Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Hotuba ya Kiongozi Muadhamu katika Maadhimisho ya Mwaka wa 26 wa Kufariki Dunia Imam Khomeini MA Chapa
04/06/2015
 Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, leo asubuhi amehutubia umati mkubwa na usio na kifani wa wananchi waaminifu wa Iran katika Haram toharifu ya mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuitaja aidiolojia ya Imam Khomeini (quddisa sirruh) kuwa ni muongozo na ni ramani ya njia iliyojaa matumaini kwa taifa la Iran na huku akigusia udharura wa kukabiliana na upotoshaji wa shakhsia ya Imam Khomeini amesisitiza kuwa: Kuitangaza tena na tena misingi ya aidiolojia ya Imam kwa hoja zilizo wazi ndiyo njia pekee ya kuweza kukabiliana na upotoshaji wa shakhsia ya mtukufu huyo; misingi kama vile kuuthibitisha Uislamu sahihi na wa asili wa Mtume Muhammad SAW na kupinga Uislamu wa Kimarekani, kuitakidi na kuwa na imani na ukweli wa ahadi za Mwenyezi Mungu na kutokuwa na imani na mabeberu na waistikbari, kutegemea na kuwa na imani na nguvu za wananchi na kupinga ukiritimba wa kiserikali, kulipa uzito wa hali ya juu suala la kuwaunga mkono na kuwasaidia wanyonge na kupinga maisha ya anasa na israfu, kuwaunga mkono na kuwasaidia watu wanaodhulumiwa duniani na kuyapinga wazi wazi na bila ya kuyaogopa madola ya kibeberu duniani, kupigania uhuru na ukombozi na kupinga ubepari na uistikbari kama ambavyo amesisitizia pia umuhimu wa kulindwa umoja wa kitaifa nchini.
Katika utangulizi wa hotuba yake kwenye maadhimisho ya mwaka wa ishirini na sita wa kukumbuka siku alipofariki dunia Imam Khomeini - rahimahullah - Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria umuhimu wa mwezi kumi na tano Shaaban (nusu ya Shaaban) na kukumbuka siku ya kuzaliwa Imam wa Zama, Imam Mahdi - Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake - na kulitaja suala la mwokozi wa ulimwengu kuwa ni jambo linalokubaliwa na dini zote za Kiibrahim.
Ameongeza kuwa: Madhehebu yote ya Kiislamu yanaamini kwamba mwokozi huyo wa ulimwengu ni kutoka katika kizazi cha Mtume wa Mwisho na jina lake ni Mahdi - Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake - ambapo sambamba na kuamini hivyo, Waislamu wa madhehebu ya Kishia, kwa kutegemea ushahidi ulio wazi na usiopingika wanaamini kuwa Imam wa Zama - Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake - ni mwana wa Imam wa 11 Imam Askari AS na wanaamini ameshazaliwa na yuko hai kwa ushahidi na hoja makini na madhubuti.
Ayatullah Udhma Khamenei amekutaja kuleta matumaini kuwa ni katika sifa kubwa kabisa za kuwa na imani ya kudhihiri Mahdi muahidiwa - Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake - na kuongeza kuwa miale inayowaka kwa nguvu na kwa wingi ya itikadi hii ya kina na iliyojaa wokovu, muda wote imewafanya Waislamu wa Kishia kuishi kwa matumaini ya mustakbali mwema katika vipindi vyote vya kiza na dhulma na kuwafanya muda wote wawe na harakati kubwa za kila namna.
Baada ya hapo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amebainisha umuhimu wa maudhui kuu na ya kimsingi ya hotuba yake ya leo yaani "kupotoshwa shakhsia ya Imam Khomeini (quddisa sirruh)" na kuongeza kuwa: Tofauti na baadhi ya watu wanavyojaribu kumuonesha kwamba alihusiana na zama zake tu, Imam wetu mtukufu, alikuwa ni dhihirisho cha harakati adhimu na ya kujenga historia ya taifa la Iran na tab'an kupotosha shakhsia yake kuna madhara makubwa dhidi ya kuendelea harakati hiyo, hivyo inabidi watu wawe macho kikamilifu kuhusu suala hilo.
Ayatullah Udhma Khamenei ameitaja aidiolojia ya kifikra, kisiasa na kijamii ya Imam Khomeini Rahimahullah kuwa ni muongozo na ni ramani ya njia kwa taifa la Iran kwa ajili ya kufikia malengo yake makubwa kama vile uadilifu, nguvu na maendeleo na kusisitiza kuwa: Haiwezekani kuendelea na muongozo na ramani hiyo ya njia bila ya kuwepo "kielelezo sahihi na kisichopotoshwa cha Imam."
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia pia upeo mkubwa wa kifikihi, kiirfani na kifalsafa wa Imam Khomeini na kusema kuwa, shakhsia ya asili ya Imam ilikuwa ni kufanikisha malengo ya Qur'ani Tukufu ambayo yanatoa sifa ya kweli ya wanaofanya jitihada katika njia ya Mwenyezi Mungu ambao wanatekeleza vilivyo jihadi ya kweli katika njia hiyo.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Imam mtukufu wa taifa la Iran alipigania kuleta mabadiliko yasiyo na mfano katika historia ya nchi hii na ya ulimwengu mzima wa Kiislamu hivyo alipambana kishujaa na kufanikiwa kuupindua utawala uliofilisika na kuchakaa, utawala ghalati wa kisultani na wa kurithishana watu wa ukoo mmoja na kufanikiwa kuanzisha utawala wa kwanza wa Kiislamu baada ya ule wa mwanzoni mwa Uislamu na akatekeleza kwa nguvu zake zote, haki ya jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu.
