Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Kiongozi Muadhamu Aonana na Viongozi wa Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu Chapa
07/07/2014
Kiongozi Muadhamu Aonana na Viongozi wa Mfumo wa Jamhuri ya KiislamuAyatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, leo jioni (Jumatatu) ameonana na maafisa, wafanyakazi na majimui ya viongozi wa ngazi za juu wa taasisi mbali mbali za nchi na za kijeshi na sambamba na kubainisha nukta kadhaa muhimu sana zinazohusiana na masuala ya ndani na nje ya Iran amesema kuwa, njama tata na za pande kadhaa za kujaribu kukwamisha na kuharibu mahesabu ya viongozi na taasisisi za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ndilo lengo kuu la hivi sasa la mabeberu hususan Marekani.
Aidha ameashiria hali nyeti mno liliyomo ndani ndani yake hivi sasa eneo la Mashariki ya Kati na dunia kiujumla ambapo hivi sasa dunia inapita kwenye kipindi nyeti sana katika historia yake na kusisitiza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu itaendelea kutegemea mahesabu yake makuu ya kimantiki yaani "kumtegemea Mwenyezi Mungu na sunna za maumbile" na "kumuelewa vizuri adui na kutomuamini hata kidogo"na itaendelea na njia yake iliyojaa fakhari kwa kutegemea uungaji mkono wa wananchi, kutumia vizuri uzoefu mbali mbali na kufanya jitihada kubwa za kufanikisha malengo matukufu ya taifa hili.
Ayatullah Udhma Khamenei aidha ameutaja mwezi wa Ramadhani kuwa ni fursa nzuri ya kujivua na vitendo vya shetani na kujipamba kwa taqwa, uchaji Mungu na vitendo vinavyozidisha rehema za Mwenyezi Mungu akiongeza kuwa: Katika mapambano baina ya haki na batili, shetani anakuwa na lengo lake maalumu na taqwa nayo ina njia yake muhimu sana. Shetani anafanya njama za kuvuruga mahesabu ya wanadamu na kuwatumbukiza kwenye makosa ya kimahesababu na kuwafanya wachukue hatua kimakosa wakati taqwa inaandaa uwanja wa welewa na utambuzi wa mwanadamu na kumpa nguvu za kupambanua vizuri haki na batili.
Amesema, kutoa vitisho na kutia tamaa ni mbinu mbili kuu zinazotumiwa na shetani ili kuwafanya wanadamu wafanye makosa katika mahesabu yao na kuongeza kuwa: Shetani kwa upande mmoja anatoa vitisho ili kuwatisha wanadamu na kwa upande wa pili anawarubuni kwa ahadi za uongo na kuwapambia mambo yao na kuwahadaa kwa mustakbali bandia wa kufikirika tu usio na uhakika wowote ambao mwishowe hutoweka ghafla mbele ya watu hao kama sarabi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia nukta muhimu katika mazungumzo yake hayo kuhusiana na kuelewa vizuri miamala ya Marekani na madola makubwa ya kibeberu akisema kuwa: Vitendo na miamala ya Marekani na madola ya kibeberu ni sawa sawa kabisa na vitendo vya shetani kwani mabeberu hao mara zote wanafanya njama za kutoa vitisho kwa upande mmoja na kutia tamaa watu kwa upande wa pili kwa kuwapa watu hao ahadi ambazo kamwe hayazitimizi na yanatumia njia hiyo kuzilazimisha nchi nyingine kuwa chini ya ubeberu wao. Shetani naye anafanya njama hizo hizo za kutoa vitisho na kutia tamaa ili kuvuruga mahesabu ya mwanadamu na kumfanya afanye makosa katika mahesabu na maamuzi yake (na ashindwe kujua nini ni haki na nini ni batili).
Ayatullah Udhma Khamenei amesema kuwa, kufanya makosa katika mahesabu ni jambo la hatari kubwa sana na kuongeza kuwa: Watu wote wanapaswa kuwa macho wasije wakatumbukia kwenye hatari hiyo kubwa kwani unapofanya makosa katika mahesabu unapoteza nguvu na uwezo wa kuchukua maamuzi kwa njia sahihi na juhudi zako zote zinakwenda bure.
Amesema, kuwa macho viongozi katika suala hilo ni jambo la dharura zaidi na kuongeza kuwa: Moja ya makosa makubwa katika mahesabu ni mtu kudharau vitu vya kimaanawi na sunna za Mwenyezi Mungu na akakumbatia tu masuala ya kimaada na yanayohisika tu na viungo vyake vya mwilini.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, mambo yenye ufanisi na utovu wa ufanisi pamoja na masuala ya maendeleo na utovu wa maendeleo si mambo ambayo yanaishia tu katika masuala ya kimaada na ambayo yanahisika kwa viungo vya hisia vya mwili wa mwandamu.
