Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Aonana na Wabunge wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu Chapa
27/05/2015
 Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, leo asubuhi (Jumatano) ameonana na Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) na wabunge wa majlis hiyo na sambamba na kusisitizia ulazima wa kuendelea na kazi kwa nguvu zote katika mwaka mmoja uliobakia wa bunge la tisa (la Iran) na kutoruhusu mjadala wa uchaguzi kuathiri kazi za bunge hilo, amekutaja kufanya kazi kwa maelewano na ushirikiano mihimili yote mikuu ya dola (Bunge, Serikali na Mahakama) hususan katika suala la kufanikisha uchumi wa kusimama kidete na kulipa umuhimu mkubwa suala hilo la uchumi wa kusimama kidete hususan katika kuchunguza na kujadili sheria ya Mpango wa Sita wa Maendeleo na bajeti ya ya mwaka 1395 (mwaka wa Kiirani wa Hijria Shamsia) na kutilia nguvu misimamo na misingi mikuu ya Jamhuri ya Kiislamu na Mapinduzi ya Kiislamu kuwa ni katika majukumu muhimu zaidi ya wabunge wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu na kusisitiza kwamba, ufunguo wa kutatulia matatizo ya kiuchumi nchini na pia suala la nyuklia ni kutegemea uwezo wa ndani na kuwa na imani na uchumi wa kusimama kidete. Hakuna kitu kukwama nchini. Njia ya utatuzi ni kutilia nguvu uzalishaji wa ndani na kuchunga kanuni na matumizi mazuri ya fedha.
Katika mkutano huo, Ayatullah Udhma Khamenei amezishukuru jitihada na kazi nzuri zilizofanywa na wabunge wa Bunge la Tisa na kuwausia watumie vizuri fursa iliyobakia ya mwaka mmoja wa bunge hilo akisisitiza kwa kuwaambia: Kuweni macho na msiruhusu muda huu uliobakia uathiriwe na masuala ya uchaguzi wa mwishoni mwa mwaka huu na msiruhusu maneno na matendo yenu yaathiriwe na uchaguzi huo, bali kigezo chenu pekee kiwe ni kupigania haki.
Nasaha za pili za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa wabunge ilikuwa ni kuupa uzito na mazingatio maalumu Mpango wa Sita wa maendeleo na kuwa macho wasije wakakumbwa na maradhi ya kupoteza hamu ya kufanya kazi katika mwaka wa mwisho wa bunge katika kujadili na kufanyia utafiti sheria za mpango huo.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema: Sheria ya Mpango wa Sita wa maendeleo ni muhimu kwani serikali zinazoingia madarakani nchini zina jukumu la kufuata mpango huo na maisha ya wananchi nayo yataathiriwa na sheria itakayotungwa kuhusiana na mpango huo.
Nasaha ya tatu ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiisamu imehusiana na suala la maelewano na kufanya kazi kwa pamoja kati ya Bunge na mihimili mingine mikuu wa dola na hususan Serikali na kuongeza kuwa: Serikali ina jukumu la kukutanisha na kuunganisha mihimili mitatu mikuu ya dola na taasisi nyinginezo nchini na kwamba pale jukumu la Serikali linapotekelezwa ipasavyo, matunda ya jambo hilo huathiri katika kazi za taasisi nyinginezo, hivyo kufanya kazi kwa malewano na Serikali ni jambo la dharura na hilo ndilo dhihirisho la kweli la kufanya kazi kwa pamoja na kwa maelewano.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametaja moja ya mambo ya lazima ya kufanya kazi kwa pamoja na kwa maelewano kwamba ni kwa kila upande kuwa na dhana nzuri na mwenzake na kuongeza kwamba: Maelewano hayawezi kupatikana kwa mtu kuwa na nia mbaya na mwenzako na kwa kutaka tu kukubali mambo yaishe huku ukiwa umebakiwa na kinyongo moyoni, na wala hayawezi kupatikana kwa kufanya usaliti na kwa kuitumia vibaya nia njema ya upande wa pili kama ambavyo kuwa na nia njema pia hakuna maana ya kukubali kila kitu na kukubali kudaganywa.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema pia kwamba, kuna tofauti baina ya kufanya muamala na kupiga tanji na kuongeza kuwa: Msingi wa wabunge na mawaziri katika miamala yao unapaswa uwe umesimama juu ya misingi ya kisheria na kulinda maslahi ya nchi na sio kukwamishana na kupigana tanji.
Aidha amelitaja suala la kuamiliana kwa heshima na adabu na mawaziri hususan katika kamisheni za bunge kuwa ni moja na mambo ya dharura ambayo wabunge wanapaswa kuyazingatia na kuongeza kuwa: Si wabunge tu ambao hawapaswi kuwaangalia mawaziri kwa jicho la dhararu na kejeli, bali serikali na mawaziri nao hawapaswi kuwaangalia wabunge kwa kiburi na kujiona bora; hivyo mambo yote yanapaswa yafanyike kwa kuheshimiana na kuchunga adabu na tabia njema.
Nasaha za tatu za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa wabunge wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ilikuwa ni kadhia ya uchumi wa kimuqawama na wa kusimama kidete.
