Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Aonana na Wahadhiri wa Vyuo Vikuu Chapa
02/07/2014
 Mamia ya wahadhiri wa Vyuo Vikuu vya Iran, alasiri ya leo wameonana na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na kubadilishana naye mawazo kuhusu masuala mbali mbali ya kielimu, masuala ya Vyuo Vikuu, ya kiutamaduni, kijamii, kiuchumi na ya kisiasa.
Mwanzoni mwa kikao hicho kilichodumu kwa zaidi ya masaa mawili, wahadhiri saba wa Vyuo Vikuu wametoa mitazamo yao tofauti kuhusu masuala mbali mbali.
Baada ya hapo Ayatullah Udhma Khamenei amesisitizia wajibu na umuhimu wa kuiendeleza kwa nguvu zote kasi ya mwamko wa pande zote wa kielimu nchini Iran akiutaja mwamko huo kuwa ndicho kitu kikuu kinachounda mustakbali bora wa Iran na ulimwengu wa Kiislamu.
Ameongeza kuwa, ufanikishaji wa lengo hilo muhimu unahitajia kufanyika kazi na usimamiaji wa kijihadi wa watu ambao ni maashiki na wenye mapenzi makubwa na maendeleo ya nchi na ya taifa lao.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekutaja kuonana kwake na wahadhiri wa Vyuo Vikuu kuwa ni moja ya vikao muhimu vinavyompendeza mno ambapo lengo kuu la vikao na mikutano kama hiyo ni kuwaenzi na kuonyesha mapenzi makubwa kwa wasomi na majimui yote ya watu wenye vipaji na vipawa vya kila namna vya kielimu na kifikra nchini.
Ayatullah Udhma Khamenei pia amesema, masuala yaliyojadiliwa na baadhi ya walimu wa Vyuo Vikuu waliozungumza kabla yake yalikuwa mazuri sana na yenye faida na kuongeza kuwa: Inshaallah majimui ya masuala hayo yatatumiwa na maafisa husika katika kupanga mipango na kubadilishana mawazo na kwamba kuna wajibu wa kuhakikisha kuwa taathira ya masuala hayo inaonekana wazi wazi.
Baada ya kutoa utangulizi huo amebainisha nukta kadhaa muhimu kuhusiana na harakati ya kielimu nchini Iran. Ulazima wa kuhakikisha kuwa harakati ya kielimu nchini haipungui kasi na wala haisimami na kuhakikisha inakwenda sambamba na harakati iliyojaa kasi ya maendeleo nchini ni nukta ya kwanza iliyoashiriwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika kikao hicho.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Harakati ya kielimu nchini Iran ni maudhui ya kimsingi kwa ajili ya mustakbali wa nchi na jamii na hata kwa ajili ya ulimwengu mzima wa Kiislamu.
Ameongeza kuwa: Baada ya kupita miaka mingi ya kutilia mkazo umuhimu wa kazi za kielimu, hivi sasa harakati ya kielimu nchini Iran imepata mafanikio makubwa kiasi kwamba inatambulika pia kimataifa na kwa hakika tunaweza kusema kuwa, mwamko wa kielimu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran umejipambanua vizuri duniani.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria wasi wasi mkubwa uliopo kuhusu maendeleo ya kielimu nchini Iran na kusema kuwa: Wasi wasi mkubwa uliopo ni kuwa mwamko wa kielimu chini ambao baada ya kufanyika kazi na juhudi kubwa sana ya miaka mingi na kupita kwenye njia nzito na ngumu, hivi sasa umefanikiwa kufikia nusu ya njia, hivyo inabidi juhudi zote zifanyike kuhakikisha usije mwamko huo ukakwama na kusimama.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kuwa: Kusimama na kukwama kwa aina yoyote ile katika njia hiyo au kupungua kasi ya injini ya kielimu nchini, bila ya shaka yoyote kutakwenda sanjari na kubaki nyuma kielimu.
