Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Kiongozi Muadhamu Ahudhuria na Kuhutubia Umati wa Wafanya Ziara katika Haram ya Imam Ridha AS Chapa
21/03/2015
Katika siku ya kwanza ya mwaka 1394 (mwaka wa Kiirani wa Hijria Shamsia), Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, leo jioni (Jumamosi), amehutubia mjumuiko mkubwa wa makumi ya maelfu ya wafanya ziara na majirani wa Harama ya Imam Ali bin Musa ar Ridha AS mjini Mash-had, kaskazini mashariki mwa Iran. Katika mkutano huo ambao umefanyika katika ukumbi wa Imam Khomeini (quddisa sirruh) na kumbi za pembeni mwake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa hotuba muhimu ambayo ndani yake amebainisha kaulimbiu ya mwaka huu ya "Serikali na Wananchi, Kupendana na Kufahamiana" na huku akisisitizia jukumu la pande mbili la uungaji mkono wa wananchi kwa serikali halali iliyochaguliwa kwa mujibu wa sheria na vile vile ulazima wa viongozi nchini Iran kuwa na kifua kipana mbele ya ukosoaji wa kimantiki, amegusia misingi minne inayounda jengo la mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na fursa pamoja na changamoto zinazoukabili mfumo huo wa utawala wa Kiislamu na kusema: Ni jambo la wajibu kwa viongozi, vyombo vya habari na hususan wanaharakati wa masuala ya kiuchumi kuwa malengo na mipango maalumu ya maendeleo na ustawi wa kiuchumi na kuyasaidia matabaka mbali mbali ya wananchi na kwamba kufanya hivyo ni jukumu kubwa la watu wote. Amesema, leo hii uwanja wa kiuchumi ni medani maalumu ya mapambano ambapo inahitajika kufanya harakati ya kijihadi kwa kutumia uwezo wote uliopo pamoja na ubunifu wa dhati na kwa kustafidi na suhula, nyezo, mbinu na siasa maalumu ili kuleta ufanisi katika medani hiyo.
Vile vile Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia mazungumzo ya nyuklia na kusisitiza akisema: Nchini Iran hakuna mtu yeyote anayepinga utatuzi wa kidiplomasia wa kadhia ya nyuklia ya taifa hili, lakini wakati huo huo taifa la Iran na viongozi wa Iran pamoja na timu ya mazungumzo ya Iran hawakubaliani kabisa na kutwishwa mambo na ubeberu wa Marekani na kwamba taifa la Iran litafanikiwa kulinda haki zake kwa kusimama kidete katika mtihani huo mkubwa.
Aidha Ayatullah Udhma Khamenei amenukuu aya moja ya Qur'ani Tukufu inayobainisha vielelezo vinne vya "Sala, Zaka, Kuamrishana Mema na Kukatazana Mabaya" na kuvitaja vielelezo hivyo kuwa ndivyo vielelezo na misingi mikuu inayounda jengo la mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuongeza kuwa: Mwenyezi Mungu Mtukufu ameahidi kwamba, atalinusuru na kulitoa chini ya udhibiti na ubeberu wa madola ya kiistikbari kila taifa ambalo litajipamba kwa sifa hizo nne.
Amesisitiza kwamba: Vielelezo na sifa hizo, kila moja ina upande wa wajibu wa utekelezaji kwa mtu binafsi na vile wa jamii nzima na kila kimoja kina umuhimu na nafasi kubwa katika muundo wa mfumo wa Kiislamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria faida za sala kwa mtu binafsi katika kumletea saada na kumjenga muumini na kuongeza kuwa: Pamoja na kuwa na faida hizo kwa mtu binafsi, Sala ina faida kubwa pia za kijamii na huziandaa nyoyo za watu katika jamii na kuzielekeza kwenye kujenga mapenzi na mshikamano baina yao na kuzikutanisha nyoyo zao wote katika dhati na Kituo Kimoja Kikuu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia pia namna Zaka inavyoandaa uwanja wa kupata nguvu moyo wa kujitolea watu na kusema kuhusu faida za kijamii za Zaka kwamba: Katika upeo wa kijamii, Zaka inathibitisha sifa ya Muislamu wa kweli ya kwamba Muislamu (ni ndugu wa Muislamu mwenzake na) haoni tofauti baina yake na watu masikini, dhaifu na wahitaji katika jamii yake.
