Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Makamanda wa Jeshi la Polisi la Jamhuri ya Kiislamu Waonana na Kiongozi Muadhamu Chapa
26/04/2015
 Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, leo asubuhi (Jumapili) ameonana na washiriki wa kongamano la makamanda, wakurugenzi na wakuu wa kiitikadi na kisiasa wa jeshi la polisi la Iran na kulitaja jeshi hilo kuwa ni dhihirisho la nguvu za kiutawala na kiusalama za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei amesisitiza kuwa, miongoni mwa majukumu makuu ya polisi ni kudhamini usalama wa watu binafsi, wa kijamii, wa kimaadili, wa kiroho na wa kisaikolojia katika jamii. Ameongeza kuwa, jeshi la polisi linapaswa kuwa chombo chenye nguvu ili liweze kulinda usalama lakini nguvu hizo zinapaswa kuchunga uadilifu, murua na huruma.
Mwanzoni mwa matamshi yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa mkono wa baraka kwa mnasaba wa kupata taufiki ya kuufikia mwezi wa Rajab na kusema kuwa, mwezi huu na mwezi ujao wa Shaaban ni fursa nzuri mno kwa ajili ya kujikurubisha kwenye matukufu ya Mwenyezi Mungu, kujijenga kiimani na kuwa utangulizi wa kuingia vizuri kwenye mwezi wa baraka wa Ramadhani. Amewataka watu wote kuitumia vizuri fursa na baraka za miezi hiyo kadiri inavyowezekana.
Ayatullah Udhma Khamenei amelitaja suala la kulinda amani kuwa ndilo jukumu kuu la jeshi la polisi na kwamba suala hilo linaonesha umuhimu mkubwa wa kujipanga vizuri jeshi hilo.
Ameongeza kuwa: Suala la kulinda usalama si suala la kipropaganda na la kusema kwa mdomo tu bali inabidi wananchi wahisi kuwa usalama wao unalindwa inavyotakiwa.
Vile vile amesisitiza kuwa, jukumu la jeshi la polisi ni kulinda usalama katika upeo wake tofauti iwe ni usalama katika safari za barabarani, usalama mijini pamoja na usalama katika mipaka na maeneo tofauti muhimu na kwamba jeshi hilo halipaswi kutosheka na kiwango fulani cha usalama, linapaswa kuhakikisha wakati wote usalama unaotakiwa upo. Amesema, kulinda usalama wa kisaikolojia katika jamii pia ni katika masuala na majukumu muhimu ya jeshi la polisi.
Ameongeza kuwa: Suala la kukabiliana na uhatarishaji wa usalama wa kisaikolojia katika jamii kama vile wasiwasi wa watu wa familia kwa vijana wao wanapotembea mitaani, au katika mabustani wasije wakatumbukia kwenye matumizi ya madawa ya kulevya au wasiwasi wa familia hizo wa kutumbukia vijana wao kwenye mambo ya ufuska na mambo mengine maovu, ni jambo lenye umuhimu mkubwa zaidi kuliko hata kupambana na vitendo vya kuvunja usalama kwa kutumia nguvu na kwamba ni lazima jeshi la polisi lilipe uzito wa hali ya juu sana suala la kupambana na hatari za namna hiyo.
Aidha amesema, vituko vinavyofanywa barabarani na baadhi ya vijana waliolewa ghururi za utajiri kwa kutumia magari ya kifakhari ni aina moja ya kuhatarisha usalama wa kisaikolojia katika jamii na kusisitiza kuwa: Jeshi la Polisi linapaswa kupambana na vitendo vya aina zote vya kuhatarisha amani.
Ayatullah Udhma Khamenei amelitaja suala la kulinda amani katika jamii kuwa ni suala linalothibitisha uimara na nguvu za jeshi hilo na kuongeza kuwa: Jeshi la Polisi ni dhihirisho la nguvu za kiusalama na kiutawala za Jamhuri ya Kiislamu hivyo ni lazima jeshi hilo liwe na nguvu za kutosha, lakini kuwa na nguvu huko hakuna maana ya kudhulumu watu au kufanya harakati isiyoweza kudhibitiwa.
Vile vile amesisitiza pia kuwa Iran haitaki kuwa na nguvu za jeshi la ki-Hollywood na za jamii za Magharibi na Marekani na kubainisha kwamba: Nguvu za aina hiyo si tu kwamba haziwezi kudhamini usalama, bali zenyewe ni aina moja ya mambo yanayohatarisha usalama.
