Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Aonana na Katibu Mkuu wa Jihadul Islami ya Palestina Chapa
16/10/2014
 Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu leo asubuhi (Alkhamisi) ameonana na Bw. Ramadhan Abdullah, Katibu Mkuu wa harakati ya Jihadul Islami ya Palestina na ujumbe alioandamana nao na huku akionesha kufurahishwa sana na ushindi wa wananchi wanamuqawama wa Ghaza katika vita vya siku 51 vya hivi karibuni na jinsi utawala wa Kizayuni ulivyokiri kushindwa kukabiliana na wananchi hao waliozingirwa kila upande, ameutaja ushindi huo mkubwa kuwa ni dhihirisho la wazi la kutimia ahadi ya nusra ya Mwenyezi Mungu na ni bishara njema na kupatikana ushindi mwingine mwingi mkubwa katika siku za usoni.
Aidha Ayatullah Udhma Khamenei amemwambia Katibu Mkuu huyo wa Jihadul Islami kwa kusisitiza kwamba, Jamhuri ya Kiislamu na wananchi wa Iran wanaona fakhari kutokana na ushindi na kusimama kwenu kidete na ni matumaini yetu kuwa mlolongo wa ushindi wa kila namna wa muqawama utazidi kushuhudiwa siku baada ya siku hadi kufikia kwenye ushindi kamili.
Ayatullah Udhma Khamenei amevitaja vita vya siku 51 na muqawama wa eneo dogo la Ghaza lenye idadi ndogo ya watu na suhula chache mbele ya utawala katili na wenye jeshi lililojizatiti kwa kila aina ya silaha na zana za kijeshi na uungaji mkono wa kila namna wa madola ya kibeberu kuwa ni suala muhimu na la kustaajabisha na kuongeza kuwa: Kwa mahesabu na uchambuzi wa kawaida, ilibidi utawala wa Kizayuni ambao una silaha na zana zote hizo za kijeshi ungelipata ushindi katika zile siku za awali kabisa za mashambulizi yake huko Ghaza lakini matokeo yake ni kuwa mwishowe umekiri kushindwa kufikia malengo yake katika vita hivyo, bali pia umelazimika kusalimu amri na kupigia magoti masharti ya muqawama.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu vile vile ameashiria ahadi mbali mbali za Mwenyezi Mungu za kuwasaidia watu wanaopigana jihadi katika njia Yake na kuongeza kuwa: Hatua ya wananchi wa Ghaza ya kuwa pamoja na muqawama kwa njia ya kustaajabisha na bila ya kuchoshwa na mashambulizi yasiyosita ya adui na kuuliwa kikatili zaidi ya wananchi elfu mbili ikiwemo idadi kubwa ya wanawake na watoto wadogo si jambo lililotokea vivi hivi bila ya kuwepo rehema na msaada wa Mwenyezi Mungu.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kuwa: Kutimia ahadi za Mwenyezi Mungu katika medani hiyo kunathibitisha kuwa ahadi hizo zitatimia pia kwenye medani kubwa na pana zaidi na amemkhutubu Katibu Mkuu wa Jihadul Islami ya Palestina akimwambia: Mapenzi ya Allah yanaonekana wazi kuwa yanataka kadhia ya Palestina ifikie ushindi kamili kwa mikono yenu.
Ameongeza kwamba, kuna udharura wa kuwa macho mbele ya njama tata za adui dhidi ya muqawama na hapo hapo amesisitizia mikakati na stratijia mbili kuu zinazopaswa kuchukuliwa katika uwanja huo.
Ayatullah Udhma Khamenei amegusia kuwa, si jambo lililo mbali kwa utawala wa Kizayuni kufanya uvamizi mwingine na kukumbusha kwamba: Mrengo wa muqawama unapaswa kuwa tayari na imara zaidi wakati wote na ujiimarishe na kuongeza nguvu zake zaidi na zaidi ndani ya Ukanda wa Ghaza.