Ameongeza kuwa: Masuala ya umaanawi na sunna zilizo muhali kubadilika za Mwenyezi Mungu ni miongoni mwa masuala yenye taathira kubwa sana ambayo hayahisiki kwa viumbe vya mwili wa mwanadamu na kwamba kudharau masuala hayo ni kosa kubwa lisiloweza kufidika kwa hali yoyote ile.
Katika kubainisha zaidi umuhimu na nafasi ya masuala ya kimaanawi na sunna za Mwenyezi Mungu, Ayatullah Udhma Khamenei ametoa ushahidi kutoka katika aya kadhaa za Qur'ani Tukufu na ushahidi wa wazi na wa kivitendo wa aya hizo na kuongeza kuwa: Mwenyezi Mungu anasema katika Qur'ani Tukufu kuwa kama mtainusuru harakati na dini ya Mwenyezi Mungu, basi kuweni na uhakika kwamba mtapata msaada wa Mwenyezi Mungu. Sunna hii ya Mwenyezi Mungu imeshuhudiwa mara nyingi sana katika historia ya mwanadamu na mfano wa karibuni kabisa ni ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran ambao ni kipindi kilichojitokeza kwa uwazi zaidi na kwa mabadiliko makubwa sana katika historia ya dunia.
Ayatullah Udhma Khamenei ametoa majumuisho ya maelezo yake hayo kuhusiana na umuhimu wa viongozi wa Iran kuwa macho na kutofanya makosa katika mahesabu yao kwa kuwasisitizia jambo hilo akiwaambia: Msiruhusu kufanyika makosa katika mahesabu yenu kwa kutoa mwanya kwa adui kuvuruga mahesabu yenu hayo kupitia vitisho na kutia tamaa.
Akiendelea na hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, mapambano makali ya mtawalia na yasiyosita baina ya Jamhuri ya Kiislamu na kambi ya kibeberu ni muendelezo wa njia ile ile ya mapambano ya Mitume na Manabii wa Mwenyezi Mungu dhidi ya mataghuti na mashetani - majini na watu - na kuongeza kwamba: Pamoja na kuwepo upambaji mkubwa wa mambo wa kidangayifu wa mashetani, lakini harakati ya taifa la Iran ya kufuata mafundisho ya Mwenyezi Mungu itaendelea kupata mafanikio na kuwa imara siku baada ya siku.
Amekutaja kushindwa mbinu mbili kuu za adui yaani "vitisho vya kijeshi" na "vikwazo" kuwa kumeifanya kambi ya kibeberu sasa kuamua kuvuruga mahesabu ya taasisi za Ira na ya viongozi wa nchi hii.
Amesisitiza kwamba: Vikwazo inabidi vifelishwe kupitia kufanya jihadi kubwa chini ya mwavuli wa uchumi wa kimuqawama na wa kusimama kidete, na vitisho vya kijeshi navyo kutokana na gharama zake kutobebeka na kutokuwa na maslahi kwa mabeberu vinaishia tu katika vitisho vya maneno visivyo na dhamana yoyote ya kutekelezwa kivitendo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa ufafanuzi zaidi kuhusu njia kuu za kukabiliana na vikwazo akisema: Kama alivyosema hapa mheshimiwa Rais, mipango ya kiuchumi inapaswa iwekwe na ifuatiliwe kwa kufaridhisha na kujengea kwamba adui hatapunguza hata punje moja ya vikwazo vyake.
Ayatullahil Udhma Khamenei ameashiria matamshi ya baadhi ya viongozi wa Marekani kuhusiana na kuendelea kuwepo vikwazo dhidi ya Iran hata kama kutafikiwa makubaliano ya mwisho ya nyuklia na kusema kuwa: Kama ambavyo tumesema mara nyingi, suala la nyuklia ni kisingizio na sababu tu, na kama kisingizio hicho hakitokuwepo, maadui watatafuta sababu na visingizio vingine kama vile haki za binadamu, haki za wanawake na masuala mengineyo na kuyafanya sababu za kulishinikiza taifa la Iran.
