Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Aonana na Wajumbe wa Baraza la Wanavyuoni Wataalamu Chapa
12/03/2015
 Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu leo asubuhi (Alkhamisi) ameonana na mkuu na wajumbe wa Baraza la Wanavyuoni Wataalamu linalomchagua na kusimamia kazi za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na kulitaja lengo kuu la mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa ni kusimamisha Uislamu kamili unaotakiwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu na huku akiashiria udharura wa kuoneshwa na kutangazwa Uislamu sahihi mbele ya njama za mabeberu za kueneza hofu na chuki dhidi ya dini tukufu ya Kiislamu kati ya mataifa ya dunia. Amesisitiza kuwa: Katika kujadili na kutafuta sababu na njia za kutatua changamoto zilizopo, ni lazima tujiweke mbali na suala kuangalia mambo kwa mtazamo finyu, bali tunapaswa kuangalia mizizi ya masuala hayo na kuamiliana nayo kwa njia za kimantiki.
Vile vile ameashiria shakhsia, historia na utumishi wa Ayatullah Yazdi, mkuu mpya wa Baraza la Wanavyuoni Wataalamu na kusema kuwa hilo hilo ni chaguo linalofaa kabisa kushika nafasi hiyo na ambalo limekuja kwa wakati unaofaa na kuongeza kuwa: Uchaguzi wa mkuu mpya wa baraza hilo umefanyika kwa uangalifu wa hali ya juu, bila ya kuingizwa ndani yake mambo ya pembeni na unaweza kuwa kigezo kizuri kwa taasisi nyinginezo nchini.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa ushahidi kutoka katika aya kadhaa za Qur'ani Tukufu na kulitaja suala la kuzingatia nguzo na mafundisho yote ya Uislamu kuwa ndilo jambo linalotakiwa na dini hii tukufu ya Mwenyezi Mungu na kusisitiza kwamba: Katika mafundisho ya Uislamu hakuna kitu kinachoitwa dini ya kiwango cha chini, bali Muislamu anatakiwa kutekeleza kiukamilifu nguzo na sehemu zote za dini hii tukufu na mara zote afanye jitihada zaidi na zaidi za kutekeleza kiukamilifu zaidi mafundisho ya Uislamu.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria udharura wa kulindwa na kutia nguvu vipengee vyote vya Uislamu katika "sura na sira" ya dini hiyo tukufu na kuongeza kuwa: Kulinda sira ya Uislamu maana yake ni kwamba katika sehemu zote ambako kuna harakati za wote za nchi, za wananchi na za viongozi, Uislamu uwe ndio lengo na shabaha, na inabidi kuwekwe mipangilio madhubuti ya kufikia kwenye ukamilifu wa suala hilo na kwamba kila mmoja anapaswa kuingia kwenye mkondo huo.
Aidha amesema kuwa, mabeberu na waistikbari duniani ndio wakwamishaji wakuu wa harakati ya kuelekea kwenye ufanikishaji wa Uislamu sahihi na kuongeza kuwa: Kueneza hofu na chuki dhidi ya Uislamu kwa kutumia vyombo vya kipropaganda na kisiasa vya Wazayuni ni uthibitisho kuwa maadui hao wa Uislamu wana hofu na woga mkubwa wa kuangamizwa manufaa yao yasiyo ya kisheria.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia matamshi ya baadhi ya maadui wa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wanaosema kuwa wanataka kubadilisha mienendo ya Jamhuri ya Kiislamu na si kuupindua mfumo wa Kiislamu nchini Iran na kuongeza kuwa: Kubadilisha mienendo ya mfumo wa Kiislamu kuna maana ya kulizuia taifa la Iran lisishikamane na misimamo yake madhubuti na isiyotetereka ya kuendeleza harakati ya kuelekea kwenye ufanikishaji wa malengo yakeo matukufu na kutekeleza kikamilifu matundisho ya Kiislamu na kwamba lengo hilo kwa hakika ndilo hilo hilo lengo la kutaka kuupindua mfumo unaotawala nchini Iran na kuangamiza sira ya dini katika harakati kuu ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu kwa njia na sura nyingine.
Aidha amesisitiza kuwa, ni jambo la dharura kikamilifu kujiepusha na suala la kuchukua maamuzi na hatua za pupa katika kukabiliana na njama za kueneza hofu na chuki dhidi ya Uislamu na kuongeza kuwa: Uhakika wa suala zima la kueneza hofu dhidi ya Uislamu ni tarjuma ya woga na kuchanganyikiwa madola ya kibeberu ya kimataifa kutokana na kushindwa kukabiliana na Uislamu wa kisiasa na Uislamu uliojikita kivitendo katika maisha ya kila siku ya mataifa mbali mbali duniani ambapo kwa kufanya Mapinduzi ya Kiislamu, taifa la Iran limeweza kuwa taifa lililoko mstari wa mbele katika kuuleta, kuutia nguvu na kuusimamisha imara Uislamu huo.