Ayatullah Udhma Khamenei amegusia nukta moja muhimu sana kuhusu suala hilo akisema: Hivi sasa hapa nchini tuna maudhui ya uchumi wa kusimama kidete na maelewano, lakini inabidi tuwe na imani pia na uchumi huo wa kusimama kidete.
Vile vile amesisitiza kuwa, ufunguo wa kutatulia matatizo ya ndani ya nchi ni uchumi wa kusimama kidete na kutia nguvu uzalishaji wa bidhaa za ndani na ametumia fursa hiyo kuwashukuru wabunge kwa kupasisha sheria ya kuondoa vizuizi katika suala la uzalishaji wa bidhaa za ndani na kuongeza kuwa: Iwapo tutaimarisha na kutia nguvu uzalishaji wa bidhaa za ndani na kutumia vizuri uwezo wetu wa ndani, basi mbali na kutatua matatizo yaliyopo ndani ya nchi tutaweza pia kutatua kirahisi matatizo yenye mfungamano na nje ya nchi kama vile kadhia ya nyuklia.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Kuna njia nzuri za kutatua kadhia ya nyuklia na zote zinategemea namna tutakavyoweza kuutumia vizuri uwezo wetu wa ndani pamoja na kuimarisha na kutia nguvu uzalishaji wa bidhaa za ndani ya nchi.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Kuhusiana na masuala yaliyopo baina yetu na Marekani, Magharibi na Uzayuni, ukiweka pembeni kadhia ya nyuklia, tunaamini kwamba yako masuala mengine ya mtawalia kama vile haki za binadamu, lakini kama tutategemea nguvu na uwezo wetu wa ndani na kutatua matatizo yetu ya ndani kwa kutumia uwezo wetu huo, basi itakuwa rahisi pia kutatua masuala hayo ya nje yaliyopo baina yetu na Marekani, Magharibi na Uzayuni.
Vile vile amewaelekea wabunge wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu akiwaambia: Ni kwa sababu hiyo ndio maana inabidi kujadili na kufanyia utafiti sheria ya Mpango wa Sita wa Maendeleo na bajeti ya mwaka ujao kwa kulipa mazingatio ya kipekee suala la uchumi wa kusimama kidete ili mianya na mapungufu yaliyopo yaweze kuondolewa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Ndugu zetu serikalini wanasema mara kwa mara kuwa wanakumbwa na mapungufu mbali mbali katika jitihada za kuimarisha na kutia nguvu sekta ya uzalishaji wa ndani. Mimi pia najua kwamba mapungufu hayo yapo na vikwazo vimeathiri katika kuwepo mapungufu hayo lakini hebu tujiulize swali moja, je, katika hali kama hii, si wajibu wetu kutafuta suluhisho la jambo hilo?
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza tena kwamba, njia ya kutatua matatizo yaliyopo ipo na kusisitiza kuwa: Kuweko uchache wa vyanzo na vitendea kazi hakuna maana ya kutowezekana kabisa kutatuliwa matatizo yaliyopo na kwamba utatuzi wa jambo hilo ni kuainisha vipaumbele kwa ajili ya kutumia vyanzo na vitendea kazi vya ndani na kuchunga vilivyo sheria na matumizi mazuri ya fedha.
Amesema: Katika hali kama hii, utaona kuwa fedha zinatumika katika maeneo ambayo hazipaswi kutumika, hivyo Serikali, Bunge na Mahakama pamoja na vikosi vya ulinzi, vinapaswa kusimamia vizuri mambo hayo na kuchunga sheria za kifedha na matumizi yake sahihi ili vyanzo na vitendea kazi viweze kugawanywa kwa njia sahihi na kupewa kipaumbele maeneo ambayo yanapaswa kupewa kipaumbele.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia baadhi ya taasisi na hasa katika upande wa taasisi za vikosi vya ulinzi ambavyo vimeweza kufanya kazi kubwa sana bila ya kuweko nyongeza yoyote katika bajeti za taasisi hizo na kuongeza kuwa: Mifano hiyo inaonesha kwamba, inawezekana kutatua matatizo yaliyopo hata wakati panapotokezea mapungufu ya vyanzo vya kutendea kazi.
Nasaha nyingine zilizotolewa na Ayatullah Udhma Khamenei kwa wabunge ni kutilia mkazo misimamo mikuu ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu. Ameashiria misimamo thabiti na inayokubalika na baadhi yake iliyosonga mbele kikamilifu iliyochukuliwa hadi hivi sasa na Majlisi ya Tisa ya Ushauri ya Kiislamu katika masuala ya kimsingi na makuu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na ya Mapinduzi ya Kiislamu na kusisitiza kwamba: Muundo wa Bunge siku zote unapaswa usimame juu ya msingi wa kuimarisha na kutia nguvu misimamo mikuu na ya asili ya mfumo (wa Jamhuri ya Kiislamu) na kwamba kielelezo na marejeo ya jambo hilo ni miongozo ya Imam wetu mtukufu (Imam Khomeini) Rahmatullahi Alayhi iliyomo kwenye wasia wake.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Iwapo Bunge wakati wote litatilia mkazo misimamo mikuu na ya kimsingi ya Jamhuri ya Kiislamu, basi haitakuwepo tena hatari ya kutumbukia kwenye mtego hatari wa mfumo wa kibepari na kibeberu, lakini iwapo - na Mungu apishie mbali - kusimama kidete huko kutaondoka, basi tutakumbwa na hatari nyingi.