Pia ameitaja jihadi ya nafsi na umaanawi wa kina na wa hali ya juu kuwa ni ukamilishaji wa jihadi ya kisiasa, kijamii na kifikra ya Imam Khomeini (quddisa sirruh) na katika kubainisha vipengee vya aidiolojia ya Imam amesema: Mhimili wa kifikra ambao unaweza kuleta mabadiliko haya adhimu umetokana na utambuzi wa kina wa dunia uliosimama juu ya msingi wa tawhidi aliokuwa nao Imam Khomeini (quddisa sirruh).
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja suala la kutopitwa na wakati kuwa ni sifa ya pili ya kipekee ya aidiolojia ya Imam Khomeini - Rahimahullah - na kusisitiza kwamba: Imam alitumia na kutegemea mhimili wake ulioshikamana barabara wa kifikra, katika kutatua masuala ya jamii ya Iran na ya jamii za wanadamu ya kuyapatia ufumbuzi matatizo ya mataifa ya dunia ambayo yalikuwa yanathamini njia hizo za utatuzi na ni kwa sababu hiyo ndio maana madras na chuo cha kifikra cha Imam Khomeini kimeweza kuenea sana kati ya mataifa mengine duniani.
Amelitaja suala la kuwa hai, kubaki katika hali yake ya asili, kuwa na wingi wa harakati na kuwa na sifa ya kutekelezeka kwamba ni jambo jengine la kipekee lililomo kwenye fikra na aidiolojia ya Imam Khomeini - Rahimahullah - na kusisitiza kuwa: Imam hakuwa kama baadhi ya watunga nadharia wanaodai kuwa na fikra huru na watoa fikra za kidhahania ambao wanapokuwa mbele ya watu wanatoa matamshi mazuri, lakini fikra zao hizo hazitekelezeki na hazina faida yoyote katika medani ya utendaji.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, taifa la Iran limeweza kupata matumaini, harakati na msukumo mkubwa wa kuendelea na jitihada zake za kujiletea maendeleo kutokana na baraka za kufuata kwake nadharia na aidiolojia ya Imam Khomeini na kuongeza kuwa: Taifa kubwa la Iran bado lina safari ndefu sana ya kuweza kufanikisha malengo yake, lakini lililo muhimu ni kuwa, taifa hili na vijana wake linaendelea na njia ya kufanikisha malengo yake hayo kwa nyoyo zilizojaa hamasa, hima na matumaini.
Amelitaja suala la kuendelea kupiga hatua kwa namna sahihi ndani ya njia hiyo iliyojaa matumaini kuwa linahitajia kuielewa kwa njia sahihi na kwa kina shakhsia ya Imam Khomeini na kufanya bidii ya kutekeleza kivitendo msingi wa fikra na aidiolojia yake na kusisitiza kuwa: Kuipotosha shakhsia ya Imam, kupotosha njia ya Imam na kufanya njama za kupotosha njia iliyonyooka ya taifa la Iran ni jambo la hatari mno; na kama njia ya Imam tutaipoteza au kuisahau au - Mwenyezi Mungu apishie mbali - tukafanya makusudi kuidharau na kuiweka pembeni, basi bila ya shaka yoyote taifa la Iran litapata pigo kubwa.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kuwa, ubeberu wa dunia na madola ya kiistikbari ulimwenguni bado yanaiangalia kwa jicho la tamaa Iran ambayo ni nchi kubwa, tajiri na muhimu katika eneo la Mashariki ya Kati na Guba ya Uajemi na kuongeza kuwa: Madola malaghai duniani yataachana na tamaa yao hiyo isiyoisha iwapo tu taifa la Iran litafikia maendeleo na nguvu ambazo zitayakatisha tamaa kabisa madola hayo.
