Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Aonana na Rais na Baraza la Mawaziri Chapa
27/08/2014
Supreme Leader Meets with President Rouhani and Cabinet MembersAyatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, leo asubuhi (Jumatabno) ameonana na Rais pamoja na wajumbe wa Baraza la Mawaziri la serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kulitaja suala la kuleta utulivu wa kiroho na kisaikolojia katika jamii, kudhibiti mfumuko wa bei na kudhibiti bei ya fedha za kigeni pamoja na kutekeleza mpango wa mfumo wa usalama wa kiafya kuwa ni miongoni mwa kazi zenye thamani na nzuri zilizofanywa na Serikali ya Kumi na Moja ya Jamhuri ya Kiislamu katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita na akawataka watumishi wote serikalini walinde, watie nguvu na wahifadhi msimamo na moyo wa kimapinduzi, wategemea uwezo wa taifa na uzalishaji wa ndani ya nchi, watekeleze ipasavyo siasa za uchumi wa kusimama kidete, waipe uzito wa kipekee sekta ya kilimo na viwanda jadidika vijijini, walipe uzito mkubwa suala la ukuaji wa kielimu na watie nguvu mashirika ya elimu msingi, wawe na misimamo ya wazi mbele ya masuala ya kieneo na kimataifa hususan suala la uingiliaji wa Marekani katika masuala ya ndani ya mataifa mengine, walinde umoja na mshikamano ndani ya serikali, wachunge mistari myekundu na wajiweke mbali na watu kama wale waliousika katika fitna ya mwaka 1388 (Hijria Shamsia - 2009 Milaadia) na vile vile wawe na vifua vipana na watulivu mbele ya ukosoaji wa kiinsafu na kiuadilifu.
Katika mkutano huo ambao umefanyika kwa mnasaba wa Wiki ya Serikali ya Iran, Ayatullah Udhma Khamenei amewaenzi na kuwataja kwa wema mashahidi Rajai na Bahonar (Rais na Waziri Mkuu wa zamani wa Iran waliouawa shahidi) na ametaja baadhi ya sifa maalumu walizokuwa nazo viongozi hao wawili wa Iran kwamba ni pamoja na kuwa na stratijia na misimamo ya wazi, kuwa na roho ya kimapinduzi na kufanya kazi zao kwa ajili ya kutafuta radhi za Allah. Ameongeza kuwa: Inabidi sisi sote ambao ni viongozi wa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, daima tuwe na misimamo iliyo wazi na roho ya kimapinduzi na lengo letu liwe ni kutafuta radhi za Allah.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha ameipongeza ripoti ya Rais Hassan Rouhani kuhusiana na kazi za mwaka mmoja uliopita za serikali ya 11 ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuongeza kuwa: Inabidi ripoti ya kazi zilizofanywa na Serikali katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita iakisiwe na ifikishwe vizuri kwa wananchi, ili sambamba na wananchi kujua kazi zilizotendeka, wapate habari pia kuhusiana na mipangilio ya baadaye ya serikali yao.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Kutangazwa vizuri ripoti kuhusiana na kazi za serikali kunawaletea matumaini wananchi. Tab'an inabidi kuwa makini katika utoaji wa ripoti hizo ili takwimu zinazotolewa ziwe za kina na zisiwe na uongezaji chumvi ndani yake.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Tab'an matumaini ya wananchi hayawezi kupata nguvu wala kuongezeka kwa kutolewa ripoti tu, bali wanachotaka wananchi ni vitendo na matokeo ya wazi ya kazi zinazofanyika.
Ayatullah Udhma Khamenei ameendelea na hotuba yake kwa kutoa nasaha kadhaa kwa Serikali ambapo kufanya kazi kwa bidii na kuwahudumia bila ya kuchoka wananchi pamoja na kujiweka mbali na masuala madogo madogo ya pembeni, ndiyo iliyokuwa nasaha yake ya kwanza kwa watumishi serikalini.
