Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Aonana na Wanafunzi wa Vyuo Vikuu Chapa
23/07/2014
Supreme Leader Meets with StudentsKaribu wanafunzi elfu moja wa Vyuo Vikuu na vituo vya elimu ya juu nchini Iran leo jioni (Jumatano) wamekwenda kuonana na Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu. Katika mkutano huo uliodumu kwa muda wa masaa mawili, wanachuo hao wameweza kutoa madukuduku, maswali na maombi yao pamoja na kuwasilisha mitazamo ya jamii ya wanachuo wa Iran kwa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu. Baada ya hapo, Kiongozi Muadhamu ametoa hotuba muhimu ambayo ndani yake amejibu madukuduku, maombi na mitazamo yao kwa kutilia mkazo vipaumbele na masuala tofauti ya ndani ya Iran na ya kieneo.
Baada ya kuwasikiliza kwa makini wawakilishi hao wa vyama, jumuiya na makundi mbali mbali ya wanachuo na ambao wamezungumza kwa muda wa dakika 90, Ayatullah Udhma Khamenei amepongeza moyo wa wanachuo hao uliojaa hamasa, moyo wa udadisi, moyo wa kuzingatia mambo kwa kina na moyo wao wa kukosoa na kukubali kukosolewa na wakati huo huo wa kujali majukumu. Aidha amebainisha vyanzo na sababu za matukio ya kutisha na ya kusikitisha mno ya Ghaza, Palestina, na kusisitiza kuwa: Jinai hizi ambazo hata akili haiwezi kuzifikiria, ndio uhalisia na dhati ya utawala wenye sifa za mbwa mwitu na muuaji wa watoto ambao dawa yake pekee ni kuangamizwa na kufutwa kabisa. Tab'an ili kuweza kufikia huko inabidi mapambano na muqawama usiotetereka wa Wapalestina na kuenea muqawama huo hadi katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan ndiyo njia pekee ya kukabiliana na utawala huo wa kihayawani na wa kinyama. Kama ambavyo uungaji mkono wa kijuba wa Marekani na Magharibi kwa jinai za Wazayuni nao unapaswa uchukuliwe kuwa ni uzoefu na funzo muhimu katika kuunda mtazamo na njia za kukabiliana na Uzayuni wa kimataifa na ni vivyo hivyo kwamba funzo hilo inabidi tulipate sisi sote katika kuamiliana kwetu na Magharibi na tutambue kuwa huo ndio uhakika na dhati ya Marekani na kwamba wananchi wa Iran katika Siku ya Quds watajitokeza kwa wingi wa ajabu kuonyesha kuwa hawatetereki katika kuwaunga mkono watu wanaodhulumiwa na pia kuwatangazia tena walimwengu kuwa wao ni maadui wakubwa wa madhalimu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria masaibu yanayoendelea kuwakumba wananchi madhulumu wa Ghaza na kuongeza kuwa: Matukio hayo ni mfano halisi wa siasa za kupenda machafuko wazi wazi na za mkono wa chuma ambazo utawala usio halali na pandikizi wa Kizayuni umekuwa ukizitumia mara kwa mara kwa muda wote huu wa miaka 66 ya umri wake na tena unajifakharisha kijuba na kijeuri kwa siasa zake hizo za kihayawani.
Vile vile amesisitiza kwamba: Kwa hakika ni kama alivyokuwa akisema Imam Khomeini (quddisa sirruh) kwamba Israel ni lazima iangamizwe. Tab'an kuangamizwa Israel ambako ndiyo njia pekee ya utatuzi wa kweli wa jakamoyo hili, hakuna maana ya kuwaangamiza Mayahudi wa kawaida katika eneo hili (la Mashariki ya Kati) bali jambo hilo lina njia yake ya kimantiki, ya busara na inayoweza kutekelezeka kivitendo ambapo tayari Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeshaipa jamii ya kimataifa utatuzi wa mgogoro huo.
