Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Ujumbe wa Nairuzi wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu wa Mwaka 1394 Hijria Shamsia Chapa
21/03/2015
Supreme Leader's Norouz Message 1394Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, ametoa ujumbe muhimu wa Nairuzi kwa taifa la Iran na kuutaja mwaka mpya wa 1394 Hijria Shamsia kuwa ni mwaka wa "Serikali na Wananchi, Kupendana na Kufahamiana."
Matini kamili ya ujumbe wake huo ni kama ifuatayo:
 

بسم الله الرحمن الرحیم
یا مقلّب القلوب و الابصار، یا مدبّر اللّیل و النّهار، یا محوّل الحول و الاحوال، حوّل حالنا الی احسن الحال
Kwa jina la Allah Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu
Ewe Mgeuzaji wa nyoyo na basari! Ewe Mpangiliaji wa Usiku na Mchana!
Ewe Mbadilishaji wa mwaka na hali! Badilisha hali zetu kuwa bora ya hali.

Assalaamu alaa Faatimati wa abiha wa ba'aliha wa baniha (Amani iwe juu ya Faatima na baba yake na mumewe na wanawe).
Kuanza kwa mwaka huu (1394 Hijria Shamsia) kulikosadifiana na siku za kukumbuka alipokufa shahidi Bibi Fatimatuz Zahra (Salamullahi Alayha) pamoja na mapenzi makubwa ya wananchi wetu kwa Ahlul Bayt wa Bwana Mtume Muhammad SAW na binti mtukufu wa Mtume Mtukufu ni mambo ambayo yana hali na sifa zake maalumu ambazo kwa yakini watu wote wanapaswa kuzichunga sifa hizo na kwa yakini zitachungwa. Ni matumaini yetu siku hizi na mwaka huu utajaa baraka za siku za "Faatimiyyah" (siku za kukumbuka kufa shahidi Bibi Fatimatuz Zahra - Salamullahi Alayha); na ni matumaini yetu pia kuwa jina lililojaa baraka la mtukufu huyo na kumbukumbu zake zitaacha taathira kubwa na za kudumu katika maisha ya watu wetu kwenye mwaka huu wa 1394 (Hijria Shamsia). Ni matumaini yetu pia mwanzo huu wa msimu wa machipuo unakokwenda sambamba na kuanza mwaka mpya wa Hijria Shamsia, utakuwa na baraka kwa taifa la Iran na mataifa yote yanayoadhimisha sikukuu ya Nairuzi. Ninatoa salamu za dhati kwa Imam Mahdi (Arwahuna Fadahu - roho zetu ziwe fidia kwake) na ninawakumbuka kwa wema Imam wetu mtukufu (Imam Khomeini - quddisa sirruh) na mashahidi wetu wema nikitaraji kwamba dua za vipenzi wetu hao na waja hao wema wa Mwenyezi Mungu zitatufikia na sisi. Nitatupia jicho kiujumla matukio ya mwaka (ulioisha hivi punde) wa 1393 (Hijria Shamsia) na nitauangalia kiujumla pia mwaka huu mpya katika muda huu wa kuanza kwake. Mwaka 93 ulikuwa ni mwaka uliojaa matukio, iwe ni ndani ya Iran au nje ya Iran na katika uga wa kimataifa. Ulikuwa ni mwaka uliojaa changamoto. Tulishuhudia pia maendeleo ndani ya mwaka huo. Mwanzoni mwa mwaka 93 tuliutaja mwaka huo kuwa ni mwaka wa azma na nia ya kitaifa na uongozi na uendeshaji wa kijihadi wa mambo. Tuliupa jina hilo kutokana na changamoto hizo. Tunapotupia jicho matukio ya mwaka ulioisha wa 93 tutaona kuwa azma na nia ya kitaifa Alhamdulillah ilijitokeza kwa uwazi kabisa. Taifa letu lilionesha azma ya kweli katika kuhimili baadhi ya matatizo liliyobebeshwa (na maadui) na pia katika siku ya Bahman 22 (Februari 11, siku zinapofikia kileleni sherehe za Mapinduzi ya Kiislamu ya nchini Iran) na vile vile katika Siku ya Quds (Ijumaa ya mwisho ya mweza mtukufu wa Ramadhani) na aidha katika mkusanyiko adhimu wa Arubaini (ya Imam Husain AS), taifa la Iran lilionesha kwa uwazi na kwa hima kubwa nia na azma yake ya kitaifa. Uongozi na uendeshaji mambo kijihadi nao Alhamdulillahi ulishuhudiwa kwa uwazi katika baadhi ya sekta. Katika sekta ambazo kumeshuhudiwa uongozi na usimamiaji ya kijihadi, kumeshuhudiwa pia maendeleo ndani yake. Hii tab'an si nasaha inayohusiana na mwaka 93 tu, bali nia na azma ya kitaifa na vile vile uongozi na uendeshaji wa mambo kijihadi unatakiwa pia mwaka huu na katika miaka yote ijayo kwa ajili ya ufanisi wa taifa letu.
