Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Aonana na Wafanyakazi wa Kona zote za Iran Chapa
29/04/2015
 Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, leo asubuhi (Jumatano) ameonana maelfu ya wafanyakazi wa kona mbali mbali za Iran na huku akibainisha majukumu ya viongozi, asasi na duru nyingine tofauti zinazoshughulikia masuala ya uzalishaji wa ndani, amesisitizia wajibu wa kupambana kikweli na kwa nguvu zote na ufisadi wa kiuchumi na magendo akisema: Ufunguo wa kutatulia matatizo ya kiuchumi ya wananchi na mashaka mengine katika jamii ya wafanyakazi hauko nje bali umo ndani ya nchi na umo ndani ya kuimarishwa na kustawishwa uzalishaji wa ndani.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha ametoa mkono wa baraka kwa mnasaba wa kukumbuka siku ya kuzaliwa Amirul Mumini Ali bin Abi Talib pamoja na Imam Jawad al Aimma Alayhimus Salaam na kusema kuwa, lengo la kukutana kwake na wafanyakazi ni kuwashukuru kwa kazi zao kubwa na muhimu mno na kuonyesha umuhimu wa kazi kwa viongozi na kwa jamii.
Ameongeza kuwa: Hatua ya Bwana Mtume Muhammad SAW ya kuubusu mkono wa mfanyakazi hakuifanya kwa kujionesha bali lilikuwa ni funzo kwetu sote.
Vile vile ameisifu jamii ya wafanyakazi nchini Iran kutokanana na ukakamavu wao, weledi wao wa mambo na uungwana wao katika kukabiliana na vishawishi vya kila siku vya ndani na nje ya nchi katika miongo mitatu iliyopita na kuongeza kuwa: Kwa haki na kwa insafu, jamii ya wafanyakazi nchini imepasi vizuri mtihani wa kutahamali mashaka na matatizo yote na katika kufanya kazi bila ya kuchoka kwa ajili ya kuiletea maendeleo nchi na kwamba viongozi nchini nao wanapaswa kujua thamani ya kujitolea na uungwana wa jamii hiyo na wafanye jitihada zao zote kwa ajili ya kutatua matatizo ya wafanyakazi nchini.
Ayatullah Udhma Khamene amegusia pia matatizo yaliyopo katika maeneo mbali mbali ya watu wanaofanya kazi za vibarua kama vile kufukuzwa kazi, kuishi bila ya kuwa na kazi za kufanya, kucheleweshewa mishahara na matatizo yao mengine mbali mbali katika maisha na kusisitiza kuwa: Matatizo hayo hayawezi kutatuliwa kwa maneno matupu, bali inabidi hatua za kweli zichukuliwe na ubunifu wa maana unahitajika kwa ajili ya kutatua matatizo hayo.
Amesema, kutia nguvu uzalishaji wa ndani kuwa ni uti wa mgogoro wa kutatua matatizo ya nchi na kufanikisha uchumi wa kimuqawama na kusimama kidete akiongeza kwamba: Kuna baadhi ya watu wanasema kuwa ni jambo lisilowezekana kupata ustawi wa uzalishaji wa ndani katika wakati wa vikwazo na mashinikizo, ni jambo lisilo na shaka kwamba vikwazo vya kidhulma dhidi ya Iran vimechangia kwa kiasi fulani kutokea matatizo hayo, lakini ni jambo lisilo na shaka hata chembe kwamba vikwazo na mashinikizo hayawezi kupambana na jitihada za umma zilizopangiliwa vizuri na kuwekewa utaratibu bora wa kutekelezwa kwa ajili ya kustawisha uzalishaji wa ndani ya nchi.
Ayatullah Udhma Khamenei ametoa ushahidi wa kushindwa vikwazo kuzuia jitihada za ndani ya nchi kwa kugusia maendeleo ya kustaajabisha ya Iran katika nyuga za viwanda vya kijeshi, bioteknolojia, ujenzi wa mabwawa, teknolojia ya Nano, sekta ya elimu za kimsingi, nyuklia na nyuga nyinginezo na kuongeza kuwa: Katika baadhi ya nyuga hizo, vikwazo na mashinikizo ni makubwa zaidi, lakini wameshindwa kuzuia jitihada na maendeleo ya nguvu ya ndani ya nchi kufikia maendeleo hayo.