Ameongeza kuwa: Kwa mujibu wa njia hiyo ya kimantiki inayokubaliwa na mataifa yote, watu wanaoishi katika ardhi hizo za Palestina na wenyeji hasa wa eneo hilo wafanyiwe kura ya maoni ya kuamua aina ya utawala wanaoutaka na kwa njia hiyo utawala pandikizi wa Kizayuni utafutwa katika uso wa dunia.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Tab'an hadi kufikia wakati huo wa kuangamizwa kikamilifu utawala huo wenye moyo wa jiwe unaoua watu kikatili, njia pekee ya kuweza kukabiliana na utawala huo angamizi ni kupambana nao vilivyo kupitia muqawama usiotetereka na hasa wa silaha.
Ameongeza kuwa: Mtu asifanye kosa kudhani kuwa kama makombora ya Ghaza yasingelikuwepo, basi utawala wa Kizayuni ungelirudi nyuma na usingelifanya jinai na uadui wake katika ukanda huo, kwani katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan hakuna makombora wala risasi na silaha pekee waliyo nayo wananchi wa huko ni mawe, lakini huko pia utawala wa Kizayuni unaua watu na kuwadhalilisha vibaya.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria namna Wazayuni walivyomdhalilisha na kumpa sumu Yasir Arafat na kusema: Utawala unaozikalia kwa mabavu ardhi za Palestina hauwajali hata watu waliokubali kufanya mapatano na utawala huo, hivyo ni kupitia kupambana vilivyo Wapalestina na utawala huo ndiko kunakoweza kuleta uwezekano wa kuuvunja nguvu na kuurudisha nyuma utawala huo dhalimu.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria pia njama za Wazayuni za kusitisha vita huko Ghaza na kusema: Utawala ambao unafanya jinai ambazo akili ya mwanadamu inashindwa hata kuzitasawari na kuzifikiria, umefikishwa pabaya na muqawama imara wa Wapalestina na sasa unapapatika kutafuta njia ya kujinasua ambapo jambo hilo linazidi kuthibitisha kuwa Wazayuni hawaelewi lugha nyingine isipokuwa ya kutumia nguvu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Ni kwa kuzingatia uhakika huo ndio maana sisi tukaamini kuwa, Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan nao unabidi ubebe silaha kama ulivyofanya Ukanda wa Ghaza na kwamba watu wenye imani na mustakbali bora wa Palestina waingie katika jambo hilo ili waweze kuwapunguzia mashaka na masaibu wananchi wa Palestina kupitia juhudi zao imara na udhaifu wa Wazayuni.
Amesema, kuwaunga mkono kisiasa wananchi wa Ghaza ni jukumu la mataifa yote ya Waislamu na ya wasio Waislamu na huku akiashiria namna mataifa ya dunia yalivyoonyesha chuki na hasira zao kwa utawala wa kihayawani wa Israel amesisitiza kuwa: Inshaallah katika Siku ya Quds dunia itaona wimbi kubwa mno la wananchi wa Iran katika maandamano ya siku hiyo na taifa la Iran litaonyesha kuwa nia na hamasa yao ya kuiunga mkono Palestina bado iko hai na bado ina nguvu katika ardhi hii ya Kiislamu.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria nara iliyotolewa na wafanya fitna nchini Iran ambao walikuwa wakisema "si Ghaza si Lebanon" kuashiria kuwa Iran isiiunge mkono Palestina wala Ghaza na kusema kuwa, kuna kijikundi cha watu kilitumia nara hiyo ili kupotosha uhalisia wa taifa la Iran, lakini wananchi wa Iran hawakuwapa mwanya watu hao na katika siku ya Ijumaa Inshaallah, wananchi wa taifa hili wataonyesha kwa mara nyingine tena kuwa daima wako pamoja na watu wanaodhulumiwa na ni maadui wakubwa wa madhalimu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekosoa vikali mno uungaji mkono wa kijuba na usio na haya wa mabeberu wakiongozwa na Marekani kwa jinai na ukatili usioelezeka unaofanywa na Wazayuni dhidi ya Wapalestina na kusema kuwa: Matukio ya Ghaza yanaumiza na kutia majonzi makubwa, lakini jambo muhimu hapa ni kuyaangalia kwa kina mambo yanayofanyika hivi sasa Ghaza na kuzingatia kwa kina misimamo ya mabeberu katika matukio hayo.