Amma katika mwaka 94, tuna matumaini makubwa kwa taifa letu azizi na kwamba matumaini yote hayo yanawezekana kufikiwa. Matumaini yetu makubwa kwa ajili ya taifa letu mwaka huu ni maendeleo ya kiuchumi, nguvu na heshima ya kieneo na kimataifa, mapinduzi ya kielimu kwa maana halisi ya neno, uadilifu wa kimahakama na wa kiuchumi pamoja na imani na umaanawi jambo ambalo ndilo muhimu zaidi kuliko yote na ndilo linalovitia nguvu vipengee vyote vingine. Kwa mtazamo wangu, matakwa na matumaini yote hayo yanawezekana kufikiwa. Hakuna hata moja kati ya mambo hayo ambalo haliwezi kufikiwa na uwezo wa kitaifa wa Iran na nguvu za kisiasa za mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu. Uwezo wetu ni mkubwa sana. Kuna mambo mengi ya kusema kuhusu suala hilo ambapo Inshaallah nitayaashiria yale muhimu zaidi katika hotuba ya jioni (ya Jumamosi Machi 21, 2015).
Ninalopenda kuliambia hivi sasa taifa letu azizi ni kwamba, uwezo huo adhimu na muhimu unawezekana kufikiwa, lakini una masharti yake; na moja na sharti muhimu zaidi ni kuweko ushirikiano wa dhati kati ya wananchi na Serikali. Kama utakuweko ushirikiano wa dhati kutoka pande zote hizo mbili, basi bila ya shaka yoyote itawezekana kufanikishwa matumaini yote tuliyo nayo; na wananchi wetu azizi wataona athari zake. Serikali ni mtumishi wa wananchi na wananchi ndio wanaoiajiri Serikali. Kadiri yanapokuwepo mapenzi na ukuruba wa dhati baina ya serikali na wananchi na kadiri ushirikiano na fikra za pamoja zinavyokuwa nyingi na kubwa baina ya wananchi na Serikali, ndivyo kazi bora zaidi zinavyoweza kufanyika. Inabidi kila upande umwamini mwenzake. Serikali iwakubali wananchi kwa maana halisi ya neno na ikubaliane kwa njia sahihi na thamani na hima na uwezo wa wananchi; na wananchi nao kwa upande wao wanapaswa waiamini vilivyo serikali kwa maana halisi ya neno kwani ndiye mtumishi na mtekelezaji wa kazi zao. Katika suala hili pia nina maneno na nasaha za kutoa na Inshaallah nitaashiria mambo hayo katika hotuba yangu (ya Jumamosi jioni). Hivyo kwa mtazamo wangu, mwaka huu inabidi uwe mwaka wa ushirikiano mkubwa baina ya serikali na wananchi. Hivyo nimeona kaulimbiu ya mwaka huu iwe: "Serikali na Wananchi, Kupendana na Kufahamiana." Ni matumaini yangu kaulimbiu hiyo itatekelezwa kivitendo na pande zote mbili zinazounda kaulimbiu hiyo yaani wananchi wetu azidi, taifa letu kubwa, taifa letu shujaa na lenye hima ya hali ya juu, taifa lenye busuri na muono wa mbali, taifa lenye utambuzi wa mambo (kwa upande mmoja) na serikali inayowatumikia wananchi (kwa upande wa pili na), wote watafanya jitihada zao zote kufanikisha inavyotakiwa kaulimbiu hiyo ili athari na matunda yake yaweze kuonekana.

Ninamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu (azitie baraka na) kuzipa maendeleo kazi zote kubwa nchini mwetu na atupe taufiki ya kuweza kufanikisha vizuri wajibu wetu.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

 

 
< Nyuma   Mbele >

^