Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Aonana na Maelfu ya Wananchi wa Qum Chapa
07/01/2015
 Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu leo asubuhi (Jumatano) ameonana na hadhara kubwa ya maelfu ya wananchi wa Qum na huku akiashiria udharura wa kukabiliana na njama za mabeberu za kupotosha ukweli kuhusiana na Mapinduzi ya Kiislamu na kujaribu kusahaulisha matukio mauhimu kama yale ya Dei 19 1356 (mwaka wa Kiirani wa Hijria Shamsia sawa na Januari 9, 1978) na Dei 9, 1388 (Disemba 30, 2009) na kuongeza kwamba: Uadui wa maadui waistikbari kwa taifa la Iran kamwe hauwezi kumalizika na kwamba viongozi nchini Iran wanapaswa kutegemea nguvu ya ndani ili kumpokonyua adui silaha yake ya vikwazo, kwani adui haaminiki hata kidogo. Aidha amesisitiza kuwa, viongozi nchini Iran wanapaswa kutegemea nukta muhimu zilizo wazi na kutekeleza vilivyo majukumu yao kwa ajili ya kufanikisha malengo matukufu na yanayong'ara ya Mapinduzi ya Kiislamu na ya taifa.
Ayatullah Udhma Khamenei aidha ametoa mkono wa baraka na fanaka kwa mnasaba wa maadhimisho ya Maulidi na Siku ya Kuzaliwa Bwana Mtume Muhammad SAW na Imam Sadiq AS na kuyataja mapambano ya Januari 9, 1978 kuwa ni tukio la kihistoria, kubwa na muhimu mno akiongeza kwamba: Kuna baadhi ya watu wanafanya njama za kuzisahaulisha siku na matukio makubwa na muhimu mno ya Mapinduzi ya Kiislamu katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita, lakini madhali taifa la Iran liko hai na nyoyo za waumini zenye imani thabiti na ndimi za kutangaza haki bado zipo, jambo hilo kamwe halitawezekana.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja suala la kuyabakisha hai matukio ya Januari 9, 1978 na ya Bahman 22, 1357 (mwaka wa Kiirani wa Hijria Shamsia sawa na Februari 11, 1979 wakati yalipofikia ushindi Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran) na Disemba 30, 2009 (Wakati wananchi wa Iran walipojitokeza kwa wingi mno katika maandamano ya kona zote za nchi ili kuvunja fitna iliyochochewa na maadui wa Mapinduzi ya Kiislamu) na matukio mengine muhimu mno ya taifa la Iran kuwa ni harakati ya kijihadi na kuongeza kuwa: Kambi inayoupinga mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilikuwa imejenga matumaini yake kwa kizazi cha tatu cha Mapinduzi ya Kiislamu ili kukifanya kizazi hicho kiachane na mapinduzi hayo, lakini ni kizazi hicho cha tatu cha Mapinduzi ya Kiislamu na ni vijana hao ndio waliojitokeza kwa wingi mno kwenye maandamano ya Dei 9 (Disemba 30) na kutoa pigo kubwa kwa wale watu ambao walikuwa wanafanya njama za kupotosha njia sahihi ya Mapinduzi ya Kiislamu kupitia fitna yao hiyo.
Vile vile Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitizia tena umuhimu wa kihistoria wa tukio la Dei 19, 1356 (Januari 9, 1978) la mjini Qum na kuongeza kuwa, tarehe 19 Dei ilikuwa ndio mwanzo wa harakati kuu ya wananchi wote na kwamba tukio hilo lililiingiza mitaani taifa zima la Iran kwa ajili ya kupambana na utawala wa taghuti na hatimaye utawala wa kiimla na kidikteta wa Shah ukafutwa kikamilifu nchini Iran.