Vile vile amekumbushia nukta hii kwamba njia ya maendeleo na nguvu za taifa la Iran zimo katika kufanya harakati ndani ya mipaka ya usuli na msingi ya madrasa ya kifikra ya Imam Khomeini - Rahimahullah - na kuongeza kuwa: Ni kwa kuzingatia masuala hayo ndipo tutakapoona hatari ya kupotoshwa shahksia ya Imam wetu mtukufu - Rahimahullah - ilivyo kubwa na inabidi hiyo iwe ni tahadhari inayopaswa kupewa uzito wa hali ya juu na viongozi na wanafikra wa Mapinduzi ya Kiislamu, wanafunzi wa zamani wa Imam, wapenzi wa njia ya Imam, vijana wote, wasomi, watu wenye hekima pamoja na watu wa Hawza na Vyuo Vikuu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja suala la kupotoshwa shakhsia ya Imam Khomeini (quddisa sirruh) kuwa ni suala lenye historia ndefu na limekuwepo tangu mwanzoni mwa Mapinduzi ya Kiislamu na kuongeza kuwa: Njama za adui zimekuwepo tangu awali kabisa ya Mapinduzi (ya Kiislamu) na tangu wakati wa uhai wa Imam - Rahimahullah - na kwamba maadui tangu wakati huo walikuwa wakifanya propaganda katika pembe mbali mbali za dunia kujaribu kumuonesha Imam kuwa ni mwanamapinduzi mwenye fikra mgando na mtumia mabavu ambaye alikuwa hapendi mabadiliko na eti alikuwa ni mtu asiye na hisia za huruma.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Imam mtukufu - Rahimahullah - alikuwa na shakhsia isiyotetereka na isiyorudi nyuma katika kupambana na madola ya kibeberu na kiistikbari, lakini wakati huo huo alikuwa ni dhihirisho la huruma, mapenzi, upole, utu na unyenyekevu mbele ya Mwenyezi Mungu na mbele ya waja wa Mwenyezi Mungu hususan tabaka la wanyonge.
Aidha ameashiria suala la baadhi ya watu ndani ya Iran la kupotosha shakhsia ya Imam Khomeini kwa kujua au kutojua na kusema: Wakati wa uhai wake Imam - Rahimahullah - kuna baadhi ya watu walikuwa wakimnasibisha Imam na kila kauli waliyoipenda wao wakati ambapo mambo hayo hayakuwa na uhusiano wowote na shakhsia huyo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Baada ya kufariki dunia Imam - Rahimahullah - mrengo huo uliendelea kuwepo na ikafikia hadi kwamba baadhi ya watu wa mrengo huo wakamuita Imam kwamba alikuwa mtu mwenye fikra za kiliberali ambaye hakuwa akichunga sheria wala mipaka yoyote ya kidini katika miamala ya kisiasa, kifikra na kiutamaduni, wakati ambapo mtazamo huo ni ghalati kikamilifu bali ni kinyume kabisa na uhalisia wa mambo.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema kuwa, njia pekee ya kuweza kuwa na utambuzi sahihi na wa kina kuhusu shakhsia ya Imam Khomeini (quddisa sirruh) ni kuitambua na kuisoma upya misingi na usuli za madrasa ya kifikra ya Imam na kusisitiza kuwa: Kama shakhsia ya Imam haitatambuliwa kwa kutumia mbinu hiyo, basi kuna uwezekano baadhi ya watu wakamtambulisha Imam kwa mujibu wa mapenzi na mitazamo yao ya kifikra ambayo ni kinyume na mitazamo yake.
Vile vile amesema kuwa, mapenzi ya Imam - Rahimahullah - kati ya wananchi ni makubwa na hayawezi kufutika na kwamba adui ameshindwa kufuta mapenzi hayo ya wananchi kwa Imam na kuongeza kuwa: Ni kwa sababu hiyo ndio maana suala la kupotosha shakhsia ya Imam iliyopenya na kukita mizizi ndani ya nyoyo za watu ikahesabiwa kuwa ni hatari kubwa sana na kwamba kusomwa upya na kutaliiwa upya usuli na misingi ya kifikra ya Imam - Rahimahullah - ndiyo njia ya kuweza kupambana na kuzuia kujitokeza hatari hiyo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameutaja usuli na misingi wa kifikra wa Imam Khomeini - Rahimahullah - kuwa inapatikana katika miongozo na hotuba zake mbali mbali katika kipindi chote cha miaka 15 ya mwamko wa Kiislamu na miaka 10 ya baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran na kuongeza kuwa: Wakati usuli na misingi hiyo inapowekwa pamoja, hupatikana jengo madhubuti la shakhsia ya kweli ya Imam Khomeini - Rahimahullah.
Kabla ya kuanza kubainisha mambo saba ambayo ni katika usuli na misingi ya kifikra ya Imam Khomeini (quddisa sirruh), Ayatullah Udhma Khamenei amebainisha kwanza nukta kadhaa kuhusiana na misingi hiyo ya kifikra ya Imam - Rahimahullah - kama ifuatavyo:
1 - Misingi hiyo ilibainishwa mara kadhaa na Imam na ni katika misimamo ya wazi kabisa ya Imam.
2 - Misingi hiyo haipaswi kubainishwa kiubaguzi na kwa kuchagua baadhi yake na kuacha mengine.
3 - Misingi ya Imam haimalizikii tu kwenye mambo hayo saba na kwamba wanafikra wanaweza kutumia kalibu na fremu hiyo iliyo wazi kuchimbua na kutoa misingi mingine ya madrasa ya kifikra ya Imam (quddisa sirruh).
Baada ya hapo ameanza kubainisha misingi saba ya madrasa ya kifikra na kiaidiolojia ya Imam Khomeini - Rahimahullah - kwa kusema: "Kuutangaza na kuutilia nguvu Uislamu wa asili wa Bwana Mtume Muhammad SAW na kupinga Uislamu wa Kimarekani," ni katika moja ya misingi hiyo ya kifikra ya Imam - Rahimahullah - ambapo muda wote alikuwa akitofautisha baina ya Uislamu wa kweli na Uislamu wa Kimarekani.