Amesema kuwa, moja ya baraka za kubadilika badilika Serikali na kuondoka serikali moja na nafasi yake kuchukuliwa na serikali nyingine ikiwa na kaulimbiu mpya ni kuingiza matumaini katika nyoyo za wananchi.
Ameongeza kuwa: Inabidi matumaini hayo yalindwe na kutiwa nguvu katika nyoyo za wananchi ambapo moja ya njia za kutia nguvu matumaini hayo katika nyoyo za wananchi, ni kuwajulisha kazi zinazofanyika.
Kulindwa mshikamano ndani ya serikali na kuwafanya watumishi wote kuwa na sauti moja, ni nasaha ya pili iliyotolewa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu. Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Inabidi kuchunga matamshi yanayotolewa ili matamshi ya viongozi serikalini yasigongane na hiyo ndiyo falsafa ya kuwa na msemaji mmoja wa serikali ili iweze kusikika sauti moja tu kuhusu masuala mbali mbali yanayohusiana na Serikali.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa nasaha yake ya tatu kwa watumishi serikalini akiwausia wajiepushe na kuifanya jamii kuwa na kambi mbili na wajiweke mbali na ugomvi wa kisiasa. Ameongeza kuwa: Suala la kuwa na mirengo tofauti ya kisiasa si kitu kibaya lakini jambo hilo lisiruhusiwe kuifanya jamii kuwa na kambi mbili kwani suala hilo litawavunja moyo na kuwachosha wananchi na kuharibu utulivu katika jamii.
Nasaha ya nne iliyotolewa na Ayatullah Udhma Khamenei ni serikali kujitoa katika udhibiti wa mirengo kwenye masuala ya kisiasa akisisitiza kwamba: Si jambo baya kwa watumishi serikalini kuwa na mirengo yao ya kisiasa, lakini Serikali na watumishi wake hawapaswi kuwa mateka wa misimamo ya mirengo yao.
Ameongeza kuwa: Katika suala la mirengo ya kisiasa, siku zote imekuwa ikisisitizwa kudumishwa urafiki, mapenzi na udugu baina ya mirengo hiyo. Hata hivyo kuna baadhi ya masuala suala hilo huwa tofauti na inakuwa ni jambo la lazima kuchunga mipaka myekundu na kujiweka mbali na mrengo fulani wa kisiasa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Suala la fitna na wafanya fitna ni miongoni mwa masuala muhimu na ni katika mistari myekundu ambayo waheshimiwa mawaziri kama walivyosisitiza wakati wa kuomba ridhaa ya kupewa nafasi ya kuwa mawaziri na kusisitiza kwao kujiweka mbali na wafanya fitna hao, inabidi hivi sasa pia waendelee kuwa na msimamo huo huo.
Ayatullah Udhma Khamenei ameifanya nasaha yake ya tano ihusiane na udharura wa kuwa na kifua kipana na utulivu mbele ya ukosoaji wa kiinsafu na kiuadilifu. Amesema: Mheshimiwa Rais amehuzunishwa na baadhi ya ukosoaji, na tab'an katika baadhi ya masuala ana haki ya kuwa hivyo kwani baadhi ya ukosoaji unakuwa wa maneno makali na mwingine unakosa insafu na hauwi wa kiuadilifu.
Ameongeza kuwa, hakuna ulazima kwa mtu kujibu kila suala au ukosoaji unaotolewa kwani baadhi ya wakati kunyamaza kimya ni bora na jingine ni kwamba si kila neno linalosemwa dhidi yetu ni lazima liwe na taathira katika jamii au kukubaliwa na watu ndani ya jamii.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza pia kuwa: Ukosoaji lazima uwepo lakini inabidi ukosoaji uwe wa maneno mazuri, utolewe kiinsafu na lengo lake nalo lisiwe ni kuaibisha upande unaokosolewa na kumdunisha mkosolewaji, kwani kufanya hivyo bila ya shaka yoyote ni ghalati na ni makosa. Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa, majibu yanayotolewa katika kujibu ukosoaji nayo inabidi yawe ya kimantiki na yatolewe kwa umakini na utulivu wa hali ya juu.