Kiongozi Muadhanmu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia amesema kuwa, Kuamrishana Mema na Kukatazana Mabaya ndio msingi wa hukumu na sheria zote za Kiislamu na huku akisisitiza kuwa Waislamu wote katika nukta yoyote ile ya dunia wana wajibu na jukumu la kuiongoza jamii kwenye kutenda mema na kuwa na matendo mazuri na kuizuia jamii kutumbkia kwenye maovu na matendo mabaya, ameongeza kwamba: Jambo ambalo linapaswa kufanywa muhimili wa mambo yote, ni kuamrishana kutenda jambo jema zaidi kuliko yote nalo ni kuunda na kulinda mfumo wa utawala wa Kiislamu.
Pia amelitaja suala la kulindwa heshima ya taifa la Iran, kuimarishwa utamaduni na usalama katika mazingira ya kimaadili, usalama katika mazingira ya familia, kuongeza na kulea kizazi bora cha vijana, kuandaa mazingira ya kuzidi kustawi Iran, kustawisha uchumi na uzalishaji wa ndani, kulifanya suala la maadili ya Kiislamu kuwa la kila mtu, kupanua na kukuza elimu na teknolojia, kusimamisha uadilifu wa kimahakama na kiuchumi, kufanya jitihada kwa ajili ya kuleta umoja wa Kiislamu pamoja na kulitia nguvu, kulistawisha taifa na kuimarisha nguvu za umma wa Kiislamu, kuwa ni miongoni mwa mambo mema zaidi ambayo kila mmoja ana wajibu wa kufanya jitihada za kuyafanikisha.
Vile vile Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia mifano ya maovu makubwa zaidi ikiwa ni pamoja na kueneza vitendo vichafu vya kimaadili na kuharibu utamaduni, kuwasaidia maadui, kujaribu kuudhoofisha mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na utamaduni wa Kiislamu na kudhoofisha uchumi, elimu na teknolojia akiongeza kuwa: Dhati ya Mwenyezi Mungu Mtukufu katika daraja la kwanza na Mtume SAW na Maimamu maasumu Alayhimus Salaam katika hatua inayofuatia, ni miongoni mwa mambo mawili bora na makubwa zaidi katika suala zima la kuamrishana mema na kukatazana mabaya na kwamba kila muumini katika nukta yoyote ile alipo katika ulimwengu wa Kiislamu ana wajibu wa kuyatekeleza ipasavyo mambo hayo akijua kuwa kufanya hivyo ni jambo la faradhi lililoamrishwa na Mwenyezi Mungu kulitekeleza.
Ayatullah Udhma Khamenei ameendelea na hotuba yake kwa kubainisha kaulimbiu ya mwaka huu mpya yaani "Serikali na Wananchi, Kupendana na Kufahamiana" na kusema kuwa kaulimbiu hiyo imechaguliwa kwa kuzingatia msingi wa vielelezo hivyo vine vikuu na kwa lengo la kuleta mshikamano wa kitaifa na wa kijamii kati ya matabaka mbali mbali ya wananchi ndani ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Kiislamu.
Ameongeza kuwa: Uislamu unaitaka mirengo yote ya kijamii kushikamana, kufanya kazi kwa pamoja na kusaidiana. Hivyo serikali yoyote ile ndani ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu inapaswa kuungwa mkono na kusaidiwa na wananchi wote, hata wale ambao hawakuipa kura zao.
Kiongozi Mudhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja suala la kuweko kauli moja baina ya wananchi na serikali hususan katika nyakati ambazo nchi imo kwenye changamoto nzito kuwa ni jambo muhimu na la dharura na kuongeza kwamba: Jukumu la matabaka mbali mbali ya wananchi leo hii ni kuwasaidia viongozi na serikali nchini na kuwaunga mkono.
Amesema, kuisaidia na kushirikiana na serikali mbali mbali zinazoingia madarakani ni msingi mkuu na wa siku zote nchini Iran na hapo hapo akabainisha udharura wa suala hilo akisema: Daghadagha na hima kuu wa serikali zote zinazoingia madarakani nchini Iran ni kutatua matatizo ya wananchi na ya nchi kwa hadiri zinavyoweza, hivyo kuna wajibu wa kuzisaidia serikali hizo katika jitihada zake za kutatua matatizo hayo.
