Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Hotuba ya Kiongozi Muadhamu Mbele ya Kamati ya Kongamano la Kuwaenzi Peshmerga Waislamu Wakurdi Chapa
11/05/2015
Ifuatayo hapa chini ni hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu wakati Alipoonana na Kamati ya Kongamano la Kuwaenzi Mashahidi wa Peshmerga wa Waislamu wa Kikurdi kwa ajili ya kongamano hilo lililoanza tarehe 11/05/2015 mjini Sanandaj, katika mkoa wa Kurdistan wa Iran.
 
Bismillahir Rahmanir Rahim.
Ninakushukuruni sana ndugu zangu azizi ambao mnafanya hima ya kuhuisha na kubakisha hai jina la wanamapambano wa Peshmerga wa Waislamu wa Kikurdi na ambao hawakuruhusu wanamapambano hao waliojitolea muhanga maisha yao katika njia ya haki wasahaulike; ninawashukuru kwa jitihada zao hizo na vile vile ninawashukuru Bwana Husseini, Kamanda [Rajabi] na Bw. Mulla Qadir, rafiki yangu wa muda mrefu kutokana na hotuba zao na yale mazuri yaliyokuwemo kwenye hotuba hizo. Inshaallah Mwenyezi Mungu akupeni nyote taufiki na msaada Wake.
Naam, kama mlivyoashiria, ndugu zetu mashujaa na wenye ikhlasi katika eneo la Kurdistan si wachache tangu zamani na katika sehemu zote za Wakurdi. Na muda wote huu wamekuwepo ndugu zetu waumini na wenye ikhlasi huko Kurdistan ambao kwa hakika Mapinduzi (ya Kiislamu) yanaona fakhari kuwa na shakhsia kama hao. Miongoni mwa vito adhimu vya shakhsia ni kuwa na vijana hao ambao walikusanyika pamoja kwenye majimui za Peshmerga ya Waislamu wa Kikurdi, wakabeba silaha na wakaelekea kwenye medani ya mapambano na wakakubali kuziingiza hatarini nafsi zao na familia zao. Hii kwa hakika ni nukta muhimu sana. Ijapokuwa katika maeneo ya Isfahan, Tehran, Yazd na Masha-had walitoka watoto wa kila familia na kwenda kwenye medani ya mapambano na kuuawa shahidi kwenye medani hiyo, na kwa hakika hilo linamfanya mtu awashukuru sana mashahidi hao na familia zao, lakini vijana hao walifanya hivyo huku kukiwa hakuna mtu aliyethubutu au aslan aliyefikiria kuwatisha vijana hao. Amma kwa upande wa Kurdistan lakini, hali ilikuwa vingine kabisa. Katika eneo la Kurdistan wakati baadhi ya familia zilipojitolea vijana wao kwenda kwenye medani ya mapambano kupambana na kuuawa shahidi, kulikuwa na watu ambao ni maadui wa Mapinduzi ya Kiislamu walikuwa wakitoa vitisho kwa vijana na familia hizo. Lakini pamoja na hayo, tuliona vijana hao wa Kikurdi wakijitolea kujiunga na majimui ya Peshmerga ya Waislamu wa Kikurdi kwa ushujaa mkubwa sana na kuingia kwenye medani ya mapambano - ambapo mimi naikumbuka vizuri na kikamilifu hali ya wakati huo na ninawajua vijana hao na nilikuwa nikienda mara kwa mara kwenye eneo hilo, nilikuwa nikiwaona vijana hao walivyokuwa katika harakati zao - naam, walikubali kuzitia hatarini roho zao na pia kuutia hatarini utulifu wa familia zao, waliingia kwenye medani ya mapambano wakijua vyema hatari zote hizo, mambo haya kwa hakika ni muhimu sana kuenziwa. Vijana hao walipasi vizuri mtihani wao. Kwa haki na kwa insafu, walipasi vizuri mno mtihani huo.
