Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Arejea Nyumbani baada ya Kumaliza Matibabu Hospitalini Chapa
15/09/2014
 Supreme Leader Discharged from HospitalAyatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, leo asubuhi (Jumatatu) ameruhusiwa kurejea nyumbani baada ya kumaliza kipindi cha matibabu na kulazwa hospitalini alikofanyiwa upasuaji wa tezi kibofu na baada ya kupona kikamilifu.
Kabla ya kuondoka hospitalini, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumza na mwandishi wa Shirika la Sauti na Televisheni la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran IRIB na sambamba na kuelezea kuridhishwa kwake kikamilifu na namna kazi ya upasuaji ilivyofanyika na namna kipindi chote cha matibabu yaliyofuatia kilivyoendeshwa amesema: Hivi sasa ninarejea nyumbani nikiwa na afya yangu kamili ya kimwili na moyo wangu ukiwa na furaha nyingi, hata hivyo ninahisi kubeba mzigo mzito sana kutokana na mapenzi makubwa waliyonionyesha watu wa matabaka tofauti katika siku hizi kadhaa nilizokuwa nimelazwa hapa hospitalini.
Vile vile amewashukuru sana watu wote wa matabaka mbali mbali, maraji'i na maulamaa wapendwa, shakhsia tofauti, viongozi wakubwa wa nchi, wanasiasa, watu wa sanaa pamoja na wanamichezo kutokana na mapenzi makubwa sana waliyomuonyesha na kusema: Mbali na mapenzi yaliyooneshwa na wananchi wa nchini mwetu (Iran), wananchi wa mataifa mengine nao wameonesha mapenzi makubwa sana kwangu katika kipindi chote hicho na hili linathibitisha kwa mara nyingine kama ambavyo nimekuwa nikisema mara zote kwamba, taifa la Iran lina kina kikubwa cha kiistratijia kwa mataifa mengine duniani.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kwamba: Hakuna mfumo wa utawala wala nchi yoyote ambayo imejizatiti kiasi chote hiki nje ya mipaka yake na kuwa na mfungamano wa kimapenzi, kiitikadi na kiimani na mataifa mengine kama ilivyo Iran na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Vile vile Ayatullah Udhma Khamenei ameishukuru sana timu nzima ya madakrani, matabibu na wauguzi wa hospitali alikokuwa amelazwa na kusema kuwa: Wakati mtu anapoona kwa karibu elimu, maarifa ya hali ya juu na uwezo mkubwa pamoja na namna madaktari wa timu ya matibabu na wauguzi walivyotabahari katika elimu ya tiba, huwa anapata nguvu ya kuona fakhari na kujivunia maendeleo hayo makubwa yaliyopigwa nchini Iran katika upande huo wa tiba na matibabu ambao ni utajiri adhimu wa kibinadamu katika upande wa afya na hiyo ni moja ya sehemu za kimsingi zaidi na muhimu zaidi katika maisha ya watu na ya jamii.
Katika sehemu nyingine ya mahojiano hayo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia nukta nyingine kwa kusema: Mimi katika kipindi cha siku hizi kadhaa nilizokuwa nimelazwa hapa hospitalini, nilipata burudani na burudani yenyewe ni pale niliposikia matamshi ya viongozi wa Marekani kuhusiana na mapambano dhidi ya kundi la Daesh matamshi ambayo kwa kweli ni aina fulani ya burudani.
Ametoa ufafanuzi zaidi akisema, matamshi ya viongozi wa Marekani kuhusiana na kupambana na Daesh ni pumba zisizo na kitu ndani yake na yanatolewa kwa malengo maalumu. Amesema hayo ikiwa ni kugusia matamshi ya msemaji wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani na msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo aliyedai hadharani kwamba Washington haitoialika Iran katika vita dhidi ya Daesh.
Ameongeza kuwa: Sisi tunaona fakhari kuona kwamba Marekani imevunjika moyo kwa kuona kuwa haiwezi kuiingiza Iran katika jambo ovu la watu wengi kwa pamoja, bali hakuna fakhari kubwa zaidi inayoona Iran zaidi ya hiyo.
Baada ya hapo, Ayatullah Udhma ametoa ufafanuzi na kufichua baadhi ya mambo kama njia ya kuonesha uongo wa Wamarekani katika kupambana na kundi la Daesh.
