Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Aonana na Rais wa Iraq Chapa
13/05/2015
 Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, leo jioni (Jumatano) ameonana na Rais Fuad Ma'asum wa Iraq na ujumbe alioandamana nao na kuitaja Iraq kuwa ni nchi muhimu sana na yenye taathira kati ya nchi za Kiarabu na Kiislamu.
Vile vile amegusia hali ya kusikitisha mno iliyopo katika eneo la Mashariki ya Kati hivi sasa ikiwa ni pamoja na katika nchi za Yemen na Syria na kusisitiza kuwa: Kwa kuzingatia nafasi yake, bila ya shaka yoyote Iraq inaweza kuwa na taathira muhimu katika masuala ya Mashariki ya Kati na inabidi uwezo na nafasi hiyo itumiwe vilivyo kadiri inavyowezekana.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameutaja uhusiano wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Iraq kuwa ni wa kina sana na wa kiudugu na amekaribisha jitihada za kupanua zaidi na zaidi uhusiano wa nchi hizo mbili kadiri inavyowezekana.
Amesema: Uhusiano wa hivi sasa wa Iran na Iraq ni wa aina yake na ni wa kipekee kabisa ikilinganishwa na miaka ya huko nyuma na hili linaonesha kuwa, hekima na tadibiri za ndugu zetu wa Iraq inabidi ziendelee kuwepo.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza pia kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko tayari wakati wote kuipatia msaada wa aina yoyote ile Iraq kwa ajili ya maendeleo, ustawi na utulivu wa nchi hiyo na kuyataja matamshi ya Bw. Fuad Ma'asum kuhusiana na uhusiano wa Tehran na Baghdad na hali ilivyo hivi sasa nchini Iraq na katika eneo la Mashariki ya Kati kuwa ni matamshi mazuri, ya kina na yaliyozingatia pande zote.
Ameongeza kuwa: Kati ya nchi za Kiarabu na Kiislamu, Iraq ni moja ya nchi chache muhimu yenye sifa za kipekee.
Amesema, suala la kuundwa serikali iliyochaguliwa na wananchi na yenye utulivu nchini Iraq ni moja ya sifa za aina yake na za kipekee za Iraq kati ya nchi nyingine za Kiarabu na kusisitiza kuwa: Viongozi na makundi mbali mbali ya Iraq yanapaswa kulinda kwa nguvu zao zote sifa hiyo ya kipekee na yasiruhusu baadhi ya tofauti zinazojitokeza hapa na pale kuyatia doa mafanikio hayo ya kihistoria ya wananchi wa Iraq.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu vile vile amegusia namna serikali ya Iraq ilivyo na taathira katika ulimwengu wa Kiarabu na kuongeza kuwa: Leo hii eneo (la Mashariki ya Kati) na ulimwengu wa Kiislamu unashuhudia masuala ya kusikitisha kabisa na yanayoliza mno kama vile kadhia ya Palestina, masuala ya eneo la kaskazini mwa Afrika, vita katika nchi za Syria na Iraq na kwamba Iraq bila ya shaka yoyote inaweza kuwa na taathira chanya katika utatuzi wa masuala hayo.
Ayatullah Udhma Khamenei amezitaja njama za maadui wa Uislamu dhidi ya Syria kuwa ni za hatari mno na kusisitiza kwa kusema: Maadui wanataka kuleta ukosefu wa utulivu na ukosefu wa amani wa kudumu nchini Syria ili kwa njia hiyo waweze kulifanya eneo hili zima lisiwe na utulivu.
Vile vile amesisitiza kuwa, njama za baadhi ya nchi za Kiarabu dhidi ya Syria ni za kuiangamiza nchi hiyo na kuongeza kuwa: Njama za nchi hizo hazina madhara kwa Syria tu, bali madhara yake yataziangamiza pia nchi hizo zinazofanya njama dhidi ya taifa la Syria.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja suala la kurejesha na kulinda utulivu nchini Syria kuwa ndilo lengo muhimu zaidi na huku akiashiria matamshi ya Rais wa Iraq kuhusiana na vitendo vya kigaidi vya kundi la Daesh na taathira zake mbaya nchini Iraq na katika eneo zima la Mashariki ya Kati ameongeza kuwa: Kuweko makundi kadhaa ya kitakfiri na kigaidi nchini Syria yakiwa na majina tofauti kwa kweli ni kwa faida ya utawala wa Kizayuni na ni kwa manufaa ya watu ambao wanataka kupandikiza ukosefu wa amani na utulivu katika eneo hili zima.