Ayatullah Udhma Khamenei amezungumzia pia njia ya pili kuu inayotumiwa na Marekani yaani vitisho vya kijeshi akisema kuwa: Masuala kama vile kuua watu, kufanya mauaji na jinai pamoja na uporaji, hakuna lolote kati ya mambo hayo linaloweza kuwazuia Wamarekani kufanya wanalotaka, isipokuwa tu uhakika wa mambo ni kuwa, hivi sasa Wamarekani hawawezi kugharamia mashambulio ya kijeshi na mashambulio hayo hayana faida kwao hivi sasa na ndio maana wachambuzi na weledi wa mambo duniani kama ilivyo kwa wananchi wa Iran, wakawa hawavipi umuhimu wala uzito wowote, vitisho hivyo vya kijeshi vya Marekani.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria namna Marekani ilivyounga mkono ukatili wa Saddam na jinsi ilivyoshambulia ndege ya abiria ya Iran na kuua kwa umati mamia ya wanawake na watoto wadogo wasio na hatia na vile vile kuua mamia ya maelfu ya watu katika nchi za Iraq na Aghanistan na kusababisha migogoro ya umwagaji damu katika nchi mbali mbali duniani kwa jina la "Mapinduzi ya Rangi" na kuongeza kwamba: Maisha ya utulivu na amani ya mataifa mengine hayana thamani yoyote kwa Wamarekani na wakati wowote wanapoona shambulio fulani lina manufaa kwao, hawasiti hata kidogo kufanya shambulio hilo.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria pia baadhi ya matamshi yanayodai kuwa Marekani imeuzuia utawala wa Kizayuni usiishambulie kijeshi Iran na kusema kuwa: Kama madai hayo yatakuwa na ukweli ndani yake, basi sababu ya Marekani kufanya hivyo ni kuwa shambulio hilo halina faida kwa Marekani na sisi tunatangaza waziwazi kwamba shambulio la kijeshi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran halitakuwa na faida kwa mtu yeyote yule.
Baada ya hapo ametoa majumuisho ya miongozo yake kuhusu suala hilo akisema: Adui amebaki mikono mitupu katika kila upande, iwe ni upande wa vitisho au upande wa vikwazo, lakini kwa sharti kwamba sisi nasi tuwe ni watu wenye imani ya kweli ya Mwenyezi Mungu na tuwepo imara katikati ya medani kwa maana halisi ya neno.
Baada ya hapo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameingia kwenye mjadala mkuu wa hotuba yake yaani njama za mabeberu na hasa Marekani za kujaribu kuingiza makosa ya kimahesabu katika akili na fikra za viongozi wa Iran na kuashiria nukta angalifu sana katika sehemu hiyo ya hotuba yake.
Amesema: Adui anatambua vyema kwamba wakati Jamhuri ya Kiislamu inapoamua kufanya jambo na kufikia lengo fulani, lazima italifikia lengo hilo, hivyo adui anafanya njama za kuvuruga mahesabu ya viongozi wa Iran ili waache kufuatilia malengo ambayo yatakwenda kinyume na manufaa ya Marekani na hivi ndivyo hivyo vita laini ambavyo tumevizungumzia miaka kadhaa iliyopita.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa njama hizi za Marekani nazo zitashindwa tu na kuongeza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu tangu siku ya kwanza kabisa imezikita siasa na miamala yake katika nguvu imara ya kimantiki ya kutegemea mambo mawili makuu yaani "kumwamini Mwenyezi Mungu na sunna za maumbile" na "kumwelewa vizuri adui na kutomwamini hata kidogo" na kwamba katika siku za usoni pia huo ndio utakaondelea kuwa msimamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Ayatullah Udhma Khamenei ametoa ufafanuzi kuhusu mambo yaliyomo kwenye nguzo hizo mbili kuu za kimantiki na kiakili akisema: Kuwategemea wananchi na mapenzi yao pamoja na misimamo yao madhubuti na ya kweli, kuamini kaulimbiu ya "tunaweza" na kutegemea uchapaji kazi wa kweli na kujiweka mbali na uvivu na ugoigoi, kutegemea nusra ya Mwenyezi Mungu, kufanya jitihada kubwa ya kutekeleza ipasavyo majukumu, kutumia vizuri uzoefu mbali mbali, kusimama kidete katika msingi wa huru na kujitegemea na kuwa makini sana mbele ya miamala ya mababeru na mataifa mengine duniani ni miongoni mwa mambo muhimu yanayounda nguvu ya kimantiki ya Jamhuri ya Kiislamu yaani msingi wa kisiasa na wa maamuzi na hatua zinazochukuliwa na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Ameongeza kuwa: Upinzani wa kambi ya kibeberu dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nao kwa hakika unatokana na mantiki hiyo hiyo kwani ukweli wa mambo ni kuwa mabeberu hawashughulishwi na jina tu la Kiislamu la utawala wa nchi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia matamshi ya mtaalamu mmoja wa serikali ya Marekani aliyesema kuwa upo uwezekana wa kufikiwa mapatano baina ya "Iran na Marekani" na lakini hakuna uwezekano kabisa wa kuwepo mapatano baina ya "Jamhuri ya Kiislamu na Marekani" na kuongeza kuwa: Matamshi hayo ni sahihi kwani Marekani haikuwa na tatizo lolote na Iran wakati wa utawala wa wafalme wa Kipahlavi kutokana na kwamba Iran ilikuwa kibaraka tu wa Marekani wakati huo, lakini kamwe Marekani haiwezi kukaa bila ya kuifanyia uadui Jamhuri ya Kiislamu ambayo inalingania uhuru, imani ya kweli kwa Mwenyezi Mungu, kujitegemea, kusimama kidete mbele ya dhulma pamoja na kupigania mshikamano na umoja kati ya Waislamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameendeleza hotuba yake mbele ya majimui ya viongozi, maafisa na wafanyakazi wa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu kwa kutoa nasaha kadhaa muhimu.
