Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Aonana na Wasoma Kasida za Ahlul Bayt AS Chapa
09/04/2015
 Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, leo asubuhi ameonana na majimui ya akinamama, washairi na wasoma kasida za Ahlul Bayt Alayhimus Salaam na sambamba na kutoa mkono wa baraka na fanaka kwa mnasaba wa maadhimisho ya siku ya kuzaliwa Bibi fatimatuz Zahra Salamullahi Alayha, ameitumia fursa hiyo kutoa maelezo muhimu kuhusiana na mazungumzo ya nyuklia kati ya Iran na kundi la 5+1 na vile vile matukio ya nchini Yemen.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameanza hotuba yake kwa utangulizi huu kwamba, kuna baadhi ya watu wanauliza, kwa nini yeye hajachukua msimamo wowote kuhusiana na maelewano yaliyofikiwa hivi karibuni kuhusiana na kadhia ya nyuklia?
Baada ya hapo amejibu swali hilo akisisitiza kwa kusema kuwa, sababu inayomfanya asichukue msimamo wowote ni kwamba, hakuna sehemu ya kuchukulia msimamo kwenye suala hilo, kwani viongozi nchini na wahusika wa kadhia hiyo ya nyuklia wanasema kuwa, hadi sasa hakuna jambo lolote lililofanyika na hakuna suala lolote ambalo limeshakuwa wajibu kutekelezwa na pande hizo mbili. Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Hali kama hii haihitajii kuichukulia msimamo.
Ameongeza kuwa: Kama mimi nitaulizwa je, unakubaliana na mazungumzo ya hivi karibuni ya nyuklia au hukubaliani nayo, nitasema siwezi kusema nakubaliana nayo au sikubaliani nayo kwa sababu hadi hivi sasa hakuna chochote kilichotokea.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Tatizo lote liko katika hili suala kwamba kuna wajibu wa kujadiliwa na kuchunguzwa vipengee vya kadhia hiyo kwani upande wa pili wa mazungumzo ni mkaidi, usio na ahadi za kutegemewa, wenye miamala mibaya, na wenye tabia ya kusubiri fursa tu ya kushambulia na kuna uwezekano wakati wa mazungumzo kikatokezea kipindi wakaizunguka nchi na taifa pamoja na timu ya mazungumzo kuhusiana na vipengee vinavyojadiliwa katika mazungumzo hayo.
Amesema: Kitu ambacho hadi hivi sasa kimetokea si asili ya makubaliano na wala si mazungumzo ya kufikiwa mwafaka na wala si jambo ambalo linadhamini kupatikana makubaliano na wala lenyewe suala hilo halitoi dhamana hata ya kufikiwa makubaliano kwenye mazungumzo hayo, hivyo kutoa pongezi kuhusu jambo hilo ni suala ambalo halina maana yoyote.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameendelea na hotuba yake kwa kutaja nukta kadhaa muhimu. Amesema: Mimi kamwe sijawahi kuwa na mtazamno mzuri kuhusiana na mazungumzo na Marekani na msimamo wangu huo hautokani na mambo ya kutasawari tu, bali unatokana na uzoefu tulio nao kuhusu Marekani.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Kama katika siku za usoni kutatangazwa vipenge vya masuala, matukio na dondoo za mazungumzo na hivi sasa ya nyuklia, basi watu wote wataelewa wasiwasi wetu unatokana na nini hasa.
Ameongeza kuwa: Licha ya kwamba sina mtazamo mzuri kuhusiana na mazungumzo na Marekani, lakini pamoja na hayo, mazungumzo haya kuhusiana na suala hili moja maalumu, nimeyaunga mkono kwa nguvu zangu zote, na ninaendelea kuyaunga mkono.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Mimi ninayaunga mkono mia fil mia mazungumzo ambayo yatadhamini heshima ya taifa la Iran, na kama atatokezea mtu na kusema kuwa ninapinga kufikiwa makubaliano, mtu huyo atakuwa anasema jambo ambalo ni kinyume na ukweli wa mambo.
