Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Mkutano wa Kiongozi Muadhamu na Wajumbe wa Kamati ya Kuadhimisha Siku ya Taifa ya Uhandisi Chapa
23/02/2015

 Miongozo na hotuba ya Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliyoitoa wakati alipoonana na wajumbe wa kamati ya kuadhimisha Siku ya Taifa ya Uhandisi nchini Iran, Februari 5, 2015, leo asubuhi imetangazwa rasmi katika kongamano lililofanyika kwa mnasaba wa maadhimisho hayo katika ukumbi wa mikutano wa mnara wa Milad, jijini Tehran.

 

Katika mazungumzo yake hayo ya Februari 5 na wajumbe wa kamati hiyo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aligusia wigo mpana wa kazi za uhandisi na nafasi na mchango wenye taathira kubwa ulitolewa na majimui za wahandisi vijana kwenye nyakati tofauti ikiwa ni pamoja na wakati wa mapambano ya Mapinduzi ya Kiislamu na katika kipindi cha vita vya kujihami kutakatifu (vita vya miaka minane vilivyoanzishwa na utawala wa wakati huo wa Iraq dhidi ya Iran) na kuongeza kuwa: Wakati wa vita vya kujihami kutakatifu, wahandisi wetu walijitolea muhanga kila kitu chao na kuhakikisha wanatumia nguvu zao zote, utaalamu na vipaji vyao vyote kulitumikia taifa lao na ikawa kila siku kunavumbuliwa kitu kipya na vijana hao wenye vipaji vya aina yake.

Ayatullah Udhma Khamenei amezitaja jitihada na mafanikio ya kielimu ya wahandisi wa Iran katika kipindi cha vita vya kujihami kutakatifu kwamba yalikuwa ni muhimu pia katika majukumu makuu na ya kimsingi na kusisitiza kwamba: Mnapaswa kufanya jitihada zaidi za kuhakikisha kwamba kaulimbiu ya “Sisi Tunaweza” inafanya kazi katika sekta zote za nchi na kuwaonyesha kivitendo wananchi mafanikio ya kaulimbiu hiyo. Aidha fanyeni utafiti wa kugundua mianya na mahitaji ya kweli ya nchi kwa kupitia kufanya kazi ambazo hadi sasa hazijawahi kufanywa pamoja na kukamilisha zile kazi ambazo zimekwama njiani.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu vile vile ameashiria taathira mbaya za kuingiza vitu nchini kiholela na kwa njia za magendo na kusema: Mashinikizo ya kuingiza bidhaa kutoka nje yanaimaliza nchi na hata takwimu za bidhaa zinazoingizwa nchini kimagendo nazo ni za kutisha sana, lakini pamoja na hayo, madai yanayotolewa ya kwamba inabidi kufungua mlango kikamilifu wa kuagizia bidhaa kwa wingi kutoka nje kama njia ya kupambana na magendo, nayo pia hayakubaliki.

Vile vile amewakhutubu wahandisi wote wa Iran akiwasisitizia kwamba: Hakikisheni mazalisho na bidhaa zinazozalishwa na vijana wenye vipaji, wenye imani thabiti ya dini, wenye uwezo wa kazi na baadhi yao wenye vipaji vya kipekee wa Iran hazizidiwi nguvu na tabia iliyokita mizizi nchini ya kuagizia vitu kutoka nje.

Aidha Ayatullah Udhma Khamenei amegusia matamshi ya katibu wa kongamano la uchumi wa kimuqawama na wa kusimama kidete na kukaririwa mno kaulimbiu na istilahi hiyo ya uchumi wa kusimama kidete katika matamshi viongozi na wanaharakati wa sekta mbalimbali nchini na kuongeza kuwa: Tab’an kurudiarudia na kukariri kwa mdomo tu maneno hayo ya uchumi wa kusimama kidete hakuwezi kusaidia chochote, bali inabidi utafiti wa kina wa suala hilo upewe uzito wa hali ya juu ndani ya Bunge na Serikalini ili uchumi huo wa kusimama kidete uweze kupata maana yake halisi iwe ni katika kazi zilizotendeka hadi hivi sasa au kazi zilizodhamiriwa kutendwa katika siku za usoni.

 
< Nyuma   Mbele >

^