Katika nasaha yake ya kwanza ameashiria hali nyeti kikamilifu iliyopo katika eneo la Mashariki ya Kati na duniani kiujumla na kuwasisitizia viongozi wote nchini Iran akiwaambia: Hivi sasa tumo katika kipindi nyeti sana cha historia kwa maana halisi ya neno, na kama hatutakuwa imara na wenye nguvu, basi sote tutafanyiwa ubeberu hivyo tunapaswa kujiimarisha kadiri inavyowezekana.
Ayatullah Udhma Khamenei ametoa ufafanuzi zaini kuhusu mambo yanayoongeza nguvu na uimara wa nchi akisema kwamba ni pamoja na kuwa na moyo wa kweli, kuangalia mambo kwa matumaini, kufanya kazi kwa bidii, kuelewa mambo yanayoharibu na kukwamisha masuala ya kiuchumi na kiutamaduni na kiusalama na kufunga njia za mambo hayo, kuzidi kuwa imara siku hadi siku taasisi hasa zenye mfungamano wa moja kwa moja na wananchi; na kusisitiza kuwa, hayo ni miongoni mwa mambo yanayoweza kuongeza nguvu za Iran.
Nasaha za pili za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa viongozi wote nchini Iran, ni kujua thamani ya fursa ya kufanya kazi za kuwatumikia wananchi.
Amewakhutubu kwa kuwaambia: Msiseme kuwa haturuhusiwi, kwani maneno hayo ambayo yalikuwa yanasemwa pia katika vipindi vya huko nyuma hayakubaliki kabisa na inabidi suhula zilizopo zitumiwe vizuri na kutopoteza fursa hata ndogo kwa ajili ya kufanya kazi kwa bidii na maarifa.
Katika usia wake mwingine, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewakhutubu viongozi wote nchini Iran kwa kusisitiza akiwaambia: Pangilieni mambo na harakati zenu kwa msingi wa usuli za Mapinduzi ya Kiislamu na jiwekeni mbali na mambo ya pembeni na yasiyo ya msingi na zingatieni zaidi njia za kutatua matatizo ya wananchi.
Kuwa na ushirikiano mzuri Mihimili Mitatu Mikuu ya dola (Serikali, Mahakama na Bunge) na kuwepo ushirikiano wa karibu baina ya sekta mbali mbali za ndani ya mihimili hiyo ni nasaha za tatu zilizotolewa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa viongozi na wafanyakazi wa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu. Kufanyika vikao vya mara kwa mara baina ya wakuu wa mihimilimi hiyo mitatu, kuitishwa vikao vya pamoja vya pande mbili baina ya mihimili hiyo, kubadilishana mawazo na kufaidika na ushauri wa kila upande baina ya pande mbili na vile vile kuwepo uongozi, usimamiaji na uendeshaji wa kijihadi wa mambo ni miongoni mwa nukta muhimu zilizokuwemo kwenye sehemu hiyo ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameendelea na hotuba yake kwa kutoa nasaha nyingine kadhaa kuhusu namna ya kuamiliana na serikali na vile vile ametoa nasaha kadhaa kuikhutubu serikali yenyewe.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema kuhusu muamala na serikali kwamba: Mimi ninaiunga mkono serikali na nitatumia nguvu zote nilizo nazo kuiunga mkono serikali na nina imani na viongozi wa ngazi za juu serikalini.