Ayatullah Udhma Khamenei ameendelea kusisitiza kuwa anaunga mkono kikamilifu makubaliano ambayo yatadhamini manufaa ya taifa na ya nchi na hapo hapo lakini amesema: Tab'an nimesema pia kwamba "kutoafikiana ni bora kuliko maafikiano mabaya" kwani kutokubali maafikiano ambayo yanataka kukanyaga manufaa ya taifa la Iran na kuangamiza heshima ya taifa ni fakhari kuliko kuwa na maafikiano ambayo yatalidunisha taifa letu.
Baada ya hapo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amejibu kwa uwazi utata ulioenea hivi sasa akisema: Baadhi ya wakati utasikia kuna watu wanasema kuwa, Kiongozi Muadhamu anafuatilia kwa karibu vipengee vyote vya mazungumzo hayo, wakati ambapo maneno hayo si makini hata kidogo.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Si kwamba mimi sifuatilii kabisa mazungumzo hayo, lakini hadi hivi sasa sijawahi kuingilia vipengee vya ndani vya mazungumzo hayo na katika siku za usoni pia sitoingilia vipengee vidogo vidogo vya mazungumzo hayo.
Ameongeza kuwa: Mimi kimsingi nimemueleza mheshimiwa Rais na katika baadhi ya matukio machache nimemueleza pia Waziri wa Mambo ya Nje kuhusu masuala makuu, mistari mikuu, kalibu na mfremu pamoja na mistari myekundu inayopaswa kuchungwa kwenye mazungumzo hayo, lakini vipengee vidogo vidogo na masuala ya ndani kabisa ya mazungumzo hayo nimewaachiwa wao.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Mimi nina imani na watu wetu wanaoendesha mazungumzo hayo, na hadi leo hii sijawa na shaka nao na Inshaallah katika siku za usoni pia iwe vivyo hivyo, lakini pia niseme kuwa nina daghadagha na wasiwasi mkubwa kuhusiana na mazungumzo ya nyuklia.
Ayatullah Udhma Khamenei amegusia pia kuwa, upande wa pili katika mazungumzo hayo ni upande watu wenye hila nyingi, wasema uongo, wanaovunja ahadi na wasiofuata mkondo sahihi na kusema kuwa, hilo ndilo linalomtia wasiwasi mkubwa. Ameongeza kuwa: Mfano mmoja wa miamala hiyo ya upande wa pili wa mazungumzo ya hivi karibuni ni pale tulipoona baada ya kupita karibu masaa mawili tu tangu kumalizika mazungumzo hayo, White House (Ikulu ya Marekani) ilitoa tamko la kurasa kadhaa kuhusiana na mazungumzo hayo na sehemu kubwa ya mambo yaliyokuwemo kwenye tamko hilo yalikuwa ni kinyume na uhalisia wa mambo.
Aidha amesema: Kuandika tamko lenye kurasa zote hizo ni jambo lisilowezekana kufanywa katika kipindi cha masaa mawili, hivyo inaonesha kuwa wakati Wamarekani walipokuwa katika mazungumzo na sisi wakati huo huo walikuwa wanaandaa tamko bandia, lisilo sahihi na linalokwenda kinyume kabisa na yale yanayojadiliwa kwenye mazungumzo hayo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza tena kuwa, upande unaofanywa mazungumzo na Iran ni wa watu wenye ahadi mbaya na wadanganyifu na kuongeza kuwa: Mfano mwingine ni kwamba baada ya kumalizika kila duru ya mazungumzo, huwa wanatoa matamshi ya hadharani mbele ya watu, lakini utawaona baadaye wanatoa matamshi ya faragha, na wanafanya hivyo ili kulinda heshima ndani ya nchi zao na kukabiliana na wapinzani wao suala hilo halituhusu kivyovyote vile sisi tunaofanya nao mazungumzo.