Vile vile amesema, ukosoaji wa kiinsafu na kiadilifu si uadui bali ni msaada kwa serikali na kuongeza kuwa: Moja ya masuala muhimu sana hivi sasa ni kulinda na kudumisha utulivu wa kisaikolojia uliopo katika jamii.
Kufanya insafu na kuwa waadilifu katika kuzikosoa siasa za serikali zilizopita, ni nasaha ya sita iliyotolewa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa watumishi wa serikali ya kumi na moja ya Jamhuri ya Kiislamu.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kuwa: Siku zote serikali mpya zinapoingia madarakani huwa na kawaida ya kukosoa utendaji na siasa za serikali zilizotangulia na wala suala hilo halina tatizo lakini ukosoaji huo inabidi ufanyike kiuadilifu, usiongezwe chumvi na kugeuzwa kuwa uharibifu kwani jambo hilo lina athari mbaya kwa watu na linawafanya wasiwe na uhakika kuhusu mustakbali wao.
Ameashiria baadhi ya matamshi yaliyoongezwa chumvi na yasiyo ya kimantiki yaliyotolewa kuhusiana na serikali zilizotangulia na kuongeza kwamba, kama matamshi hayo yatakosa insafu, basi siku za usoni pia wakosoaji watakosa insafu kuhusu kazi zetu. Kama baadhi ya siasa au baadhi ya utendaji wa serikali za vipindi vilivyopita hatukubaliani nao, njia bora tunayopaswa kufanya ni kutafuta njia sahihi zaidi ya utendaji wa majukumu tuliyopewa na kufanya hivyo ni bora kulikoni kukaa na kukosoa tu bila ya insafu.
Kuwa na misimamo ya wazi na isiyotetereka mbele ya masuala ya kieneo na kimataifa, ilikuwa ni nasaha ya saba iliyotolewa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa serikali ya kumi na moja ya Jamhuri ya Kiislamu.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema kuwa, misimamo iliyochukuliwa na Serikali katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita ni mizuri na kuongeza kuwa: Misimamo ya wazi na isiyotetereka iliyochukuliwa na serikali kuhusu masuala kama vile Palestina, utawala wa Kizayuni, Ghaza, Syria, Iraq, makundi ya kitakfiri (yanayokufurisha Waislamu wengine) na uingiliaji wa Marekani ni misimamo mizuri na imekuwa ni kwa manufaa ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na wala misimamo hiyo haikinzani na lugha inayotumika ya kidiplomasia pamoja na kufanya mazungumzo.
Amesisitiza kuwa: Kuchukua misimamo ya wazi na iliyo bayana kuhusu masuala mbali mbali ndio muundo jumla wa mfumo wa Kiislamu na ndilo jambo litakalolinda dira ya kiistrajitia ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu kwa mataifa mengine.
Nasaha ya nane iliyotolewa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ni kuendelea kwa kasi kubwa na ustawi wa kielimu nchini na kuyasaidia na kuyaunga mkono mashirika ya elimu msingi pamoja na ramani muhimu mno ya utafiti wa kiistratijia na utafiti wa masuala ya kimsingi nchini.
Ayatullah Udhma Khamenei ameutaja mpango wa mfumo wa usalama wa kiafya kuwa ni moja ya hatua nzuri mno zilizochukuliwa na serikali ya kumi na moja ya Jamhuri ya Kiislamu na katika nasaha yake ya tisa amesema: Inabidi mpango huo wa usalama wa kiafya uungwe mkono na uendelezwe na vile vile watu wawe makini ili baadhi ya maamuzi yasije yakauharibu mpango huo.