Ameongeza kuwa, iwapo mwamko na harakati ya kielimu nchini Iran itasimama, itakuwa ni vigumu mno kuirejesha katika hali iliyokuwa nayo kabla yake hivyo kila mtu anapaswa kufanya juhudi zake zote kusaidia maendeleo ya kielimu nchini.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, hamu ya maadui na madola ya kiistikbari ya kutaka kuikwamisha na kuisimamisha harakati ya kielimu nchini Iran ni moja ya njama kuu za kambi ya maadui wa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na kuhusiana na sababu ya yeye kutumia mara kwa mara neno "adui" amesema: Kuna baadhi ya watu wanaguswa vibaya wanapoona tunatumia neno "adui" na kulikariri mara kwa mara neno hilo, wakati ambapo hata katika Qur'ani Tukufu pia maneno kama shetani na ibilisi yametajwa na kukaririwa mara nyingi ambapo ujumbe na falsafa ya jambo hilo ni kuwa, watu wawe macho wakati wote na wawala sighafilike na wasimsahau hata sekunde moja shetani na adui.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Kusisitizia mno suala la kuwa macho mbele ya adui hakuna maana ya kusahau na kutozingatia matatizo na mapungufu ya ndani ya nchi, lakini kumsahau na kughafilika na adui wa nje ni kosa kubwa la kiistratijia ambalo madhara yake ni makubwa sana.
Amesisitiza pia kuwa: Kukabiliana na njama na changamoto za kihasidi za adui kunahitajia kuweko harakati na uongozi na usimamiaji wa kijihadi katika masuala ya kielimu na kukabiliana - kwa njia sahihi na kwa utaalamu na kwa mwamko wa hali ya juu maafisa na wahadhiri wa Vyuo Vikuu - na njama na changamoto hizo za maadui.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewataka kwa kusisitiza maafisa wa Wizara ya Sayansi, Utafitia na Teknolojia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pamoja na Vyuo Vikuu pamoja na walimu wa vyuo hivyo kuwa macho mno mbele ya suala la kuendelea kwa kasi kubwa na harakati ya kielimu nchini akiongeza kwamba: Inasikitisha kuona kuwa katika kipindi fulani tulikuwa na mifano isiyotakiwa katika Vyuo Vikuu ambapo vijana wenye vipaji walikuwa wakishawishiwa kuondoka nchini na kwa miaka fulani tuliona baadhi ya watu wakifanya mambo ya kukwamisha harakati ya kielimu ndani ya Wizara ya Sayansi; na kwa kweli inabidi hali hiyo isiruhusiwe kutokea tena.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Vyuo Vikuu havipaswi kuwa mikononi mwa watu ambao wanayaona maendeleo ya kielimu nchini si kitu chochote bali vinatakiwa viwe mikononi mwa watu ambao ni maashiki na wenye mapenzi makubwa sana ya maendeleo ya kielimu ya Iran na wanaoelewa vilivyo umuhimu wa maendeleo hayo katika mustakbali wa nchi na wa taifa.
Vile vile Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, maendeleo ya kielimu nchini Iran yana faida kubwa pia hata katika upande wa malengo ya muda mfupi kama vile katika kupambana na kuvishinda vikwazo vya maadui wa taifa la Iran.
Ameongeza kuwa: Adui anataka - kupitia wenzo wa vikwazo - kuiweka chini ya mashinikizo heshima ya kitaifa ya Wairani na kulidhalilisha taifa, lakini mwamko na maendeleo ya kielimu yataufanya wenzo huo nao kutokuwa na athari zozote.
Amelitaja suala la viongozi wa Iran kuyapa umuhimu mkubwa mashirika ya elimu za kimsingi kuwa ni miongoni mwa mambo muhimu katika kuunganisha pamoja elimu, ufundi na kilimo na kuongeza kuwa: Mashirika ambayo kwa yakini ni mashirika ya elimu za kimsingi yenye viwango bora vinavyotakiwa, yanao uwezo wa kutoa mchango mkubwa sana katika uendelezaji wa mwamko wa kielimu nchini.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria hatua ya baadhi ya watu wa mimbari wanaotilia shaka maendeleo ya kielimu ya Iran na kusema kuwa: Watu hao wanasema maneno hayo kutokana na kutokuwa na taarifa sahihi kuhusu maendeleo hayo na inabidi watu wa namna hiyo wapewe nuru ya elimu katika nyakati na minasaba tofauti ili nuru hiyo iwawezeshe kuona maendeleo ya kujivunia ya Iran katika nyuga za tiba, nyuklia, Nano, seli shina na katika nyuga nyinginezo na wasikae wakazungumza mambo wasiyo na taarifa nayo.