Ayatullah Udhma Khamenei emefafanua zaidi suala hilo kwa kusema kwamba, wanapokuwa hadharani wanasema jambo fulani na wanapokuwa faraghani wanasema jambo jengine ili kulinda heshima zao na utawasikia wanasema Kiongozi wa Iran naye anapinga mazungumzo haya wakati hayo siyo maneno yao hasa, bali wanayatoa huko kwao ili kulinda heshima zao tu ndani ya nchi hizo wakati ambapo hata hawajui nini kinaendelea ndani ya Iran.
Amesisitiza kuwa: Matamshi yangu na wananchi wetu ninayatoa kwa msingi wa kuaminiana na kama ambavyo wananchi wameniamini mimi mja dhaifu wa Mungu, mimi pia ninawaamini kikamilifu wananchi na ninaamini kwamba Inshaallah msaada wa Mwenyezi Mungu utakuwa pamoja na watu hawa milele.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia amesema: Kushiriki kwa wingi mno wananchi wa Iran katika maadhibisho ya "rasilimali" ya Bahman 22 (Februari 11, siku zinapofikia kileleni sherehe za Mapinduzi ya Kiislamu ya nchini Iran), na pia katika joto kali la mwezi mtukufu wa Ramadhani ili kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Quds (Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani) zote hizo ni dalili za kuweko msaada wa Mwenyezi Mungu na ni kwa msingi huo ndio maana nina imani kamili na wananchi wetu na matamshi ninayotoa kwa wananchi nayo ninayatoa kwa kuhisi ukweli, uaminifu na muono wa mbali wa wananchi.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza pia kuwa: Mimi nina daghadagha na wasiwasi na miamala ya upande wa pili wa mazungumzo. Baadaye amesema: Haipasi kutia chumvi au kufanya pupa katika kupinga na kuunga mkono mazungumzo hayo, bali inabidi watu wasubiri na kuona nini kitatokea.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia amewasisitizia viongozi nchini Iran kwamba wanapaswa kuwaeleza wananchi na hususan watu wenye vipawa nchini namna mazungumzo hayo yanavyoendelea na kuwapasha habari za kila kinachoendelea kwenye mazungumzo hayo kwani hakuna kitu chochote cha siri katika mazungumzo hayo.
Ayatullah Udhma Khamenei amelitaja suala la kuwaeleza wananchi na hasa watu wenye vipawa nchini mambo yote yanayohusiana na mazungumzo ya nyuklia kuwa ni dhihirisho la wazi la kuweko mapenzi baina ya viongozi na wananchi na kusisitiza kuwa: Kupendana si kitu cha "kidesturi" (si kitu cha kununua au cha kupigia mahesabu kwa kuzingatia maslahi fulani kwamba nikitoa moja nitapata faida ya mbili kwa mfano) bali ni kitu ambacho inabidi kiandaliwe, kiletwe, kijengwe na kiendelezwe ambapo hali iliyopo hivi sasa nchini ni fursa nzuri kwa ajili ya kudumisha mapenzi baina ya viongozi na wananchi.