Baada ya hapo Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria njama zilizopo za kupotosha ukweli na kujaribu kuficha maovu yaliyokuwa yanafanywa na utawala wa Kipahlavi wa kabla ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu nchini Iran na kutaja sifa kadhaa za utawala huo wa kidikteta wa Shah akisema: Udikteta uliokuwa ukitumia mbinu na njia mbaya mno na za kinyama sana za mateso katika jela za kuogofya ni moja ya sifa kuu uliokuwa nazo utawala wa Kipahlavi na ambao madola yote ambayo leo hii yanajifanya kutetea haki za binadamu, yalikuwa yanauunga mkono kwa nguvu zao zote utawala huo wa kidikteta.
Vile vile ameashiria ameashiria nafasi waliyokuwa nayo Wazayuni na Wamarekani katika uanzishaji na uendeshaji wa taasisi ya kikatili ya Savak (Polisi ya siri, taasisi ya usalama wa ndani na ya kijasusi yenye rekodi ya kufanya jinai nyingi iliyoanzishwa na dikteta wa Iran kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Mohammad Reza Shah kwa msaada wa Shirika la Kijasusi la Marekani CIA na Wazayuni) na ameongeza kuwa: Mambo yaliyofichuliwa hivi karibuni kuhusu jela za siri na mateso yanayofanywa na Shirika la Kijasusi la Marekani CIA huko nchini Marekani, pia yanazidi kuthibitisha kwamba madai ya Wamarekani ya kupigania uhuru wa kusema hayaendani hata chembe na uhakika wa mambo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameutaja utegemezi wa kidhalili kwa madola makubwa kuwa ni sifa nyingine uliyokuwa nayo utawala wa Kipahlavi wa nchini Iran kabla ya Jamhuri ya Kiislamu na kuongeza kuwa: Katika kipindi hicho, kila kitu ambacho kilikuwa kinalinda maslahi ya mabeberu hususan Marekani yalikuwemo kwenye siasa na miamala ya ndani ya Iran, ya kieneou na ya kimataifa, na wamba wananchi wa Iran walidhalilishwa vibaya na watawala wa wakati huo.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Sababu inayowafanya Wamarekani kulikasirikia na kulifanyia bugdha, chuki na uadui taifa la Iran na Mapinduzi ya Kiislamu ni kwamba ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu umewapokonya maadui hao nchi muhimu ambayo ina sifa na nafasi ya aina yake ya kiistratijia yaani Iran.
Vile vile ametaja sifa nyingine ya utawala wa Kipahlavi akisema kuwa, sifa hiyo ya tatu ya utawala huo wa kiimla na kidikteta ilikuwa ni kukumbwa na kila aina ya ufisadi wa kijinsia, kifedha na kimaadili tena kwa kiwango kikubwa sana cha kiserikali na kuongeza kuwa: Katika utawala huo khabithi na uliofisidika, wananchi walikuwa hawazingatiwi wala kupewa umuhimu wa aina yoyote ile na kwamba maoni na rai za wananchi hazikuwa na nafasi yoyote bali uhusiano baina ya wananchi na utawala ulikuwa umekatika kikamilifu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja suala la kutojali maendeleo ya kielimu, kueneza fikra na mawazo ya kujiona duni, kukuza kupindukia utamaduni wa Magharibi, kuwazoesha watu kupenda kuchupa mipaka bidhaa za nje badala ya kuhuisha na kutia nguvu uzalishaji wa ndani, kuangamiza sekta ya kilimo na uzalishaji wa taifa wa viwandani kuwa ni sehemu nyingine ya historia nyeusi ya utawala wa Kipahlavi na kuongeza kuwa: Wakati taifa lenye welewa na vipaji vingi la Iran lilipokuwa linaona udhalilishaji, dhulma na ufisadi wote huo, lilikuwa linaumia sana hadi mtu wa Mwenyezi Mungu yaani Imam wetu mtukufu (Imam Khomeini - quddisa sirruh) alipoingiza mguu wake katika medani ya mapambano na hatimaye kuyafikisha kwenye ushindi Mapinduzi ya Kiislamu nchini.
