Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Aonana na Wasimamiaji wa Amali ya Hija ya 1435 Hijria Chapa
28/10/2014
 Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, leo asubuhi (Jumanne) ameonana na viongozi na maafisa wa Iran waliosimamia amali ya Hija ya 1435 Hijria na kusema kuwa, ni jambo la dharura mno kuwa na mipangilio mizuri ya kuhakikisha kwamba faida na manufaa ya ibada ya Hija yanakuwa mengi zaidi na zaidi kupitia kuwa na mtazamo wa kimapinduzi na kiubunifu katika kutoa majibu ya mahitaji ya kimaanawi na kifikra ya walengwa na vile vile katika kupambana na shubha na propaganda za uongo zinazoenezwa na maadui dhidi ya Uislamu.
Amesisitiza kuwa, kujaribu kuweka ukuta baina ya Jamhuri ya Kiislamu na sehemu nyingine za ulimwengu wa Kiislamu ni moja ya njama zinazofanywa na maadui wa umoja wa umma wa Kiislamu na kwamba inabidi fursa ya Hija ambayo ni mkusanyiko mkubwa mno wa umma wa Kiislamu, itumiwe vizuri kwa ajili ya kuvunja ukuta huo bandia unaowekwa na maadui na vile vile fursa hiyo itumiwe kwa njia bora zaidi katika kusahihisha mitazamo na imani zisizo sahihi zilizojengeka katika fikra za baadhi ya watu kutokana na propaganda za uongo za maadui.
Ayatullah Udhma Khamenei amebainisha pia suala la kustawisha na kuongeza faida za ibada tukufu ya Hija katika nyuga mbili za kustawisha huduma na vile vile kudhamini mambo matukufu ya ndani ya Hija yanayohitajiwa na Mahujaji na kuongeza kuwa: Kuongeza inavyopasa manufaa na faida za Hija kutaweza kufanikishwa kupitia kutoa majibu ya mahitaji ya kifikra na kimaanawi ya Mahujaji ambapo katika suala hilo, inabidi kuwekwe mipangilio mizuri itakayoongeza ubora wa utekelezaji wa amali zinazofanyika hivi sasa kama vile usomaji na uenezaji wa dua ya Kumeil, amali ya kujibari na washirikina na kufanyika semina na makongamano mbali mbali na vile vile kutolewa majibu kwa mtazamo wa kimapinduzi na kiubunifu kuhusu mahitaji ya kifikra ya Mahujaji kuhusiana na masuala muhimu yaliyopo leo hii kwenye ulimwengu wa Kiislamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amefafanua zaidi jambo hilo kwa kuashiria suala muhimu la umoja na mshikamano wa Kiislamu ambalo ndilo jambo linalohitajiwa mno hivi sasa katika ulimwengu wa Kiislamu na kuongeza kuwa: Umoja na udugu baina ya Waislamu ni moja ya misingi mikuu ya dini yetu ya Kiislamu na kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haiumuogopi wala kumuonea haya mtu yeyote katika juhudi zake za kufanikisha suala hilo muhimu.
Vile vile amebainisha kuwa, umoja na mshikamano wa Kiislamu hauna maana ya kuachana na itikadi za kimadhehebu za makundi mbali mbali ya Waislamu na kuongeza kuwa: Umoja wa Waislamu ambao ndiyo nara na kaulimbiu kuu ya Jamhuri ya Kiislamu una maana ya kuhakikisha kuwa umma wa Kiislamu haufanyiani uadui na unasaidiana katika masuala muhimu duniani.