Vile vile ameashiria namna ambavyo amekuwa akiziunga mkono serikali zote zilizochaguliwa na wananchi katika vipindi vyote vya huko nyuma na kuongeza kuwa: Serekali zote hizo zimekuwa na mambo chanya na hasi na kwamba kuzikosoa serikali zilizopita kunapaswa kufanyike kiutaalamu kama ambavyo ukosoaji juu ya mimbari za umma hauonekani kuwa na maslahi sana.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Tab'an kuhusu serikali ya hivi sasa pia, ukosoaji wa aina yoyote ile unapaswa uwe kwa kiinsafu, kiadilifu, kiheshima na wenye mapenzi ndani yake na inabidi wakosoaji wahakikishe wanajiepusha na aina yoyote ile ya maudhi na kukwamisha mambo.
Ayatullah Udhma Khamenei alikuwa pia na nasaha maalumu kwa Serikali. Kuzipa uzito wa hali ya juu siasa za uchumi wa kimuqawama na wa kusimama kidete ndizo zilizokuwa nasaha zake za kwanza kabisa kwa Serikali. Amesema: Mheshimiwa rais na baadhi ya viongozi serikalini wamezungumza kwa kiasi fulani kuhusu uungaji mkono wao kwa siasa za uchumi wa kusimama kidete, lakini kinachotakiwa hasa ni vitendo na si sahihi kusema tu kuwa tunaunga mkono uchumi wa kusimama kidete, lakini tukawa tunachukua hatua dhaifu sana za kivitendo za kufanikisha siasa hizo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza pia kuwa: Msingi wa uchumi wa kusimama kidete ni kutegemea uzalishaji wa ndani na kuimarisha muundo wa ndani ya nchi wa kiuchumi.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Ustawi wa kiuchumi nao utapatikana tu kwa kutegemea uzalishaji wa ndani na kuwa na kazi zenye umakini mkubwa na nyingi pamoja na kututumia vizuri uwezo wa ndani ya nchi na si kwa kitu kingine.
Aidha kuhusiana na utekelezaji wa siasa uchumi wa kusimama kidete ametoa nasaha pia kwa benki mbali mbali nchini Iran na vile vile kwa sekta ya viwanda na madini nchini.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuhusu benki mbali mbali nchini Iran kwamba: Benki zinapaswa kutoa mchango mzuri na chanya katika ufanikishaji wa utekelezaji wa siasa za uchumi wa kusimama kidete na zijitabikishe na siasa na mipango ya serikali katika ufanikishaji wa suala hilo muhimu.
Amma nasaha za kugogoteza za Ayatullah Udhma Khamenei kwa sekta ya viwanda na madini ilikuwa ni kwamba sekta hiyo iongeze jitihada na kazi zake kwani mzigo wa asili wa kujitoa katika uzorotaji wa kiuchumi uko juu ya mabega ya sekta ya viwanda na madini.
Vile vile amesema kuwa sekta ya kilimo ina umuhimu mkubwa mno na huku akisisitizia ulazima wa kuweko siasa na sera za serikali za kusaidia vilivyo sekta hiyo muhimu sana amesema: Inabidi matatizo ya wakulima na wafugaji yapatiwe ufumbuzi unaotakiwa katika siasa za kuunga mkono na kusaidia sekta ya kilimo nchini.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameendelea na hotuba yake kwa kugusia kaulimbiu ya Serikali ya Kumi na Moja ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo ni "misimamo ya wastani" na kusema kuwa, kaulimbiu hiyo ni nzuri mno na anaiunga mkono kwani siku zote misimamo mikali haikubaliki na ni kitu kinachopaswa kulaaniwa.
Aidha Ayatullah Udhma Khmenei ametoa nasaha maalumu kwa Serikali kuhusiana na kaulimbiu yake ya "misimamo ya wastani" akiiambia: Kuweni macho na chukueni tahadhari kubwa msije mkaiweka pembeni mirengo ya watu waumini katika masuala ya siasa nchini kwa kutumia kaulimbiu ya misimamo ya wastani kwani ni mrengo huo wa waumini ndio ambao unakuwa wa kwanza kujitokeza mbele wakati yanapotokezea matatizo na ndiyo inatojitokeza mbele kuisaidia kikweli kweli serikali.