Akizungumzia mkakati na stratijia ya pili, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, kuna haja ya kuweka mipango kabambe na madhubuti ya kulifanya eneo la Ukingo wa Magharibi wa mto Jordan nalo lisimame kupambana na utawala wa Kizayuni (kama unavyofanya Ukanda wa Ghaza) na kwamba suala hilo linapaswa kuwa mpango wa kimsingi wa wanamuqawama.
Amesisitiza kwamba, vita na utawala wa Kizayuni ni vita muhimu mno ambavyo inabidi vilifikishe taifa la Palestina kwenye ushindi kamili na inabidi kuwekwe mipangilio mizuri katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan ambayo itamfanya adui Mzayuni akumbwe na woga ule ule unaomkumba kila anapoufikiria Ukanda wa Ghaza.
Mwishoni mwa miongozo yake, Ayatullah Udhma Khamenei amesema kuwa, hali iliyopo hivi sasa katika eneo la Mashariki ya Kati ni nyeti na tata mno na kuongeza kwamba: Tab'an mustakbali wa matukio yanayojiri katika eneo hili uko wazi na ni mzuri na kwamba ni matumaini yetu kuwa, Mwenyezi Mungu Mtukufu atatuongoza katika kile chenye maslahi kwa umma wa Kiislamu na Palestina na ambacho kitaweza kubatilisha njama zote za adui.
Katika mazungumzo hayo, Bw. Ramadhan Abdullah, Katibu Mkuu wa harakati ya Jihadul Islami ya Palestina naye ameelezea kufurahishwa kwake na hali njema na uzima wa kiafya aliomuona nao Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na amesema akimkhutubu Kiongozi Muadhamu kwamba: Ndugu wote wa muqawama pamoja na Jihadul Islamu wanakuombea dua za mafanikio na afya njema kila wanaposali na tunamuomba Mwenyezi Mungu atuwafikishe kufika katika wakati ambao tutasali pamoja na wewe ndani ya Masjidul Aqsa.
Vile vile ametoa ripoti ya vita vya siku 51 vya hivi karibuni vya Ghaza na kumpongeza Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kutokana na ushindi wa kujivunia waliopata wanamuqawama katika vita hivyo.
Amesema, ni jambo la yakini na lisilo na chembe ya shaka kwamba ushindi huo umepatikana kutokana na misaada na uungaji mkono wa kila hali wa Jamhuri ya Kiislamu kwa taifa la Palestina na lau kama si misaada ya maana na ya kiistratijia ya Iran, basi wananchi wa Palestina huko Ghaza wasingeliweza kusimama kidete wala kupata ushindi mbele ya uvamizi wa utawala wa Kizayuni.
Bw. Ramadhan Abdullah ameongeza kuwa, miongozo iliyokuwa inatolewa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu wakati vita vya siku 51 vilipokuwa vinaendelea huko Ghaza na kusisitiza kwake kuhusu umuhimu wa kuzatitiwa kwa silaha Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan ili uweze kukabiliana ipasavyo na siasa za kupenda vita za utawala wa Kizayuni kama unavyofanya Ukanda wa Ghaza, ni suala muhimu la kiistratijia na ni njia bora ya utatuzi ambayo itazidi kuwatia moyo na kuwaongezea nguvu maradufu wanamapambano wa Palestina.
Katibu Mkuu wa Jihadul Islami ya Palestina aidha ameashiria ahadi zilizotolewa na baadhi ya nchi duniani za kusaidia katika kuujenga upya Ukanda wa Ghaza na kusema kuwa: Sisi hatuna matumaini sana na ahadi zilizotolewa na nchi hizo, bali matumaini yetu makubwa yako kwa Mwenyezi Mungu, kwani tunaamini kuwa ni Yeye Ndiye atakayetusaidia kuijenga upya Ghaza kutokana na hasara zilizosababishwa na mashambulizi ya utawala dhalimu wa Kizayuni.
 
< Nyuma   Mbele >

^