Ayatullah Udhma Khamenei aidha amesema ni jambo linalowezekana kabisa kubadilisha njama za kueneza hofu na chuki dhidi ya Uislamu kutoka kitisho na kuzifanya kuwa fursa nzuri ya kuuimarisha Uislamu na kuongeza kuwa: Njama zisizosita za kuyatia hofu mataifa na vijana duniani kuhusiana na dini tukufu ya Kiislamu zimezusha swali kubwa katika fikra za walio wengi ulimwenguni ya kwamba ni nini hasa lengo la hujuma na mashambulizi yote haya dhidi ya Uislamu?
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja suala la kutoa majibu ya swali hilo kupitia kuyaonesha na kuyatangazia mataifa ya dunia sura ya Uislamu sahihi na halisi kuwa lina baraka nyingi zisizo na mwisho na kuongeza kwamba: Tunapaswa tutumie uwezo wetu wote kufanikisha suala hilo.
Vile vile amebainisha sifa kadhaa za kipekee za Uislamu wa kweli na halisi akiongeza kuwa: Mpango wa kuutangaza Uislamu unaowasaidia watu wanaodhulumiwa na unaopinga dhulma na ambao utawavutia vijana wa kila kona ya dunia, Uislamu ambao unaleta hamasa, uchangamfu na msisimko katika nyoyo za vijana hao na kuwafahamisha namna dini hii ya Mwenyezi Mungu inavyowalinda watu wanaodhulumiwa na wasio na pa kukimbilia, kwa hakika unahitajia mikakati ya kielimu ya kuufanikisha.
Ayatullah Udhma Khamenei ameutaja Uislamu unaounga mkono suala la kufanya mambo kimantiki na unaopinga mitazamo finyu na fikra mgando zisizopenda mabadiliko na ambao unapinga upotofu na "khurafa" kwamba ni sifa nyingine ya kipekee ya Uislamu sahihi na kuongeza kuwa: Inabidi tuutangaze kwa walimwengu Uislamu wa uwajibikaji ili kupinga Uislamu usiojali mambo; Uislamu ulio hai ndani ya maisha ya kila siku ya wanadamu mbele ya Uislamu wa kisekula; Uislamu wa urehemevu na huruma kwa watu dhaifu na Uislamu wa kupambana na mabeberu na wakati tutakapofanya hivyo tutakuwa tumezibadilisha njama za maadui za kueneza hofu dhidi ya Uislamu kuwa fursa nzuri ya kuyafanya mataifa ya dunia yauzingatie Uislamu wa asili na ulio sahihi.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria changamoto zilizopo baina ya Iran na Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya likiwemo suala zima la mazungumzo ya nyuklia na kuongeza kuwa: Inabidi kujiepusha na kuangalia mambo kijuujuu na kuziangalia changamoto na matatizo yaliyopo kiundani ili kwa njia hiyo iweze kupatikana njia ya kimantiki ya kutatua changamoto na matatizo hayo.
Ametoa mfano mmoja ulio wazi hivi sasa kwa kuashiria madhara yanayotokana na vikwazo na kusema: Uchunguzi wa kina kuhusiana na suala hilo unabainisha wazi kwamba sababu ya kuwepo madhara yanayotokana na vikwazo vilivyowekwa na maadui dhidi ya taifa la Iran ni kutokana na Iran kutegemea uchumi wa kiserikali na kutokuweko wananchi ndani ya uchumi huo.
Baada ya hapo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameuliza maswali kadhaa akisema: Hivi kama uchumi wa nchi yetu na maisha ya taifa letu usingelikuwa unategemea mafuta na lau kama ungelijiepusha na kufanya makosa ya mwanzoni mwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya kuifanya serikali kuhodhi na kusimamia kila kitu na lau kama wananchi wangelishiriki inavyotakiwa katika masuala ya kiuchumi, je, adui angeliweza kusababisha madhara hayo kupitia vikwazo vyake vya mafuta na vikwazo vyake dhidi ya taasisi za serikali?
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kuwa: Kama tutayazingatia na kuyatafutia ufumbuzi wa namna hiyo masuala hayo basi matatizo yataondoka na wala hakutakuwa na mawazo ya kusubiri faraja na mapenzi ya adui.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia pia faida za kuwa na mtazamo huo wa kina na wa kimantiki katika kuamiliana na changamoto za wazi na zilizojificha pamoja na changamoto zinazosababishwa na wapenda makuu duniani zikiwemo zile zilizomo kwenye kadhia ya nyuklia na kuongeza kuwa: Timu ya mazungumzo ya nyuklia iliyoundwa na mheshimiwa Rais (wa Iran) kwa hakika inafanya kazi vizuri sana, ni timu ya watu waaminifu na inafanya kazi inayokubalika na ni ya watu wenye uchungu na nchi na taifa lao, lakini pamoja na hayo mimi nina wasiwasi kwani upande wa pili wa mazungumzo ni wa watu wenye vitimbi na makri nyingi, ni wadanganyifu na maayari ambao wanasubiri fursa tu kukushambulia.