Aidha amelitaja suala la kubuni na kutunga ramani kuu ya kielimu nchini kuwa ni suala la kiistratijia na ndio msingi wa hati za kielimu zilizobuniwa katika sekta mbali mbali nchini Iran na kuongeza kuwa: Inabidi Vyuo Vikuu vyote nchini viainishiwe kazi zao katika ufanikishaji wa ramani hiyo kuu ya kielimu ili vituo mbali mbali vya kielimu nchini viweze kufanyia kazi hati hiyo muhimu kulingana na uwezo na sifa maalumu za kila kituo cha elimu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, ni jambo la dharura na la kimsingi kuhakikisha kuwa maendeleo ya kielimu nchini Iran yanalandana na kutabikiana na mahitaji ya nchi haraka iwezekanavyo na kuongeza kuwa: Ni jambo lililo wazi kuwa makala za kielimu za wahadhiri wa Vyuo Vikuu wa Iran ambavyo ni marejeo ya kielimu dunia ni jambo la kujivunia kwa taifa hili na ni ushahidi wa kupiga hatua kubwa za kielimu taifa la Iran lakini pamoja na hayo inabidi makala na harakati nyinginezo za utafiti wa kielimu zilenge kwenye kukidhi mahitaji ya ndani ya Iran ili Vyuo Vikuu nchini viweze kutekeleza ipasavyo majukumu yake ya kuwasaidia viongozi wa nchi kuliletea maendeleo taifa.
Nukta nyingine muhimu iliyobainishwa na Ayatullah Udhma Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika mkutano na wahadhiri wa Vyuo Vikuu vya Iran ni taathira maalumu yaliyo nayo maneno, vitendo na mwenendo wa maisha wa wahadhiri hao kwa wanafunzi wao.
Amesisitiza kuwa: Ubora wa kielimu wa mwalimu unampa nafasi maalumu na ya kipekee katika akili na shakhsia ya mwanachuo na inabidi nafasi hiyo muhimu ya mhadhiri ndani ya nafsi na akili ya mwanafunzi wake itumiwe vizuri kulea vijana wenye moyo mzuri, wenye matumaini, wenye mtazamo mzuri, mashujaa, wanaoangalia mbali, wenye imani thabiti za kidini, wanaojiamini, wanaoamini misingi ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, wenye moyo wa kuitumikia nchi na taifa na wanaoshikamana na masuala ya kimaanawi na kitaifa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameukosoa mrengo ulioghilibiwa na kutekwa na fikra za Magharibi na kusema kuwa: Mrengo huo hata ukidai kiasi gani kuwa ni wa kitaifa, na ni wa watu wenyewe wa wenye wenye fikra za utaifa, ujue kuwa kwa njia ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja unadhalilishwa na kufanyiwa istihzai na unapelekea wanachuo kutetereka, kuvunjika moyo na kutojiamini na jambo hilo ni ghalati na ni kosa kubwa kabisa.
Ayatullah Udhma Khamenei vile vile ameyataja masomo ya maarifa ya Kiislamu katika Vyuo Vikuu kuwa ni fursa yenye thamani kubwa sana na kuongeza kuwa: Kama wahadhiri watatumia vizuri vipaji vyao kuwafikishia wanachuo kwa njia bora maarifa ya kidini kwa kutegemea elimu iliyofanyiwa utafiti wa kina na inayokwenda na wakati basi watailetea nchi na jamii yetu faida kubwa mno na kwamba vitengo vya wawakilishi wa Fakihi Mtawala katika Vyuo Vikuu vinapaswa kulifuatilia kwa kina suala hilo na kuliwekea mipango mizuri inayotakiwa.
Ayatullah Udhma Khamenei ameyataja mabadiliko ya kimsingi katika masomo ya Sayansi ya Jamii kuwa ni mahitaji muhimu na ya kimsingi nchini Iran lakini wakati huo huo akasema kuwa: Maana ya kuleta mabadiliko ya kimsingi katika masomo ya Sayansi ya Jamii si kutupa nje kikamilifu na kutokuwa na haja kabisa na kazi za kielimu na kiutafiti zilizofanywa na Wamagharibi.