Ayatullah Udhma Khamenei amezitaja kura za wananchi kuwa ndizo zinazoandaa mazingira ya kupata uhalali serikali hizo na kuongeza kuwa: Jambo muhimu hapa si idadi ya wananchi waliompigia kura Rais fulani, bali serikali yoyote inayoingia madarakani baada ya kupata kura nyingi za wananchi huwa ni serikali halali kwa mujibu wa Katiba na wananchi wote wanapaswa kuisaidia kadiri wanavyoweza serikali hiyo halali.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameendelea kutoa miongozo yake hiyo muhimu kuhusiana na udharura wa kuweko ushirikiano, kusaidiana na kulindwa haki za pande zote kwa kugusia suala la kuweko wakosoaji na namna ukosoaji huo unavyotakiwa kufanywa na jinsi wanaokosolewa nao wanavyotakiwa kuamiliana na ukosoaji huo.
Amegusia kuweko mwenendo wa daima na unaotegemewa kuwepo wakati wote wa kuweko wakosoaji wa serikali yoyote ile inayoingia madarakani na kusema: Serikali ya hivi sasa pia, kama ilivyojiri kwa serikali zilizoitangulia, nayo ina watu wanaoikosoa na hakuna tatizo wala kizuizi chochote katika hilo, yaani hakuna tatizo wala kizuizi chochote cha kuweko watu ambao wanaamua kuikosoa serikali kutokana na kwamba hawakubaliani na mbinu, miamala, matamshi na siasa za serikali fulani, lakini tab'an inabidi ukosoaji huo ufanyike kwa busara, mantiki na hekima.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kusema kuwa: Hata na mimi pia nimekuwa nikizikosoa serikali mbali mbali kwa kila jambo ambalo huwa nahisi linapasa kukosolewa. Sijawahi hata mara moja kuacha kuzikumbusha wajibu wake kila inapolazima, lakini mara zote nimekuwa nikihakikisha nafanya hivyo katika nyakati na sura zinazofaa.
Baada ya hapo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amebainisha fremu na kalibu za ukosoaji wa kimantiki akisema kuwa: Ukosoaji unapaswa uwe kwa namna ambayo haitaondoa imani ya wananchi na kuwafanya kuwa na mtazamo mbaya kuhusiana na viongozi wanaowatumikia wananchi. Vile vile ukosoaji haupaswi kufanywa kwa madharau, kuwadhalilisha watu wengine na wala kwa namna ya kueneza chuki.
Aidha ameitaja miamala iliyosimama juu ya msingi wa udugu wa Kiislamu, kusaidiana, kupendana na kuhurumiana kuwa ni vielelezo vingine vya lazima vinavyopaswa kuchungwa wakati wa kukosoa kitu na kuongeza kwamba: Tab'an nasaha hizi nazitoa kwa ajili ya pande zote mbili, kwa viongozi wa mihimili yote mitatu mikuu ya dola (Serikali, Bunge na Mahakama) kwamba kila mmoja achunge mipaka hiyo na kuamiliana vizuri na watu wanaowakosoa bila ya kumdhalilisha au kumvunjia heshima mtu, na wote watambue kuwa kama viongozi watawavunjia heshima watu wanaowakosoa, basi kufanya hivyo ni kinyume kabisa na hekima na tadibiri.
Ayatullah Udhma Khamenei pia amesema kwa kusisitiza kwamba: Mimi si kwamba ninawataka wananchi wetu azizi wawe watu wasiojali mambo au wasiodadisi kitu, bali ninalowataka mimi ni kudadisi, kufuatilia na kuguswa na masuala ya nchi yao lakini wakati huo huo ninapenda kumwambia kila mtu, iwe ni wananchi au viongozi, wote kwa pamoja kwamba wanapaswa kufanya ukosoaji kwa kuchunga mipaka na kujiepusha na kuharibu mambo na wajiepushe na pia wajiweke mbali na kuwadhalilisha na kuwavunjia heshima watu wengine kwa jina la ukosoaji.