Ameongeza kuhusu suala hilo kwamba: Baadhi ya tawala za Magharibi na hasa Marekani na Uingereza khabithi wanaunga mkono wazi wazi jinai ambazo hakuna mwanadamu yeyote mwenye akili salama anayeweza kuziunga mkono na kwamba Rais wa Marekani licha ya kuona mauaji yote haya ya watoto wadogo na uharibifu mkubwa unaofanywa na Wazayuni huko Ghaza pamoja na mateso na masaibu makubwa mno waliyotwishwa wakazi wa Ukanda huo, anajitokeza hadharani na kuzungumza kwa kejeli kubwa kwamba Israel ina haki ya kulinda usalama wake! Lakini je, Wapalestina wao hawana haki ya kulinda usalama wao na kulinda maisha yao?
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Viongozi wa nchi za kiistikbari hawaelewi kuwa wanajitia aibu na kuzidunisha nchi zao wanaposimama kutetea jinai za Wazayuni makatili waharibifu mbele ya mataifa ya walimwengu na kwa hakika historia itatoa somo kubwa sana kwao kutokana na kushiriki kwao katika jinai hizo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia kwa kina sababu za ujuba na jeuri hizo za Wamagharibi akisema: Kuunga mkono jinai za Wazayuni ndio msingi mkuu katika mfumo wa demokrasia ya kiliberali ambao hauchungi wala kuheshimu hata chembe matukufu wa kiakhlaki kwani ni mfumo ambao hauna chembe ya hisia za kibinadamu.
Baada ya hapo ametoa muhtasari wa maelezo yake kuhusu kadhia hiyo akisisitiza kuwa: Huu ndio uhakika na uhalisia wa Marekani ambayo inapingana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika masuala tofauti. Tunapaswa kuzidi kuielewa dhati ya Marekani kupitia jambo hili na kuitambua kwetu huko liwe funzo muhimu katika kuamiliana kwetu na Marekani na tulifanye suala hilo kuwa nguzo ya misimamo ya taifa letu, wanafunzi wetu wa Vyuo Vikuu, wasomi na wanafikra wetu na kila mmoja wetu katika kuamiliana na Marekani.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu vile vile amesema: Misimamo na vitendo vya mababeru, na dhulma kubwa wanayofanyiwa wananchi wa Ghaza inaonesha wazi kuwa mabeberu hawajali kabisa utu, wala haki za binadamu na wala ubinamu na kwamba kila wanapozungumzia uhuru na haki za binadamu huwa wanaufanyia istihzai na kejeli tu uhuru na haki hizo za binadamu.
Aidha kwa mara nyingine tena amesisitiza kuwa: Maneno haya siyasemi kwa kutaka yawe nasaha kwa viongozi wa Marekani bali nasaha hizi nazitoa kwa ajili yetu sisi wenyewe ili tujue nini tunapaswa kufanya na tuelewe katika uchanganuzi wetu wa mambo kwamba ni watu wa namna gani waliotukabili.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Nara na kaulimbui zinazosikika katika kila pembe ya dunia zikiilaani Marekani na Magharibi na ubeberu zinaakisi uhakika wa mambo ulivyo kuhusu hisia za walimwengu kuhusiana na Marekani lakini kuna baadhi ya watu wanafanya makosa; wanadhani kuwa nara na kaulimbiu hizo zinatokana na taasubu na hazina mantiki yoyote.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Kuweko msimamo na mtazamo ulio dhidi ya Marekani na dhidi ya Magharibi nchini Iran ni jambo la kimantiki kabisa lililotokana na uzoeufu na mahesabu sahihi.
