Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Kiongozi Muadhamu Aonana na Mafisa Wizara ya Mambo ya Nje, Mabalozi, Wawakilishi wa Iran Nje ya Nchi Chapa
13/08/2014
 Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, leo asubuhi, (Jumatano) ameonana na Waziri wa Mambo ya Nje, mabalozi na wakuu wa Vitengo vya Utamaduni vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vya nje ya nchi na kusema kuwa, taasisi ya kidiplomasia ya Iran ni mtetezi aliyeko mstari wa mbele wa malengo na manufaa matukufu ya taifa pamoja na rasilimali za Wairani.
Vile vile amebainisha sifa za kipekee ilizo nazo taasisi ya kidiplomasia ya Iran na udharura wa kuweko udiplomasia amilifu, erevu na unaoangalia mbali katika kipindi hiki muhimu mno cha kuvuuka kwenye mfumo mpya wa dunia, na ametoa maelezo muhimu kuhusiana na kutokuwa na faida miamala na mwingiliano na Marekani.
Amebainisha umuhimu wa kazi ya kidiplomasia kwa kusema: Udiplomasia unaofanyika kwa umakini n uweledi wa mambo, amilifu na wenye muono wa mbali unaweza kuliletea taifa manufaa muhimu ya kisiasa, kiuchumi, kibinadamu na kijamii. Udiplomasia huo kamwe hauwezi kusababisha kutokea vita vyenye hasara na hatari kubwa na uhakika huo unathibitisha uzito na nafasi ya taasisi ya kidiplomasia kiasi kwamba taasisi hiyo iko katika daraja ya kwamba uongozi wa nchi umo mikononi mwake.
Ayatullah Udhma Khamenei vile vile amesema kuwa, matukio ya miaka mingi sasa katika eneo la Mashariki ya Kati yanatilia nguvu uhakika huo na kuongeza kuwa: Madola ya kibeberu yanafanya njama za kudhamini manufaa yao ya kibeberu kupitia silaha na kutumia mabavu lakini njama hizo zimeshindwa. Hata hivyo kuna watu katika eneo hili wameweza kudhamini vizuri maslahi yao kwa kutumia hekima ya hali ya juu, busara na kwa kuchukua hatua zinazofaa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameitaja Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran kuwa ni jeshi la kidiplomasia lenye nidhamu la nchi na kuongeza kwamba: Ijapokuwa taasisi nyinginezo za nchi nazo zina taathira katika suala la siasa za nje, lakini Wizara ya Mambo ya Nje ndiyo yenye jukumu kuu na kubwa zaidi katika suala hilo kwani ni taasisi iliyopewa jukumu hilo na ni jeshi lenye nidhamu.
Vile vile amebainisha sifa na masharti inayotakiwa kuwa nayo taasisi ya kidiplomasia yenye mafanikio kuwa ni pamoja na kuanisha kwa kina na kwa uwazi kabisa malengo yake. Ameongeza kuwa: Baadhi ya malengo yana shabaha na malengo ya kitaifa, baadhi ya malengo hayo ni ya kiistratijia na ya kieneo na baadhi yake nyingine ni ya muda mfupi na muda maalumu na yanahusiana tu na hali mahsusi. Amesema, malengo yote hayo inabidi yawe ya kina na ya wazi katika hatua zake zote ili kila muhusika katika taasisi ya kidiplomasia aweze kutekeleza vizuri majukumu yake kwa uwazi na kwa umakini wa hali ya juu.
Ayatullah Udhma Khamenei amekutaja kuwa na mipangilio mizuri kuwa ni sharti jingine la udiplomasia wenye mafanikio na kuongeza kuwa: Inabidi mipangilio hiyo iratibiwe kwa kuzingatia malengo na kwa kutilia maanani uwezo uliopo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekutaja kuwa na nguvukazi inayofaa, yenye sifa zinazotakiwa na inayostahiki kufanya kazi hiyo kuwa ni sharti jingine la udiplomasia wenye mafanikio.
