Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Ujumbe wa Hija 1435 Hijria Chapa
03/10/2014
Bismillahir Rahmanir Rahim

Na hamdu zote zinamstahikia Allah, Mola Mlezi wa viumbe wote na rehema na amani ziwe juu ya Muhammad na Aali zake watoharifu.
 Salamu na pongezi zangu zinazotokana na shauku kubwa zikufikieni nyote mliofanikiwa kuitikia labeika mwito wa Qur'ani Tukufu na kukimbilia kwa shauku kubwa kuwa wageni wa Nyumba ya Allah. Maneno yangu ya kwanza kabisa ni kwamba, thaminini vilivyo neema hii kubwa na muzingatie vipengee vya mtu binafsi na vya kijamii vya kiroho na kimataifa vya faradhi hii isiyo na mfano wake kwa ajili ya kufanya jitihada za kuyakurubia kadiri inavyowezekana malengo ya amali hii tukufu na kumuomba msaada na tawfiki Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye nguvu, azitie baraka jitihada zenu hizo. Mimi nami kwa upande wangu niko pamoja nanyi na kwa wakati mmoja ninamuomba maghufira na msaada Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema na ukarimu akutimizieni neema Zake, akupeni taufiki katika safari yenu ya Hija, akupeni nguvu za kutekeleza kikamilifu amali ya Hija, akutakabalieni amali zenu na akurudisheni makwenu mkiwa wazima wa afya, Inshaallah.
Mbali na kuitoharisha na kuijenga nafsi kimaanawi na kiroho suala ambalo ndilo lengo bora na la kimsingi zaidi la Hijja, mahujaji wanapaswa kutumia vizuri pia fursa yenye faida kubwa na ya kipekee ya Hija kwa ajili ya kuzingatia masuala ya ulimwengu wa Kiislamu na kuwa na mtazamo mpana na wa kila upande kuhusu masuala muhimu zaidi na vipaumbele vikubwa zaidi vinavyohusiana na umma wa Kiislamu. Hayo ni katika majukumu makubwa mno ya mahujaji.
Miongoni mwa masuala hayo muhimu na yanayostahiki kupewa kipaumbele kikubwa zaidi hivi sasa ni suala la mshikamano na umoja wa Waislamu na kutatua matatizo ambayo yanazusha mifarakano katika makundi mbali mbali ya umma wa Kiislamu. Hija ni dhihirisho la umoja na mshikamano na ni nguzo ya udugu na kusaidiana umma wa Kiislamu. Watu wote wanapaswa wapate somo la kuzingatia masuala yanayowaunganisha Waislamu na kuondoa hitilafu zao kupitia amali tukufu ya Hija. Mikono michafu ya siasa za kikoloni tangu zamani sana imekuwa ikizipa kipaumbele kikubwa njama za kuwafarakanisha Waislamu ili kufikia malengo yao maovu. Lakini leo hii siasa za kuzusha mizozo na mifarakano kati ya Waislamu zimekuwa kubwa zaidi kutokana na umma wa Kiislamu kuuelewa vizuri uadui wa kambi ya kibeberu na Kizayuni kwa baraka za mwamko wa Kiislamu na kutokana na kwamba tayari umma wa Kiislamu umeshachukua msimamo kuhusiana na uadui huo. Adui mwenye hila na kedi nyingi amekusudia kueneza moto wa vita na chuki kati ya Waislamu ili kuwapokonya Waislamu nia na azma ya muqawama na kupigana jihadi na hivyo kutoa mwanya kwa utawala wa Kizayuni na madola ya kibeberu wanaounga mkono jinai za utawala huo kuishi kwa salama na amani. Kuanzisha makundi ya kigaidi na kitakfiri na mfano wake ni moja ya mbinu zinazotumiwa na mabeberu katika nchi za eneo la magharibi mwa Asia katika siasa zake hizo za kibeberu. Hili ni onyo na tahadhari kubwa kwetu sisi sote ambayo inatuhimiza kwamba kadhia ya umoja na mshikamano wa Waislamu leo hii tuifanye kuwa suala muhimu zaidi katika majukumu yetu ya kitaifa na kimataifa.
Suala jingine muhimu ni kadhia ya Palestina. Baada ya kupita miaka 65 ya tangu kuundwa utawala huo ghasibu na kushuhudiwa hali mbali mbali za kupanda na kushuka zilizoandamana na suala hilo nyeti na muhimu mno, hususan matukio ya umwagaji damu ya miaka ya hivi karibuni, hivi sasa kuna masuala mawili muhimu makuu yako wazi zaidi katika kadhia hiyo. Mosi ni kwamba utawala wa Kizayuni na waungaji mkono wake watenda jinai, hawakujiwekea mipaka yoyote katika kufanya ukatili na ubedui wao na kukanyaga misingi yote ya kibinadamu na kimaadili. Kwa kweli hawakujiwekea kizuizi chochote cha kutenda jinai, kufanya mauaji ya kizazi, kufanya uharibifu, kuua watoto wadogo na wanawake wasio na pa kukimbilia na kutenda kila aina ya dhulma na uonevu wanaoweza kuufanya, bali hata wanaona fakhari kufanya ukatili na jinai hizo. Matukio ya kuliza na kuhuzunisha mno ya vita vya siku 50 vya hivi karibuni huko Ghaza ni mfano wa karibuni kabisa wa unyama huo wa kihistoria ambao tab'an katika nusu karne iliyopita, matukio kama hayo yameshuhudiwa sana.