Akiendelea na hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa pendekezo kwa viongozi nchini akisema: Viongozi wa nchi yetu ambao ni watu wakweli na wenye uchungu na manufaa ya taifa, wanapaswa kuwaita wakosoaji wakuu wa mazungumzo hayo na kuzungumza nao, na kama katika matamshi yao kutakuwa na nukta za kuzingatiwa, wazizingatie na kuzitumia katika mazungumzo hayo na kama hakutakuwa na nukta hizo, wawakinaishe wakosoaji hao. Aidha amesisitiza kuwa, hilo ndilo dhihirisho la kweli la kupendana na kuzifanya nyoyo na matendo kuwa kitu kimoja.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Inawezekana viongozi wakasema kuwa, muda wa miezi mitatu wa hadi kufikia makubaliano ya mwisho ni mdogo kiasi kwamba hauruhusu kukaa na kuzungumza na wakosoaji. Lakini inabidi kujibu mtazamo huo kwa kusema, fursa hii ya miezi mitatu si suala ambalo haliwezi kubadilika, na hakuna tatizo lolote kuongezewa muda miezi hiyo kama ambavyo huko nyuma pia upande wa pili wa mazungumzo, uliyaongezea muda wa miezi saba mazungumzo hayo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa mara nyingine alisisitiza kuwa, mazungumzo na Marekani yanahusiana na maudhui ya nyuklia tu na hayahusiani na kitu chochote na kuongeza kuwa: Tab'an kufanya mazungumzo haya kuhusu kadhia ya nyuklia ni uzoefu mzuri. Kama upande wa pili utaachana na tabia yake ya kupindisha mambo, uzoefu huu unaweza kushuhudiwa pia katika masuala mengine, lakini kama upande huo wa pili utaendelea na upindishaji wake wa mambo, uzoefu wetu wa huko nyuma wa kutoiamini Marekani utapata nguvu kubwa zaidi.
Vile vile Ayatullah Udhma Khamenei ameelezea kusikitishwa kwake na baadhi ya misimamo ya upande pili ambao unajifanya kuwa ni jamii ya kimataifa na kuongeza kuwa: Upande unaolikabili taifa la Iran ambao ni upande wa watu wenye ahadi mbaya yaani Marekani na nchi tatu za Ulaya, hauwezi kuwa jamii ya kimataifa. Jamii ya kimataifa ni mjumuiko wa nchi 150 ambapo viongozi na wawakilishi wa nchi zinazounda jamii hiyo ya kimataifa, miaka michache nyuma walikutaka mjini Tehran katika kikao cha Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM). Hivyo kudai kuwa upande unaokabiliana na taifa la Iran ni jamii ya kimataifa, kwa kweli ni madai yasiyo na msingi wowote.
Baada ya hapo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia masuala ambayo amezungumza na viongozi wa Iran katika vikao vya faragha kuhusiana na kadhia ya nyuklia na kuongeza kwa kusema: Mimi ninawasisitizia viongozi nchini kuyahesabu mafanikio yaliyopatikana hadi hivi sasa kuwa ni muhimu sana, na wasiyaone ni madogo au kuyapunguzia umuhimu wake.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kuwa, utaalamu na teknolojia ya nyuklia ni jambo la dharura kwa Iran na kuongeza kuwa: Matamshi ya watu wanaojifanya wana mtazamo huru na wa mbali wanajaribu kutia shaka kwa kudadisi hivi teknolojia ya nyuklia ina faida gani, ni matamshi ya hila yaliyojaa udaganyifu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha ameashiria namna Iran inavyohitajia sana teknolojia ya nyuklia katika masuala yake ya nishati, kuzalisha dawa za mionzi, kugeuza maji ya bahari kuwa maji safi ya kunywa na kutumia teknolojia hiyo katika masuala ya kilimo na kuongeza kuwa: Sifa muhimu zaidi ya teknolojia ya nyuklia nchini ambayo inalifanya suala la kuwa na teknolojia hiyo kuwa muhimu mno, ni kule kuona kuwa, teknolojia hiyo imepelekea kufumuka kwa wingi vipaji vya dhati vya vijana wa Kiirani, na kwamba mwenendo huu wa maendeleo na ustawi katika teknolojia ya nyuklia, lazima uendelezwe.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia pia madai ya baadhi ya nchi za watenda jinai kama vile Marekani ambayo imewahi hata kutumia bomu la nyuklia kufanya mauaji ya umati pamoja na Ufaransa ambayo imefanya majaribio hatari sana ya silaha za nyuklia na kusema: Nchi hizo zinatutuhumu sisi kuwa tunafanya juhudi za kuwa na bomu la nyuklia wakati ambapo mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kutegemea msingi wa fatwa na kidini na pia kwa kutegemea msingi wa kimantiki, kamwe haijawahi kufanya juhudi za kumiliki silaha za nyuklia na katika siku za usoni pia haitofanya hivyo, kwani inazihesabu silaha hizo kuwa hazina jambo jengine ghairi ya mashaka na matatizo.
