Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Kiongozi Muadhamu Aonana na Viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu na Mabalozi wa Nchi za Kiislamu Chapa
29/07/2014
Supreme Leader's Sermons at Eid ul-Fitr PrayersKiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei leo ameonana na mamia ya viongozi na wananchi wa matabaka mbali mbali pamoja na mabalozi wa nchi za Kiislamu walioko nchini Iran na kuwataka Waislamu wote kuwasaidia wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina akisisitiza kuwa: Ulimwengu wa Kiislamu unapaswa kuweka pembeni hitilafu zilizomo ndani yake na Waislamu watumie nguvu zao zote kuwadhaminia mahitaji yao wananchi wa Ghaza ili sambamba na kukabiliana na jinai zisizo na kifani za Wazayuni, zijiweke mbali pia na waungaji mkono wa Wazayuni hususan Marekani na Uingereza.
Aidha ametoa mkono wa baraka na fanaka kwa mataifa yote ya Waislamu duniani kwa mnasaba wa sikukuu ya Idul Fitr akisema kuwa sikukukuu hii ni sikukuu ya umma mzima na kuongeza kuwa: Inasikitisha kuona kuwa, tofauti na yanavyosisitiza mafundisho ya Uislamu, leo hii misimamo ya kisiasa na misukumo ya uroho wa madaraka imeutumbukiza kwenye mizozo na mifarakano umma mzima wa Kiislamu.
Ayatullah Udhma Khamenei ametoa mwito kwa viongozi wa nchi za Kiislamu kuachana na misukumo hiyo ya kisiasa na kuungana pamoja kuunda umma wa Kiislamu ulioshikama na wenye nguvu na uwezo mkubwa na kusisitiza kuwa: Iwapo uroho wa madaraka, kuwa tegemezi na ufisadi usingelileta utengano katika ulimwengu wa Kiislamu, basi dola lolote la kibeberu lisingelithubutu kufanya uchokozi wa aina yoyote ile katika nchi za Kiislamu na wala usingeliweza kuzilazimisha tawala wa nchi hizo kufanya unayoyataka.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameutaja ujuba na jeuri inayofanywa na Wazayuni ya kuua watu kwa umati huko Ghaza kuwa unatokana na mizozo iliyopo katika ulimwengu wa Kiislamu na kuongeza kuwa: Uchujaji mkubwa wa habari ulioko katika nchi za Magharibi unazuia wananchi wa huko kujua ukubwa wa jinai zinazofanywa na Wazayuni huko Ghaza lakini pamoja na hayo jinai hizo ni kubwa na ni za kutisha kiasi kwamba hata pale vyombo vya Magharibi vinapoakisi sehemu ndogo tu ya jinai hizo, zinaziumiza na kuzishitua nyoyo za watu wa mataifa yasiyo ya Waislamu na kuwafanya wamiminike barabarani kulaani jinai hizo.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria upweke walio nao wananchi wasio na sehemu ya kukimbilia wa Ghaza na kuongeza kwamba: Ujumbe wetu wa wazi ni kuwa, tawala za nchi za waislamu zinapaswa kuwasaidia watu wanaodhulumiwa na zinapaswa kuonesha kivitendo kuwa, ulimwengu wa Kiislamu hauwezi kukaa kimya mbele ya dhulma na ukandamizaji.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Ili kulifanya lengo hilo lifikiwe tawala zote za nchi za Waislamu zinapaswa kuweka pembeni tofauti zao za kisiasa na zisizo za kisiasa na zote kwa pamoja ziunganishe nguvu zao kuwasaidia watu wanaodhulumiwa ndani ya makucha ya mbwa mwitu Mzayuni anayejifakharisha kumwaga damu za watu wasio na hatia.
Pia amesema, kuna wajibu wa kuyaingiza kwenye ajenda kuu majukumu mawili ya kimsingi katika ulimwengu wa Kiislamu ambayo mosi ni kuwadhaminia wananchi wa Ghaza mahitaji yao muhimu ya lazima na pili kuchukua msimamo mkali na unaotakiwa katika kupambana na utawala unaomwaga damu za watu pamoja na waungaji mkono wake.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia namna wananchi wanamuqawama waliokumbwa na masaibu mengi wa Ghaza wanavyohitajia mno bidhaa za chakula, maji, madawa na mahitaji mengine ya hospitalini na kujengwa upya nyumba na makazi yao akiongeza kuwa: Taifa la Palestina linahitaji kupewa silaha ili liweze kujilinda.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, kwa mara nyingine tena amezikhutubu tawala za nchi za Waislamu akisema: Njooni tushirikiane na tuunganishe nguvu zetu kuwasaidia wananchi wa Ghaza na kupambana na masaibu wanayotwishwa na Wazayuni. Njooni tuunganishe pamoja nguvu zetu katika kutekeleza majukumu yetu ya kidini na kibinadamu.