Amesema: Tangu katika zile siku nzito za mashambulizi ya Daesh huko Iraq, balozi wa Marekani nchini Iraq alimuomba balozi wetu nchini humo kwamba Iran na Marekani ziitishe kikao cha kujadiliana na kufanya uratibu wa pamoja kuhusu kupambana na Daesh.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameendelea kusema: Balozi wetu alilifikisha humu nchini suala hilo ambapo baadhi ya viongozi wetu humu nchini hawakupinga kufanyika kikao kama hicho, lakini mimi nilipinga na nikasema, sisi hatuwezi kushirikiana na Wamarekani katika suala hili kwani Wamarekani wana nia mbaya na mikono yao ni michafu, sasa itawezekana vipi sisi kushirikiana na Wamarekani katika mazingira kama haya?
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria pia matamshi ya siku chache zilizopita ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ambaye naye alidai kuwa Marekani haitoialika Iran kujiunga na umoja ya kupambana na Daesh na kuongeza kuwa: Huyo huyo Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani (ambaye hivi sasa anatoa madai hayo) ndiye yeye mwenyewe aliyemuomba Dk Zarif (Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran) kwamba na sisi tushirikiane na Marekani katika suala hilo lakini Dk Zarif alilikataa ombi hilo.
Vile vile amesema: Hata Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani naye ambaye ni mwanamke na watu wote wanamjua, katika mazungumzo yake na Bw. Araqchi (Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran) kwa mara nyingine alirudia ombi hilo lakini Bw. Araqchi na yeye alilikataa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria namna Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inavyopinga wazi wazi kushirikiana na Marekani katika kupambana na kundi la Daesh na kusema: Hivi sasa Wamarekani wanasema uongo wanapodai kwamba hawatoialika Iran katika suala hilo wakati ambapo tangu mwanzo kabisa Iran ilipinga kushiriki katika muungano wa namna hiyo.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza pia kuwa: Kabla ya hapo pia, Wamarekani walipiga makelele mengi na kuzusha zogo kubwa na kukusanya nchi kadhaa kuunda umoja dhidi ya Syria lakini wameshindwa kufanya "upuuzi" wowote huko Syria na kuhusiana na Iraq pia hali itakuwa vivyo hivyo.
Aidha ameashiria kwamba Wamarekani hawalipi uzito unaotakiwa suala la kupambana na Daesh na kuongeza kwamba: Wamarekani wenyewe, bali hata hao Daesh wenyewe wote wanatambua vyema kwamba harakati ambayo imewavunja nguvu Daesh nchini Iraq si hatua zilizochukuliwa na Marekani, bali ni hatua zilizochukuliwa na vikosi vya wananchi pamoja na jeshi la Iraq katika kupambana na Daesh. Wairaq wamejifunza vizuri namna ya kupambana na Daesh na wametoa mapigo makubwa kwa kundi hilo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kwamba, vipigo kutoka kwa vikosi vya wananchi na jeshi la Iraq vitaendelea kuikumba Daesh na kuongeza kuwa: Uhakika wa mambo ni kuwa wanachotafuta Wamarekani ni kisingizio na sababu tu ili waweze kufanya nchini Iraq na nchini Syria yale yale wanayoyafanya nchini Pakistan ambako licha ya kuweko serikali huru na jeshi lenye nguvu, lakini Wamarekani wanaingia bila ya ruhusa katika ardhi ya nchi hiyo na kushambulia maeneo tofauti ya Pakistan.
Vile vile amesema kwa kusisitiza kuwa: Wamarekani watambue kwamba kama watafanya kitu kama hicho, basi kwa mara nyingine tena watakumbwa na matatizo yale yale yaliyowakumba miaka 10 iliyopita wakati walipoivamia Iraq.
Mwishoni mwa mahojiano hayo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Alaakullihaal, katika kipindi hiki cha siku kadhaa zilizopita, matamshi ya viongozi wa Marekani yalikuwa ni kiburudisho kwangu wakati nilipokuwa nimelazwa hospitalini.
Leo pia na baada ya kuruhusiwa kurejea nyumbani kutoka hospitalini, Ayatullah Udhma Khamenei kabla ya kuondoka hospitalini hapo ameonana na mataktari na wauguzi kadhaa na kuwashukuru.
Vile vile Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kabla ya kuondoka hospitalini, amekwenda kumjulia hali Ayatullah Mahdavi Kani, Mkuu wa Baraza la Wanachuoni Wataalamu (linalomchagua na kusimamia kazi za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu).
 
< Nyuma   Mbele >

^