Ayatullah Udhma Khamenei aidha ametoa tahadhari nyingine kwa viongozi nchini Iran akiwataka wasiuamini upande wa pili wa mazungumzo na kuongeza kuwa: Hivi karibuni, mmoja wa viongozi wetu nchini alisema wazi kuwa sisi hatuna imani na upande wa pili wa mazungumzo; kuwa na misimamo kama hiyo, ni jambo zuri.
Vile vile amesisitizia wajibu wa kutohadaiwa na vicheko na tabasamu za upande wa pili wa mazungumzo wala kuamini ahadi za upande huo na kuongeza kuwa: Mfano wa wazi wa suala hilo, ni misimamo na matamshi yaliyotolewa na Rais wa Marekani baada ya kutolewa tamko la hivi karibuni.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, miongoni mwa mambo aliyowataka viongozi nchini wahakikishe kuwa yanatekelezwa ni kuondolewa vikwazo vyote kwa mkupuo mmoja mara baada ya kuanza utekelezaji wa makubaliano yoyote yanayotarajiwa kufikiwa na kuongeza kuwa: Suala hili ni muhimu sana na inabidi vikwazo vyote viondolewe kikamilifu siku ile ile ya makubaliano.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Kama suala la kuondolewa vikwazo litatumbukizwa kwenye mchakato mwingine mpya, wakati huo mazungumzo hayo hayatakuwa na maana yoyote, kwani lengo la mazungumzo hayo ni kuondolewa vikwazo vyote mara moja.
Ayatullah Udhma Khamenei ameendelea na hotuba yake kwa kusisitiza kwamba: Kwa hali yoyote ile haipasi kuruhusu watu baki kuingia kwenye mipaka ya masuala ya usalama na ya kiulinzi ya nchi kwa kisingizio chochote kile kama vile madai ya kusimamia miradi ya nyuklia ya Iran, na viongozi wa masuala ya ulinzi nchini wasiruhusu kivyovyote vile madola ya kibeberu kuingia kwenye mipaka hiyo kwa madai ya kusimamia na kuchunguza miradi ya nyuklia au kuzuia ustawi na maendeleo ya kijeshi ya Iran.
Ameongeza kuwa: Ni jambo la lazima kuhakikisha kuwa, uwezo wa kijeshi wa Iran unaendelea kuwa ngome madhubuti ya taifa katika upande wa kijeshi na inabidi uwezo huo uimarishwe zaidi na zaidi na siku baada ya siku. Vile vile mazungumzo hayo kwa namna yoyote ile hayapaswi kutia doa katika uungaji mkono wetu kwa ndugu zetu wana muqawama katika kona mbali mbali za dunia.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuhusu namna ya kutekeleza usimamiaji wa miradi ya nyuklia kwa kusema: Mbinu yoyote ile ya usimamiaji isiyo ya kawaida ambayo watataka kuifanya nchini Iran tu na kutoihusisha na nchi nyinginezo haikubaliki, na kwamba usimamiaji huo unapaswa kufanyika katika maeneo husika tu. Pia sheria hiyoa ya kusimamia iwe ni sheria ya usimamiaji wa nyuklia kwa nchi zote za dunia na si zaidi ya hapo.