Ayatullah Udhma Khamenei ameendelea na hotuba yake kwa kugusia kadhia ya nyuklia akisema: Misimamo yetu kuhusu masuala ya nyuklia ni ile ile ambayo tumeitangaza hadharani kwa wananchi, masuala hayo pia tumeyabainisha pia kwa uwazi na kwa maandishi na kuwakabidhi viongozi na maafisa wanaoshughulikia masuala hayo. Tab'an yako baadhi ya mambo ambayo tumezungumza na viongozi nchini kwa njia ya faragha na kwenye vikao maalumu kwa ajili ya kutilia mkazo na kubainisha kwa uwazi zaidi misimamo hiyo ya kimsingi.
Amesisitiza kuwa, hivi sasa viongozi na maafisa wanaofanya mazungumzo ya nyuklia wanafanya jitihada kubwa za kulinda haki za taifa la Iran na kuongeza kuwa: Viongozi na maafisa wanaoshiriki kwenye mazungumzo hayo wanapaswa kutilia mkazo na kulinda kikamilifu misimamo ya Jamhuri ya Kiislamu na ni matumaini yetu wataweza kulinda na kudhamini maslahi ya nchi na ya mfumo (wa Jamhuri ya Kiislamu).
Mwanzoni mwa hotuba yake, Ayatullah Udhma Khamenei amegusia fursa nyingi zilizomo ndani ya miezi mitatu mitukufu ya Rajab, Shaaban na Ramadhani na kuwataka viongozi wote nchini wakiwemo wabunge waziimarishe nafsi zao kwa kuongeza jitihada za kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu na kusema kuwa: Inabidi kutumia vizuri dua zilizothibiti katika miezi hii mitukufu kwa ajili ya kuwa na ukuruba zaidi na Qur'ani na amali za sunna ili kwa njia hiyo tuweze kujikurubisha zaidi na zaidi kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Amesema kuwa, sisi sote lazima tujue kwamba tuna jukumu na mas'ulia mbele ya Mwenyezi Mungu katika matendo yetu yote kwenye kipindi chote cha utumishi wetu na tutakwenda kuulizwa kwa kila tulilolitenda na kusisitiza kwa mara nyingine kuwa, mwaka wa mwisho wa kutekeleza majukumu ni muhimu sana.
Ameongeza kuwa: Tunapaswa kufanya juhudi za kuhakikisha kwamba daima mambo yetu yote yanatendeka chini ya msingi wa kuchunga haki ya Mwenyezi Mungu, kusema kweli tunapozungumza na kuangalia mambo katika uhakika na uhalisia wake.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Bw. Ali Larijani, Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) ametoa ripoti fupi kuhusu kazi zilizofanywa na Bunge la Tisa katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita na kusema kuwa: Katika kipindi hicho, Bunge limepasisha sheria 120 ambapo sehemu kubwa ya sheria hizo zimelenga kwenye kukidhi mahitaji ya kiuchumi katika sekta ya uzalishaji wa bidhaa za ndani.
Spika w Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu amegusia suala la kupasishwa sheria za kuondoa vizuizi katika uzalishaji wa bidhaa za ndani, kupambana na magendo ya bidhaa na fedha za kigeni, kudhamini bidhaa za kimsingi kwa ajili ya watu wa tabaka la chini na sheria ya bajeti katika Bunge la Tisa na kuongeza kuwa: Kuipa kipaumbele na mazingatio makubwa sekta ya usalama wa kiafya, kutia nguvu na kuimarisha mfumo wa kiulinzi nchini na kuandaa uwanja wa kukabidhiwa sekta binafsi, miradi iliyotekelezwa nusu, kuwa ni katika kazi na hatua nyingine zilizofanywa na Bunge la Tisa la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Bw. Larijani amezungumzia pia hatua za usimamiaji wa Bunge na vile vile kazi za kitengo cha mahesabu, kituo cha utafiti cha Bunge, kamisheni ya Kifungu cha 90 ( ncha Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran) na jopo la kusimamia utekelezaji wa sheria; na amma kuhusiana na msimamo wa Bunge la Tisa katika masuala makuu na masuala yanayohusiana na eneo la Mashariki ya Kati na ya kimataifa amesisitiza kuwa: Mikakati na stratijia za Bunge ni kulinda kwa nguvu zake zote haki za taifa la Iran mbele ya ubeberu wa waistikbari kwa kutegemea fikra ya kimsingi ya Imam Khomeini Rahimahullah na vile vile kutilia mkazo na kuzingatia uchumi unaotegemea vyanzo vya ndani pamoja na kadhia nzima ya miradi ya nyuklia.
 
< Nyuma   Mbele >

^