Ayatullah Udhma Khamenei amekumbushia ubunifu uliofanywa na Imam Khomeini (quddisa sirruh) katika kuifanya kaulimbiu na shaari ya Umoja wa Kiislamu kuwa siasa rasmi na ya wazi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuongeza kwamba, njama zinazofanywa na maadui za kujaribu kuvunja siasa hizo za Imam Khomeini (qudissa sirruh) ziko wazi, nazo ni kujaribu kujenga ukuta utakaoitenganisha Iran na maeneo mengine ya ulimwengu wa Kiislamu na kusisitiza kuwa: Kila mtu ana jukumu la kufanya juhudi za kuuvunja ukuta huo bandia na kwamba ibada tukufu ya Hija nayo ambayo ni "mahshar" na mkusanyiko mkubwa wa Waislamu, inabidi itumiwe kwa njia bora zaidi katika jitihada hizo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameendelea na hotuba yake kwa kuashiria "shubha," utata na propaganda kubwa za uongo zinazoenezwa na adui kwa lengo la kupandikiza fikra potofu na taswira zisizo sahihi kuhusiana na madhehebu ya Kishia, Jamhuri ya Kiislamu na Iran yetu azizi, ikiwa hiyo ni moja ya njama za maadui za kujaribu kuitenga Jamhuri ya Kiislamu na sehemu nyingine za ulimwengu wa Kiislamu na kusisitiza kuwa: Kuandika tu vitabu kujibu "shubha" na utata huo unaoingizwa na maadui, hakutoshi, bali inabidi kufanyike utafiti wa kina kuhusu namna ya kutumia vizuri mbinu za kila namna na nyingi za mawasiliano zilizopo duniani hivi sasa, ili kusahihisha mitazamo hiyo bandia iliyopandikizwa kupitia propaganda za uongo za maadui.
Mwishoni mwa hotuba yake, Ayatullah Udhma Khamenei amesisitizia udharura wa kuchunguza na kugunduliwa njia na mbinu zinazotumiwa na maadui zinazopelekea watu kuziamini propaganda za uongo zinazoenezwa na maadui na kutafuta njia bora za kupambana na propaganda hizo.
Mwanzoni mwa mkutano huo, Hujjatul Islam Walmuslimin Kadhi Askari, Mwakilishi wa Fakihi Mtawala na Msimamiaji wa Mahujaji wa Kiirani, ametoa ripoti fupi kuhusiana na ratiba zilizokuwemo kwenye amali ya Hija ya mwaka 1435 Hijria na kusema kuwa: Kulipa uzito wa hali ya juu suala la kusoma Qur'ani, tafsiri na hifdhi ya Qur'ani Tukufu, kutekelezwa kwa ufanisi wa hali ya juu ratiba za kusoma dua ya Kumeil na dua ya Arafa, kutumia vizuri wataalamu na wanavyuoni wenye uzoefu katika kubainisha mafundisho ya amali tukufu ya Hija, kuzienzi familia za mashahidi na kuwakirimu majeruhi wa vita, kufanya vikao vya kubadilishana mawazo na fikra wanavyuoni mbali mbali katika Hija na kufanyika semina na makongamano tofauti yakiwa na mada za kutia nguvu mafundisho na imani za dini, kadhia ya Palestina, Ahlul Bayt Alayhimus Salaam na umoja na mshikamano katika ulimwengu wa Kiislamu, ni miongoni mwa ratiba na kazi zilizofanywa na Biitha ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika msimu uliopita wa Hija.
Naye Bw. Awhadi, Mkuu wa Taasisi ya Hija na Ziara ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa ripoti fupi kuhusu ratiba za taasisi hiyo katika msimu uliopita Hija na kusema kuwa, katika msimu huo, kulikuwa na mahujaji 64 elfu wa Iran waliokwenda Hija kupitia misafara 451 na kuongeza kuwa: Kutokana na juhudi zilizofanyika, asilimia 50 ya mahitaji ya Mahujaji wa Kiislamu yalidhaminiwa ndani ya Iran na kwamba suhula muhimu kama vile sehemu za kufikia, usafiri na mahitaji ya chakula ya Mahujaji yalikuwa katika sura inayotakiwa kabisa.
 
< Nyuma   Mbele >

^