Ametoa ufafanuzi zaidi kuhusu wajibu wa kuweko mabadiliko katika masomo ya Sayansi ya Jamii akisema: Misingi ya masomo ya Sayansi ya Jamii huko Magharibi imejengeka juu ya masuala ya kimaada na kidunia na kuweka pembeni upande wa kimaanawi na mafundisho ya Mwenyezi Mungu wakati ambapo masomo ya Sayansi ya Jamii yanaweza kuwa na faida ya kweli kwa mtu binafsi na kwa jamii kama tu yatajengeka juu ya msingi wa mafundisho ya kidini na ya Kiislamu, hivyo kuna haja ya kufanya mambo kwa kasi ya kimantiki bila ya kuzorota katika kazi hiyo au kufanya mambo kwa pupa.
Mwishoni mwa hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa mara nyingine tena amesisitizia nukta muhimu mno akisema: Maafisa husika na viongozi wa Vyuo Vikuu wanapaswa walipe umuhimu mkubwa sana suala la kuviweka mbali vituo vya kielimu nchini na viwanja vya harakati za mirengo ya kisiasa.
Amelitaja suala la kubadilishwa Vyuo Vikuu kuwa vilabu vya kisiasa kuwa ni mshare angamizi wa harakati ya kielimu nchini na kuongeza kuwa: Inasikitisha kusema kuwa, kuna wakati tulishuhudia jambo hilo lenye madhara makubwa katika baadhi ya vituo vyetu vya kielimu.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitizia na kuunga mkono suala la wanafunzi wa Vyuo Vikuu kuwa na mitazamo, welewa na hisia za kisiasa akisisitiza kuwa: Suala hilo linatofautiana kikamilifu na kugeuzwa vituo vya elimu kuwa kambi na klabu za mirengo ya kisiasa.
Vile vile amekumbusha kuwa, kuweko utulivu katika Vyuo Vikuu kunaandaa uwanja wa kuongezeka kasi ya harakati ya kielimu nchini na iwapo - Mwenyezi Mungu apishie mbali - itatokezea utulivu huo kutoweka basi harakati ya kielimu nayo itasimama na wakati huo Iran itarudi nyuma kimaendeleo.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria anga nyofu na ya kimaanawi na ya ukweli na ikhlasi ya mwezi mtukufu wa Ramadhani na kuwausia watu wote wazitumie vizuri fursa aali za mwezi huu mtukufu kwa kadiri wanavyoweza na kuimarisha taqwa na kujikurubisha zaidi na zaidi kwa Mwenyezi Mungu pamoja na kuimarisha anga ya matumaini, kujiamini, mapenzi na kupendeleana mema katika uhusiano wa wanajamii.
Mwanzoni mwa mkutano huo, wahadhiri 7 wa Vyuo Vikuu tofauti nchini Iran walipata fursa ya kutoa maoni na mitazamo yao kuhusu masuala mbali mbali.
Dk Sayyid Ahmad Reza Khezri - Mhadhiri Kamili wa Chuo Kikuu cha Tehran katika masomo ya dini na historia ya ustaarabu.
Dk Abbas Ali Abadi - Mjumbe wa Jopo la Wahadhiri wa Vyuo Vikuu vya Tehran, Esfahan na Malik Ashtari katika masomo ya uhandisi wa mekanika.
Dk Ibrahimpur Jam - Mhadhiri Msaidizi katika Chuo cha Kilimo cha Chuo Kikuu cha Tarbiat Modares.
Dk Shahla Baqeri - Mhadhiri Msaidizi katika somo la elimu jamii Chuo Kikuu cha Kharazmi.
Dk Sayyid Mahdi Rezayat - Mhadhiri Kamili wa Chuo Kikuu cha Elimu ya Tiba cha Tehran katika somo la famakolojia na taaluma ya dawa za tiba.
Dk Muhammad Baqer Khoramshad - Mhadhiri Msaidizi katika Chuo Kikuu cha Allama Tabatabai somo la Sayansi ya Siasa.
Na Dk Shahram Alamdari - Mhadhiri Msaidizi wa Chuo Kikuu cha Elimu ya Tiba cha Shahid Beheshti ambaye ni mtaalamu bingwa wa Endokrinolojia na Umetaboli (uvunjajivunjaji wa kemikali mwilini) ambapo wote wamezungumza kabla ya hotuba ya kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na kujadili mambo yafuatayo:
- Uchumi wa kimuqawama na wa kusimama kidete, njia pekee ya kuendeleza na kuongeza maendeleo ya nchi katika mazingira ya aina yoyote ile.
- Udharura wa kutambua uwezo, vipaji na nukta dhaifu na zenye nguvu za suala la uchumi wa kusimama kidete.
