Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Kiongozi Muadhamu Aonana na Washiriki wa Kongamano la Mirengo ya Kitakfiri kwa Mtazamo wa Maulamaa Chapa
25/11/2014
 Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu leo asubuhi (Jumanne) ameonana na maulamaa, wanavyuoni, wasomi na wageni walioshiriki kwenye Kongamano la Kimataifa la Mirengo ya Kitakfiri kwa Mtazamo wa Maulamaa wa Kiislamu na kulitaja suala la kuzuka upya makundi ya kitakfiri katika miaka ya hivi karibuni kuwa ni tatizo lililopandikizwa na mabeberu katika ulimwengu wa Kiislamu. Vile vile ameashiria namna vitendo vya kikhabithi vya makundi hayo yanayokufurisha Waislamu wengine vinavyotumikia malengo ya Marekani na madola ya kikoloni na utawala wa Kizayuni na hasa hasa njama za makundi hayo za kujaribu kulififilizisha na kulisahaulisha suala muhimu zaidi la ulimwengu wa Kiislamu yaani kadhia ya Palestina na Masjidul Aqsa na kusisitiza kuwa, kuleta mwamko wa kielimu, kimantiki na mkubwa kwa ajili ya kung'oa mizizi ya fikra za kitakfiri, kuamsha watu kuhusiana na njama za mabeberu za kufufua makundi hayo ya kitakfiri na kulipa umuhimu mkubwa suala linalopiganiwa na wote yaani kadhia ya Palestina likiwa ni suala kubwa zaidi katika ulimwengu wa Kiislamu, ni miongoni mwa majukumu makubwa zaidi yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza na maulamaa wa ulimwengu wa Kiislamu hivi sasa.
Mwanzoni mwa hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewashukuru Maayatullah Makarim Shirazi, Sobhani na maulamaa wengine wakubwa wa Qum, Iran, kwa kulipa umuhimu mkubwa suala la kufanyika kongamano hilo na kuanzisha harakati kubwa ya kielimu baina ya maulamaa wa ulimwengu wa Kiislamu kuhusiana na suala zima la kukabiliana na makundi ya kitakfiri na kusema kuwa, inabidi kuzingatia nukta hii muhimu katika kujadili fikra hizo za hatari sana za kitakfiri kwamba kadhia muhimu zaidi hapa ni kupambana kwa pande zote na njama nzima ya kufufua fikra za kitakfiri, suala ambalo ni kubwa zaidi ikilinganishwa na kundi moja tu linaloitwa Daesh kwani kwa hakika Daesh ni sehemu moja tu ya matawi ya mti huo khabithi.
Baada ya hapo, Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria nukta moja muhimu na isiyokanushika akisisitiza kuwa, fikra za kitakfiri na tawala zinazounga mkono fikra hiyo yanatumikia kikamilifu malengo ya kibeberu yaani Marekani na madola ya kikoloni ya Ulaya na utawala wa Kizayuni, na ijapokuwa tawala zinazounga mkono fikra hizo zinaonekana kuwa ni za Waislamu, lakini katika uhalisia wake zinatumikia malengo ya mabeberu.
Ameendelea na hotuba yake kwa kutoa mifano kadhaa ya wazi inayothibitisha kuwa, fikra ya kitakfiri inatumikia malengo ya kibeberu dhidi ya ulimwengu wa Kiislamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja suala la kujaribu kupotosha harakati ya mwamko wa Kiislamu kuwa ni ushahidi wa kwanza wa kuthibitisha kwamba fikra ya kitakfiri inatumikia malengo ya mabeberu na kuongeza kuwa: Mwamko wa Kiislamu ni harakati iliyo dhidi ya Umarekani, iko dhidi ya ukandamizaji, iko dhidi ya watu wanaojifanya vibaraka wa Marekani lakini makundi ya kitakfiri yamezuka ili kukabiliana na harakati hiyo adhimu iliyo dhidi ya ubeberu na kuifanya kuwa vita vya wenyewe kwa wenyewe na mauaji ya Waislamu kwa Waislamu.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa, mstari wa mbele wa mapambano ya Waislamu wa eneo hili ni Palestina inayokaliwa kwa mabavu, lakini makundi ya kitakfiri yamegeuza mstari huo na kuingia kwenye mitaa na miji ya nchi za Iraq, Syria, Pakistan na Libya na kwamba hiyo ni moja ya jinai kubwa sana zisizoweza kusahaulika zinazofanywa na makundi hayo ya kitakfiri.
Amesema, kupotosha harakati ya mwamko wa Kiislamu ni kuitumikia Marekani, Uingereza na utawala wa Kizayuni pamoja na mashirika yao ya kijasusi. Ameongeza kuwa: Ushahidi mwingine unaothibitisha kwamba vitendo vya makundi hayo vinatumikia malengo ya mabeberu ni kwamba wanaoendesha fikra hiyo ya kitakfiri hawasemi lolote dhidi ya utawala wa Kizayuni bali wanafikia hata kushirikiana na utawala huo dhidi ya Waislamu. Lakini hao hao utawaona wako mstari wa mbele katika vitendo vya kutoa pigo kwa nchi na mataifa ya Waislamu.