Aidha ameashiria maneno aliyosemwa hivi karibuni wakati alipoonana na viongozi wa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na wafanyakazi nchini akisema: Kama tulivyowahi kusema huko nyuma, lengo kuu wa adui ni kuzilazimisha taasisi zetu zifanye makosa katika mahesabu yake, kwani kama mfumo wa mahesabu wa nchi utafanya makosa, basi hata data zake nazo hazitakuwa sahihi na hazitakuwa na faida yoyote kwa nchi hiyo.
Ayatullah Udhma Khamenei ameorodhesha baadhi ya uzoefu walioupata Wairani kutokana na vitendo na miamala ya Wamagharibi katika miongo kadhaa iliyopita akisema: Kuwaingiza madarakani watawala madikteta na madhalimu nchini Iran (kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu), kuikalia kwa mabavu Iran katika muongo wa 20, kupora utajiri wa mafuta wa Iran, kufanya mapinduzi ya kijeshi ya Mordad 28 (1336 - mwaka wa Kiirani wa Hijria Shamsia sawa na Agosti 19, 1953 wakati Marekani ilipofanya mapinduzi ya kijeshi nchini Iran ili kumrejesha madarakani mfalme wa wakati huo wa Iran, Mohammed Reza Shah Pahlavi), kumuunga kwa kila hali dikteta Mohammad Reza, kufanya kila njama ili kukwamisha ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, uungaji wa pande zote wa mabeberu kwa Saddam na makumi kwa makumi ya njama nyingine, ni uzoefu muhimu sana ambao umelifanya taifa la Iran kujua dhati na sura halisi ya Marekani. Hata hivyo wasomi wenye misimamo ya Kimagharibi kwa vile mahesababu yao yana matatizo, wanashindwa hata kuona uzoefu wote huo mchungu na hivyo wanashindwa kuchukua misimamo sahihi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekutaja kuhuishwa mantiki sahihi ndani ya taifa la Iran kuwa ni huduma kubwa sana iliyotolewa na Mapinduzi ya Kiislamu na kuongeza kuwa: Tofauti na linavyotaka taifa na wananchi wa Iran, kuna baadhi ya watu wanataka udhalilishaji ule ule waliokuwa wanafanyiwa wananchi wa Iran na Magharibi urejee katika masuala ya nchi yetu na kwa kweli kuna wajibu wa kupambana vilivyo na harakati hiyo na kusimama kidete kukabiliana na watu wa namna hiyo na kwa hakika kufanya hivyo ni jambo sahihi na la kimantiki kabisa.

 

Amma mwanzoni kabisa wa hotuba yake, Kiongozi Mudhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameutaja mkutano wake wa leo na wanafunzi wa Vyuo Vikuu kwamba ulikuwa mzuri na ulioonyesha moyo wa imani na hamasa, uchangamfu na mantiki walio nao vijana wa Iran na kuongeza kuwa: Masuala ambayo yamezungumwa leo na wawakilishi wa vyama na jumuiya za wanachuo yanazidi kuthibitisha kuwa huo ndio moyo walio nao wanafunzi wa Vyuo Vikuu nchini.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Inawezekana baadhi ya masuala yaliyosemwa hapa yasiwe ya kimantiki, au yasiwe sahihi au yasiyotekelezeka, lakini muhimu katika suala hili ni kuwepo roho na moyo wenye nguvu wa kudadisi na kujifunza mambo ndani ya wanafunzi wa Vyuo Vikuu na jambo hilo kwa kweli linatia moyo na kufurahisha sana.
Vile vile amesisitiza kuwa: Kijana mwanachuo anapaswa kuwa mdadidisi wa mambo, awe na malengo makubwa na hima ya hali ya juu, aweko tayari wakati wote kuingia katika medani ya vitu mbali mbali na ajue vizuri mambo ya nchi yake na Alhamdulillah kwa taufiki ya Mwenyezi Mungu hivi sasa jambo hilo linashuhudiwa ndani ya wanafunzi wa Vyuo Vikuu nchini Iran.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Tab'an, moyo wa udadisi na kukosoa mambo kati ya wanachuo unapaswa upambwe kwa sifa ya kuchunga maadili, kuwa na insafu na kuchunga mipaka ya kisheria pamoja na kujiepusha na kutamka maneno ambayo mtu hana elimu wala yakini nayo.