Ayatullah Udhma Khamenei pia amesisitiza kuwa, maendeleo na mafanikio mengi pamoja na mwamko na nafasi bora liliyo nayo hivi sasa taifa la Iran katika eneo (la Mashariki ya Kati) ni mambo ambayo yanatokana na kuondolewa kizuizi kikubwa yaani utawala wa Kipahlavi uliofisidika, wa kidhalimu, tegemezi na kibaraka.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia pia kuanza uadui wa kambi ya kibeberu dhidi ya taifa la Iran baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kusisitiza kuwa: Mtu yeyote asitasawari wala isimpitikie kabisa akilini kwamba adui ataachana na ukhabithi na uadui wake kwa taifa la Iran.
Ayatullah Udhma Khamenei ametoa ufafanuzi zaidi kuhusu suala hilo akisema: Wakati mtakapokumbwa na mghafala katika kukabiliana na adui au iwapo mtamwamini adui, basi hatasita hata kidogo kutumia fursa hiyo kufanikishia malengo yake humu nchini lakini kama mtakuwa imara msiotetereka na mkawa mnamjua vizuri adui, basi mabeberu watalazimika kufikiria upya uadui wao kwa taifa hili.
Ameongeza kuwa, mashinikizo ya hivi sasa ya kambi ya mabeberu wa dunia kwa taifa la Iran yanatokana na uadui wao usioisha na kusema: Ingawa hadi hivi sasa bado tuna safari ndefu ya kufikia kwenye malengo makuu matukufu kama vile uadilifu wa kijamii na akhlaki na maadili ya Kiislamu, lakini tofauti na matamshi ghalati yasiyo sahihi yanayotolewa na baadhi ya watu kuhusu kutopata mafanikio taifa la Iran katika jitihada zake za kufikia malengo hayo matukufu; taifa hili linaendelea kupiga hatua katika njia ya kufanikisha malengo hayo matukufu na limepata mafanikio makubwa katika njia hiyo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewakosoa wale watu ambao wanadharau na kujifanya hawayaoni mafanikio ya taifa la Iran yakiwemo maendeleo yake makubwa ya kielimu na kuhoji akiwaambia: Kwa nini mnakosa busara na mnajifanya hamyaoni mafanikio ya kielimu ya taifa la Iran wakati hata taasisi kubwa za kielimu duniani zinakiri kuwepo maendeleo hayo? Kwa nini mnatoa matamshi ghalati na yasiyo na insafu kujaribu kutia shaka katika maendeleo na mafanikio ya taifa la Iran licha ya kwamba hata maadui wa taifa hili wamelazimika kukiri na kulisifu taifa la Iran kwa mafanikio yake hayo?
Vile vile Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria hali ya wakati wa awali ya Uislamu na enzi za Bwana Mtume Muhammad SAW na kuongeza kuwa: Hata wakati huo pia haikuwezekana kufikia malengo yote matukufu lakini lililo muhimu lilikuwa ni kwamba, harakati ya kufanikisha malengo hayo matukufu iliendelea ambapo leo pia taifa la Iran nalo linafuata njia hiyo hiyo kwa ufakhari, kwa uimara na kwa kutotetereka.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameendelea na hotuba yake kwa kubainisha vipaumbele vya nchi na jamii ya Iran na kuutaja umoja na mshikamano wa taifa kuwa ndiyo mambo yanayohitajika zaidi hivi sasa nchini.
Amesisitiza kuwa, kuzusha hitilafu na mifarakano miongoni mwa wananchi ni jambo linalokwenda kinyume na juhudi za kufanikisha malengo matukufu hata kama litafanywa kwa sababu na dalili yoyote iwayo.