- Kuendeleza kwa kasi kubwa mwamko wa kielimu na kutia nguvu moyo wa kujiamini.
- Kupanua kiubora elimu ya juu hususan katika daraja la Shahada ya Kwanza.
- Kulipa kipaumbele kikubwa na kuwa na mipango mizuri kuhusiana na suala la kuleta uhusiano wa karibu baina ya Vyuo Vikuu na sekta ya ufundi.
- Nyuga na njia za kuhuisha ustaarabu wa Kiislamu, Kiirani.
- Kusisitizia harakati ya programu za kopmyuta ikiwa ni injini kuu ya kuundika ustaarabu mpya wa Kiislamu - Kiirani.
- Pendekezo la kuundwa timu ya wataalamu ya kufanyia marekebisho miundo ya kiutawala na kiserikali katika sekta ya kilimo.
- Kuweka mipango mizuri kwa ajili ya kusimamia soko na mazao ya kilimo kwa manufaa ya wazalishaji.
- Kurekebisha kigezo cha ulaji vyakula na kuzingatia siasa za matangazo sahihi yanayokubaliana na kigezo hicho.
- Udharura wa kuwa na hisia kali maalumu maafisa na viongozi wa Wizara ya Sayansi katika kulinda na kudumisha utulivu katika vituo vya elimu ya juu na kujiepusha na kutumia mambo yanayoweza kuleta matatizo.
- Udharura wa kuizingatia ramani kuu ya utamaduni katika uchanganuaji wa masuala ya kijamii, kiuchummi na kisiasa.
- Kubuni masomo na kozi mpya kwa ajili ya kutia nguvu uzalishaji wa elimu za kiutamaduni na kubuni aidiolojia za kiutamaduni.
- Udharura wa Wizara ya Sayansi, Utafiti na Teknolojia ya Iran kulipa umuhimu na kulizingatia sana suala la miswada inayopitishwa na Baraza la Mabadiliko katika Sayansi ya Jamii.
- Umuhimu wa kuundwa mfumo maalumu wa kiutamaduni.
- Kukosoa kazi zisizo na uratibu wa pamoja na zinazotofautia kupindukia za asasi za kiutamaduni.
- Udharura wa kuongeza faida ya kazi za utafiti.
- Maendeleo ya kupigiwa mfano katika nyuga za teknolojia ya Nano kunakothibitisha vipaji na uwezo wa Wairani katika sekta mbali mbali za kielimu.
- Ulazima wa kupanuliwa wigo wa uungaji mkono wa hatua zote za mlolongo na myororo wa uzalishaji elimu hadi uzalishaji wa bidhaa.
- Ulazima wa kufuatilia kwa karibu na kwa sura endelevu mabadiliko yanayotokea kwa kasi katika eneo la Mashariki ya Kati na duniani kiujumla kwa ajili ya kuchukua hatua zinazotakiwa kwa wakati mwafaka na kwa busara ya hali ya juu katika kukabiliana na mabadiliko hayo.
- Udharura wa kuchukua hatua za haraka asasi ya kidiplomasia ya Jamhuri ya Kiislamu katika eneo la Mashariki ya Kati na katika ulimwengu wa Kiislamu katika kuamiliana matukio mbali mbali.
- Kuchunguza mambo yanayouletea madhara mwamko wa Kiislamu na umuhimu wa kueneza na kutia nguvu fikra na tafakuri za maana ndani ya mirengo iliyo amilifu katika mwamko huo.
- Kuwa macho na kuchukua tahadhari kubwa mbele ya mrengo wenye fikra mgando wa kitakfiri ambao ndio unaodhamini malengo ya kambi ya kibeberu duniani.
- Pendekezo la kulipa mazingatio maalumu suala la kusimamia na kuongoza vizuri migogoro na ulinzi tulivu katika Mpango wa Sita wa Maendeleo nchini Iran.
- Umuhimu wa kubadilisha mtazamo na mfumo wa utoaji elimu na maarifa kwa kuzingatia uleaji wa kizazi cha watu wenye hekima.
- Kubadilishwa siasa Kuu za Usalama wa Kiafya kuwa vielelezo vya wastani vya kielimu na ambavyo vinavyoweza kufanyiwa tathmini.
- Na umuhimu wa kuzingatiwa vielelezo vya usalama wa kimaanawi katika hatua tofauti za kutafuta elimu.
 
< Nyuma   Mbele >

^