezeka zaidi na zaidi chuki za maadui hao kwa taifa hili na kuongeza kuwa: Mabeberu na waistikbari wa dunia ambao wanamchukia mno Imam Khomeini (quddisa sirruh) na Mapinduzi ya Kiislamu na taifa la Iran, kamwe hawawezi kuachana na hila na njama zao na ni kwa sababu hiyo ndio maana taifa na viongozi wa Iran wanapaswa kuwa macho sana.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu vile vile ameashiria matukio yanayoendelea hivi sasa katika eneo la Mashariki ya Kati na kusisitiza kuwa: Maadui wa Uislamu leo hii wamewekeza sana kwenye kuzusha vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya mataifa ya Waislamu ili kuwagombanisha wananchi wa mataifa hayo kwa kutumia fitna za kikaumu, kikabila na kimadhehebu.
Ayatullah Udhma Khamenei amezitaja propaganda zinazofanywa na mabeberu kuhusiana na matukio ya Iraq na ya baadhi ya nchi za eneo la Mashariki ya Kati kwamba zinaonesha kuwa maadui hao wana matumaini makubwa ya kufanikisha njama zao kupitia kuzusha vita baina ya Waislamu ya Kishia na Kisunni na kuongeza kuwa: Huko nchini Iraq mabaki ya utawala wa Saddam na vibaraka wa Magharibi wanashirikiana na watu waliokumbwa na mghafala, majahili na walio mbali na welewa na umaanawi; kufanya jinai dhidi ya watu wasio na hatia; huku maadui wa Uislamu wakitumia fursa hiyo kuwatangazia walimwengu kuwa hivyo ni vita baina ya Waislamu wa Kishia na Kisunni lakini hiyo ni ndoto tu ya Wamagharibi.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Maadui wa Uislamu wanaeneza propaganda za uongo kuwa matukio ya Iraq ni vita baina ya Waislamu wa Kishia na Kisunni wakati uhakika wa mambo ni kuwa hivyo ni vita baina ya magaidi na wapinzani wa ugaidi, ni vita baina ya vibaraka wanaopigania kufanikisha malengo ya Marekani na Magharibi huko Iraq na baina ya wapigania ukombozi wa mataifa ya dunia na hivyo ni vita baina ya utu na ubinaadamu kwa upande mmoja na unyama na uhayawani kwa upande wa pili.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia njama za maadui wa Uislamu za kujaribu kuyafanya matukio ya Iraq yatokee pia katika nchi nyingine za Waislamu na kusisitiza kuwa: Wananchi wa mataifa ya Kiislamu wanapaswa kuwa macho, wana wajibu wa kuuangalia kwa kina uchochezi huu wa maadui na watambue kuwa adui hasiti kufanya jambo lolote lile ambalo litapelekea kutoweka uhuru na heshima ya Waislamu.
Ayatullah Udhma Khamenei ameitaja sababu kuu inayoifanya kambi ya kiistikbari na ya kibeberu kuamua kuanzisha njama hiyo ya kutaka kuzusha vita baina ya Waislamu wa Kishia na Kisunni kuwa ni kujaribu maadui hao wa Uislamu kujipapatua kutoka katika hofu ya mwamko wa Kiislamu na harakati za ukombozi katika ulimwengu wa Kiislamu.
Amesema miongoni mwa njama kubwa zinazotumiwa na mabeberu hao kuhusu jambo hilo ni kupambana na mfumo wa demokrasia ya kidini ambao ni nakala isiyo na mbadala inayoweza kutatua matatizo yaliyopo hivi sasa.
Ameongeza kuwa: Taifa azizi na shujaa la Iran kwa taufiki ya Mwenyezi Mungu, hadi hivi sasa limeweza kulinda vizuri umoja wake, kuwa kwake macho na kuwa kwake na muono wa mbali na hivyo kufanikiwa kuzishinda njama zote za maadui.
Amesema, katika siku za usoni pia taifa hili litabatilisha njama na mashambulizi yote ya kambi ya mabeberu ambayo bila ya shaka yoyote hatimaye itashindwa tu katika kukabiliana na mwamko wa Kiislamu.
Mwishoni mwa hotuba yake, Ayatullah Udhma Khamenei amewausia wananchi wa matabaka yote, wasomi, watu wenye vipaji, watu wa sanaa, waandishi, wanafikra na wanafunzi wa Vyuo Vikuu kulinda na kuuhifadhi vizuri urithi wenye thamani kubwa wa mashahidi waliojaa fakhari wa Mapinduzi ya Kiislamu na kutekeleza vizuri majukumu yao mbele ya adhama ya mashahidi hao.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Hujjatul Islamu Walmuslimin Shahidi Mahallati, Mwakilishi wa Fakihi Mtawala (Waliyyul Faqih) ambaye pia ni Mkuu wa Taasisi ya Mashahidi na Masuala ya Kujitolea katika Njia ya Haki ameutaja utamaduni wa jihadi, kufa shahidi na kujitolea katika njia ya haki kuwa ndiyo nguzo kuu ya mafanikio na uimara wa Mapinduzi ya Kiislamu na huku akiashiria vipaumbele vya kiutamaduni katika taasisi yake amesema: Kuanzishwa sekretarieti ya Baraza Kuu la Kustawisha na Kueneza Utamaduni wa Kufa Shahidi na Kujitolea katika Njia ya Haki, kuongeza uimara wa watu wanaojitolea katika njia ya haki na kuwashukuru na kuwapongeza watu hao kupitia mpango maalumu wa kutoa shukrani pamoja na kuongeza ushirikiano baina ya taasisi hiyo na taasisi nyingine za utendaji nchini; ni miongoni mwa mipango na ratiba muhimu za Taasisi ya Mashahidi na Masuala ya Kujitolea katika Njia ya Haki ya Iran.
Pambizoni mwa mkutano huo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei amezungumza kwa karibu na kwa mapenzi makubwa na majeruhiwa wa kivita waliokuwepo kwenye sehemu hiyo.
 
< Nyuma   Mbele >

^