Ameongeza kusema: Tab'an kama vikwazo visingelikuwepo kuna uwezekano tungelipata maendeleo makubwa zaidi katika baadhi ya nyuga hizo lakini upo pia uwezekano kwamba kama vikwazo visingelikuwepo tungelitegemea fedha za mafuta tu na tusingeliweza kupata maendeleo haya ya kustaajabisha tuliyo nayo hivi sasa.
Ayatullah Udhma Khamenei ameitaja kadhia ya kuzingatia na kulipa uzito wa hali ya juu suala la uzalishaji wa ndani kwamba mbali na kutatua matatizo ya kiuchumi, litapelekea kuzidi kupatikana heshima na kujitegemea kitaifa nchini na kuongeza kuwa: Kuimarisha muundo wa nguvu za ndani ikiwa ni pamoja na upande wa kiuchumi kutawaongezea nguvu wanaofanya mazungumzo na madola ya kigeni katika meza ya mazungumzo, vinginevyo, upande wa pili wa mazungumzo utaendelea daima kuweka masharti haya na yale na kuendelea kutoa matamshi chapwa yasiyo na mfungamano wowote na mazungumzo hayo.
Baada ya kubainisha udharura wa kuzingatiwa ustawi wa uzalishaji wa ndani ya nchi, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameanza kubainisha mambo ya lazima na ya dharura ya kuweza kufikia na kufanikisha malengo makuu ya taifa.
Amelitaja suala la maelewano na mafahamiano kati ya watu na duru zote zinazohusika katika suala la uzalishaji wa ndani kuwa ni jambo linaloandaa mazingira ya kuondolewa matatizo mazito na kufanyika kazi kubwa na kuongeza kuwa: Wawekezaji wa ndani ambao ni moja nguzo muhimu za kustawisha na kutia nguvu uzalishaji za ndani wanapaswa kuelekeza nguvu, suhula na uwekezaji kwenye upande huo.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Mwekezaji yeyote ambaye atatumia uwekezaji wake kwa ajili ya kuimarisha uzalishaji wa ndani na kutobabaishwa na faida kubwa za madalali na za nyuga zisizo za uzalishaji unaotakiwa, ajue kuwa yumo katika ibada wake wakati wote wa uwekezaji wake huo.
Vile vile amesema kuwa, kufanya kazi kwa umakini wa hali ya juu na kwa jitihada kubwa katika uzalishaji wa bidhaa za ndani kunaipa nguvu sehemu kubwa ya wafanyakazi na kuongeza kuwa: Watumiaji wa bidhaa hizo ambao wana insafu, nao wasizubaishwe na majina makubwa makubwa ya mashirika yanayozalisha bidhaa za nje wakaacha bidhaa zao za ndani, bali wafanye hima ya kutumia bidhaa za ndani kwa maslahi ya nchi yao.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia pia upana na wingi wa taasisi za kiserikali na kusema kuwa, serikali ndiye mtumiaji mkuu wa bidhaa na amemsisitizia Waziri wa Kazi akimwambia: Ishinikize serikali ihakikishe kuwa taasisi zote za serikali zinatumia tu bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi na kwamba ijue kuwa ni haramu kutumia bidhaa zozote za nje wakati zinapokuwepo bidhaa kama hizo zilizozalishwa ndani ya nchi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema pia kuhusu udharura wa taasisi za serikali kutumia bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi akisema: Serikali inapaswa kuzuia kupenda wepesi, na - Mungu apishie mbali - kutumiwa vibaya manunuzi ya bidhaa zinazohitajiwa na taasisi za Serikali.
Ayatullah Udhma Khamenei pia amelitaja suala la kupambana vilivyo na magendo kuwa ni jambo jengine muhimu katika kukuza na kutia nguvu uzalishaji wa ndani ya nchi.
Amesema: Tab'an suala la kuingia nchini baadhi ya bidhaa za kigeni liko mikononi mwa sekta binafsi, lakini pamoja na hayo, serikali inaweza kusimamia na kuongoza vizuri uingizaji wa bidhaa hizo na kuzuia kupata madhara sekta ya uzalishaji wa ndani.
