Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Aonana na Matabaka Mbali Mbali ya Wananchi Chapa
13/10/2014
 - Kwa mnasaba wa sikukuu tukufu ya Ghadir
Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, leo asubuhi (Jumatatu) ameonana na maelfu ya wananchi wa matabaka mbali mbali katika maadhimisho ya sikukuu tukufu ya Ghadir.
Katika mkutano huo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, kuteuliwa Amirul Muminin (Imam Ali AS) kuwa Imam na hatua ya Uislamu ya kuzingatia siasa na utawala ni masuala mawili muhimu na ya kimsingi ya tukio la Ghadir Khum na kusisitizia udharura mkubwa mno wa kuweko umoja na mshikamano kati ya Waislamu.
Ameongeza kuwa, mtu yeyote au hatua yoyote ile itakayopelekea kuchochea chuki na hisia mbaya za upande fulani wa Waislamu na kueneza chuki baina ya Waislamu wa Kishia na Kisuni basi itakuwa ni kwa faida ya Marekani, Uingereza khabithi na Uzayuni yaani waliozusha makundi ya kijahili, yenye fikra mgando na ya kitakfiri ya vibaraka wao.
Ayatullah Udhma Khamenei aidha ametoa mkono wa baraka kwa mnasaba wa sikukuu tukufu ya Ghadir na kulitaja tukio muhimu na lenye matukufu mengi la Ghadir Khum kuwa ni katika masuala yaliyothibiti na yasiyo na shaka hata chembe katika historia ya Uislamu akiongeza kuwa: Hakuna mfuasi wa kundi lolote lile la Waislamu anayepinga asili ya kutokea tukio la Ghadir Khum au anayepinga maneno matukufu ya Mtume Mtukufu wa Mwisho SAW yaani aliposema, yeyote ambaye mimi ni walii ninayesimamia mambo yake basi na huyu Ali ni walii na msimiaji wa mambo yake.
Ameongeza kuwa: Utata unaoingizwa kwenye fikra za baadhi ya watu kuhusu maana ya maneno hayo ya kihistoria ya Bwana Mtume Muhammad SAW ndio ule ule uliokuwa ukisemwa miaka elfu moja nyuma na ambao maulamaa wakubwa tayari wameupatia majibu yake tangu zamani.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria maana maarufu ya maneno hayo matukufu ya Bwana Mtume Muhammad SAW katika siku ya Ghadir Khum yaani kumteua Amirul Muminin Ali Alayhis Salaam kuwa Imam na pia wasii wake na kuongeza kuwa: Maneno hayo ya Bwana Mtume yana pia maana nyingine muhimu ambayo hatupaswi kuisahau nayo ni namna Uislamu ulivyolipa umuhimu mkubwa suala la uongozi na siasa katika umma wake.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria pia propaganda zenye malengo maalumu zinazofanywa na maadui wa umma wa Kiislamu za kujaribu kuuvua Uislamu na siasa na kuifanya dini hiyo tukufu kuwa ya watu binafsi tu na kuongeza kuwa: Tukio la Ghadir Khum ni mantiki ya wazi na madhubuti sana ya Uislamu ya kupinga mtazamo huo wa kisekula wa kutenganisha dini na siasa kwani Ghadir Khum ni dhidirisho la namna Uislamu unavyozingatia na kutilia mkazo mno suala la utawala na siasa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu vile vile amepinga fikra inayosema kwamba kuteuliwa Imam Ali AS na Bwana Mtume Muhammad SAW kuwa Imam wa Waislamu kwamba kulifanyika kwa masuala ya kimaanawi tu na kuongeza kwamba: Masuala ya kimaanawi si kitu cha mtu kuteuliwa, hivyo maana halisi ya tukio lililojaa baraka la Ghadir ni kuzingatia suala la utawala pamoja na kuongoza na kusimamia mambo ya jamii na kwamba hilo ni somo na funzo kubwa la tukio la Ghadir kwa Waislamu wote.
Ayatullah Udhma Khamenei amelitaja suala la Ghadir kuwa ni suala la kiitikadi, la kiusuli na la kimsingi la Waislamu wa Kishia na hapo hapo akaongeza kuwa: Sehemu ya kuweza kujadiliwa na kutolewa mantiki yenye nguvu na hoja madhubuti za Waislamu wa Kishia kuhusiana na Ghadir Khum ni mikusanyiko ya kielimu na kiutaalamu hivyo mjadala wa suala hilo haupaswi kuingizwa kwenye maisha ya Waislamu wote na kulitumia kuzusha mizozo na mijadala ya chuki na uhasama katika safu za Waislamu.