Ameongeza kuwa, si uhalifu na wala si makosa kutokezea watu wakawa na wasiwasi na daghadagha kuhusiana na masuala muhimu ya nchi yao, na hakuna kizuizi chochote katika jambo hilo. Hata hivyo kuwa na hisia hizo kusimruhusu mtu kumtuhumu mwingine na kudhararu jitihada na huduma zake zote alizotoa na katika upande wa pili pia serikali na wafuasi wa serikali hiyo nao wajiepushe na kuwadhalilisha na kuwavunjia heshima watu wanaoonyesha wasiwasi wao kuhusiana na uendeshaji wa nchi yao.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia tabia yake ya kawaida na ya kila siku ya kuziunga mkono serikali zote zinazongia madarakani nchini Iran, iwe serikali ni ya hivi sasa au za kabla ya hivi sasa na kusisitiza kuwa: Serikali iliyopo madarakani hivi sasa ninaiunga mkono, tab'an hiyo haina maana ya kwamba ninaunga mkono kila kinachofanywa na serikali, bali msimamo wangu kwa serikali unategemea kazi na jitihada za watumishi wake.
Akiendelea na hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia fursa kubwa ilizo nazo Iran pamoja na changamoto zinazoikabili na kusema kuwa: Inawezekana kuzishinda changamoto zote hizo kwa taufiki ya Mwenyezi Mungu na kwa kuwa na mipango mizuri na kwa kutumia kwa wakati fursa zinazojitokeza na uwezo uliopo nchini.
Ayatullah Udhma Khamenei amekutaja kuwa na nguvukazi bora, ya watu wabunifu na hususan ya vijana, pamoja na kujitokeza wananchi na hasa vijana katika kuutumikia mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu kwamba ni miongoni mwa fursa kubwa ilizo nazo Iran na kuongeza kuwa: Pamoja na kuwepo mashambulizi makubwa ya vyombo vya habari vya mabeberu dhidi ya vijana wa Iran ili kuwakatisha tamaa na kuwavunja moyo kuhusu mustakbali wao kwa lengo la kukabiliana na Jamhuri ya Kiislamu au kueneza fikra potofu na kutojali mambo kati ya vijana wa Iran, lakini pamoja na hayo, makumi ya maelfu ya vijana wa Iran wanaendelea kujitokeza katika matukio mbali mbali hususan kwenye maandamano ya Bahman 22 (siku zinapofikia kileleni sherehe za Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran) na kuonesha uungaji mkono na mapenzi yao makubwa kwa Jamhuri ya Kiislamu na kwa Imam Khomeini (quddisa sirruh).
Vile vile ameyataja maendeleo makubwa ya kielimu iliyopata Iran katika kipindi cha vikwazo vya kila namna dhidi yake kuwa ni miongoni mwa fursa kubwa ilizo nazo Iran na kuongeza kuwa: Maendeleo mbali mbali makubwa ya kielimu iliyopata Iran katika miaka ya hivi karibuni ikiwa ni pamoja na kuanzisha miradi mikubwa na tata ya viwandani ukiwemo mradi mkubwa wa eneo la 12 la uchimbaji wa gesi katika eneo la Pars Kusini, na kuoneshwa zana na vifaa vya kisasa vilivyowastaajabisha maadui katika luteka na manuva ya kijeshi ya vikosi vya ulinzi vya Iran; ni maendeleo ambayo yote yamepatikana licha ya Iran kuwa chini ya vikwazo na mashinikizo ya kila namna kutoka kwa madola yanayolitakia mabaya taifa hili na ambayo yanadai kuwa yameiwekea vikwazo vya kuifanya kilema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyataja mashinikizo na vikwazo vilivyopo hivi sasa kuwa pia ni fursa kwa taifa la Iran licha ya kuweko matatizo yanayosababishwa na vikwazo hivyo na baada ya hapo amebainisha baadhi ya changamoto zinazoikabili Jamhuri ya Kiislamu akisema: Moja ya changamoto kubwa zaidi zilizopo hivi sasa ni suala la uchumi wa taifa na kutatua matatizo ya kiuchumi na ya kimaisha ya wananchi ambapo suala hilo linahitajia harakati ya kweli kama ambavyo pia linahitajia kufanyika kazi kubwa.