Katika kubainisha muundo na utambulisho wa Uislamu wa Kimarekani, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, Uislamu huo uko wa aina mbili na hauna aina ya tatu na aina hizo mbili ni "Uislamu wa kisekula" usiojali kabisa mafundisho ya dini na "Uislamu wa fikra mgando" na kuongeza kuwa: Imam - Rahimahullah - daima alikuwa akiwaweka watu ambao walikuwa na fikra za kuitenga dini na jamii na mambo ya kijamii ya watu katika fungu la watu ambao wanaiona dini kuwa ni kitu kilichopitwa na wakati, kinachombakisha nyuma mwanadamu kimaendeleo, kitu chenye fikra mgando na ambacho wanadamu wa leo wenye fikra na mitazamo mipya wanashindwa kuyaelewa mafundisho yake.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kuwa, matawi yote hayo mawili ya Uislamu wa Kimarekani, siku zote yamekuwa yakiungwa mkono na kusaidiwa na mabeberu wa dunia na Marekani na kuongeza kuwa: Leo hii pia, makundi yenye fikra mgando ya Daesh na al Qaida ambayo kidhahiri na kijuu juu yanaonekana ni makundi ya Kiislamu lakini hayajui chochote kuhusu fikihi na sharia za Kiislamu, yanaungwa mkono na Marekani na Israel.
Amesema: Kwa mtazamo wa Imam - Rahimahullah - Uislamu wa kweli ni Uislamu unaotegemea Qur'ani na Sunna jambo ambalo linahitajia kuwa na mtazamo wa wazi na unaofaa kuhusiana na mazingira yaliyopo katika wakati na sehemu alipo mtu, kuelewa vizuri mahitaji ya wakati huo ya jamii za Waislamu na jamii yote ya mwanadamu na kuzingatia mbinu za adui na vile vile kwa kueneza mafundisho hayo ya Qur'ani na Sunna kwa kutumia mbinu na njia zinazokubalika na zilizokamilika za kielimu katika Hawza (Vyuo Vikuu vya kidini).
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Katika madrasa ya kifikra ya Imam - Rahimahullah - masheikh wa majumba ya kifalme na Uislamu wa Kidaesh kwa upande mmoja na Uislamu usiojali jinai za utawala wa Kizayuni na Marekani na Uislamu unaoangalia kwa jicho la tamaa misaada na uungaji mkono wa madola ya kibeberu kwa upande wa pili, makundi yote hayo mawili yanaishia kwenye nukta moja na yote hayakubaliki.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kuwa: Mtu ambaye anajihesabu ni katika wafuasi wa Imam Khomeini - Rahimahullah - anapaswa kuweka mipaka iliyo wazi baina yake na Uislamu wa fikra mgando na wa kisekula.
Amelitaja suala la kutegemea msaada wa Mwenyezi Mungu na kuwa na imani na ahadi za kweli za Mwenyezi Mungu katika mkabala wa kutokuwa na imani na madola ya kiistikbari na kibeberu duniani kwamba ni msingi wa pili wa kifikra wa Imam Khomeini (quddisa sirruh) na kuongeza kuwa: Imam wetu mtukufu, daima alikuwa na imani ya kweli na ahadi za Mwenyezi Mungu na hakuwa na imani kabisa na ahadi za mabeberu na madola ya kiistikbari duniani.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu vile vile amesema: Sifa hizo za kipekee na zilizo wazi zilimfanya kuwa na shakhsia ya kutangaza wazi misimamo yake isiyotetereka bila ya kumuogopa wala kumuonea haya mtu yeyote.
Ayatullah Udhma Khamenei amegusia pia majibu ya Imam Khomeini (quddisa sirruh) kwa barua za baadhi ya viongozi wa madola ya kibeberu ambapo alibainisha misimamo yake kwa uwazi na kwa msimamo usioyumba hata kidogo na wakati huo huo lakini kwa kuchunga heshima na maadili mema na kuongeza kuwa: Imam amefanikiwa kulifanya suala la kutawakali kwa Mwenyezi Mungu lienee na kutembea katika mishipa ya damu ya taifa la Iran kama inavyotembea damu kwenye mwili wa mwanadamu kiasi kwamba hivi sasa wananchi wa Iran wamekuwa ni watu wa kutawakali kwa Mwenyezi Mungu na wenye imani thabiti ya kupata nusra kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Vile vile amegusia namna Imam - Rahimahullah - alivyokuwa hawaamini hata chembe mabeberu na jinsi alivyokuwa akipuuza kikamilifu ahadi za waistikbari na kuongeza kuwa: Hivi sasa suala hili tumelidiriki kwa uwazi kabisa ya kwamba kwa nini hatupaswi kuwa na imani na ahadi za mabeberu kwani katika vikao vya faragha, waistikbari wanazungumza mambo tofauti kabisa na yale wanayoyazungumza katika vikao vya wazi na kwenye matendo yao.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kwamba, kuwa na imani na Mwenyezi Mungu na kutawakali kwake na kutokuwa na imani na mabeberu ni katika misingi ya wazi kabisa ya madrasa ya kifikra ya Imam Khomeini - Rahimahullah - na kuongeza kuwa: Tab'an suala hilo halina na maana ya kukataa kuwa na uhusiano na madola mengine duniani kwani yalikuwepo mahusiano ya kiwango cha kawaida na ya kuheshimiana baina ya Iran na madola mengine duniani, lakini Tehran haikuwa na imani kabisa na mabeberu na vibaraka wao.