Baada ya hapo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa nasaha muhimu kwa baadhi ya mirengo ya kisiasa na vyombo vya habari akivikhutubu kwa kuviambia: Usalama wa kifikra na kiakili wa wananchi ni jambo muhimu sana. Hivyo si sahihi kutangaza na kuzusha mambo yasiyo na mashiko na kuakisi maneno ya vyombo vya habari vya watu baki na vya kibeberu ili kucheza na akili za wananchi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameendelea mbele na hotuba yake kwa kuashiria kadhia ya nyuklia na kuitaja kadhia hiyo kuwa ni nyeti sana na huku akiunga mkono hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu suala hilo la nyuklia amesema: Uhakika wa mambo ni kuwa, katika kadhia hiyo upande wa pili unaofanya mazungumzo na Iran umefikiria kifo ili sisi turidhike na homa (Umefikiria kitu kibaya zaidi dhidi ya Iran ili kuilazimsha Tehran ikubali kitu wanachotaka wao).
Ayatullah Udhma Khamenei ameitaja kadhia muhimu mno ya kiwango cha ya kurutubisha urani kuwa ni moja ya masuala yenye mzozo kati ya Iran na upande wa pili na kuongeza kuwa: Lengo la upande huo wa pili wa mazungumzo ni kuifanya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikubaliane na urutubishaji urani wa wa mikondo elfu 10 lakini wameanza na mikondo 500 na mikondo 1000 ambapo mikondo 10 ndiyo inayoweza kuzalishwa na karibu mashinepewa elfu 10 za zamani tulizokuwa nazo zamani wakati ambapo kwa mujibu wa wataalamu wengi, mahitaji ya Iran ni mikondo laki moja na 90 elfu.
Ameyadaja madai ya Marekani ambayo inapinga teknolojia ya kisasa ya nyuklia liliyo nayo taifa la Iran - ambayo taifa hili limefanikiwa pia kuifanya iendane na hali yake ya ndani - kwa madai kuwa ina wasiwasi na kumiliki Iran silaha za atomiki kuwa ni madai yasiyo sahihi na yasiyoingilika akilini hata kidogo.
Amesema, njia za kuweza kuizuia nchi fulani isimiliki silaha za nyuklia ziko wazi na zina taasisi zake maalumu na kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haina tatizo lolote na suala hilo na tayari imeshatoa dhamana kupitia njia hizo, lakini vile vile, Marekani haina haki ya kudai ina wasi wasi na silaha za atomiki, kwani yenyewe Marekani ina historia ya kutumia silaha hizo na hivi sasa pia imejilimbikizia maelfu kadhaa ya mabomu ya atomiki za maangamizi ya umati.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewakhutubu Wamarekani akiwaambia: Suala la kuwa na wasi wasi na silaha za atomiki halikuhusuni kabisa kutokana na faili la matumizi mabaya ya nyuklia mlilo nalo nyinyi.
Ayatullah Udhma Khamenei aidha amesisitiza kwa kusema: Tab'an sisi tuna imani na timu ya nyuklia ya nchi yetu na tuna uhakika kuwa haitaridhika hadi itakapopata haki za nchi, taifa na heshima ya taifa la Iran, na kamwe haiwezi kuruhusu kuchezewa haki na heshima ya taifa la Iran.
Suala la kufanya utafiti na kupanua wigo wa masuala ya nyuklia, ni jambo jingine ambalo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema ni lazima lichungwe vizuri katika mazungumzo hayo.
Ameongeza kuwa: Suala jingine muhimu ambalo upande wa pili una hisia kali sana nalo ni kulindwa taasisi na mchakato mzima wa teknolojia ya nyuklia ya Iran ambao ni muhali kwa maadui kuweza kuuharibu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Kuhusu taasisi ya nyuklia ya Fordow, utausikia upande huo wa pili wa mazungumzo ukisema kuwa, kwa vile taasisi hiyo ya nyuklia ya Fordow haipatikani kirahisi na haiwezekani kuishambulia kijeshi, basi ni lazima ifungwe. Matamshi kama haya ni kichekesho kikubwa!
Ayatullah Udhma Khamenei ameendelea na hotuba yake kwa kuzungumzia masuala ya eneo la Mashariki ya Kati na hususan fitna iliyoanzishwa nchini Iraq akisema: Kwa taufiki ya Mwenyezi Mungu, wananchi wenye imani thabiti wa Iraq watafanikiwa kuizima fitna hiyo na mataifa ya eneo la Mashariki ya Kati nao watazidi kupata ustawi wa kimaada na kimaanawi, siku baada ya siku.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake amezungumzia mwezi mtukufu wa Ramadhani na kuutaja kuwa ni mwezi wa toba, kujijenga kinafsi, kurejea kwa Mola Muumba na kujiandalia mazingira ya kuepushwa na adhabu ya moto na kupata neema ya pepo kwa kujiweka mbali na maovu na kujipamba kwa mienendo mizuri.