Ayatullah Udhma Khamenei amevitaja vitendo vya kuangamiza miundombinu yenye thamani kubwa ya nchi za Kiislamu vinavyofanywa na makundi hayo yanayoeneza fitna katika ulimwengu wa Kiislamu kuwa ni mfano mwingine unaothibitisha kwamba makundi hayo yanatumikia malengo ya maadui wa Uislamu na kuongeza kuwa: Hatua nyingine ya kikhabithi zaidi ya makundi ya kitakfiri ni kupotosha sura halisi ya Uislamu ambayo ni dini ya mapenzi, ya kimantiki, ya kufanya mambo kiakili na ya kuhurumiana, na kuonesha picha za jinai kubwa zinazofanywa na makundi hayo kama za kuchinja watu wasio na hatia, kupasua mwili na kutoa moyo wa Muislamu na kuutafuna tafuna kwa meno mbele ya kamera tena kwa jina la Uislamu!
Amesema, ushahidi mwingine wa kwamba makundi ya kitakfiri yanayotumikia malengo ya mabeberu ni kutojali kwao hata kidogo jinai zilizofanywa na utawala wa Kizayuni katika mashambulizi yake ya siku 50 huko Ghaza na kuwatelekeza Wapalestina katika mashambulizi hayo ya Ghaza akiongeza kuwa, ushahidi mwingine ni namna makundi hayo ya kitakfiri yanavyopotosha hamasa na mwamko walioupata vijana wa ulimwengu wa Kiislamu baada ya kutokea mwamko wa Kiislamu katika ulimwengu huo na inasikitisha kuona kuwa makundi hayo yanatumia vibaya hamasa hizo za vijana wa Kiislamu na moto walioua nao vijana hao, katika kuua Waislamu wengine wasio na hatia.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametaja mfano mwingine kuwa ni hatua ya hivi karibuni na ambayo imekuwa ikikaririwa mara kwa mara ya ndege za Marekani kulirushia silaha za kijeshi kundi linaloitwa Daesh huko Iraq na kusisitiza kuwa: Pamoja na Marekani kufanya hivyo lakini inadai kuwa imeunda muungano wa kupambana na Daesh, jambo ambalo kwa hakika ni uongo wa wazi kwani lengo kuu la muungano huo ni kuhakikisha kwamba fitna ya vita na mapigano kati ya Waislamu inaendelea kuwepo, lakini tab'an hawataweza kufikia malengo yao hayo.
Baada ya hapo, Ayatullah Udhma Khamenei ameendelea na hotuba yake kwa kuzungumzia majukumu makubwa waliyo nayo maulamaa wa ulimwengu wa Kiislamu hivi sasa na kuongeza kuwa: Moja ya malengo hayo ni maulamaa hao wa madhehebu mbali mbali kuleta mwamko wa kielimu, wa kimantiki na mkubwa kwa ajili ya kung'oa kikamilifu mizizi ya fikra ya kitakfiri.
Amesema: Mrengo huo wa kitakfiri unatumia kaulimbiu ya uongo ya kudai kuwa ni Salafus Salih, hivyo inabidi kutumia lugha ya dini, elimu na mantiki kuthibitisha kuwa Salafus Salih iko mbali kabisa na vitendo vya mrengo huo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Inabidi vijana wasio na hatia waliokumbwa na mkumbo huo khabiti waokolowe kupitia mwamko huo wa kielimu na kimantiki, na kwamba hilo ni jukumu linalopaswa kufanywa na maulamaa.
Ayatullah Udhma Khamenei amelitaja suala la kuamsha watu kuhusiana na nafasi ya siasa za Marekani, Uingereza na utawala wa Kizayuni katika kufufua mrengo huo wa kitakfiri kuwa ni moja ya majukumu makubwa ya maulamaa katika nchi za Kiislamu na kuongeza kuwa: Jukumu la tatu muhimu la maulamaa ni kuipa umuhimu wa hali ya juu kadhia ya Palestina na Masjidul Aqsa na kuzuia kusahauliwa kadhia hiyo ambayo ndilo suala muhimu zaidi katika ulimwengu wa Kiislamu.