Ayatullah Udhma Khamenei amewakhutubu wanachuo akiwambia: Ni matumaini yangu kuwa roho na moyo huu wa kuhisi wajibu wa kutekeleza majukumu, kudadisi mambo, kukosoa na kukubali kukosolewa, mtaendelea kuwa nao hata wakati baadhi yetu watakapokuja kuwa viongozi wa nchi katika siku za usoni. Amesema: Inabidi muendelee kuwa na moyo huo huo kwani kama mtakuwa hivyo, nchi itaokoka.
Vile vile ameashiria maombi ya wanachuo ya ulazima wa kuweko muongozo katika mfumo mzima wa kielimu nchini kuelekea kwenye kulitia nguvu suala la kujishughulisha na elimu zenye manufaa kwa taifa na kwa ajili ya kutatua matatizo yaliyopo katika jamii na kuongeza kuwa: Leo hii jitihada za kielimu nchini Iran na katika Vyuo Vikuu nchini ni jitihada zilizo hai, zilizopata mafanikio makubwa na zinazostahiki kupongezwa. Amma jitihada hizo za kielimu zinapaswa kuwa ni utangulizi tu wa kuwezesha kupatikana utatuzi wa kweli wa mambo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Kusambaza makala za kielimu katika mitandao yenye itibari ya kielimu duniani ni hatua ya kielimu inayopaswa kupongezwa, lakini kitu kinachotakiwa baada ya yote hayo ni kufanya kazi za kielimu kwa kuzingatia mahitaji ya kielimu ya nchi yetu.
Kuwepo mawasiliano na mfungamano baina ya mbinu ya kusimamia masuala ya kiuchumi pamoja na zile za kusimamia masuala ya kiutamaduni katika jamii ni suala jengine walilolisisitizia wawakilishi hao wa wanafunzi wa Vyuo Vikuu ambapo Ayatullah Udhma Khamenei ametoa maelezo kuhusu jambo hilo akisema: Tunakubali kuwa inawezekana mbinu za kusimamia na kuendesha masuala ya kiuchumi zinaweza kuwa na taathira katika misimamo na mikakati ya kiutamaduni, lakini jambo lililo muhimu zaidi hapa ni kuwa inabidi mtazamo na msimamo wa kiutamaduni uzingatiwe zaidi kwani ndio unaopaswa kuzingatiwa kwanza katika ngazi zote.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria masuala mengine mbali mbali yaliyozungumziwa na wanachuo mbali mbali katika mkutano huo kuhusiana na maudhui tofauti na kuyatolea ufafanuzi na majibu kwa muhtasari.
Vile vile Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewausia wanachuo kujenga tabia ya kutafakari vizuri mambo na kutoamua masuala yao kwa hamasa zisizo na busara au kwa kufuata mkumbo na pia akawaambia: Si sahihi hata kidogo kuustaajabia upande wa upinzani au kuwa na woga nao, bali inabidi watu waimarishe misingi yao mikuu na kutia nguvu misimamo yao na kuingia katika medani ya ushindani kwa uimara na nguvu kubwa ili kuulazimisha upande wa upinzani uwakubali na ushindwe kuwafumbia macho watu hao.
Mwanzoni mwa hotuba hiyo wawakilishi wa vyama na jumuiya mbali mbali za wanafunzi wa Vyuo Vikuu nchini Iran wametoa mitazamo, maombi na kuuliza maswali kuhusu masuala tofauti muhimu hasa yanayohusiana na nchi yao pamoja na mazingira yao ya masomo na Vyuo Vikuu.

 
< Nyuma   Mbele >

^