Tahadhari nyingine iliyotolewa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ilikuwa ni kuhusiana na udharura wa kuendelea na ustawi wa kiufundi katika miradi ya nyuklia ya Iran. Amesisitiza kwamba: Ustawi wa kielimu na kiufundi inabidi uendelee katika upeo wake mbalimbali. Tab'an yumkini timu ya mazungumzo ya nyuklia inapaswa kuelewa pia kuwa, inabidi ikubaliane na baadhi ya mipaka, na hakuna tatizo katika suala hilo, lakini kwa hali yoyote ile, maendeleo na ustawi wa kiufundi unapaswa kuendelea na kusonga mbele kwa nguvu kubwa zaidi.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza pia kwamba: Kudhaminiwa matakwa hayo ni jukumu la wafanya mazungumzo hayo na inabidi watumie mitazamo na fikra za wataalamu waaminifu na hata mitazamo ya wakosoaji ili kupata mbinu sahihi za kuendelea na mazungumzo hayo.
Baada ya hapo Ayatullah Udhma Khamenei amegusia katika sehemu nyingine ya hotuba yake, matukio na mabadiliko muhimu ya nchini Yemen na kusisitiza kuwa: Kitendo cha Wasaudia cha kuivamia Yemen ni kosa na tayari wamepanda mbegu ya bida'a katika eneo hili.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyataja mashambulio ya serikali ya Saudia huko nchini Yemen hivi sasa kuwa yanashabihiana na jinai za Wazayuni huko Ghaza, Palestina na baada ya hapo ameanza kuzungumzia pande mbili muhimu za suala hilo.
Ameitaja hatua ya kulivamia na kuanza kulishambulia taifa la Yemen kuwa ni jinai, ni mauji ya kimbari na ni suala ambalo watendaji wake wanapaswa kufuatiliwa kisheria kimataifa na kuongeza kuwa: Kuwaua watoto wadogo, kuharibu nyumba za watu, kuangamiza miundombinu na utajiri wa taifa fulani, ni jinai kubwa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Ni jambo lisilo na shaka hata chembe kuwa Wasaudia watapata hasara na madhara katika kitendo chao hicho na kamwezi hawatopata ushindi kwenye mashambulizi yao hayo.
Aidha Ayatullah Udhma Khamenei amesema kuhusu kushindwa Wasaudia katika mshambulizi yao huko Yemen kwamba: Dalili za kushindwa huko ziko wazi, kwani nguvu za kijeshi za Wazayuni ni kubwa zaidi ikilinganishwa na za Wasaudia, na eneo la Ghaza nalo ni eneo dogo tu ikilinganishwa na nchi kubwa na pana ya Yemen, lakini pamoja na hayo, Wazayuni wameshindwa kuidhibiti Ghaza, wakati ambapo Yemen ni nchi kubwa na pana, yenye makumi ya mamilioni ya watu (Vipi Wasaudia na uwezo huo walio nao wataweza kuidhibiti nchi kama hiyo?).
Vile vile Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kwamba: Ni jambo lisilo na shaka hata chembe kuwa Wasaudia watapa pigo kwenye mashambulizi yao hayo na "pua zao zitarambishwa mchanga" huko Yemen.
Aidha ameashiria historia ya Wasaudia katika masuala yanayohusiana na siasa za nje na kusema: Sisi tuna hitilafu za mitazamo katika masuala mbali mbali ya kisiasa na Wasaudia, lakini pamoja na hayo mara zote tulikuwa tukisema kuwa, Wasaudia ni makini na wanafanya mambo kwa hekima katika siasa zao za nje. Hata hivyo hivi sasa vijana wachache wasio na uzoefu wamehodhi masuala ya nchi hiyo na hivi sasa wanaufanya upande wa ukatili uuzidi nguvu upande wa umakini na ule wa kujidhihirisha kwa sura nzuri Saudia huko nyuma, na kwamba jambo hilo bila ya shaka yoyote ni kwa madhara ya nchi hiyo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewakhutubu viongozi wa serikali ya Saudi Arabia akiwaambia: Harakati yenu hii haikubaliki katika eneo hili na ninakutahadharisheni kuwa, mnapaswa kuacha mara moja kutenda jinai huko Yemen.