Vile vile ameashiria uamuzi wa hivi karibuni wa Baraza la Mawaziri la utawala wa Kizayuni la kudai kuwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu ni ya Mayahudi na kuongeza kuwa: Utawala wa Kizayuni unapigania kuiteka kikamilifu Quds na Masjidul Aqsa na kuzidi kuwadhoofisha Wapalestina. Mataifa yote ya Kiislamu pamoja na maulamaa, wanapaswa kuzitaka tawala za nchi zao kulipa umuhimu mkubwa suala la Palestina.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria hatua iliyochukuliwa na Imam Khomeini (quddisa sirruh) ya kutangaza siasa za kuiunga mkono Palestina na kuufanya adui utawala wa Kizayuni na kusisitiza kuwa: Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, serikali na wananchi wote wa Iran, wote kwa pamoja wana msimamo mmoja katika suala zima la kuiunga mkono Palestina na kuufanya adui utawala wa Kizayuni na kwamba hawajakwenda kinyume na njia hiyo iliyochorwa na Imam Khomeini (quddisa sirruh) kwa miaka 35 sasa.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza pia kuwa taifa na vijana wa Iran wanawaunga mkono wananchi wa Palestina kwa moyo wao wote na ni maashiki wa mapambano dhidi ya utawala wa Kizayuni na kuongeza kuwa: Alhamdulillah kwa uwezo na taufiki ya Mwenyezi Mungu, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haikufungwa na mipaka ya hitilafu za kimadhehebu na kama ambavyo inaisaidia Hizbullah ya Waislamu wa Kishia huko Lebanon ni vivyo hivyo inavyozisaidia Hamas, Jihadul Islami na makundi mengine ya Waislamu wa Kisuni huko Palestina na kwamba itaendelea kutoa misaada kwa makundi hayo.
Amesema, kuwatia nguvu ndugu zetu wa Kipalestina huko Ghaza ni mfano wa wazi wa misaada ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa wananchi wa Palestina na kusisitiza kuwa: Kama ambavyo tumetangaza huko nyuma, Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan nao inabidi uzatitiwe kwa silaha na uwe na uwezo wa kujilinda, na bila ya shaka yoyote jambo hilo litatendeka.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha amesema, maadui wa ulimwengu wa Kiislamu ni dhaifu mno hivi sasa kuliko huko nyuma na huku akiashiria matatizo ya kisiasa, kiuchumi na kiusalama ziliyo nayo nchi za Ulaya na vile vile matatizo makubwa zaidi na mabaya zaidi iliyo nayo Marekani katika masuala ya maadili, masuala ya kisiasa na husuasan masuala ya mali na kifedha pamoja na kulinda heshima inayodai kuwa nayo Marekani ya kujiona kuwa ni dola kubwa na kuongeza kuwa, utawala wa Kizayuni nao ni dhaifu mno hivi sasa ikilinganishwa na huko nyuma. Kwani utawala huo ndio ule ule utawala ambao katika miaka ya huko nyuma ulikuwa ukijigamba kuwa unapigania kuunda dola kubwa linaloanzia Mto Nile hadi Mto Furat, lakini hivi sasa katika vita vya siku 50 vya Ghaza, ilitumia nguvu na uwezo wake wake na ikashindwa kuangamiza mahandaki na njia za chini ya ardhi za Hamas na Jihadul Islami (katika eneo dogo tu la Ghaza).
Ayatullah Udhma Khamenei amekumbushia matatizo na kushindwa maadui wa Uislamu katika eneo la Mashariki ya Kati hususan katika nchi za Iraq, Syria na Lebanon na kusema kuwa: Mfano mwingine wa udhaifu wa adui ni kadhia ya nyuklia ya Iran. Marekani na nchi nyingine za kikoloni za Ulaya zote zimekusanyika pamoja ili kuipigisha magoti Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika suala la nyuklia lakini zimeshindwa, na katika siku za usoni pia zitashindwa tu.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Maudhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Hujjatul Islam Walmuslimn Alizadeh Mousavi, Katibu wa Kongamano la Mirengo ya Kufurutu Ada na Kitakfiri kwa Mtazamo wa Maulamaa wa Kiislamu ametoa ripoti fupi kuhusiana na namna kongamano hilo lilivyofanyika kwa ufanisi na kusema kuwa: Katika siku mbili za kufanyika kongamano hilo, kuliundwa kamati mbali mbali za kiutaalamu na kiistratijia na kuchunguza na kutafakari kwa kina mizizi ya makundi ya kitakfiri, masuala yao ya kisiasa na vile vile njia za kuweza kung'oa mizizi ya fikra nzima ya kitakfiri.
Vile vile amegusia namna kulivyofanyika vikao vingine mbali mbali kabla ya kongamano hilo katika nchi za Syria na Pakistan na kuwasilishwa zaidi ya makala 700 kwa sekretarieti ya kongamano hilo na kuongeza kuwa: Kongamano hilo limewakutanisha pamoja maulamaa 315 wa ulimwengu wa Kiislamu na kwamba makala 144 bora zilizoandikwa kwa lugha za Kifarsi na Kiarabu, zimekusanywa na kuchapishwa katika jildi nane za vitabu.
 
< Nyuma   Mbele >

^