Kuwa na imani na irada na nguvu za wananchi na kupinga ukiritimba wa kiserikali ni msingi wa tatu katika misingi ya madrasa ya kifikra ya Imam (ridhwanullahi alayhi) ulioashiriwa na Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei katika hotuba yake hiyo.
Vile vile amesisitiza kuwa Imam wetu mtukufu (quddisa sirruh) alikuwa akiwapa umuhimu mkubwa wananchi katika mambo mbalimbali. Alikuwa daima akiipa umuhimu mkubwa na wa kweli nafasi ya wananchi katika masuala ya kiuchumi, kijeshi, ujenzi wa nchi, tablighi na muhimu kuliko yote, masuala yanayohusiana na uchaguzi na alikuwa akiwategemea sana wananchi. Aidha amesema: Katika kipindi cha miaka 10 ya uhai wake Imam (radhiallahu anhu) wa baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ambapo miaka minane kati ya hiyo ilikuwa ni kipindi cha vita vya kulazimishwa vya kujihami kutakatifu (vilivyoanzishwa na utawala wa wakati huo wa Iraq dhidi ya utawala mchanga wakati huo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran), kulifanyika karibu chaguzi kumi nchini Iran na hakuna uchaguzi wowote uliochelewa japo kwa siku moja, bali chaguzi zote zilifanyika katika wakati uliopangwa kwani Imam (quddisa sirruh) alikuwa akiheshimu mno maoni, rai na maamuzi ya wananchi kwa maana halisi ya neno.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Hata katika mambo ambayo kulikuwa na uwezekano maamuzi ya wananchi yakawa kinyume na mtazamo wa Imam (Ridhwanullahi Alayhi) lakini pamoja na hayo aliheshimu maamuzi hayo ya wananchi.
Ayatullah Udhma Khamenei amegusia pia matamshi ya Imam Khomeini (quddisa sirruh) ambaye alikuwa akisema mara chungu nzima kwamba anawaheshimu sana wananchi na yeye ni mtumishi wa wananchi na kusisitiza kuwa: Matamshi hayo yanaonesha nafasi kubwa ya wananchi, na nafasi isiyo na kifani ya fikra, rai na maamuzi yao pamoja na kushirikishwa kwao katika mambo yote, kwenye madrasa ya kifikra ya Imam Khomeini (quddisa sirruh). Tab'an wananchi nao walitoa majibu mazuri katika kila sehemu ambayo ilinyooshewa kidole na Imam (quddisa sirruh) na walijitokeza kwa wingi mno kwenye medani hizo kwa nyoyo na roho zao.
Akitoa muhtasari wa matamshi yake kuhusu sehemu hiyo ya hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kwamba: Kulikuwa na mahusiano ya pande mbili baina ya Imam (quddisa sirruh) na wananchi. Imam alikuwa akiwapenda sana wananchi na wananchi nao walimpenda sana Imam.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameendelea na hotuba yake kuhusiana na misingi ya kifikra ya Imam Khomeini (Ridhwanullahi Alayhi) kwa kusema: Katika upande wa masuala ya ndani ya nchi, Imam alikuwa ni muungaji mkono mkubwa wa wanyonge na watu wenye suhula chache na alikuwa akipinga vikali mno ukosefu wa usawa wa kiuchumi na maisha ya anasa na ya kifakhari.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza pia kuwa, Imam Khomeini (quddisa sirruh) alikuwa ni muungaji mkono mkubwa wa uadilifu wa kijamii kwa maana halisi ya neno. Jambo hilo ni moja ya masuala yaliyokuwa yakisemwa na kukaririwa mno na Imam katika matamshi yake na ni moja ya misisimamo isiyotetereka aliyokuwa nayo Imam na kuongeza kuwa: Imam (Ridhwanullahi Alayhi) kwa upande mmoja alikuwa akisisitizia mno suala la kung'olewa mizizi ya umaskini na kupambana vilivyo na utovu wa maendeleo na kwa upande wa pili aliwahimiza mno viongozi nchini kujiepusha na maisha ya anasa, israfu na ya kifakhari.