Ayatullah Udhma Khamenei amezungumzia pia kadhia ya kusikitisha mno ya Yemen na kusisitiza kwamba: Wasaudia wamefanya kosa kubwa kuivamia na kuishambulia Yemen na bila ya shaka yoyote athari mbaya za jinai wanazofanya huko Yemen zitawarejea wenyewe.
Vile vile amesisitiza kuwa, inabidi mauji dhidi ya wananchi madhlumu wa Yemen yakomeshwe haraka iwezekanavyo na kuongeza kuwa: Masuala ya Yemen yanaonesha kuwa kuna fikra isiyo na hekima wala busara na ya kijahili ndani ya Saudia ambayo ndiyo inayochukua maamuzi kuhusiana na masuala ya Yemen.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, sababu zinazotolewa na Wasaudia za kujaribu kuhalalisha uvamizi wao nchini Yemen ni za kijinga na kuongeza kuwa: Wasaudia wameivamia na kuishambulia Yemen kwa madai ya kuombwa na rais aliyejiuzulu na kukimbia Yemen na ambaye amefanya usaliti mkubwa dhidi ya nchi hiyo tena katika mazingira magumu sana.
Ayatullah Udhma Khamenei amelitaja suala la kuchukua msimamo na kutoa mchango unaotakiwa Iraq katika masuala hayo kuwa ni jambo lenye umuhimu mkubwa na huku akiashiria kuwa ana matumaini makubwa kuhusu mustakbali mzuri wa Iraq, ameisifu na kuipongeza serikali ya nchi hiyo kutokana na kuwaingiza wananchi katika medani na kutumia nguvu ya wananchi pembeni mwa jeshi la nchi hiyo kwa ajili ya kukabiliana na changamoto nzito zinazoikabili nchi hiyo hususan katika mapambano dhidi ya kundi la kigaidi la Daesh.
Amesema, vijana wa Iraq kila mmoja kiasili ni shujaa anayeweza kuonesha na kuunda hamasa kubwa katika mazingira mwafaka na kwenye nyuga tofauti. Ameongeza kuwa: Sisi nchini Iran tumepata uzoefu mzuri wa jambo hilo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia amemuuliza Rais Fuad Ma'asum hali ya kiafya ya Bw. Jalal Talabani, Rais wa zamani wa Iraq na kumuomba Mwenyezi Mungu ampe afya na siha nzuri ya haraka.
Katika mazungumzo hayo yaliyohudhuriwa pia na Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Rais Fuad Ma'asum wa Iraq ameelezea furaha yake kubwa kwa kupata fursa ya kuonana na kuzungumza na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na amemwambia: Tunaamini kuwa, ukiwa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu na ukiwa marja'a mkubwa wa kidini, kwa sifa zote hizo mbili unaweza kutusaidia mno katika kustawisha kadiri inavyowezekana uhusiano wa Iran na Iraq na vile vile kutuonyesha njia za kuweza kutatua masuala mbali mbali ya Iraq.
Rais wa Iraq vile vile amesema kuwa taifa na nchi yake kamwe haitosahau misaada ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wakati wa shambulio la Daesh na katika wakati mgumu uliolikumba taifa hilo na kuongeza kuwa: Daesh ya nchini Iraq na Daesh ya nchini Syria hazina tofauti yoyote kwani kundi hilo ni hatari kwa eneo hili zima.
Rais Fuad Ma'asum wa Iraq pia amesema kuwa mazungumzo yake na Rais Hassan Rouhani yalikuwa mazuri na kuelezea matumaini yake kuwa mazungumzo hayo yatafungua uwanja wa kupanuliwa zaidi na zaidi ushirikiano wa nchi hizi mbili ndugu.
 
< Nyuma   Mbele >

^