Vile vile ameitaja kazi muhimu na kubwa ya vyombo vya habari katika kueneza tabia na utamaduni wa kutumia bidhaa za ndani na jukumu la Bunge katika kutunga sheria nzuri kuhusiana na uwekezaji kuwa ni mambo mengine muhimu ya kustawisha na kutia nguvu uzalishaji wa ndani ya nchi.
Ameongeza kuwa: Watu waliopewa majukumu ya kazi za kiutamaduni nao wanapaswa kufanya kazi zao vizuri kwa namna ambayo uweze kupata nguvu katika jamii; utamaduni wa kuchukia ugoigoi na uvivu na iweze kuthaminiwa tabia ya kupenda kufanya kazi nzito.
Sehemu nyingine muhimu iliyokuwemo kwenye hotuba ya leo ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu mbele ya wafanyakazi wa kona zote za Iran ni suala la kupambana na ufisadi wa kiuchumi.
Amekosoa mno watu wanaopenda kusemasema sana maneno lakini wakawa hawatekelezi kivitendo mambo wanayoyasema katika kukabiliana na ufisadi na kusisitiza kuwa: Kwa kusema tu "mwizi mwizi" mwizi hawezi kuacha kuiba inabidi azuiwe kuiba.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Viongozi nchini si magazeti ambayo kila siku na mara zote yanazungumzia suala la ufisadi, bali wanapaswa wachukue hatua za kivitendo za kupambana vilivyo na ufisadi na kwa maana halisi ya neno.
Baada ya hapo Ayatullah Udhma Khamenei ametoa muhtasari wa aina fulani wa miongozo yake hiyo kwa kusisitiza akisema: Ufunguo wa kutatua matatizo ya kiuchumi hauko Lausanne, wala Geneva na wala New York, bali umo ndani ya nchi na kwamba watu wote wanapaswa kutekeleza ipasavyo majukumu yao katika suala zima la kustawisha na kutia nguvu uzalishaji wa ndani ikiwa ndiyo njia pekee ya kutatua matatizo yaliyopo ya kiuchumi.
Aidha amegusia jitihada na kazi kubwa inayofanywa na serikali ikiwa na mapenzi makubwa kwa nchi na taifa na kuweko watu weledi wa mambo ndani ya Baraza la Mawaziri na kuongeza kuwa: Inshaallah kwa kufanya kazi na jitihada kubwa zaidi, suala la uzalishaji wa ndani nalo litatatuliwa kama ambavyo taifa na viongozi wa Iran wameweza kutatua matatizo makubwa zaidi ya hilo katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita.
Mwanzoni mwa mkutano huo, Bw. Rabei, Waziri wa Kazi, Ushirika na Ustawi wa Jamii wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sambamba na kutoa mkono wa baraka kwa mnasaba wa kukumbuka siku ya kuzaliwa Imam Jawad al Aimma na Amirul Muminin Imam Ali Alayhimus Salaam na sambamba na kuienzi Wiki ya Wafanyakazi nchini amesema: Viongozi wa jamii ya wafanyakazi nchini wanaelewa kuwa ni jukumu lao kufanya jitihada zao zote katika kustawisha na kuboresha maisha ya watu wenye shida na vile vile kulinda matunda ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Vile vile amelitaja suala la kutumia vizuri fursa ya kuwepo nguvu kazi kubwa na yenye thamani kama ambavyo amezungumzia pia namna jumuiya ndogo ndogo za uzalishaji zinavyoungwa mkono pamoja na taasisi za elimu za kimsingi kuelekea kwenye uchumi wa ndani ya nchi kikamilifu. Vile vile amebainisha ajenda kuu na misimamo ya Wizara ya Kazi, Ushirikia na Ustawi wa Kijamii katika masuala mbali mbali.
Bw. Rabei amelitaja suala la kupewa bima Wairani wote, kuongezwa bima ya watu wa vijijini na kufanywa nyongeza za mishahara ya wafanyakazi kuwa kubwa zaidi ikilinganishwa na kiwango cha mfumuko wa bei kuwa ni miongoni mwa kazi muhimu zilizofanywa na serikali ya kumi na moja ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Ameongeza kuwa, kutiliwa nguvu misingi ya uadilifu wa kijamii na kuondolewa madhara yanayoweza kuyakumba makundi mbali mbali ya kijamii nchini kuwa ndilo jukumu kuu la wizara yake.
 
< Nyuma   Mbele >

^