Amegusia pia namna Imam Khomeini (quddisa sirruh) alivyokuwa akisisitiza mno juu ya haja ya viongozi nchini kuwa na imani na kuwategemea wananchi wa matabaka dhaifu na ya wanyonge na kuongeza kuwa: Imam wetu mtukufu (Ridhwanullahi Alayhi) daima alikuwa akisema kuwa, ni watu maskini na wanaoshi kwenye maeneo ya wanyonge ndio ambao wanaojitokeza kwenye medani mbali mbali bila ya kulalamikia matatizo na mashaka yao katika maisha wakati ambapo matabaka ya wenye nacho ndiyo yanayoonesha kulalamika mno wakati wa matatizo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amebainisha usuli na msingi wa tano wa fikra za Imam Khomeini (quddisa sirruh) na kuongeza kuwa: Katika upeo wa siasa za nje ya nchi pia, Imam (Ridhwanullahi Alayhi) alikuwa akiyapinga wazi wazi madola ya kibeberu na kiistikbari duniani na wakati wote alikuwa akiyaunga mkono mataifa yanayodhulumiwa na alikuwa hamuogopi mtu yeyote katika siasa zake hizo.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kuwa, Imam Khomeni (Ridhwanullahi Taala Alayhi) alikuwa hakubaliani kivyovyote vile na waistikbari na alitumia ibara ya "Shetani Mkubwa" kuiita Marekani na huo ukawa ni ubunifu wa kipekee na wa kustaajabisha wa Imam Khomeini (quddisa sirruh) na kusisitiza kuwa: Wigo wa kuielewa na kuamiliana nayo kivitendo ibara ya "Shetani Mkubwa" ni mpana na ni mkubwa sana kwani wakati mtu anapopewa lakabu ya shetani lazima mtu huyo atakuwa na sifa za kishetani katika matendo, hisia na mambo yake yote (na hivyo ndivyo ilivyo Marekani).
Ameongeza kuwa: Imam (Ridhwanullahi Alayhi) hadi siku za mwisho za uhai wake alikuwa na hisia hizo hizo kuhusiana na Marekani na alikuwa akiuamini kikamilifu msimamo na itikadi yake hiyo ya kwamba Marekani na Shetani Mkubwa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Katika mkabala wa msimamo huo - awali ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu - kulikuwa na watu nchini Iran ambao walikuwa hawaioni nafasi ya Marekani katika kuukuza na kuuimarisha utawala wa taghuti uliopinduliwa na wananchi wa Iran hivyo walikuwa wanakubaliana na kuweko Wamarekani nchini Iran bali hata kuendelea kufanya kazi baadhi ya asasi za Marekani nchini.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema kuwa, hiyo ndiyo tofauti kubwa iliyokuwa nayo serikali ya muda nchini Iran na fikra za Imam (quddisa sirruh) katika miaka ya mwanzoni mwa Mapinduzi ya Kiislamu na kuongeza kuwa: Watu hao walishindwa kujua kwamba kama Marekani itapewa fursa basi haitasita kulisababishia madhara makubwa taifa la Iran lakini Imam (Ridhwanullah Alayhi) alilielewa vizuri jambo hilo na alikuwa akichukua misimamo ya wazi kuhusu suala hilo na hata msimamo uliochukuliwa na Imam kuhusiana na kutekwa na wanafunzi wa Vyuo Vikuu vya Iran - "pango la kijasusi" (ubalozi wa Marekani mjini Tehran) - aliuchukua kwa msingi huo huo.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria pia matukio ya hivi sasa katika eneo la Mashariki ya Kati na namna baadhi ya mirengo ilivyopata hasara kubwa kwa kuiamini Marekani na kuongeza kuwa: Fikra za Imam (quddisa sirruh) zilikuwa zimesimama juu ya msingi huo, daima alikuwa akichukua msimamo thabiti wa kukabiliana na Marekani na taasisi zake za kisiasa na kiusalama na katika upande wa pili alikuwa muda wote akiyahami na kuyatetea mataifa yanayodhulumiwa hususan wananchi wa Palestina kwa mapenzi makubwa na kwa msimamo usioyumba kabisa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, hivi sasa pia tunaweza kufuata fikra za Imam kwa ajili ya kutatua masuala yaliyopo leo hii katika eneo hili na duniani kiujumla ndani ya kalibu na fremu ya mantiki hiyo ya Imam (Ridhwanullahi Alayhi). Ameongeza kuwa: Sisi leo hii tunapinga vitendo vya kidhulma vya polisi ya FBI ya Marekani ndani ya nchi hiyo kwa kiwango kile kile tunachopinga vitendo vya kinyama na kidhulma vya kundi la Daesh katika nchi za Iraq na Syria; vitendo vya pande zote hizo mbili tunaviona ni sawa sawa.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kuwa: Sisi tunapinga kuzingirwa kidhulma wananchi madhlumu wa Ghaza kwa kiwango kile kile tunachopinga kushambuliwa na kuuliwa wananchi wasio na pa kukimbilia wa Yemen na kwa kiwango kile kile cha ukandamizaji wanaofanyiwa wananchi wa Bahrain na mashambulizi ya ndege zisizo na rubani za Marekani dhidi ya wananchi wa Afghanistan na Pakistan.
Vile vile amesisitiza kuwa hivi sasa pia Iran inatumia mantiki iliyo wazi ya Imam Khomeini (quddisa sirruh) kuwaunga mkono watu wanaodhulumiwa na kupinga madhalimu na kuongeza kuwa: Ni kwa sababu hiyo ndio maana kadhia ya Palestina hadi leo hii ni suala kuu kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kamwe halijawahi kutoka katika ajenda za mfumo wa Kiislamu wa nchini Iran.
Kiongozi Muadhamu wa Mapineduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Kadhia ya Palestina ni medani ya jihadi ya wajibu na ya lazima ya Kiislamu na hakuna jambo lolote linaloweza kututenganisha na suala la Palestina.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Inawezekana wakatokezea baadhi ya watu wakashindwa kutekeleza majukumu yao kuhusiana na Palestina lakini jambo tunaloliunga mkono sisi na kulitetea ni wananchi na ni wanamapambano wa Palestina.