Baada ya hapo, Ayatullah Udhma Khamenei amekumbushia utabiri wake wa miaka kadhaa iliiyopita uliohusiana na nia ya adui ya kuelekeza zaidi mashambulizi yake kwenye uchumi wa Iran na ulazima wa viongozi nchini kuwa tayari kwa ajili ya kukabiliana na mashambulizi hayo na kuongeza kuwa: Watu wanaolitakia mabaya taifa la Iran wanasema wazi wazi kuwa, lengo lao la kuiwekea vikwazo vya kiuchumi Iran ni kufanikisha lengo lao la kisiasa yaani kuwafanya wananchi wa Iran waoneshe kutoridhishwa na viongozi na mfumo wao wa utawala na hivyo kuvuruga usalama na amani nchini kwa kuwafanya wananchi wa Iran wapambane na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu.
Amesisitiza kuwa, suala la kukabiliana na changamoto hiyo linahitajia ushirikiano na fikra za pamoja za nguvukazi zote pamoja na viongozi wote nchini sambamba na kulipa uzito wa hali ya juu suala la kustawisha uchumi. Baada ya hapo ametolea ufafanuzi zaidi changamoto zilizopo kwa kukumbushia nukta nne tofauti.
Nukta ya kwanza kabisa iliyoashiriwa na Ayatullah Udhma Khamenei, ni wajibu wa kuweko harakati ya kijihadi ya kukabiliana na siasa za chuki za Marekani katika medani ya mapambano ya kiuchumi. Kuhusiana na suala hilo amegusia mitazamo miwili iliyopo nchini Iran kuhusu njia za kutatua masuala na matatizo ya kiuchumi.
Amesema: Kuna mtazamo humu nchini unaoamini kuwa, maendeleo na ustawi wa kiuchumi utaweza kupatikana kwa kutumiwa nguvu na uwezo wa ndani ya nchi ambao hadi sasa umezingatiwa kidogo sana na baadhi ya wakati uwezo huo haujatumiwa kabisa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Mtazamo wa pili unapingana kikamilifu na mtazamo huo wa kwanza. Ni mtazamo unaoamini kuwa, ustawi na maendeleo ya kiuchumi yanaweza kupatikana kwa kutegemea msaada kutoka nje ya mipaka ya Iran. Hivyo kwa mujibu wa mtazamo huo, inabidi siasa za mambo ya kigeni za Iran zibadilike na zikubaliane na kila wanachotaka mabeberu na waistikbari, ili kwa njia hiyo tuweze kutatua matatizo yaliyopo ya kiuchumi!
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kwamba: Mtazamo huu wa pili ni ghalati kikamilifu, ni tasa na hauna faida yoyote.
Baada ya hapo ametoa sababu zinazoufanya mtazamo huo wa pili kuwa ghalati kwa kusema: Vikwazo vya madola ya Magharibi vilivyopo hivi sasa dhidi ya taifa la Iran, ni ushahidi wa wazi kabisa wa kutokuwa sahihi mtazamo huo unaosema kwamba ustawi wa kiuchumi utaweza kupatikana nchini kwa kutegemea madola ya kigeni na sababu ni kwamba, madola hayo ya kigeni kamwe hayawezi kuachana na siasa zao za kibeberu kwa kadiri yoyote ambayo taifa fulani litajipendekeza kwao. Vile vile huwa kunatokezea masuala ya ghafla na yasiyotegemewa katika vile mpango wa kupunguza bei ya mafuta duniani ambayo hutoa pigo kwa uchumi wa nchi.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Leo hii njama kubwa zinazofanywa na madola yanayolitakia mabaya taifa la Iran ni kukuza na kutia nguvu huo mtazamo wa pili na ni kwa sababu hiyo ndio maana Rais wa Mrekani katika ujumbe wake wa Nairuzi kwa wananchi wa Iran alisema kuwa, kama mtakubaliana na matakwa yetu katika mazungumzo ya nyuklia, basi kutashuhudiwa ustawi wa kiuchumi na kuongezeka nafasi za kazi na uwekezaji nchini Iran.