Tangu siku ya kwanza kabisa, adui aliwekeza na kuelekeza nguvu zake kwenye eneo la Wakurdi. Alielekeza nguvu zake kwa sababu mbili: Moja ni kutokana na muundo wa kikaumu na kikabila wa eneo hilo na mwingine ni kwa ajili ya madhehebu. Maadui walikuwa na matumaini kwamba wangeliweza kujipenyeza kwenye eneo hilo. Walitaka kujipenyeza vivyo hivyo huko Baluchistan na pia katika eneo la Turkmen Sahra na pia katika eneo la Kurdistan. Tumeweza kupata nyaraka na ushahidi mwingi unaohusiana na eneo la Kurdistan na ambao ulikuwa umefichwa kwenye maeneo ya siri ya kiusalama ya utawala wa taghuti. Kwa nyaraka hizo tunajua vyema siasa zao zilikuwa ni zipi na ni njama gani walikuwa wakizifanya.Walikusudia kutumia siasa hizo pia baada ya ushindi wa Mapinduzi (ya Kiislamu) na kuligeuza eneo la Kurdistan kuwa nukta ya kuweza kujipenyeza na kuleta madhara kwa Mapinduzi ya Kiislamu; hilo ndilo lililokuwa lengo lao. Walikuwa wakitoa kaulimbiu mbali mbali; baadhi yao wakitoa kaulimbiu za misimamo ya kushoto na wengine wakitoa kaulimbiu za Kiislamu. Katika eneo hilo la Kurdistan walikuweko watu waliokuwa wakipinga Mapinduzi na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ambao walikuwa wanasoma pia Qur'ani - na tab'an sote tunakumbuka; watu waliokuwa wanafuatilia mambo hayo wanakumbuka vizuri jambo hilo - lakini pamoja na kwamba walikuwa wanasoma Qur'ani, lengo lao lilikuwa ni kuyapiga vita Mapinduzi (ya Kiislamu) kwa manufaa ya Marekani na utawala wa Kizayuni; na walitumia nguvu zao zote kujaribu kufanikisha njama zao na kulifanya eneo la Kurdistan likose amani, lakini wameshindwa, kwani eneo hilo limeendelea kuwa na amani hadi leo hii. Naam, vijana wetu walijitolea kwenda kwenye maeneo mbali mbali ya Kurdistan, lakini lau kama wananchi Wakurdi wasingelikuwa wanayapenda Mapinduzi ya Kiislamu, je, vijana wetu hao wangeliweza kufanya chochote? Ni wazi kwamba wasingeliweza kufanya lolote; na hata kama tungelituma askari mara kumi zaidi ya wale tuliowatuma Kurdistan lakini ikawa nyoyo za wananchi wa eneo hilo haziko pamoja na Mapinduzi ya Kiislamu, wasingeliweza kufanya lolote. Lakini wananchi Wakurdi na maulamaa wengi wa Kikurdi nyoyo zao zilikuwa pamoja na vijana hao kiasi kwamba baadhi ya maulamaa wa Kikurdi wameuliwa shahidi na maadui hao wa Mapinduzi ya Kiislamu ambapo mwanachuoni wa karibuni kabisa ni huyu aliyeuawa shahidi miaka michache iliyopita, marhum Sheikhul Islam huko Sanandaj. Mwanachuoni huyu mwenye ikhlasi na msafi wa maadili, naye ameuliwa shahidi na maadui wa Mapinduzi. Hivyo mafanikio yote yaliyopatikana katika eneo la Kurdistan yamechangiwa na ndugu zetu (wa Kikurdi).
Mimi nina kumbukumbu nyingi kuhusu suala hilo; na kuhusiana na eneo la Paveh na tayari amesema hapa Bwana Mulla Qadr kuhusiana na eneo hilo; ninakumbuka vyema siku ya kwanza nilipokwenda Paveh baada ya matukio mbali mbali yaliyotokea. Wakati huo hali ya hewa ilikuwa baridi, nikaenda kwenye eneo lile la juu (ya mji) na nikaonana na vijana waliokuwepo hapo, tukaenda pamoja msikitini. Kwa kweli wananchi wa eneo hilo na heshima zao kubwa walizo nazo katika nyumba zao, walipigania vilivyo mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na kuutumikia kwa nguvu zao zote. Hivyo kwa hakika ndivyo hali ilivyokuwa. Naam, Alhamdulillah jambo hili limesaidia kwani hadi leo hii hali ni hiyo hiyo katika maeneo hayo. Lililo muhimu ni kuwa, tutambue kwamba, adui hajakaa kimya; tusije tukadhani hata mara moja kuwa adui anaweza kutulia, hapana, adui ataendelea kutufanyia uadui kwa kadiri anavyoweza, na ataendelea kufanya njama na kuchukua hatua dhidi yatu; maadui wana fedha, njia zao za kiusalama na kiujasusi nazo ni nyingi na ni pana, vyombo vyao vya kupigia propaganda navyo ni vingi na vipana, na wanafanya njama dhidi yetu; hivyo tunapaswa kuwa macho, ni wajibu wetu kuwa macho. Kama nilivyosema, suala hili la Usuni na Ushia ni suala muhimu. Maadui wameelekeza nguvu zao kwenye suala la Ushia na Usuni; wanafanya njama za kupandikiza chuki na taasubu katika kila upande; yaani wanawasha moto wa taasubu upande wa Kishia na vile vile upande wa