Ametoa ufafanuzi kuhusu maana ya watu waliotimiza masharti ya kufanya kazi ya kidiplomasia kuwa ni mfano wa watu wenye weledi na utambuzi wa kazi ya kidiplomasia, watu walio wepesi wa kufanya kazi kulingana na mazingira yaliyopo kwa kubadilisha hali hiyo kwa faida ya taifa, kutotetereka katika hali za dharura na wanaoshikamana vilivyo na malengo matukufu kiuaminifu na kiukweli.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa ufafanuzi kuhusu weledi na werevu wa kidiplomasia kwa kusema: Sifa hiyo inamfanya mtu kuwa na uwezo wa kutabiri vizuri shabaha na harakati za upande wa pili katika mazungumzo na kupangilia mambo yake na kuyatekeleza kivitendo kwa kuzingatia utabiri wake sahihi.
Ayatullah Udhma Khamenei ametoa ufafanuzi kuhusu maana ya umahiri, ujuzi na ustadi katika kazi za kidiplomasia kwa kusema kuwa ni kutumia kwa wakati unaofaa uwezo wa kubadilisha malengo na mipango kwa umakini wa hali ya juu na kuongeza kuwa: Maana nyingine ya sifa hiyo ni kuwa na ulaini wa kishujaa ambapo suluhu iliyofanywa na Imam Hasan al Mujtaba Alayhis Salaam ni mfano wa wazi kabisa wa suala hilo katika historia.
Ameongeza kuwa, kinyume kabisa na jinsi baadhi ya watu wanavyoifasiri sifa hiyo; ulaini wa kishujaa una maana iliyo wazi kabisa na mfano wake unatumika pia katika mashindano ya mieleka ambapo katika pambano la mieleka ambalo lengo la mwanamichezo ni kumshinda mpinzani wake ni kwamba moja ya sifa anazotakiwa kuwa nazo mwanamichezo ni kunyumbulika na kubadilika kulingana na hali kwani hata kama mtu atakuwa na nguvu nyingi lakini akashindwa kuwa mtu laini wa kuweza kubadilika kulingana na hali, basi atashindwa tu, lakini kama atatumia kwa pamoja sifa zote hizo mbili, kuwa laini na kuwa na nguvu, mwanamichezo huyo hufanikiwa kumpiga mweleka mpinzani wake na kumbwaga na kumbiringisha chini.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa ufafanuzi kuhusu suala la kushikamana kwa kina na kiukweli na kiuaminifu na shabaha na malengo matukufu kwa kusema: Kama mtu hatokuwa na imani wala kuyaamini kwa kina malengo anayoyapigania katika uga wa kidiplomasia, basi bila ya shaka yoyote hatoweza kufanikiwa katika kufanikisha malengo hayo.
Ayatullah Udhma Khamenei ameufananisha uwanja wa kidiplomasia na medani ya vita na kuongeza kuwa: Uhakika wa mambo ni kwamba medani ya kidiplomasia ni medani ya kutupa makucha na koleo na kama mtu atafanya jambo hilo bila ya kuwa na imani kamili na malengo yake, basi imma atashindwa hapo hapo au mwisho wa jambo lake, lakini atashindwa tu.
Kuwa na harakati nyingi na zisizosita ni sharti jingine ambalo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitolea ufafanuzi katika mambo ya lazima ya kazi za kidiplomasia zenye mafanikio. Ameongeza kwamba: Kuwa na harakati nyingi mno ni jambo la lazima lisilotenganishika kabisa na kazi ya kidiplomasia na inabidi suala hilo lizingatiwe na lipewe uzito wa hali ya juu sana.