Vile vile amesisitiza kuwa: Kuyategemea madola ya kigeni kuja kututatulia masuala ya kiuchumi kamwe hakuwezi kuwa na mafanikio. Hivyo inabidi siku zote na wakati wote tutafute njia za kuweza kutumiwa uwezo wa ndani ya nchi kutatua matatizo hayo na ndio maana fikra ya "Uchumi wa Kusimama Kidete" ikapokewa vizuri na wataalamu wote wa kiuchumi. Uchumi huo unategemea uwezo wa ndani ya nchi na wa taifa kwa ajili ya kuimarisha na kustawisha uchumi.
Nukta ya tatu iliyokumbushiwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusiana na masuala ya kiuchumi, ni ulazima wa viongozi nchini kujiwekea malengo na kuwa na sera na siasa maalumu za kiuchumi na kujiepusha na kutegemea mbinu na njia za namna moja kila siku.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema: Lengo kuu ambalo mwaka huu (1394 Hijria Shamsia) inabidi lipewe umuhimu mkubwa na viongozi pamoja na wananchi nchini, ni kutoa hima ya kipekee kwa suala la kukuza na kustawisha uzalishaji wa ndani ya nchi.
Baadaye amebainisha njia mbali mbali za kukuza na kustawisha uzalishaji wa ndani ya nchi akisema: Kuungwa mkono na kusaidiwa asasi kubwa, za wastani na ndogo za kiuchumi, kuzitia nguvu asasi za elimu msingi, kuleta mwamko wa kupunguza uuzaji mali ghafi, kuwarahisishia kazi wawekezaji, kupunguza kiwango cha bidhaa za matumizi kutoka nje pamoja na kupambana na magendo ni miongoni mwa njia za kuunga mkono na kusaidia uzalishaji wa ndani ambao tab'an benki mbali mbali nchini zinaweza kusaidia na kulitia nguvu jambo hilo kama ambavyo zinaweza pia kuharibu, hivyo viongozi waandamizi wa benki nchini wanapaswa kulipa uzito wa hali ya juu na kulizingatia mno suala hilo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza pia kuwa, kutekeleza mambo hayo na kuyafanya yalete athari ni jambo gumu lakini wakati huo huo amesisitiza kuwa: Viongozi nchini wanapasa kufanya kazi nzito na ngumu kwani suala la uchumi na ustawi wa kiuchumi ni muhimu sana.
Ayatullah Udhma Khamenei amezungumzia pia nafasi ya uwekezaji na mchango wa wananchi katika kusaidia uzalishaji wa ndani akisema kuwa nafasi hiyo ni muhimu mno na kuongeza kwamba: Kuelekeza uwekezaji katika masuala ya uzalishaji wa ndani, na kujenga utamaduni wa kupenda kutumia bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi na kujiepusha na kufanya israfu ni miongoni mwa njia za kukuza na kutia nguvu uzalishaji wa ndani ya nchi.
Katika kubainisha nukta ya nne na ya mwisho kuhusiana na uchumi wa taifa, Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kuwa: Vikwazo ndiyo silaha pekee aliyo nayo adui katika kukabiliana na taifa la Iran, hivyo kama kutakuwa na mipangilio na tadibiri sahihi na kama tutategemea nguvu za ndani na kuweko mipangilio mizuri inayotekelezwa kivitendo, basi athari za vikwazo vya maadui zitapungua na baadaye havitakuwa na taathira zozote.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, kama viongozi wa serikali na matabaka mbali mbali ya wananchi pamoja na wanaharakati wa masuala ya kiuchumi watatia hima na kama vyombo vya habari vya umma navyo vitasaidia, basi tutaona kwa macho yetu namna vikwazo vinavyoshindwa kulizuia taifa la Iran kupiga hatua za kimaendeleo.
Akiendelea na hotuba yake, Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria mazungumzo ya nyuklia na kubainisha ndani yake nukta kadhaa kuhusu mazungumzo hayo.
Amegusia namna upande wa pili unaofanya mazungumzo na Iran unavyoweka mipango na siasa za kina hususan Marekani na kusema: Wamarekani wanayahitajia mno mazungumzo hayo na kwamba hitilafu zinazoonekana ndani ya Marekani kuhusu mazungumzo hayo zinatokana na kwamba mrengo unaopinga serikali ya hivi sasa ya Marekani hautaka faida za mazungumzo hayo ziende kwa serikali na kuwa na manufaa kwa chama tawala.