Ayatullah Udhma Khamenei amelitaja suala la kuwasaidia viongozi na serikali kuwa ni jukumu la kila mtu nchini na huku akisisitiza tena kuhusiana na udharura wa kujijenga na kujitathmini wenyewe ameongeza kuwa: Watu wa serikali nao wajue kuwa kitu pekee kinaweza kuwasaidia kufanikisha vizuri majukumu yao ni kuwategemea wananchi na nguvu za ndani ya nchi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia vikwazo vya kidhulma vya maadui dhidi ya taifa la Iran na kuongeza kuwa: Ni kweli kuwa vikwazo vimeisababishia matatizo nchi, lakini kama adui atatoa masharti ya kuondolewa vikwazo hivyo kuwa ni kuachana taifa la Iran na suala fulani la kimsingi na malengo yake matukufu kama vile kuitaka Iran iachane na Uislamu au uhuru au maendeleo yake ya kielimu, basi bila ya shaka yoyote hakuna kiongozi yeyote wa Iran atakayekubaliana na jambo hilo.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Tab'an hivi sasa adui hasemi waziwazi kuwa anayalenga malengo yetu matakatifu lakini kama tutalegeza kamba, basi baadaye ataingia kwenye malengo yetu hayo matukufu, hivyo inabidi tuwe macho na tuzitambue vizuri shabaha za mapendekezo, matamshi na hatua zinazochukuliwa na adui.
Ameitaja njia pekee ya kuweza kuifanya Iran kuwa na kinga mbele ya vikwazo kuwa ni kumpunguzia adui uwanja wa kufanyia "manuva" yake na kusisitiza kwamba: Hiyo ndiyo maana halisi ya uchumi wa kimuqawama na wa kusimama kidete na kwamba jukumu kuu la viongozi nchini ni kuhakikisha kuwa jambo hilo muhimu linafanikiwa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia sisitizo lake la mara kwa mara kuhusiana na udharura wa kukata utegemezi kwa mapato yatokanayo na mafuta na kuongeza kuwa: Viongozi nchini na viongozi serikali hawapaswi kuwa na mawazo ya kupata msaada kutoka kwa wageni na wajue kuwa kama watalegeza kamba na kurudi nyuma hata kwa hatua moja, basi adui atapiga hatua mbele, hivyo inabidi kufikiria utatuzi wa kimsingi na kulitegemea taifa na nguvu za ndani kiasi kwamba hata kama adui hataondoa vikwazo, basi jambo hilo lisiyadhuru maendeleo, ustawi, ujazi na ufanifu wa wananchi.
Ayatullah Udhma Khamenei ametoa ufafanuzi zaidi kuhusu suala hilo akisema: Inabidi tumpokonye adui silaha ya vikwazo kwani kama mtamkodolea macho ya tamaa adui, basi vikwazo vitaendelea kuwepo kama ambavyo leo hii Wamarekani wanasema kwa jeuri na kwa kiburi kikubwa kwamba hata kama Iran italegeza kamba katika kadhia ya nyuklia, vikwazo vitaendelea kuwepo na havitaondoshwa kwa mara moja na wala havitaondolewa vyote.
Vile vile amehoji kwa kusema, kwa kuwepo hali yote hiyo, je, inawezekana kumwamini adui kama huyu?
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Mimi sipingi suala la kufanya mazungumzo, lakini ninaamini kuwa kuna udharura na haja ya kuzielekeza nyoyo kwenye nukta zinazoleta matumaini ya kweli na si katika nukta za kidhahania na za kufikirika.
Mwishoni mwa hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Viongozi nchini Iran, wanaendelea vyema na kazi zao kwa taufiki ya Mwenyezi Mungu na kila mtu anapaswa kuisaidia Serikali, lakini na watu wa serikali nao wanapaswa kuwa macho, wasijiingize kwenye masuala ya pembeni yasiyo na maana, na sambamba na kujiepusha na kutoa maneno yasiyo ya lazima, wasifanye mambo ambayo yatazusha mizozo na utengano bali waelekeze jitihada zao katika kuleta umoja, imani na hima ya taifa katika masuala sahihi.
Ayatullah Udhma Khamenei aidha amesema, mustakbali wa Iran azizi unang'ara na unameremeta kikamilifu na kuongeza kuwa: Kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu, njia hiyo iliyojaa fakhari ya kufanikisha malengo matakatifu itaendelea na vijana nchini kuna siku watashuhudia kwa macho yao namna maadui mabeberu na madhalimu wanavyolazimika kuwapigia magoti na kuwanyenyekea wao.
 
< Nyuma   Mbele >

^