Ayatullah Udhma Khamenei ameendelea na hotuba yake mbele ya Waziri wa Mambo ya Nje wa maafisa wa taasisi ya kidiplomasia ya Iran kwa kukitaja kipindi cha hivi sasa kuwa ni kipindi cha kupita katika mfumo mpya wa dunia na kuongeza kuwa: Mbali na madola yenye ushawishi wa jadi, hivi sasa yamejitokeza madola mapya katika mabara ya Asia, Afrika na Amerika ya Latini na kuingia katika medani hiyo na kwamba madola hayo nayo yanataka kuwa na nafasi muhimu katika mfumo mpya wa dunia.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Katika kipindi hiki, kuna udharura maradufu wa kuwa na udiplomasia wenye nguvu na makini na ni kwa sababu hiyo ndio maana leo hii kazi ya Wizara ya Mambo ya Nje ikawa nyeti zaidi kuliko huko nyuma.
Ameongeza kuwa: Kama katika kipindi cha hivi sasa taasisi ya kidiplomasia nchini itaweza kuwa na harakati bora, kuwa macho na kuwa makini zaidi katika kazi zake basi nafasi na umadhubuti wa Jamhuri ya Kiislamu katika makumi ya miaka inayokuja utakuwa mkubwa na muhimu sana katika mfumo mpya wa dunia, vinginevyo itashindwa kuwa na nafasi ya maana na inayotakiwa katika ulimwengu unaokuja mbele yetu.
Kuwinda fursa na kuzitumia vizuri na kwa njia sahihi, ni nukta nyingine iliyosisitiziwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika hotuba yake mbele ya wanadiplomasia waandamizi wa Iran.
Ameongeza kuwa: Mabadiliko katika eneo la Mashariki ya Kati na duniani kiujumla yanatokea kwa kasi sana na inabidi kuyafuatilia kwa kina na bila ya kuchelewa hata kidogo na kufanyia utafiti na uchanganuzi mara moja kila tukio na kila jambo linalotokea ili kwa kutumia harakati ya hali ya juu na kuelewa malengo ya tukio hilo, tuweze kuchukua na kubainisha kwa uwazi msimamo wetu kuhusiana na tukio hilo.
Hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu mbele ya viongozi wa taasisi ya kidiplomasia ya Iran imeendelea kwa kutilia mkazo malengo na siasa kuu za Iran ambazo inabidi zizingatiwe mtawalia na bila ya kusita na viongozi na maafisa wa saisa za nje nchini.
Hapo hapo amesisitizia wajibu wa kuiimarisha na kuitangaza vilivyo mantiki ya Jamhuri ya Kiislamu yaani demokrasia ya kidini na kusema kuwa jambo hilo ndilo lengo kuu na pia amewalenga moja kwa moja wanadiplomasia wa Iran kwa kuwaambia: Ingieni katika kazi ya kufanikisha lengo hilo bila ya pupa kwani ni jambo lisilo na shaka hata kidogo kwamba, lengo hilo linaweza kufanikishwa ipasavyo hasa katika ulimwengu wa Kiislamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekutaja kukuza na kuzitangaza ipasavyo sifa za kipekee za kazi ya kidiplomasia ya Iran kuwa ni lengo jingine muhimu la maafisa wa siasa za nje za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Ameongeza kuwa: Kushikamana mtu binafsi na kijamii na misingi na mipaka ya kisheria katika nyuga mbali mbali za kidiplomasia na kutotishwa wala kugopeshwa na haiba na majivuno ya madola makubwa likiwemo dola la Marekani ni miongoni mwa sifa za kipekee za kazi za kidiplomasia za Iran na inabidi sifa hiyo izingatiwe na ipewa umuhimu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Kutoogopeshwa na madola ya kibeberu, kulikokuja baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran ni moja ya sifa kuu katika siasa za mambo ya nje za Jamhuri ya Kiislamu na kwamba sifa hiyo ya aina yake imeyavutia mataifa mengine na pia wanasiasa wa dunia ni sawa tu wanasiasa hao wakiri jambo hilo au wafiche, lakini siasa hizo za Tehran zimewalazimisha wanasiasa hao waliheshimu na kulisifu taifa la Iran kutaka na kukataa.