Nasaha zilizofuatia baadaye za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, kimsingi zimehusiana na masuala ya kiuchumi. Katika nasaha yake ya kumi, Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria ulazima wa kutegemea uwezo wa ndani na kuunga mkono uzalishaji wa taifa na kuongeza kuwa: Ufunguo wa ustawi wa kiuchumi ambao unaungwa mkono pia na mheshimiwa Rais ni suala la uzalishaji wa taifa. Inabidi uwezo mkubwa uliomo ndani ya nchi utumike vizuri katika kuimarisha na kutia nguvu uzalishaji wa taifa ili liweze kufanikishwa suala la ustawi wa kiuchumi na ongezeko la bidhaa zisizo za mafuta zinazosafirishwa nje ya nchi.
Ayatullah Udhma Khamenei ameutaja utekelezaji wa siasa za uchumi wa kusimama kidete kuwa ni muhimu mno katika kutia nguvu uwezo wa ndani na kuufanya uelekee upande wa uzalishaji wa ndani ya nchi na kusisitiza kuwa: Serikali inapaswa kutabikisha kifurushi cha siasa zake za kiuchumi na siasa za uchumi wa kusimama kidete na ikiona kuna baadhi ya mambo katika siasa zake za kiuchumi hayakubaliani na siasa za uchumi wa kusimame kidete, iyatoe katika siasa zake.
Vile vile amelitaja suala la kudhibitiwa thamani ya fedha za kigeni na kudhibiti mfumuko wa bei kuwa ni miongoni mwa hatua zenye thamani kubwa zilizochukuliwa na Serikali katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita na kuongeza kuwa, si sahihi kutosheka na hatua hizo kwani masuala hayo ni hatua za awali tu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia pia mfumo wa kibenki na utendaji kazi wake akisisitiza kuwa: Serikali inapaswa kulishughulikia kwa uzito wa hali ya juu suala hilo na kulitatua kwani benki zinapaswa zitumikie uzalishaji wa taifa na ni wakati benki zinapotumikia uzalishaji wa taifa ndipo matatizo mengi yanapoweza kutatuka.
Kuipa mazingatio maalumu sekta ya kilimo na bidhaa za viwandani ni nasaha ya kumi na moja iliyotolewa na Ayatullah Udhma Khamenei kwa serikali ya kumi na moja ya Jamhuri ya Kiislamu. Amesisitiza kuwa: Sekta ya kilimo ni moja ya sekta za kiistratijia ambayo inazipa msaada wa kipekee nchi zote duniani na kwamba Serikali inapaswa kuipa umuhimu na uzito wa kipekee sekta ya kilimo.
Vile vile Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekumbusha kuwa: Njia ya kuleta ustawi vijijini ni kuwa na bidhaa jadidika katika vijiji hivyo.
Ayatullah Udhma Khamenei ametaja nasaha yake ya kumi na mbili kuwa ni udharura wa kuipa mazingatio maalumu sekta ya madini, thamani ya nyongeza na uzalishaji wa nafasi za kazi katika sekta hiyo. Baada ya hapo ameashiria madhara ya kuingiza bidhaa kutoka nje bila ya mpangilio na taathira zake mbaya katika uzalishaji wa ndani ikiwa ni nasaha yake ya kumi na tatu kwa serikali ya kumi na moja ya Jamhuri ya Kiislamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kwamba, suala la uingizaji bidhaa kutoka nje ya nchi haliwezi kutatuliwa kwa njia ya ushuru tu na kuongeza kwamba: Serikali inapaswa ilipe uzito wa hali ya juu sana suala la kupambana na uingizaji wa bidhaa zisizo za dharura na za anasa na isiruhusu kabisa bidhaa kama hizo kuingizwa nchini.
Nasaha ya kumi na nne ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu imehusiana na tatizo la maji yanayotumika katika kilimo ambapo Ayatullah Udhma Khamenei sambamba na kuunga mkono siasa za Wizara ya Nishati kuhusiana na maji amesema: Moja ya njia za kutatua kikamilifu tatizo la maji nchini, ni kubana matumizi yake katika kilimo kwa kutumia mbinu mpya za kisasa za umwagiliaji maji.