Ameongeza kuwa: Miongoni mwa mafundisho mazuri sana na matukufu anayoyapata mwanadamu katika dua za mwezi mtukufu wa Ramadhani ni kutekeleza amali zake kwa maarifa kamili na kwa malengo maalumu, kujiweka mbali na uvivu na ugoigoi na kujiepusha na kuvunjika moyo, kudharau mambo, kutoruhusu kuwa na moyo wa jiwe, kuwa na mawazo mgando na kukumbwa na mghafala. Amesema, viongozi nchini wana wajibu mkubwa zaidi wa kuchunga mambo hayo na kutekeleza kivitendo mafundisho hayo matukufu.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Hujjatul Islam Walmuslimin Rouhani, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria baraka na uongofu wa kimaadili na kiutamaduni wa mwezi mtukufu wa Ramadhani na kusema kuwa, lengo kuu la Mapinduzi ya Kiislamu ndilo lile lile lengo ambalo Mwenyezi Mungu Mtukufu amewatuma kwalo Manabii na Mitume wake, yaani kukamilisha maadili yaliyo bora.
Amesema: Serikali inaamini kuwa jukumu muhimu zaidi kwake hivi sasa ni jukumu la kiutamaduni na vile vile kutekeleza siasa kuu za uchumi wa kusimama kidete hususan katika mwaka huu ambao umepewa jina la utamaduni na uchumi.
Rais Hassan Rouhani amekutaja kutekeleza hati tatu muhimu za "uhandishi wa kiutamaduni" na "mabadiliko ya kimsingi katika Wizara ya Elimu na Malezi" pamoja na "watu wenye vipaji" kuwa ni mipango muhimu zaidi inayotekelezwa na serikali katika masuala ya kiutamaduni kwa mwaka huu.
Ameongeza kuwa: Sehemu kubwa ya majukumu ya kiutamaduni iko juu ya mabega ya taasisi za kidini na kijamii kama vile Hawza (Chuo Kuu cha Kidini), walimu, wasanii na wapenzi wa masuala ya utamaduni.
Amesema, nafasi ya marajii taqlidi na asasi za kidini ni muhimu na ni yenye thamani kubwa sana na haina na mbadala na kuongeza kuwa, leo hii taasisi ya umarjaa ni kizuizi madhubuti na ni taasisi yenye nguvu katika kupambana na njama za kibeberu na Kizayuni ambapo mfano wake wa wazi kabisa ni kile kilichoshuhudiwa nchini Iraq (hasa baada ya taasisi hiyo kutoa fatwa kwa wananchi kujilinda; na watu wakajitokeza kwa wimbi kubwa mno kutekeleza fatwa hiyo).
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameendelea na hotuba yake kwa kusema: Serikali inalipa umuhimu mkubwa suala la kuyatia nguvu mashirika ya elimu za kimsingi na imetenga maelfu ya mabilioni ya Tumani (jina jingine la sarafu ya Iran) kwa ajili ya mfuko wa ubunifu na kutafuta na kukuza vipaji kama njia ya kuyasaidia na kuyaunga mkono mashirika hayo.
Sehemu iliyofuatia baada ya nukta hiyo katika ripoti ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imehusiana na namna serikali ilivyofanyia kazi masuala ya kiuchumi kwa kulenga zaidi kwenye vielelezo viwili muhimu ambavyo ni "mfumuko wa bei" na "kukuza uchumi."
Rais Rouhani ametoa tathmini jumla kuhusu kazi zilizofanywa na serikali kwenye masuala ya kiuchumi katika kipindi cha miezi 11 ya tangu serikali yake iingie madarakani na kusema kuwa, katika baadhi ya vielelezo, serikali imefanya kazi kiufanisi zaidi ya iliyotarajiwa ikiwa ni pamoja na kupunguza mfumuko wa bei nukta kwa nukta kutoka asilimia 45 mwezi Khordad 92 (mwezi Juni 3013) na kufikia asilimia 14.6 katika mwezi wa Khordad mwaka huu (mwezi Juni, 2014).
Amesema, kiwango hicho cha kupunguza mfumuko wa bei ambacho kimewezekana kwa msaada wa Bunge, Mahakama, Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Kiislamu na vikosi vya ulinzi, ni mafanikio ya aina yake ikilinganishwa na serikali zilizotangulia.
