Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Kiongozi Muadhamu Aonana na Viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu na Wageni wa Mkutano wa Umoja wa Kiislam Chapa
09/01/2015
 Katika maadhimisho ya Maulidi na Siku ya Kuzaliwa Nabii wa rehema na baraka, Bwana Mtume Muhammad SAW na Imam Sadiq Aal Muhammad AS, Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, leo ameonana na matabaka tofauti ya wananchi, viongozi mbali mbali nchini, wasomi, maulamaa na wanavyuoni walioshiriki kwenye mkutano wa Umoja wa Kiislamu pamoja na mabalozi wa nchi za Kiislamu wanaowakilisha nchi zao mjini Tehran na kuutaja umoja na mshikamano kuwa ni funzo na somo kubwa lililotolewa na Bwana Mtume Muhammad SAW ambaye ndiye Mtume wa Mwisho na kwamba umoja na mshikamano ndilo jambo linalohitajiwa mno hivi sasa na umma wa Kiislamu. Amesisitiza kuwa: Kumuenzi na kumtukuza Bwana Mtume SAW - mtukufu wa daraja - hakupaswi kuishia tu kwenye maneno, bali inabidi kufanyike jitihada za kweli za kufanikisha kivitendo ujumbe wa mshikamano ulioletwa na mtukufu huyo, na suala hilo liwe kipaumbele kikuu cha nchi za Kiislamu na mataifa ya Waislamu.
Ayatullah Udhma Khamenei ametoa mkono wa baraka kwa minasaba hiyo miwili mitukufu na kusema kuwa, siku hii azizi ya kuzaliwa Mtume wa Uislamu ni siku ya kuzaliwa elimu, akili, maadili, rehema na mshikamano na kusisitiza kuwa: Suala la kuhakikisha mafuhumu na maana hiyo yenye upeo wa kina na yenye kuleta ufanisi inafanikisha malengo yake matukufu, inalifanya jukumu la viongozi, wanasiasa, maulamaa na watu wenye vipaji na ushawishi katika nchi za Kiislamu kuwa kubwa na zito zaidi.
Aidha ameelezea kusikitishwa kwake mno na namna maadui wanavyofanikisha mipango yao ya kuzusha mifarakano katika safu za Waislamu na kusisitiza kuwa: Laiti kama mataifa ya Waislamu yangelishikamana katika masuala yao makuu, si lazima kushikamana kwenye masuala madogo madogo, basi suhula na neema kubwa zilizoko katika ulimwengu wa Kiislamu na sifa za kipekee ulizo nazo ulimwengu huo zitapelekea kustawi na kupata hadhi kubwa umma wa Kiislamu na kwamba kuakisiwa kimataifa umoja na mshikamano katika ulimwengu wa Kiislamu utakuwa chimbuko la furaha, heshima, hadhi na utukufu kwa Bwana Mtume Muhammad SAW.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, utekelezaji uliofana wa ibada ya Sala ya Idul Fitr katika kona zote za dunia na kila walipo Waislamu pamoja na mjumuiko mkubwa wa Waislamu katika ibada ya Hija ni mifano miwili inayoonesha adhama na utukufu wa umma wa Kiislamu na kuongeza kuwa: Katika maadhimisho ya Arubaini ya Imam Husain AS ya mwaka huu pia, mamilioni ya Waislamu walishiriki huku Waislamu wa Kisuni nao wakiwemo kwenye maadhimisho hayo, ni tukio kubwa, adhimu na la kustaajabisha ambapo kuakisiwa kwake kimataifa, ukiwa ni mkusanyiko mkubwa zaidi wa Waislamu kutoka kona zote za dunia, kumeandaa uwanja wa kupata heshima na utukufu ulimwengu mzima wa Kiislamu.
Aidha ametumia fursa hiyo kuishukuru na kuisifu serikali, wananchi na watu wa makabila ya kuhamahama ya Iraq kwa kujitolea muhanga na kufanya kazi kubwa na nzuri sana ya kuwahudumia wafanya ziara walioshiriki katika maadhimisho ya Arubaini ya Imam Husain AS mwaka huu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amebainisha pia mambo yanayoweza kuleta umoja na mshikamano katika ulimwengu wa Kiislamu kuwa ni pamoja na kujiepusha kudhaniana vibaya na kukashifiana makundi na madhehebu tofauti ya Kiislamu kama vile ya Kishia na Kisuni na kusisitiza kuwa, kujiepusha na jambo hilo ni suala muhimu mno. Vile vile ameashiria namna mashirika ya kijasusi ya Magharibi yanavyofanya njama kubwa sana za kueneza mizozo na mifarakano kati ya Waislamu na kuongeza kuwa: Ule Ushia ambao una mfungamano na shirika la kijasusi la MI6 la Uingereza na ule Usuni ambao una mfungamano na Shirika la Kijasusi la Marekani CIA, makundi yote hayo mawili yako dhidi ya Uislamu na ni dhidi ya Bwana Mtume.
