Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Aonana na Majimui ya Makamanda wa Kijeshi Chapa
24/09/2014
 Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, ambaye pia ni Amirijeshi Mkuu wa vikosi vyote vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu, leo asubuhi (Jumatano) ameonana na majimui ya makamanda wa ngazi za juu wa kijeshi na kukitaja kipindi cha vita vya kujihami kutakatifu (vita vya miaka minane vilivyoanzishwa na utawala wa zamani wa Iraq dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran) kuwa ni nembo ya heshima kwa taifa la Iran.
Amesisitiza kuwa, kipindi hicho cha kujihami kutakatifu kimethibitisha kwamba, licha ya kuwepo mashinikizo makubwa na uhaba wa fedha na matatizo mengine mengi, lakini inawezekana kukabiliana vilivyo na madola ya kibeberu duniani na kuvunja ndoto zao zisizo na maana kwa kutegemea nia ya kweli na kutawakali kwa Mwenyezi Mungu.
Katika mkutano huo uliofanyika kwa mnasaba wa maadhimisho ya Wiki ya Kujihami Kutakatifu, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu vile vile amekitaja kipindi cha kujihami kutakatifu kuwa ni suala muhimu na lenye vipengee tofauti na kuongeza kwamba kusimama kidete taifa la Iran katika vita hivyo vya miaka minane kulizidi kuimarisha nia na imani ya shakhsia muhimu na akili za wanaharakati wa nchi za Kiislamu na zisizo za Kiislamu wanaoamini kwamba inawezekana kujihami hata kwa mikono mitupu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, kumbukumbu, matukio na mafunzo yaliyopatikana katika kipindi cha miaka minane ya kujihami kutakatifu ni utamaduni wa kudumu na ni chemchemu ambayo kama itaeleweka na kutumiwa vyema, bila ya shaka yoyote itakuwa ni kwa manufaa ya taifa la Iran na mustakbali bora wa nchi.
Aidha ameashiria hatua ya madola ya Mashariki na Magharibi na vibaraka wao katika eneo la Mashariki ya Kati ya kuunda kambi kubwa ya kijeshi kwa ajili ya kukabiliana na Iran wakati wa vita hivyo na kuongeza kuwa, lengo la kambi hiyo lilikuwa ni kuudhoofisha na kuuondolea itibari mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na kuutumbukiza kwenye matatizo ya ndani na hatimaye kuandaa mazingira ya kuanguka Jamhuri ya Kiislamu, lakini mfumo huu wa Kiislamu na taifa la Iran lilikabiliana vilivyo na kambi hiyo na kutoka kwa heshima katika medani ya mapambano licha ya kwamba wakati huo Iran ilikuwa na matatizo mengi ukiwemo uchache wa suhula na zana za kijeshi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu vile vile ameashiria gharama zilizosababishwa na vita hivyo hasa mashahidi watukufu wa Mapinduzi ya Kiislamu na kuongeza kuwa, pamoja na kwamba gharama za kimaada na kimaanawi za vita hivyo vya kulazimishwa zilikuwa kubwa, lakini matunda yake kwa taifa la Iran yalikuwa makubwa mno ikilinganishwa na gharama hizo.
Mwanzoni mwa mkutano huo, Meja Jenerali Dk. Firuzabadi, Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa hotuba fupi na sambamba na kumshukuru Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa kuwaruhusu makamanda wa kijeshi kumtembelea, ameelezea kufurahishwa kwake na hali nzuri ya kiafya aliyomuona nayo Amirijeshi Mkuu wa vikosi vyote vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Aidha ametoa mkono wa baraka na fanaka kwa mnasaba wa maadhimisho ya Wiki ya Kujihami Kutakatifu na kusisitiza kuwa vikosi vya ulinzi nchini Iran viko imara katika kulinda matunda ya Mapinduzi ya Kiislamu.
 
< Nyuma   Mbele >

^