Ameongeza kuwa: Polisi wa Marekani wanawafanyia dhulma kubwa na kuwanyanyasa vibaya watu weusi licha ya kwamba rais wa hivi sasa wa nchi hiyo ni mtu mweusi, na vitendo hivyo bila ya shaka yoyote ndivyo vinavyopelekea kuzuka machafuko nchini humo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia pia namna vilivyoongezeka vitendo vya polisi wa Marekani wanaowakandamiza watu weusi nchini humo na kusema kuwa, huo ni moja ya mifano ya nguvu za kidhulma za polisi.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza pia kuwa: Nguvu zinazotakiwa na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, ni kutotetereka katika utekelezaji wa majukumu lakini wakati huo huo kchunga uadilifu, muruwa na huruma kama ilivyo dhati ya Mwenyezi Mungu Mtukufu Ambaye sambamba na kuwa Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu, lakini wakati huo huo adhabu Yake ni kali sana.
Amesema kuwa, ni jambo la dharura na muhimu sana kuheshimiwa sheria katika pande zote mbili, katika kuamiliana na watu na ndani ya taasisi yenyewe ya jeshi la polisi na kuongeza kuwa: Kutokana na upana wa maingiliano ya jeshi la polisi na wananchi, usalama wa jeshi hilo ndani ya taasisi hiyo ni muhimu mno kiasi kwamba jeshi la polisi ambalo linatekeleza vizuri majukumu yake linaweza kuwa chimbuko la heshima ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu mbele ya wananchi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitizia pia ulazima wa kuimarishwa masuala ya kidini na kimaadili ndani ya jeshi la polisi na vile vile kujiimarisha jeshi hilo kielimu na ubunifu wa kielimu na kuongeza kuwa, viongozi na wakuu wa sehemu mbali mbali za jeshi hilo wanapaswa kuwa na ushirikiano wa kina baina yao ili kufanikisha suala hilo.
Katika sehemu nyingine ya miongozo yake, Ayatullah Udhma Khamenei amelishukuru jeshi la polisi la Iran kwa juhudi na kazi zake kubwa za kupigiwa mfano hususan wakati wa siku za Nairuzi (sikukuu ya mwaka mpya wa Kiirani wa Hijria Shamsia).
Kabla ya hotuba ya Amirijeshi Mkuu wa vikosi vyote vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Brigedia Jenerali Ashtari, Kamanda wa Jeshi la Polisi la Jamhuri ya Kiislamu ametoa ripoti fupi kuhusu kazi, mipango na ratiba za jeshi hilo na kusema: Kuongezeka kiwango cha kugundua uhalifu, kuendelea kupambana na watu wenye tamaa za kujinufaisha binafsi wanaofanya magendo ya madawa ya kulevya, kujiimarisha vilivyo jeshi hilo kwa ajili ya kulinda usalama mipakani, kupunguza kwa asilimia 7 hasara na maafa yanayotokana na ajali za barabarani, kupanuliwa mawasiliano baina ya jeshi la polisi na watu wenye vipawa nchini, harakati yenye kazi kubwa katika upande wa elimu na teknolojia, kulinda vilivyo matukufu ya Mapinduzi na ya Kiislamu ni miongoni mwa kazi muhimu zilizofanywa na jeshi la polisi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Kamanda wa jeshi la polisi la Iran amebainisha pia kuwa haiwezekani kupiga hatua kubwa bila ya kujipanga vizuri, kujiimarisha kwa imani ya kidini na kimapinduzi sambamba na kueneza fikra ya kujitolea ya kibasiji na kuendesha na kusimamia mambo kijihadi kama ambavyo jambo hilo haliwezekani pia bila ya kuwepo maelewano, mafahamiano na mapenzi baina ya jeshi la polisi na wananchi na taasisi nyingine zote nchini.
Ameongeza kuwa: Tutatumia uwezo wetu wote kwa nia safi na kwa ikhlasi kwa ajili ya kuhakikisha kuwa jeshi la polisi la Iran linazidi kukaribia kwenye jeshi lenye hadhi ya jeshi la Jamhuri ya Kiislamu.
 
< Nyuma   Mbele >

^