Hapo hapo pia Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia siasa kuu za waistikbari na mabeberu duniani yaani kuzusha na kupalilia mizozo na mifarakano kati ya madhehebu na makundi tofauti ya Waislamu hususan baina ya Waislamu wa Kishia na Kisuni na kuongeza kuwa: Mizozo kati ya Waislamu bila ya shaka yoyote inapelekea nguvu, hima na misukumo yote ya Waislamu ielekezwe kwenye mizozo ya ndani na kusahauliwa maadui wakubwa na wa asili wa Waislamu wote na hilo ndilo lengo la wakoloni na waistikbari ambao wameliwekea mipangilio kabambe ya kulifanikisha.
Ayatullah Udhma Khamenei amelitaja suala la kukabilia ana fikra zenye mvuto mkubwa na zinazotoa muongozo mzuri za Jamhuri ya Kiislamu kuwa ndilo lililowafanya mabeberu wawekeze sana katika suala la kueneza chuki na mizozo kati ya Waislamu na kuongeza kuwa: Marekani, Uzayuni na bingwa mkongwe wa kueneza mifarakano yaani serikali khabithi ya Uingereza, zimeelekeza nguvu zao kwenye kuzusha hitilafu na kupotosha fikra za Waislamu wa Kishia na Kisuni tangu baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran ili kuwafanya Waislamu wasishughulishwe na maadui wao wakubwa na wa asili na wajishughulishe tu na mizozo na mifarakano baina yao.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekutaja kuzuka makundi ya kitakfiri katika nchi za Iraq na Syria na kwenye baadhi ya nchi nyingine duniani kuwa ni matunda ya mipango ya mabeberu na waistikbari ya kuzusha mifarakano na mizozo kati ya Waislamu na kuongeza kuwa: Mabeberu wameanzisha makundi ya al Qaida na Daesh kwa ajili ya kuzusha mizozo na kukabiliana na Jamhuri ya Kiislamu lakini leo hii balaa la makundi hayo limewakumba hata wao wenyewe.
Vile vile ameashiria matukio yanayoendelea hivi sasa katika eneo la Mashariki ya Kati na kuongeza kuwa: Mtazamo wa kina na uliofanyiwa uchunguzi makini wa matukio hayo unaonesha kuwa katika madai yao yao uongo ya kukabiliana na kundi la Daesh, Marekani na waitifaki wake wanalenga zaidi katika suala la kuzidisha uadui na mizozo kati ya Waislamu na wala hazilengi kuliangamiza kundi hilo (ambalo wao wenyewe ndio waliolianzisha na kulitia nguvu).
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza pia kuwa kila mtu ambaye ameshikamana na Uislamu na ambaye anaukubali utawala wa Qur'ani Tukufu, ni sawa tu awe Muislamu wa Kishia au Muislamu wa Kisuni ajue kuwa, siasa za Kimarekani - Kizayuni ndiye adui mkuu na wa asili wa Uislamu na Waislamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja suala la kuwa makini na kujiepusha kikamilifu na kuchochea hisia za makundi mengine ya Waislamu kuwa ni jukumu kuu la Waislamu wote na kuongeza kuwa: Waislamu wa Kishia na Kisuni watambue kwamba hatua yoyote ile au neno lolote lile ikiwa ni pamoja na kuvunjia heshima matukufu ya upande wa pili, hupelekea kuzuka hisia kali na moto wa chuki katika nyoyo za watu na jambo hilo bila ya shaka yoyote ni kwa faida ya adui wa Waislamu wote kwa pamoja.
Mwishoni mwa hotuba yake, Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria kushindwa njama zote za mabeberu wa dunia katika kipindi chote cha miaka 35 iliyopita (ya tangu kupata ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran na kuundwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu) na kusisitiza kuwa: Kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu, njama za maadui wa taifa hili hivi sasa pia zitashindwa na kwamba Waislamu wote wanaoishi katika Iran ya Kiislamu nao wataendelea kutekeleza vizuri majukumu yao kwa busuri na kwa muono wa mbali.
 
< Nyuma   Mbele >

^