Ayatullah Udhma Khamenei amekuta kuwatetea waziwazi, kikweli kweli na bila ya kutetereka; wanyonge na watu wanaodhulumiwa, kuwa ni sifa nyingine ya kipekee ya kazi za kidiplomasia za Iran na kuongeza kuwa: Sifa hiyo imejidhihirisha kwa uwazi zaidi katika kulihami na kulitetea taifa na wanamapambano wa Palestina, Lebanon na sehemu nyinginezo mfano wa hizo katika kipindi chote hiki cha baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekutaja kuupinga vikali mfumo wa kibeberu kuwa ni sifa nyingine ya wazi ya siasa za kigeni za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuongeza kwamba: Viongozi wetu wameonesha ujasiri na kutokuwa na woga wala muhali mbele ya madola ya kibeberu na hasa Marekani katika sehemu yoyote ile duniani.
Ayatullah Udhma Khamenei amekutaja kulindwa na kudhaminiwa manufaa ya taifa kuwa ni miongoni mwa malengo ya pamoja ya taasisi zote za kidiplosia duniani na kuongeza kuwa: Katika taasisi ya kidiplomasia ya Iran pia, mbali na kufanyika jitihada za kudhamini na kulinda manufaa ya taifa, suala la kulinda maliasili za taifa pia ni muhimu sana kwani kama tutapoteza maliasili ya taifa basi taasisi ya kidiplomasia itabaki bila ya kinga na wakati huo haitawezekana kulinda na kudhamini manufaa ya taifa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameutaja utambulisho wa kitaifa, utambulisho wa Kiislamu, wa kimapinduzi na wa kihistoria kuwa ni rasilimali za taifa za Wairani na kuongeza kwamba: Uhuru ulioletwa na Mapinduzi ya Kiislamu, dini, taifa la waumini, vijana wanamapinduzi, msimamo usitetereka mbele ya madola yanayopenda makuu, wasomi na wataalamu, watu wenye vipaji na harakati za kielimu ni miongoni mwa rasilimali za taifa la Iran ambazo inabidi zilindwe katika kazi za kidiplomasia ili kwa kulindwa rasilimali hizo, ndipo iwezekane kulindwa na kuhifadhiwa manufaa na maslahi ya taifa.
Katika sehemu ya mwisho ya hotuba yake kwenye mkutano huo, Ayatullah Udhma Khamenei amezungumzia suala la miamala na mwingiliano na mataifa ya dunia.
Ametilia mkazo matamshi ya siku mbili zilizopita ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu mbele ya mabalozi na wafannyakazi wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran kuhusiana na kuwa na miamala na maingiliano na dunia nzima. Hata hivyo ameongeza kuwa: Madola mawili yanavuliwa katika maingiliano na miamala hiyo, utawala wa Kizayuni na Marekani.
Ayatullah Udhma Khamenei ametoa dalili na ushahidi kadhaa wa kutilia nguvu maneno yake kuhusu kutokuwa na faida kuwa na maingiliano na Marekani akisema: Uhusiano na Marekani na kufanya mazungumzo na nchi hiyo, ukiachilia mbali katika masuala maalumu, si tu hakuna faida yoyote kwa Jamhuri ya Kiislamu, bali hata kuna madhara kwake na kwamba ni mtu gani mwenye akili zake timamu anayeweza kujiingiza katika mambo yasiyo na faida kwake!?