"Kupigania uhuru na kutokubali kufanyiwa ubeberu" ni msingi wa sita wa madrasa ya kifikra ya Imam Khomeini (quddisa sirruh) uliogusiwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika hotuba yake hiyo.
Ayatullah Udhma Khamenei ametoa maana ya neno ‘istiklali' kuwa ni uhuru kulingana na mazingira na sifa za taifa husika na kuzungumzia mgongano usiokubalika uliopo kati ya baadhi ya watu wanaodai kupigania uhuru wa watu binafsi lakini ukweli ni kuwa wanavunja na kupinga ‘istiklali' ya nchi na uhuru wa mataifa mengine na kuongeza kuwa: Ni jambo la kusikitisha kuona kuwa baadhi ya watu wanatoa nadharia mbalimbali na kuitaja ‘istiklali' kuwa ni jambo linaloifanya nchi na taifa litengwe au wanaliona ni jambo lisilo na thamani ili kwa njia hiyo waweze kupinga uhuru wa taifa na nchi hiyo wakati ambapo kufanya hivyo ni kosa kubwa na la hatari sana.
Vile vile amegusia itikadi thabiti na isiyotetereka aliyokuwa nayo Imam Khomeni (quddisa sirruh) kuhusiana na suala la istiklali na uhuru na kupinga ubeberu na uistikbari na amesema kwamba mambo mengi yanayofanywa na adui kama vile vitisho na vikwazo yanalenga kuutia doa msingi huo wa kifikra wa Imam (Rahimahullah) na kuongeza kuwa: Adui wa istikalali na uhuru wetu ameelekeza mashambulizi yake kwa nchi yetu ya Iran hivyo watu wote nchini Iran wanapaswa kuzitambua vyema shabaha hizo za adui na kukabiliana nazo kwa welewa na busara ya hali ya juu.
Msingi wa "umoja wa kitaifa na kupambana na njama za adui za kuzusha mizozo na mifarakano" ni usuli na msingi wa saba na wa mwisho na ulio wazi wa madrasa ya kifikra ya Imam Khomeini ambao Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameusisitizia kwenye hotuba yake ya leo.
Amesema, kuzusha mizozo ya kimadhehebu na mifarakano ya kikaumu ni sehemu ya siasa za kila siku za adui wa taifa la Iran na kuongeza kwamba: Imam wetu mtukufu tangu mwanzoni kabisa mwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu alianza kupambana na njama hiyo na alikuwa akisisitizia mno na kwa sura ya ajabu na ya kipekee; suala la umoja wa kitaifa na mshikamano kati ya matabaka yote ya wananchi wa Iran.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia pia suala la kuendelea siasa za kuzusha mizozo na kulitaja suala la kuleta mifarakano ndani ya ulimwengu wa Kiislamu kuwa ni katika siasa kuu za mabeberu na Wamarekani na kusisitiza kwamba: Katika kupambana na njama hizo, mtazamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni mtazamo wa kujenga umma wa Kiislamu na muda wote imekuwa ikipigania kujenga umma wa kweli wa Kiislamu na ni kwa sababu hiyo pia ndio maana Iran kama ilivyo na uhusiano na ndugu zake wa Kishia wa Hizbullah, ni hivyo hivyo ina uhusiano mzuri na ndugu zake wa Kisunni huko Palestina.
Ayatullah Udhma Khamenei ameutaja mpango wa "Hilal ya Kishia" uliotolewa na vibaraka wa daraja la pili wa Marekani na namna Wamarekani wanavyoyalegezea kamba au kuyasaidia makundi ya kigaidi katika nchi za Iraq na Syria kama vile Daesh kuwa ni katika ushahidi wa wa wazi wa siasa za kuzusha mizozo na mifarakano ya kimadhehebu zinazoendeshwa na mabeberu katika ulimwengu wa Kiislamu na kuongeza kuwa: Waislamu wote, wawe Waislamu wa Kisuni au wa Kishia kila mmoja anapaswa kuwa macho asije akatekwa na mchezo huo mchafu wa adui.
Amesisitiza pia kuwa: Yule Msuni ambaye anatengenezwa na Marekani na yule Mshia ambaye anatengenezwa na London (Uingereza) na kusambazwa duniani, wote hao wawili ni ndugu wa shetani na ni vibaraka na vitimbakwiri vya ubeberu na Magharibi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amefafanua zaidi kwa kusema kuwa, hata kaulimbiu ya mwaka huu (mwaka wa Kiirani wa 1394 Hijria Shamsia) yaani mwaka wa kupendana na kufahamiana imetolewa kwa ajili ya kusisitizia wajibu wa kupambana na njama za maadui za kuleta mizozo na mifarakano nchini Iran na kuongeza kuwa: Adui anatishia usalama na asili ya Uislamu wenyewe, hivyo watu wa kaumu na madhehebu yote wanapaswa kuishi kwa salama baina yao na kuwa na mshikamano na wasiruhusu adui ajipenyeze katika ardhi kubwa na pana ya ulimwengu wa Kiislamu.