Ameashiria pia ujumbe wa Nairuzi uliotolewa na Rais wa Marekani na matamshi yasiyo na ukweli yaliyotolewa na Rais huyo kwenye ujumbe wake huo na kuongeza kuwa: Katika ujumbe wake, Rais wa Marekani amesema kuwa, nchini Iran kuna watu ambao wanapinga utatuzi wa kidiplomasia wa kadhia ya nyuklia wakati ambapo matamshi hayo si kweli, kwani nchini Iran hakuna mtu yeyote anayepinga kutatuliwa kadhia ya nyuklia kwa njia za mazungumzo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Kitu ambacho kinapingwa na taifa la Iran ni ubeberu na utwishaji wa mambo unaofanywa na serikali ya Marekani na kwamba taifa la Iran limesimama imara kukabiliana na ubeberu huo.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza pia kuwa: Si viongozi peke yao na wala si timu ya mazungumzo tu na wala si wananchi wa Iran peke yao, bali kila mtu nchini Iran hawezi kukubaliana kivyovyote vile na ubeberu wa Marekani.
Aidha amesisitiza kwa mara nyingine tena kuhusu suala la mazungumzo yanayoendelea hivi sasa baina ya Iran na Marekani akisema kwa msisitizo kuwa mazungumzo hayo ni kuhusu suala la nyuklia tu na hayahusiana na suala jingine lolote lile. Amesema: Sisi hatuwezi kamwe kufanya mazungumzo na Marekani kuhusu masuala ya ndani, ya kieneo pamoja na suala la silaha na sababu yake ni kwamba siasa za Marekani katika eneo hili ni za kuleta machafuko na kukabiliana na mataifa ya eneo hili pamoja na kuzuia mwamko wa Kiislamu, siasa ambazo zinapingana kikamilifu na siasa kuu za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia matamshi yanayotolewa mara kwa mara na Wamarekani kwamba hata baada ya kufikiwa makubaliano vikwazo dhidi ya Iran havitaondolewa ila baada ya kuifanyia uchunguzi miamala na mienendo ya Iran na kuyataja matamshi hayo kuwa ni hila na hadaa. Ameongeza kuwa: Matamshi hayo hayakubaliki kabisa, kwani kuondolewa vikwazo ni sehemu ya mazungumzo na si matunda ya mazungumzo, hivyo, kama alivyosema wazi wazi mheshimiwa Rais wa Iran, vikwazo dhidi ya Iran vinapaswa kuondolewa mara baada ya kufikiwa makubaliano.
Ayatullah Udhma Khamenei vile vile ameguasia matamshi ya Wamarekani kwamba maamuzi yoyote ya Iran katika makubaliano yoyote yanayotarajiwa kufikiwa si kitu cha kurudi nyuma na kusema: Matamshi hayo pia hayakubaliki kwani kama wao wanajipa haki ya kurejesha vikwazo kwa kisingizio chochote kiwacho hata kama kutatiwa saini makubaliano ya nyuklia, basi hawana sababu yoyote ya kutufanya na sisi tukubaliane na madai yao hayo ya kutorudi nyuma kwenye maamuzi yetu.
Amesisitiza kuwa: Sekta ya teknolojia ya nyuklia ya Iran ni sekta ya ndani ya nchi na ni ya wananchi ambayo inabidi isonge mbele kwani ni sehemu ya asili na ni dhati ya kila suala la kiufundi na kiteknolojia nchini.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria madai mengine ya Wamarekani wanaodai kuwa Iran inafanya juhudi za kumiliki silaha za nyuklia na kuongeza kuwa: Hata Wamarekani wenyewe wanajua kuwa sisi katika mazungumzo hayo tumeshikamana na tumeheshimu ahadi zote za kimataifa pamoja na ahadi za maadili ya kisiasa na kamwe hatujakwenda kinyume na ahadi yoyote ile bali hata hatujajaribu kwenda kinyume na ahadi hizo, lakini katika upande wa pili, Wamarekani wamevunja ahadi na kufanya hila na udanganyifu pamoja na kuendesha siasa za nyuso mbili katika misimamo na matamshi yao.