Baada ya hapo, Ayatullah Udhma Khamenei amegusia namna Marekani inavyoilinda na kuiunga mkono serikali ya Saudi Arabia na kuongeza kuwa: Hii ndiyo tabia ya Marekani, siku zote haiko pamoja na watu wanaodhulumiwa. Badala ya kuwaunga mkono watu wanaodhulumiwa, siku zote Marekani inamuunga mkono dhalimu. Lakini Wamarekani nao watapata pigo katika jambo hili na siasa zao zitafeli tu.
Vile vile ameashiria madai ya eti Iran kuingilia mgogoro wa Yemen na kusema: Ndege zao zinazotenda jinai zimeondoa usalama na amani kabisa katika anga ya Yemen na baadaye wanaeneza propaganda na kutoa madai ya kipumbavu ambayo Mwenyezi Mungu hakubaliano nayo, wala mataifa ya dunia na wala sheria za kimataifa. Wanafanya jinai zote hizo huko Yemen na hapo hapo wanadai kuwa huko si kuingilia mambo ya ndani ya nchi hiyo na badala yake wanaituhumu Iran kwa mambo yasiyo sahihi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, taifa la Yemen ni taifa lenye historia kongwe, na lina uwezo wa kutosha wa kujiainisha lenyewe utawala linaoutaka na kwa mara nyingine akasisitiza kuwa: Serikali ya Saudia inapaswa kuachana mara moja na jinai zake zinazosababisha maafa makubwa huko Yemen.
Ayatullah Udhma Khamenei pia amesema kuwa, hatua ya awali iliyokusudiwa na madola yanayolitakia mabaya taifa na wananchi wa Yemen ilikuwa ni kuifanya nchi hiyo isiwe na serikali yenye nguvu sawa sawa kabisa na walivyofanya huko Libya kwa kuitumbukiza nchi hiyo kwenye hali mbaya na ya kusikitisha mno. Aidha amesema: Kwa bahati nzuri hatua hiyo ya kwanza ya njama hiyo ya kiadui dhidi ya Yemen imefeli, kwani vijana wenye imani thabiti, wenye uchungu na nchi yao na walioshikamana vilivyo na njia ya Amirul Muminin (Imam Ali) Alayhis Salaam, iwe ni Waislamu wa Kishia au wa Kisunni, wa Kizaidi au wa Kihanafi, wote wamesimama kidete kupambana na njama hiyo na katika siku za usoni pia vijana hao watafelisha njama zote za maadui wa Yemen.
Mwanzoni mwa hotuba yake, Ayatullah Udhma Khamenei ametumia fursa hiyo kumkumbuka kwa wema, marhum Aahi, msoma kasida na mashairi ya Ahlul Bayt AS aliyekuwa ameshikamana vyema na mafundisho ya watukufu hao, aliyekuwa na msimamo usiotetereka, mpigania kheri na aliyefanya jitihada zisizochoka katika nyuga mbali mbali bila ya kuchoka na hapo hapo akawakumbusha wasoma kasida na mashairi ya Bwana Mtume SAW na Ahlul Bayt AS mambo kadhaa muhimu.
Kujua thamani ya kujitokeza kwa wingi mno vijana katika "majalis" za kuwakumbuka na kuwaenzi Ahlul Bayt Alayhimus Salaam na wajibu wa kueneza mafundisho ya kidini na mtindo wa maisha ya Kiislamu na kuwaelekeza walengwa kwenye kutekeleza ipasavyo majukumu yao ya kidini ilikuwa ni nukta ya kwanza kabisa iliyoashiriwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu akiwakumbusha wajibu wao wasoma kasida za Ahlul Bayt AS.
Kujiepushe na mambo yasiyo sahihi na yaliyopotoshwa na kutilia nguvu imani sahihi ndani ya nyoyo za vijana ni jukumu jingine ambalo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewakumbusha wasoma kasida za Ahlul Bayt AS.
 
< Nyuma   Mbele >

^