Uhakika wa pili ni kwamba uhayawani na ukatili huo mkubwa umeshindwa kufanikisha malengo ya viongozi wa utawala ghasibu wa Kizayuni na waungaji mkono wao. Tofauti na tamaa za kipumbavu walizo nazo wanasiasa makhabithi wa utawala wa Kizayuni wanaotamani kuufanya utawala huo kuwa imara na wenye nguvu kubwa; kadiri siku zinavyopita ndivyo utawala huo unavyozidi kukaribika kusambaratika na kuangamia. Kusimama kidete kwa muda wa siku khamsini wananchi wa Ghaza - waliozingirwa kila upande wakiwa hawana sehemu ya kukimbilia - mbele ya nguvu zote za utawala wa Kizayuni ulizozitumia katika mashambulizi yake dhidi ya ukanda huo, hatimaye kumeulazimisha utawala huo ghasibu kurudi nyuma na kusalimu amri mbele ya masharti ya muqawama na huo ni uthibitisho wa wazi kabisa wa udhaifu, utule na udhalili wa utawala huo mbele ya irada thabiti ya taifa la Palestina. Hii ina maana kwamba taifa la Palestina linapaswa kuwa na matumaini makubwa zaidi kuliko huko nyuma, wanamapambano wa Jihadul Islami na Hamas nao wanapaswa kuongeza jitihada, nia na hima yao, Ukingo wa Magharibi (wa Mto Jordan nao) ufuate njia ya siku zote na iliyojaa fakhari kwa nguvu zake zote na kwa uimara mkubwa, watu wa mataifa ya Kiislamu nao wazitake tawala zao kuiunga mkono kikwelikweli Palestina na tawala za Waislamu nazo zifuate njia hiyo kiukweli na kiikhlasi.
Suala la tatu muhimu na ambalo inabidi lipewe kipaumbele kikubwa hivi sasa, ni mtazamo wanaopaswa kuwa nao wanaharakati wenye uchungu wa ulimwengu wa Kiislamu nao ni mtazamo wa kuchanganua mambo vizuri na kujua tofauti iliyopo baina ya Uislamu wa kweli wa Bwana Mtume Muhammad (SAW) na Uislamu wa Kimarekani, wawe macho wasije wakafanya makosa katika kutofautisha aina hizo mbili za Uslamu na wawatahadharishe wengine kuhusu suala hilo. Mtu wa kwanza kuingiza istilahi hiyo katika kamusi ya kisiasa ya ulimwengu wa Kiislamu alikuwa ni Imam wetu mtukufu (Imam Khomeini - quddisa sirruh) ambaye alitutia hima ya kutofautisha baina ya aina mbili hizo za Uislamu. Amma Uislamu wa asili na wa kweli ni Uislamu ulionyooka na wenye umaanawi, ni Uislamu wa kujiepusha na maasi, ni Uislamu wa kidemokrasia, ni Uislamu wa أَشِدَّاء عَلَى الْكُفَّارِ رُحَمَاء بَيْنَهُمْ wana nguvu mbele ya makafiri, na wanahurumiana wao kwa wao (Suratul Fat'h 48: 29). Amma Uislamu wa Kimarekani ni wa kuvaa mavazi ya Kiislamu na kuwa kibaraka wa wageni na maadui wa umma wa Kiislamu. Ni Uislamu wa kuwasha moto wa fitna na mifarakano kati ya Waislamu. Ni Uislamu wa watu ambao, badala ya kutegemea ahadi za Mwenyezi Mungu, wanawatemegea maadui wa Mwenyezi Mungu na badala ya kupambana na Uzayuni na ubeberu wanapigana na ndugu zao Waislamu. Ni Uislamu wa watu ambao wanaungana na dola la kibeberu la Marekani dhidi ya mataifa mengine ya Waislamu. Huo si Uislamu, huo ni unafiki wa hatari sana na wenye kuangamiza ambao kila Muislamu mwenye imani ya kweli anapaswa kupambana nao.
Kwa hakika kuwa na mtazamo wa mbali na wa kina kuhusu matukio na masuala muhimu kunaweka wazi uhakika wa ulimwengu wa Kiislamu kwa kila mtu anayetafuta haki na kunambainishia kwa uwazi kabisa jukumu na wajibu anaotakiwa kuufanya katika wakati husika bila ya utata wa aina yoyote ile. Hija na amali zake ni fursa nzuri sana kwa ajili ya kuwa na muono wa mbali. Ni matumaini yangu kuwa nyinyi nyote mliofanikiwa kwenda kutekeleza ibada tukufu ya Hija mtastafidi vizuri mno na kikamilifu na zawadi hiyo ya Mwenyezi Mungu. Ninakuombeeni kila la kheri kutoka kwa Mwenyezi Mungu nikimuomba akutakabalieni jitihada na ibada zenu.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullah.

Sayyid Ali Khamenei,
Mwezi Tano Dhilhijja 1435 (Hijria) sawa na tarehe 8 Mehr 1393 (Hijria Shamsia)
(Septemba 29, 2014 Milaadia).

 
< Nyuma   Mbele >

^