Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Wasimamiaji wa Amali ya Hija Waonana na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Chapa
07/09/2014
Wasimamiaji wa Amali ya Hija Waonana na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya KiislamuAyatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, leo asubuhi (Jumapili) ameonana na wasimamiaji wa amali ya Hija ya mwaka huu na kusema kuwa, Hija ni fursa kubwa ya kuweza kustafidi umma wa Kiislamu na rehema za kimaanawi za ardhi ya wahyi na kuimarisha uhusiano wake na Mwenyezi Mungu. Vile vile amesema, Hija ni fursa nzuri kwa umma wa Kiislamu kuweza kubadilishana mawazo na kutatua matatizo ya ulimwengu wa Kiislamu kwa umoja wao. Amesema kuna njama kubwa zinafanya na madola ya kibeberu na vibaraka wao kwa lengo la kuzusha mizozo na mifarakano katika umma wa Kiislamu hivyo umma wa Kiislamu unapaswa kutumia vilivyo fursa ya kipekee ya Hija kuleta mshikamano na maelewano baina yao na kuondoa mambo yanayosababisha mizozo na suutafahumu katika safu za Waislamu.
Katika mkutano huo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa mkono wa baraka kwa mnasaba wa maadhimisho ya siku ya kuzaliwa Imam wa Nane, Imam Ridha Alayhis Salaam na kuitaja haram takatifu ya mtukufu huyo iliyoko mkoani Khorasan, kaskazini mashariki mwa Iran kuwa ni chemchemu ya baraka na ni kituo cha dhikri, tawhidi na kumzingatia Mwenyezi Mungu Mtukufu. Aidha ameashiria njia na mipangilio makini aliyokuwa nayo mtukufu huyo katika kupambana na njama za watawala wa kisiasa madikteta na madhalimu wa zama zake amesema: Imam Ridha AS alitawakali kwa Mwenyezi Mungu na kwa tadibiri ya Allah na muono wake wa kina uliotokana na kuwa kwake Imam, alifanikiwa kubadilisha njama na hila zilizokuwa zimewekwa dhidi yake na maadui kuwa harakati adhimu ya kueneza mafundisho ya Qur'ani na ya Ahlul Bayt Alayhimus Salaam katika fikra za watu kwenye ulimwengu wa Kiislamu.
Baada ya hapo, Ayatullah Udhma Khamenei amezungumzia amali ya Hija na kusema kuwa, msimu wa Hija ni fursa kubwa yenye thamani ya kipekee kwa ajili ya kurekebisha masuala ya kidini na kimaanawi na kutengeneza masuala muhimu ya ulimwengu wa Kiislamu.
Ameongeza kuwa: Waislamu wanapaswa kutumia vizuri fursa za kujiimarisha kiimani wanazozipata katika safari ya kimaanawi ya siku za Hija na waimarishe uhusiano wao na Mwenyezi Mungu kwa namna ambayo baada ya safari yao ya Hija kuweze kushuhudiwa mabadiliko ya kweli kwa hujaji.
Amma kuhusiana na umuhimu wa kutumiwa vizuri fursa ya Hija kwa ajili ya kujadili masuala muhimu ya ulimwengu wa Kiislamu na kubadilishana mawazo kuhusu njia za kutatua matatizo hayo amesema: Hivi sasa ulimwengu wa Kiislamu umo katika hali ya hatari sana na kwamba moja ya masuala muhimu zaidi yanayoukabili ulimwengu huo ni njama na hila za madola makubwa ya kibeberu za kuzusha mizozo na kudhaniana vibaya watu katika safu za Waislamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, inabidi katika siku za Hija Waislamu watumie uwezo wao wote kuzinyoosha na kuzisafisha nyoyo zao na kupunguza chuki na uhasama uliopandikizwa kati yao. Amesema: Inasikitisha kuona kuwa kuna baadhi ya Waislamu, iwe ni Mashia, iwe ni Masuni, wamekumbwa na mghafala na wanaeneza tuhuma na uongo uliopandikizwa na maadui wa umma wa Kiislamu ikiwa ni katika kutumikia malengo ya Marekani na Uzayuni kwa madhara ya Waislamu.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Waislamu wanapaswa kuwa macho na watumie busara na mshikamano baina yao ili kumpokonya adui silaha anayoitumia kuwafarakanisha.