Ayatullah Udhma Khamenei ametoa muhtasari wa sehemu hiyo ya miongozo yake kwa kusema kuwa, usuli na misingi ya kifikra ya Imam Khomeini (quddisa sirruh) ilikuwa na mvuto na msukumo wa aina yake na kuongeza kwamba: Misingi ya fikra za Imam haiishii tu kwenye mambo hayo saba, bali wasomi na wanafikra wanaweza kupiga mbizi na kutafuta mambo mengi zaidi mazuri ndani ya mipaka ya misingi hiyo lakini asitokezee mtu akamnasibisha Imam (Ridhwanullahi Alayhi) na mambo yake mwenyewe, bali matamshi yote yanayotolewa yanapaswa yawemo ndani ya mipaka ya usuli na misingi hiyo na kutoka kwenye vyanzo vya Imam mwenyewe tena kila siku na kwa sura ya kuendelea.
Mwishoni mwa hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia uhakika mwengine muhimu akisisitiza kwa kusema: Watu wote watambue kuwa, lengo la adui ni kuirejesha Iran katika kipindi cha unyonge na cha kukubali kufanyiwa ubeberu bila ya kuweza kufanya chochote na kwamba kununa, kucheka, ahadi na vitisho vya adui; lengo na shabaha yake pekee ni kufanikisha jambo hilo.
Amesema, sababu inayowafanya maadui waifanyie uadui dini tukufu ya Kiislamu ni kutokana na dini hiyo kupinga kurejea ubeberu huo na kuongeza kuwa: Adui ana chuki na Uislamu kwani Uislamu umesimama kidete kukabiliana na ubeberu huo. Amesema: Maadui wana chuki na taifa la Iran kwani taifa hili limesimama imara mithili ya jabali katika kukabiliana na njama zao.
Ayatullah Udhma Khamene amegusia pia matamshi ya mwanasiasa mmoja mkongwe wa Marekani aliyesema kuwa makundi ya kigaidi na kitakfiri hayana umuhimu wowote kwa Magharibi na zinachopaswa kufanya nchi za Magharibi ni kuichukulia Iran kuwa ndiye adui yao kutokana na Jamhuri ya Kiislamu kupigania kuleta ustaarabu adhimu wa Kiislamu na kuongeza kuwa: Siasa hizo zinaonesha kuweko umuhimu na udharura mkubwa wa kuundwa umma na ustaarabu wa Kiislamu katika ulimwengu wa Kiislamu na kila mtu anapaswa kuelewa kwamba adui anafanya juhudi zake zote ili kuzuia harakati hiyo ya Kiislamu pamoja na maendeleo na ustawi wa taifa la Iran.
Vile vile amesisitiza kuwa: Adui anaelekeza uadui wake zaidi kwa kila taifa na kila mtu ambaye anasimama kidete zaidi kukabiliana na adui huyo. Maadui wanawafanyia uadui mkubwa zaidi watu waumini, watu wa Mwenyezi Mungu na asasi na taasisi zote za kimapinduzi kwani wanajua kuwa watu na taasisi hizo ni kizuizi kikubwa na madhubuti ya kupenyeza uadui wao kwenye mataifa mengine.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Hujjatul Islam Walmuslimin Sayyid Hasan Khomeini ametoa hotuba fupi na sambamba na kumkaribisha Kiongozi Muadhamu na wafanya ziara wengine katika haram ya mwasisi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Imam Khomeini (quddisa sirruh), amegusia matukio ya Iraq, Syria, Yemen na Bahrain na kusema kuwa watu wenye fikra finyu na mgando wamelitumbukiza eneo la Mashariki ya Kati kwenye vurugu na machafuko. Ameongeza kuwa: Jamii ya Kiislamu hivi sasa inashuhudia matukio machungu sana na wasababishaji wa matukio hayo ni watu ambao wamejaa chuki na uadui dhidi ya dini tukufu ya Kiislamu.
Mfawidhi huyo wa Haram ya Imam Khomeini (quddisa sirruh) ameongeza kuwa: Kundi la watu makatili limeelekeza mashambulizi yake dhidi ya ustaarabu wote wa Kiislamu na dhidi ya jina la Mtume SAW na dini tukufu ya Kiislamu. Amesema, kundi hilo la makatili linafanya mauaji ya watu kwa uungaji mkono wa wageni na wa Wazayuni ili kuonyesha sura mbaya kabisa sura ambayo kwa hakika haina uhusiano wowote na Uislamu.
Hujjatul Islam Walmuslimin Sayyid Hasan Khomeini amesisitiza kuwa, Iran ni ardhi ya Imam Khomeini (Ridhwanullahi Taala Alayhi) na dunia nzima imeona jinsi taifa la Iran lilivyopasi vizuri mitihani yake.
Ameongeza kuwa: Kama atatokezea mtu yeyote na kufanya chokochoko dhidi ya nchi hii, basi taifa la Iran ambalo liko chini ya kivuli cha amirijeshi wake mkuu (Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei) kamwe halitavumilia uchokozi dhidi ya nchi hii na litasimama imara kuilinda ardhi yote ya Iran na kuuhami vilivyo uhuru wa nchi hii.
 
< Nyuma   Mbele >

^