Amekutaja kupambana na kukabiliana na wasababisha wa dhulma ya kihistoria huko Ghaza kuwa ni jukumu jingine la ulimwengu wa Kiislamu na kuongeza kuwa: Watenda jinai Wazayuni na waungaji mkono wao wanatafuta visingizio vya kila namna kujaribu kuhalalisha mauaji yao ya kutisha ya watoto wachanga na malaika wa Mungu huko Ghaza na kwamba hicho ndicho kilele na ukomo wa ukhabithi na ukosefu wao wa haya na soni.
Ayatullah Udhma Khamenei amekitaja kitendo cha madola ya kibeberu zikiwemo Marekani na Uingereza cha kuunga mkono wazi wazi jinai za Wazayuni huko Ghaza na hatua ya jamii ya kimataifa ya kuunga mkono jinai hizo kwa njia isiyo ya moja kwa moja au ya moja kwa moja ukiwemo Umoja wa Mataifa na kwa njia hiyo madola na jamii hizo za kimataifa kushiriki katika jinai hizo za Wazayuni wafyonza damu za watu.
Ameongeza kuwa: Mataifa ya Waislamu na tawala za nchi za Waislamu zina jukumu la kutangaza kujibari na kujiweka mbali kwao na waungaji mkono wa jinai zinazoendelea kutendwa na Tel-Aviv na ikiwezekana wawasusie kiuchumi na kisiasa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelipongeza taifa la Iran kutokana na msimamo wake usiotetereka wa kuwaunga mkono wazi wazi wananchi wa Ghaza na kusimama kwao imara katika kukabiliana na jinai na ukhabithi wa kupindukia wa Wazayuni ameongeza kuwa: Katika Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani, walimwengu walisikia sauti kubwa kutoka Iran ya kuwaunga mkono watu wanaodhulimiwa na mbali na uungaji mkono huo mkubwa wa wananchi wa Iran kwa watu wanaodhulumiwa, taifa hili pia liko tayari kufanya lolote linaloweza kwa uimara kamili katika kuwasaidia wanyonge na watu wanaodhulumiwa.
Mwanzoni mwa mkutano huo, Hujjatul Islam Walmuslimin Hasan Rouhani, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa hotuba fupi na kutumia fursa hiyo kutoa mkono wa idi na kusema kuwa idi hii ni idi ya "fitra" na maumbile ya kibinadamu na ndiyo sikukuu inayosherehekewa mno na Waislamu.
Rais Rouhani amegusia pia matukio ya Ghaza na kusisitiza kuwa: Kufunga saumu hakukubaliani na matendo maovu na kunyamazia kimya jinai za wapenda vita na watenda jinai.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa eneo la Mashariki ya Kati na ulimwengu wa Kiislamu hivi sasa unateseka kwa madonda ndugu mawili ya kensa. Donda ndugu la kwanza ni utawala wa Kizayuni ambao hivi sasa unafanya ukatili na uharibifu mkubwa wa kuzigeuza jangwa ardhi za mizaituni na kuua kinyama na kikatili watoto wadogo wasio na hatia.
Aidha ameashiria donda ndugu la pili la kensa kuwa ni kuufanya Uislamu kuwa dini ya kupigania ukhalifa na ukubwa, donda ndugu ambalo linapelekea Waislamu kuuliwa bila ya sababu. Amesema: Utafiti wote unaonesha kuwa, chanzo cha madonda ndugu yote hayo mawili ni sehemu moja.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vile vile ameutaja ukatili unaoendelea kufanywa hivi sasa na Wazayuni huko Ghaza kuwa ni jinai dhidi ya binadamu na kusisitiza kwamba: Jamii na taasisi zote za kimataifa zinazojigamba kutetea haki za binadamu, zinapaswa kuandaa mazingira ya kupandishwa kizimbani na katika mahakama za kimataifa watenda jinai ambao siku baada ya siku ukhabithi wao unazidi kudhihirika.
Rais Rouhani ameongeza kuwa: Ili kuweza kutatua mgogoro huo mkubwa, ulimwengu wa Kiislamu hauna njia nyingine isipokuwa kuungana na kuwa kitu kimoja, kuutangaza Uislamu wa kweli na kujiepusha na misimamo mgando na isiyoheshimu wala kuvumilia fikra za watu wengine.
Aidha amesema, stratijia na mkakati wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kimataifa ni kuleta amani na uadilifu na katika ulimwengu wa Kiislamu ni kuleta udugu na mshikamano pamoja na kuunda umma mmoja wa Kiislamu.
Mwishoni mwa hotuba yake, Rais Hasan Rouhani amesisitiza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inafanya jitihada zake zote kuhakikisha kuwa kunapatikana utulivu na amani katika eneo hili na kuzuia kutokea mauaji na umwagaji wa damu sambamba na kupigania amani na uadilifu katika eneo zima la Mashariki ya Kati na ulimwengu mzima wa Kiislamu kwa msaada na taufiki ya Mwenyezi Mungu. Amesema ana imani jambo hilo litafanikiwa kwa msaada wa Mwenyezi Mungu na kwa mwamko na kuwa macho pamoja na mshikamano kati ya Waislamu.
 
< Nyuma   Mbele >

^