Ameongeza kuwa: Kuna baadhi ya watu wanajaribu kuonesha kwamba, kama tutakaa katika meza ya mazungumzo basi matatizo mengi yatatuka. Tab'an sisi tulikuwa tunajua kuwa dhana hiyo si sahihi, lakini matukio ya mwaka mmoja uliopita - kwa mara nyingine tena na tena - imethibitisha ukweli huo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kwamba: Huko nyuma hakukuwa na uhusiano wowote baina ya viongozi wa nchi yetu na viongozi wa Marekani, lakini katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita na kutokana na masuala nyeti na muhimu sana ya nyuklia na uzoefu uliotajwa kuwa utapatikana katika mazungumzo hayo ilikubaliwa kuwa viongozi wa nchi yetu wawe na mawasilisano na viongozi wa Marekani, wakutane nao na wafanye mazungumzo nao kwa daraja na kiwango maalumu kilichoainishwa lakini pamoja na hayo hakuna kitu chochote cha maana kilichopatikana katika mazungumzo hayo, bali hata msamiati unaotumiwa na Wamarekani kuhusiana na Iran umekuwa mkali zaidi, wa kejeli na madharau zaidi na Wamarekani wamekuwa na tamaa na matarajio ya kupata mambo makubwa zaidi katika vikao vya mazungumzo na mimbari zao za umma.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameendelea kuzungumzia suala hilo kwa kuashiria kuongezeka vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran na kusema kuwa: Si tu kwamba Wamarekani hawajapunguza uadui wao kwa taifa la Iran, bali hata wameongeza vikwazo vyao dhidi ya taifa hili! Tab'an wanasema kuwa vikwazo hivyo si vipya, lakini ukweli wa mambo ni kuwa vikwazo hivyo ni vipya na kwamba hata mazungumzo kuhusiana na vikwazo nayo hayakuzaa matunda yoyote.
Amesema: Tab'an sisi hatupingi kuendelea mazungumzo ya nyuklia na kwamba kazi ambayo imeanzishwa na Dk Zarif (Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran) na timu yake hadi hivi sasa imekwenda vizuri na inaendelea vizuri, lakini pia huo ulikuwa ni uzoefu mwingine muhimu ketu sisi sote kwamba tuelewe kuwa, kukaa pamoja na Wamarekani na kuzungumza nao, hakuna taathira ya aina yoyote ile katika kupunguza uadui wao, na ni jambo ambalo halina faida kabisa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia madhara yatokanayo na kufanya mazungumzo na Wamarekani kwa kusema: Mazungumzo hayo yanawafanya watu wa mataifa mengine na tawala za nchi nyingine kututuhumu kuwa tunatapatapa na Wamagharibi wanatumia propaganda zao kubwa sana kupandikiza fikra kwa walimwengu kuwa Jamhuri ya Kiislamu imekuwa na siasa za nyuso mbili na haijui cha kufanya.
Ameyataja madhara mengine ya kukaa na kuzungumza na Marekani kuwa ni kuandaa uwanja wa kupata tamaa Wamarekani na kuwa na matarajio makubwa zaidi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa muhtasari wa hotuba yake kwa kubainisha wazi kuwa, muamala na utawala wa Kizayuni ni suala ambalo halimo kabisa katika hesabu kwani haliwezekani kabisa na kuhusu Wamarekani amesema: Madhali hali iliyopo hivi sasa yaani uadui wa Marekani na matamshi ya chuki ya serikali na Congress ya Marekani yataendelea kuwepo dhidi ya Iran, kuwa na maingiliano na kufanya muamala na Wamarekani nako kutaendelea kuwa ni jambo lisilowezekana kabisa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia namna mataifa ya dunia yanavyozidi kuichukia Marekani kutokana na kushirikiana kwake na utawala wa Kizayuni kufanya jinai za kutisha huko Ghaza na kuongeza kuwa: Hakuna mtu yeyote duniani ambaye anaweza kusema kuwa Marekani haihusiki katika jinai na mauaji ya kizazi yanayofanya utawala ghasibu, wenye sifa za mbwa mwitu, katili, muuaji, kafiri na dhalimu wa Kizayuni huko Ghaza, hivyo Wamarekani hivi sasa wako katika nafasi dhaifu na mbaya zaidi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia hali ya siku za sasa hivi ya wananchi madhlumu wa Ghaza na kusisitiza kuwa: Mantiki ya Wapalestina katika suala la kusimamisha vita ni mantiki sahihi. Wapalestina wanasema kuwa, kukubali kusimamisha vita kuna maana ya kwamba utawala unaofyonza damu za watu na katili wa Kizayuni uliotenda jinai kubwa kiasi chote hicho uachwe vivi hivi tu na hali iachwe iendelee kuwa vile vile ilivyokuwa kabla ya mashambulizi hayo yaani kushadidishwa mzingiro na mashinikizo bila ya mabadiliko yoyote.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Kama wanavyosema Wapalestina, baada ya utawala wa Kizayuni kufanya jinai zote hizo, inabidi uwepo uwezo wa kukomesha kuzingirwa Ukanda wa Ghaza na hakuna mtu yeyote mwenye insafu ambaye ataweza kupinga matakwa hayo ya haki ya Wapalestina.