Amesema, fikra za kitakfiri za kukufurisha Waislamu wengine hivi sasa ni moja ya silaha zinazotumiwa na maadui wa Uislamu ili kuzusha mizozo na mifarakano kati ya Waislamu na kuwafanya washughulikie masuala madogo madogo yasiyo na maana baina yao ili wasahau kadhia kubwa ya ulimwengu wa Kiislamu nayo ni Palestina, na kuupa fursa utawala wa Kizayuni ufanikishe malengo yake maovu. Amesema: Kadhia ya Palestina ndiyo kadhia nambari moja katika ulimwengu wa Kiislamu ambayo inabidi izingatiwe na ipewe uzito wa hali ya juu katika siku za Hija.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Kwa bahati nzuri hivi sasa Waislamu wamezidi kulielewa suala la Palestina na kwamba matukio yaliyoshuhudiwa katika vita vya siku 50 vilivyomalizika hivi karibuni huko Ghaza na kushindwa utawala wa Kizayuni katika vita hivyo licha ya kwamba utawala huo ni nembo ya nguvu za madola ya Magharibi katika eneo la Mashariki ya Kati tena mbele ya watu wachache waliozingirwa kila upande huko Ghaza na tena walio na suhula chache mno, ni mfano wa wazi kabisa wa uhakika huo.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Ushindi walioupata wananchi wa Ghaza hivi karibuni umethibitisha kwamba Waislamu ni watu wenye nguvu sana na uwezo mkubwa mno na wanao uwezo wa kupambana na adui yeyote yule na kujihami na kujilinda vizuri sana.
Ameongeza kuwa: Nguvu za Uislamu na za Qur'ani na za kiimani na za umma wa Kiislamu tusizidharau hata kidogo na tuelewe kuwa tunao uwezo wa kupambana vilivyo na dhulma za mifumo yote ya kiistikbari na kibeberu.
Mwishoni mwa hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekumbushia kuongezeka huduma na usahilishaji wa mambo kimaada na kimaanawi kwa ajili ya mahujaji wa Kiirani katika miaka ya hivi karibuni na kuongeza kuwa, haipasi kutosheka na kiwango hicho cha usahilishaji na ustawi uliofikiwa hivi sasa bali inabidi juhudi za ziada zifanyike kuhakikisha mianya yote iliyopo inazibwa ili mahujaji waweze kufaidika vizuri zaidi na fursa za siku za Hija kwa kadiri inavyowezekana.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Hujjatul Islam Walmuslimin Kadhi Askari, Mwakilishi wa Fakihi Mtawala na Msimamiaji wa Mahujaji wa Kiirani, sambamba na kutoa mkono wa baraka kwa mnasaba wa kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa Imam Ridha Alayhis Salaam, amesema kuwa, uongozi na usimamiaji wa masuala ya Hija ni usimamiaji wa kijihadi, wa kujitolea na unaohitajia ushirikiano wa pande zote. Amesisitiza kuwa: Kwa kuzingatia hali ilivyo katika eneo la Mashariki ya Kati na katika ulimwengu wa Kiislamu kiujumla na kwa ajili ya kuhakikisha kuwa fursa ya safari ya kimaanawi ya Hija inatumiwa vizuri sana, kaulimbiu ya mwaka huu ya mahujaji wa Iran imeamuliwa kuwa ni "Hija, Umaanawi, Kujitambua na Mshikamano wa Kiislamu" ili iweze kuingiza ndani yake ratiba na mipango yote ya mwaka huu ya Hija.
Hujjatul Islam Walmuslimin Kadhi Askari ametaja baadhi ya ratiba hizo kuwa ni pamoja na kutoa huduma bora kabisa kwa ajili ya mahujaji na kuifanya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa kigezo kwa nchi nyingine katika suala zima la Hija, kuwaelimisha mahujaji wa Kiirani falsafa wa Hija, kutoa mafunzo yanayotakiwa kwa wasimamiaji wa Hija na kuitisha vikao vya kiutaalamu na warsha na makongamano ya uelimishaji na uoneshaji njia kwa ajili ya kufanya amali ya Hija ifanyike kwa namna iliyo bora kabisa. Amesema hizo ni katika ratiba mbali mbali zilizomo kwenye Biitha ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei.
Naye Bw. Awhadi, Mkuu wa Taasisi ya Hija na Ziara ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa ripoti fupi kuhusu kazi za taasisi hiyo. Ametaja miongoni mwa kazi hizo kuwa ni pamoja na kufanyia mabadiliko asilimia 25 ya wafanyakazi watendaji wa masuala ya Hija, kutoa huduma za tiba na afya usiku na mchana, kupunguza gharama za kwenda Hija, kuongeza kwa asilimia 150 idadi ya bidhaa zinazohitajiwa na mahujaji huko Saudi Arabia, na kutoa huduma kwa mahujaji wa Kiirani waliokwenda Hija mwaka huu. Amesema, mwaka huu mahujaji 64 elfu wa Kiirani watakwenda Hija Inshaallah kupitia misafara 450 katika viwanja 19 tofauti vya ndege.
Kabla ya mkutano huo, Kiongozi Muadhamu, Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei ametembelea maonyesho ya picha za maeneo matakatifu ya Makka na Madina na vile vile bidhaa za kiutamaduni za Biitha ya Hija ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.
 
< Nyuma   Mbele >

^