Ameongeza kuwa: Malengo ya serikali ni kwamba mwaka 1394 (Hijria Shamsia sawa na 2014 Milaadia) mfumuko wa bei ushuke na kuwa chini ya asilimia 20 na mwaka 1395 (2016 Milaadia) asilimia hiyo iwe ya tarakimu moja.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa, kuleta uchumi usiotetereka ni jambo zito zaidi kulikoni hata kuzuia kiwango cha mfumuko wa bei na kuongeza kwamba: Serikali imekusudia kikweli kweli kuvunja rekodi katika utekelezaji wa siasa kuu za uchumi wa kusimama kidete na kuuelekeza uzalishaji wa ndani upande wa kukubali ushindani na usafirishaji nje bidhaa na kwamba mipango ya kujitoa katika hali ya kuzorota kiuchumi watatangaziwa wananchi karibuni hivi.
Rais Rouhani amesema: Jambo la lazima katika ustawi wa kiuchumi ni kuwepo mawasiliano na muamala mzuri na wenye faida na mataifa ya dunia hususan mataifa jirani na kwamba Serikali imechukua hatua zenye taathira nzuri katika uwanja huo.
Ripoti kuhusu hali ya usalama wa kiafya na mpango wa kufanya mabadiliko makubwa katika suala hilo, ilikuwa ni sehemu iliyofuatia ya nukta zilizokuwemo kwenye ripoti ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Ametangaza habari ya kufaidika watu milioni moja na laki mbili na mpango wa mabadiliko ya usalama wa kiafya na kuhudumiwa zaidi ya watu milioni nne na bima ya usalama wa kiafya.
Rais Rouhani ameendelea na hotuba yake kwa kutoa ufafanuzi kuhusu mikakati na kazi zilizofanya na Serikali katika upande wa siasa za nje na kwamba kwa sasa ukuta wa kueneza chuki dhidi ya Iran na kutafuta visingizio kambi ya kiistikbari umeshaanguka.
Ameongeza kuwa, katika ukuta wa vikwazo vya kidhulma vilivyowekwa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia kuna nyufa nyingi ambazo hazizibiki tena.
Amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu inashiriki katika mazungumzo ya nyuklia ikiwa imejizatiti kwa hoja za kimantiki na haiwezi kurudi nyuma hata kwa chembe moja katika kulinda haki za taifa la Iran ikiwemo haki isiyokanushika ya kustafidi kwa njia za amani na teknolojia ya nyuklia bali serikali inafanya juhudi pia ya kupata haki ya taifa la Iran ya kuwa na nafasi katika soko la uwekezaji na teknolojia.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa: Kama leo mazungumzo ya nyuklia yatavunjika kutokana na kupenda makuu adui, dunia nzima itatambua kuwa mkosa katika suala hilo ni upande wa pili wa mazungumzo na si Iran kwani Tehran imefuata njia za kisheria huku ikiwa na uungaji mkono wa kila namna na wa kila upande wa wananchi.
Bw. Rouhani ameashiria mkakati na stratijia nyingine muhimu ya serikali akisema: Mpango wa mabadiliko ya kiuchumi wa serikali katika mwaka huu na miaka ijayo umesimama juu ya msingi wa kuvunja na kukomesha kikamilifu vikwazo, na hata kama adui atafanya ukaidi, taifa la Iran litaendelea na njia yake ya maendeleo na ustawi kwa uwezo na taufiki ya Mwenyezi Mungu.
Sehemu ya mwisho ya hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imehusiana na matukio na machafuko ya hivi sasa katika eneo la Mashariki ya Kati.
Rais Rouhani amekutaja kuzusha makundi ya kueneza fitna na mifarakano kati ya Waislamu kwa kutumia majina matakatifu kama vile "Jihadi ya Kiislamu" ni mbinu chafu inayotumiwa na watu wasioutakia mema umma wa Kiislamu ili kuzuia kuenea na kupata nguvu ujumbe mbali mbali muhimu wa Mapinduzi ya Kiislamu kama vile demokrasia ya kidini, uhuru, kusimama imara na kuunda umma mmoja wa Kiislamu.
Ameongeza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatekeleza majukumu yake katika kuleta utulivu, amani na kupambana na ujinga, misimamo mikali, machafuko na vitendo vya kihayawani na inaamini kuwa umwagaji wa damu na kuua watu pamoja na ukosefu wa utulivu ni mambo ambayo hayana manufaa kwa mtu yeyote yule.
Mwishoni mwa hotuba yake, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa: Serikali yake inayahesabu mafanikio yake yote kuwa yanatokana na ushirikiano mzuri, umoja na mshikamano wa wananchi chini ya kivuli cha miongozo ya busara ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na taufiki na auni ya Mwenyezi Mungu pamoja na msaada wa Imam wa Zama, Imam Mahdi (Mwenyezi Mungu ahatakishe kudhihiri kwake kutukufu).
 
< Nyuma   Mbele >

^