Ayatullah Udhma Khamenei vile vile ameasiria namna Imam Khomeini (quddisa sirruh) alivyokuwa amebeba bendera ya kupigania umoja na mshikamano katika safu za Waislamu na jitihada zisizochoka za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika suala hilo na kuongeza kuwa: Asilimia kubwa ya misaada ya Iran katika kipindi cha miaka 35 iliyopita (ya tangu kupata ushindi Mapinduzi ya Kiislamu na kuasisiwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu nchini Iran) imekwenda kwa ndugu zetu Waislamu na aghlabu yao ni Waislamu wa Kisuni na kwamba kutokana na Jamhuri ya Kiislamu na taifa la Iran kuendelea bila kuchoka kuliunga mkono taifa la Palestina na wananchi wa nchi za eneo la Mashariki ya Kati limethibitisha kivitendo mshikamano wake wa kivitendo na kaulimbiu ya umoja na mshikamano kati ya Waislamu.
Aidha amewakhutubu wanasiasa, maulamaa na wasomi wa ulimwengu wa Kiislamu kwa kuwauliza swali kwamba: Wakati mabeberu duniani wanafanya njama kubwa za kueneza chuki dhidi ya Uislamu na kuharibu sura iliyojaa nuru ya Uislamu, je, kutoa matamshi ya kuzusha mifarakano na kuharibu umoja wa Waislamu kwa kukashifiana na kupondana makundi ya Waislamu si kinyume na hekima, busara na siasa inayopasa kuchukuliwa?
Ayatullah Udhma Khamenei amezitaja siasa za baadhi ya nchi za eneo la Mashariki ya Kati za kujikita siasa zao za kigeni katika kuipiga vita Iran kuwa ni siasa za makosa na kuongeza kuwa: Tofauti na siasa hizo zisizo za kimantiki, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika siasa zake za nje, daima imekuwa ikizingatia misingi ya kuimarisha urafiki na udugu kati yake na nchi nyingine za Waislamu zikiwemo za eneo la Mashariki ya Kati.
Aidha amekosoa vikali suala la kuenezwa fikra ya "Pluralism" na kusema kuwa, wanaoeneza fikra hiyo wana welewa ghalati na wa kimakosa kuhusiana na Qur'ani Tukufu na matini na marejeo mengine ya Kiislamu.
Ameongeza kuwa: Aya za Qur'ani Tukufu zinabainisha wazi namna Uislamu unavyopinga vikali fikra ya Pluralism.
Vile vile Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja suala la kutilia mkazo maslahi ya Kiislamu na mshikamano katika ulimwengu wa Kiislamu kuwa ndiko kunakoweza kudhamini manufaa ya kila nchi ya Kiislamu na kusisitiza kuwa: Waislamu sote tunapaswa tushikamane na tutegemee vilivyo aya za Qur'ani Tukufu ikiwemo ile inayosema: أَشِدَّاء عَلَى الْكُفَّارِ رُحَمَاء بَيْنَهُمْ wana nguvu mbele ya makafiri, na wanahurumiana wao kwa wao (Suratul Fat'h 48: 29) na kwamba inabidi tuwe makini, wenye nguvu na tusiotetereka katika kukabiliana na uistikbari na donda ndugu na hatari la kensa yaani Uzayuni wa kimataifa na juu yao kabisa yakiwemo madola ya kibeberu ya Marekani na utawala ghasibu wa Israel lakini wakati huo huo tupendane, tushikamane na tuhurumiane Waislamu sisi kwa sisi.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa mkono wa baraka kwa mnasaba wa maadhimisho siku ya kuzaliwa Bwana Mtume Muhammad - swalawatullahi Alayhi Waalih - na Imam Jaafar Sadiq - Alayhis Salaam - na kusema: Leo hii ulimwengu wa Kiislamu unahitajia zaidi sira na mafundisho ya Bwana Mtume Muhammad - swalawatullahi Alayhi Waalih - kuliko wakati mwingine wowote pamoja na kuhurumiana, kuwa kitu kimoja, kusameheana, kuheshimu sheria na kushikamana barabara.
Rais Rouhani ameongeza kuwa: Wale watu ambao hawatumii busara na ambao wanatumia jina la Jihadi, dini na Uislamu, kuua watu na kufanya ukatili na vitendo vya kuchupa mipaka wajue kuwa wametumbukia kwenye shimo la kueneza chuki dhidi ya Uislamu na kuupaka matope dini tukufu ya Kiislamu, watake wasitake.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa, vitendo vya machafuko na ugaidi vinapaswa kulaaniwa popote vinapotokea, iwe ni katika nchi za Mashariki ya Kati au barani Ulaya na Marekani na kusisitiza kuwa: Tuna furaha kubwa kuona kuwa wananchi Waislamu wa eneo hili, kuanzia Iraq, Syria, Lebanon na Palestina hadi Pakistan na Afghanistan, kote wamesimama imara kupambana na machafuko na vitendo vya ugaidi na kadiri siku zinavyopita ndivyo wananchi hao wanavyozidi kupata ushindi.
Rais Rouhani ameongeza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima ni muungaji mkono wa mataifa ambayo yanasimama kidete kupambana na ugaidi.
Mwishoni mwa mkutano huo, baadhi ya wageni walioshiriki kwenye mkutano wa Umoja wa Kiislamu wamezungumza kwa karibu na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika anga iliyojaa mapenzi, udugu na kushibana.
 
< Nyuma   Mbele >

^