Mwishoni mwa hotuba yake, Ayatullah Udhma Khamenei amezungumzia kadhia ya Iraq na kusema: Inshaallah kwa kutangazwa Waziri Mkuu mpya huko Iraq, itawezekana kuondolewa vizuizi vya kuundwa serikali mpya ili iweze kufanya kazi na kutoa somo na funzo zuri kwa watu ambao walikuwa na nia ya kueneza fitna nchini Iraq.
Vile vile amewaombea dua za kupata taufiki katika kazi zao viongozi na wahusika wote wa kazi za kidiplomasia nchini akiongeza kuwa: Wakati wote ninamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu ampe taufiki Waziri wa Mambo ya Nje na wafanyakazi wenzake wote katika wizara hiyo.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Dk Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa ripoti fupi kuhusu kongamano la mabalozi na wakuu wa vitengo vya utamaduni vya Jamhuri ya Kiislamu nje ya Iran akitalitaja lengo la kufanyika kongamano hilo kuwa ni kubadilishana mawazo na fikra, kutathnini na kuweka sawa siasa za nje kwa mujibu wa hati zitokazo juu na kufaidika na miongozo ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Vile vile amemshukuru Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa uungaji mkono wake na kukitaja kipindi cha hivi sasa kuwa ni muhimu sana katika historia ya taifa la Iran akiongeza kuwa: Hali ya hivi sasa kimataifa ni tepetepe, vyanzo vya nguvu vimekuwa vingi na uwezekano wa madola mapya kuwa na taathira duniani nao umeongezeka na hayo ni miongoni mwa mambo yanayotawala duniani hivi sasa na katika eneo la Mashariki ya Kati.
Bw. Zarif ameongeza kuwa: Jukumu la taasisi ya siasa za nje ni kutumia vizuri fursa za kipekee zilizozopo ndani na nje ya nchi na kuongeza kuwa: Nguvu zenye maana maalumu za Jamhuri ya Kiislamu hivi sasa zilizosimama juu ya msingi wa kiaidiolojia na miongozo ya Imam (Khomeini - quddisa sirruh) na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pamoja na siasa za demokrasia ya kidini na kupigania malengo matukufu kwa kuzingatia uhalisia wa mambo, zimeiletea Iran utulivu wa ndani na kuifanya Jamhuri ya Kiislamu kuwa dola lenye nguvu kieneo na vile vile kueneza fikra ya muqawa na kupenda Uislamu katika eneo hili.
Aidha ameashiria jukumu la Wizara ya Mambo ya Nje ambayo ni mlinzi wa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na kusema kuwa: Tuko tayari wakati wote kutekeleza vlivyo kabisa na kwa njia iliyo bora siasa za nje zilizotolewa miongozo yake na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na tunatawakali na kumtegemea Mwenyezi Mungu Mtukufu katika utekelezaji wa siasa hizo na hakuna dola lolote ambalo tunalihesabu kuwa ni dola kubwa.
Bw. Zarif vile vile amesema: Tunajiamini na tunategemea na kuiamini nguvu yetu ya kitaifa na uwezo wetu wa kiutaalamu na ni kwa kutegemea imani hiyo ndio maana tunasema kwa kujiamini kuwa hatuwezi kushindwa na madola ya kibeberu ambayo yanaonekana kidhahiri kuwa yana nguvu.
 
< Nyuma   Mbele >

^