Ayatullah Udhma Khamenei pia amesema kuwa, miamala na mienendo ya Wamarekani katika mazungumzo hayo ni somo kwa wananchi wa Iran la kuzidi kutambua siasa za kibeberu za Wamarekani na kuongeza kuwa: Mwenendo wa Marekani ni somo pia kwa watu wenye fikra huru nchini ambalo linazidi kuwathibitishia kwamba ni mtu wa namna gani anayefanya mazungumzo na Iran na ni namna gani Marekani inaamiliana na mazungumzo hayo.
Aidha ameashiria baadhi ya vitisho vinavyotolewa na Marekani vya uwezekano wa kuongezwa vikwazo au kufanyika harakati za kijeshi dhidi ya Iran kama makubaliano hayatafikiwa na kusisitiza kuwa: Vitisho hivyo havilitishi taifa la Iran, kwani taifa hili limesimama kidete na litatoka kwa mafanikio kamili kwenye mtihani huu mkubwa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameitaja taufiki na msaada wa Mwenyezi Mungu kuwa ndiyo sababu kuu ya mafanikio ya taifa la Iran katika njia hiyo na kuongeza kuwa: Serikali na wananchi wa Iran wana majukumu na kazi kubwa ya kufanya na miongoni mwa kazi na majukumu hayo ni suala la umoja wa Kiislamu, kuyasaidia mataifa dhaifu na kueneza ushawishi wa umaanawi wa Kiislamu katika eneo hili suala ambalo Iran hivi ssa ndiyo iliyobeba bendera yake ya kulifanikisha.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake hiyo muhimu, Ayatullah Udhma Khamenei, amegusia historia kongwe ya Nairuzi na kuzitaja sherehe za hivi sasa za Nairuzi kuwa ni ubunifu wa kihekima na busara nyingi wa Kiislamu na kuongeza kuwa, sherehe za kale za Nairuzi zilikuwa na sura ya sherehe za kifalme na zilikuwa ni fursa kwa wafalme na watawala madikteta ya kuyaonesha mataifa mengine ukubwa na nguvu, majivuno na ufakhari wao, hata hivyo hivi sasa Wairani Waislamu wameondoa kabisa mambo hayo na kuzibadilisha sherehe za Nairuzi kwa sura nzuri, ya busara na iliyojaa hekima.
Amesema kuwa, uhakika wa Nairuzi ni uhakika wenye sura ya wananchi na kusisitiza kwamba: Sherehe za hivi sasa za Nairuzi sizo tena zile sherehe za kale za Nairuzi, bali Nairuzi ya hivi sasa ni Nairuzi ya Kiirani, ni sherehe za Nairuzi ya taifa la Waislamu ambao wameweza kuzibadilisha sherehe hizo na kuzifanya kuwa rasilimali ya kuelekea kwenye ufanikishaji wa malengo ya kimaanawi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Hivi sasa katika siku za Nairuzi na katika ile sekunde na lahadha ya kubadilika mwaka na kuingia mwaka mpya, utaona kuwa maeneo yenye msongamano mkubwa zaidi wa watu, yenye idadi kubwa zaidi ya wananchi wa nchi hii kubwa na pana, ni maeneo matukufu ya Maimamu na wana wa Maimamu (Alayhimus Salaam).
Vile vile Ayatullah Udhma Khamenei amegusia kusadifiana sherehe za Nairuzi mwaka huu na siku za "Fatimiyah" (za kukumbuka kufa shahidi Binti Mtukufu wa Bwana Mtume Muhammad SAW, Bibi Fatimatuz Zahra - Salamullahi Alayha) na kusema kuwa: Kwa kuzingatia mtazamo wa kihekima na kibusara wa Wairani kuhusiana na Nairuzi, sherehe za Nairuzi mwaka huu hazipaswi kwa namna yoyote ile zikinzane na suala la kuheshimu na kutukuza siku alipokufa shahidi bibi huyo mtukufu katika ulimwengu wa Kiislamu, Bibi Fatimatuz Zahra SA, na kwa yakini hakuna mkizano wala mgongano wowote utakaotokea katika suala hilo.
 
< Nyuma   Mbele >

^