Kisuni. Kuna baadhi ya watu kutokana na mghafala wao daima wamekuwa wakitekwa na mambo hayo. Lakini mtu mwenye uchungu na mpenzi wa nchi yake anapaswa awe macho kikamilifu asije akawa mateka wa njama hizo. Kwa kweli hivyo ndivyo hali ilivyo. Yule mtu ambaye anajifanya ni mpenzi wa madhehebu ya Kisuni na kuonyesha uadui wake kwa kushambulia madhehebu ya Kishia, kwa kweli mtu huyo hana mfungamano wowote na madhehebu ya Kisuni na wala dini tuku ya Kiislamu. Hali ni hiyo hiyo kwa upande wa Kishia. Kuna watu wanachochee moto wa taasubu ndani ya madhehebu ya Kishia dhidi ya Masuni wakati ambapo watu hao hawana uchungu wowote na dini. Sasa watu hawa wanawatumia watu wa namna gani? Wanawatumia watu ambao hawana welewa wowote kuhusu pande mbali mbali za kadhia hiyo; watu ambao ingawa wana mapenzi na dini na madhehebu yao, lakini hawana busara, wala mazingatio na wala hekima inayotakiwa na wala akili ya kuwawezesha kufahamu lengo la adui. Maadui wanawachezea watu hao kutoka pande zote mbili; hivyo kila mmoja wetu anapaswa kuwa macho; tusiruhusu njama hizo kuzaa matunda. Mimi tangu zamani sana nimekuwa nikisema kwamba Waingereza ni maarufu mno katika suala hili, wanawashinda Wamarekani katika jambo hilo; Waingereza ndio maarufu zaidi kwa kueneza khitilafu baina ya Mashia na Masuni; naam wanajua wafanye nini ili kuzifanya pande hizo mbili za Waislamu zizozane. Baadhi ya wakati utawaona wanatamka maneno ambayo yanaonekana kana kwamba wanawapenda Waislamu wa Kisuni. Tumeona wenyewe namna Baraza la Congress la Marekani lilivyopitisha muswada wa eti kuwaunga mkono Waarabu Masuni nchini Iraq! Amma cha kujiuliza ni kwamba, hivi kweli Wamarekani wanawapenda Waislamu wa Kisuni? (Hapana!) Bali Wamarekani wanapinga kitu chochote kile chenye jina la Uislamu haijalishi kitu hicho ni cha Waislamu wa Kishia au wa Kisuni. Kuna wajibu wa kuizingatia vilivyo nukta hiyo. Hivyo ni muhimu sana watu kuwa macho na kadhia hii ya madhehebu. Kwa bahati nzuri «...» [Maadui] hawawezi kulitumia suala la Ukurdi kueneza hitilafu (nchini Iran); ingawa katika nchi nyingiezo wametumia vizuri suala la Ukurdi (kueneza fitna na migawanyiko) lakini hawawezi kutumai suala hilo nchini Iran, lakini pamoja na hayo (hawajakata tamaa) wanaendelea kufanya propaganda kubwa kwa ajili ya kutumia vibaya suala la ukabila kama ambavyo wanafanya propaganda kubwa sana kwa kutumia silaha ya kueneza hitilafu za kimadhehebu. Inabidi tuwapokonye maadui visingizio vyote wanavyoweza kuvitumia kueneza hitilafu na mifarakano baina yetu.
Kazi za kiutamaduni zilizozungumziwa hapa na Bwana Mulla Qadr ni jambo sahihi kikamilifu, naam, kazi za kiutamaduni ni jambo zuri sana. Hata hii harakati mnayoifanya kuhusiana na kuwaenzi Peshmerga Waislamu wa Kikurdi, yenyewe nayo ni kazi ya kiutamaduni; kama kazi hiyo itafanyika vizuri na kwa usafi na kwa kuzingatia pande zote, Inshaallah itazaa matunda mazuri. Hiyo ni kazi ya kiutamaduni yenye thamani kubwa na inabidi iendelee. Inabidi kufanyike pia kazi za kutoa huduma na za kushughulikia masuala ya kiuchumi. Kwa hakika hatupaswi kuruhusu vijana wetu wakose ajira kwa njia yeyote ile kwani kutokuwa na kazi ni chimbuko la ufisadi na masuala yanayohusiana na vijana ni masuala ya daraja la kwanza kabisa. Ni matumaini yetu Inshaallah Mwenyezi Mungu Mtukufu atakupeni nyote taufiki ili muweze kuzifanya na kuzimaliza kazi hizi mlizozianzisha kwa ufanisi na kwa ubora wa hali ya juu.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Kongamano hilo lilifunguliwa tarehe 11/05/2015 mjini Sanandaj, katika mkoa wa Kurdistan wa Iran. Kabla ya hotuba hiyo ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Hujjatul Islam Walmuslimin Sayyid Muhammad Hussein Shahroudi, (mwakilishi wa Fakihi Mtawala - Walii Faqiih - mkoani Kurdistan), Brigedia Jenerali 2 Mohammad Hussein Rajabi (Kamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH ambaye pia ni katibu wa kongamano hilo) na Mamosta Mulla Qadir Qaderi (Imam wa Ijumaa wa mji wa Paveh) wametoa hotuba fupi fupi mbele ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei.
 
< Nyuma   Mbele >

^