Kulipa uzito mkubwa suala la kuukamilisha mradi wa ujenzi wa nyumba kwa ajili ya wananchi unaojulikana kwa jina la mpango wa "Maskane Mehr" ilikuwa ni nasaha ya kumi na tano na ya mwisho iliyotolewa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika mkutano wake na watumishi wa serikali ya kumi na moja ya Jamhuri ya Kiislamu.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema: Hata kama itatokezea kuwa baadhi watu wanapinga asili ya mradi wenyewe wa "Maskane Mehr" au njia inayotumiwa na kuingia itibari za kibenki katika mradi huo, lakini inabidi itambulike pia kwamba hivi sasa kuna milioni kadhaa za watu wanasubiri kwa hamu kukamilishwa mradi huo hivyo inabidi mradi wa "Maskane Mehr" ukamilishwe na suala hilo lipewe uzito wa hali ya juu.
Mwishoni mwa hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewakhutubu watumishi wa serikali ya kumi na moja ya Jamhuri ya Kiislamu akiwaambia: Mtegemeeni Mwenyezi Mungu na mutawakali Kwake kwani mkiwa na imani na msaada wa Mwenyezi Mungu basi bila ya shaka yoyote Mwenyezi Mungu atakusaidieni na eleweni pia kwamba, kufanikiwa kwenu ni kufanikiwa taifa na ni fakhari kwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Hujjatul Islam Walmuslimin Hassan Rouhani, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa ripoti fupi kuhusu kazi zilizofanywa na serikali yake katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
Rais Rouhani ameashiria hamasa ya kisiasa waliyoionesha wananchi wa Iran katika uchaguzi wa Rais wa serikali ya kumi na moja ya Jamhuri ya Kiislamu na kuongeza kuwa, serikali yake imeelekeza nguvu zake zote katika kuleta utuvu na utulivu katika jamii na kuwapa matumaini wananchi kuhusiana na ustawi wa nchi yao na kwamba leo hii moja ya mafanikio makubwa ya serikali yake ni kuleta hali ya utulivu na kuondoa hofu na wasiwasi katika jamii. Baada ya hapo ametoa takwimu tofauti kuhusu kazi zilizofanywa na serikali yake katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
Amma katika upande wa siasa za nje Rais Rouhani amesema, serikali yake imewaunga mkono kikamilifu wananchi wa Iraq, Syria, Lebanon na hasa hasa wananchi wa Palestina na imetumia uwezo wake wote kuwaunga mkono kisiasa, kijamii na kiuchumi watu wa mataifa hayo.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa, ana matumaini katika siku za usoni eneo la Mashariki ya Kati litashuhudia ushindi wa mataifa ya eneo hili dhidi ya ugaidi na dhidi ya utawala wa Kizayuni mtenda jinai na amani na utulivu utatawala katika eneo hili.
Rais Rouhani vile vile amesema kuwa, ukuta wa kueneza dhuki dhidi ya Iran umepungua duniani na kuhusiana na vikwazo vya kidhulma vilivyowekwa na madola ya Magharibi dhidi ya Iran amesema: Kumeshachukuliwa hatua mbali mbali za kupunguza na kuondoa kikamilifu vikwazo hivyo na katika siku za usoni pia serikali yake itachukua hatua kubwa zaidi katika suala hilo.
Rais Rouhani pia amesema kuhusu mkakati wa serikali yake katika mazungumzo kuwa, upande wa Iran umeonyesha wazi wazi nia yake njema, misimamo yake ya kimantiki na kupenda kwake amani na usalama na kwamba itaendelea kufanya mazungumzo hayo kwa misimamo hiyo hiyo na kama kupenda makuu kwa baadhi ya madola ya kibeberu kutakwamisha mazungumzo hayo, basi watu wote duniani watayabebesha lawama madola hayo yanayopenda makuu.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vile vile amesema kuwa, serikali yake inayahesabu mafanikio yake yote kuwa yanatokana na rehema na msaada wa Mwenyezi Mungu pamoja na msaada wa Imam wa Zama (Imam Mahdi AS) na uungaji mkono wa wananchi pamoja na msaada na miongozo ya busara ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.
 
< Nyuma   Mbele >

^