Vile vile amegusia kosa ambalo limezoeleka kufanywa na watu wengi la kudhani kwamba watu wenye nguvu huwa hawana haja ya kufanya makri, hila na udanganyifu na kuongeza kuwa: Kuna baadhi ya watu wanadhani kuwa, kwa vile Marekani ina nguvu za kisiasa, kiuchumi na kijeshi, basi haihitajii kufanya ghashi na ubazazi lakini uhakika wa mambo ni kinyume kabisa na hivyo, kwani Wamarekani wanahitajia mno ghashi na ghiliba na hata hivi sasa pia wanaendelea kufanya vivyo hivyo, na kwa hakika uhakika huo usiopingika ndio unaotutia wasiwasi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitizia wajibu wa kuwa macho mbele ya ghiliba za Marekani na kuongeza kuwa: Kila unapokaribia wakati wa kuainishwa mwisho wa mazungumzo utawaona Wamarekani wanayafanya makali matamshi yao, wanakuwa wakali na wagumu zaidi ili kufanikisha malengo yao, hivyo kuna wajibu wa kuwa macho mbele ya makri, hila na vitimbi hivyo vya Wamarekani.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria pia matamshi ya kipuuzi na ya kuchefua moyo yaliyotolewa na Wamarekani katika wiki na siku za hivi karibuni na kuongeza kuwa: Kikaragosi na kikaramba kimoja cha Kizayuni kilienda huko (Marekani) na kuzungumza (katika Baraza la Senate); na viongozi wa Marekani nao wakasema haya na yale kumjibu Mzayuni huyo ili waonekane wamejivua na matamshi yake, lakini wakati huo huo walipokuwa wanatoa matamshi hayo, hapo hapo wakaituhumu Iran kuwa inaunga mkono ugaidi, matamshi ambayo kwa hakika ni kichekesho kikubwa.
Ameongeza kuwa: Wamarekani na waitifaki wao katika eneo (hili la Mashariki ya Kati) ndio waliounda magaidi makhabithi zaidi na makatili zaidi yaani "Daesh" na mfano wao na hadi leo hii wanaendelea kuwaunga mkono magaidi hao, halafu wanathubutu kutoka hadharani na kulisingizia mambo hayo taifa la Iran na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran!
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekumbushia pia kitendo cha Marekani cha kuunga mkono utawala pandikizi wa Wazayuni na kuongeza kuwa: Washington inakiri rasmi kuwa inaunga mkono vitendo vya kigaidi vinavyofanyika kwa sura mbaya na ya kikatili kabisa na wakati huo huo inatoka hadharani na kuituhumu Jamhuri ya Kiislamu kuwa eti inaunga mkono ugaidi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia amesema kuwa, barua ya hivi karibuni ya maseneta wa Marekani kwa Iran ina dalili nyingi zinazoonesha kuporomoka maadili ya kisiasa ndani ya mfumo wa utawala wa Marekani na kuongeza kuwa: Nchi zote duniani huendelea kuheshimu na kushikamana na mikataba iliyokubaliwa kimataifa hata kama viongozi katika serikali za nchi hizo watabadilika na kuja viongozi wengine lakini maseneta wa Marekani wametangaza rasmi kuwa kama serikali ya hivi sasa ya Marekani itaondoka basi itakuwa ni kana kwamba hakuna lolote lililokubaliwa na kutiwa saini, je, huu si ukomo wa kuporomoka maadili ya kisiasa na kusambaratika ndani kwa ndani mfumo wa utawala wa Marekani?
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu wanajua wanachokifanya na wanajua wanapaswa kufanya nini kama makubaliano yatafikiwa ili kuizuia Marekani isiweze kuyafanya lolote makubaliano hayo baada ya kutiwa saini.
Vile vile Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amemkumbuka kwa wema marhum Ayatullah Mahdavi Kani (Mkuu aliyetangulia wa Baraza la Wanavyuoni Wataalamu wanaomchagua na kusimamia kazi za Kiongozi Muadhamu) na kumtaja kwamba alikuwa mwanachuoni mwanaharakati aliyefanya jitihada kubwa zenye taathira nzuri na za kudumu na amemuombea maghufira na rehema kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema.
 
< Nyuma   Mbele >

^