Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Aonana na Waziri Mkuu wa Iraq Chapa
17/06/2015
 Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, leo jioni (Jumatano) ameonana na Bw. Haider al Abadi, Waziri Mkuu wa Iraq na ujumbe alioandamana nao katika ziara yake nchini Iran na kulitaja suala la kuwa macho kwa ajili ya kulinda umoja na mshikamano wa kisiasa na kitaifa wa Iraq kuwa ni jambo la dharura mno na huku akiashiria nia ya kweli, hima na ushujaa wa vijana wa Iraq katika kupambana na magaidi amesisitiza kuwa: Nguvu na uwezo mkubwa wa vikosi vya kujitolea vya wananchi ni jambo lenye taathira kubwa na muhimu mno kwa ajili ya mustakbali na maendeleo ya Iraq katika nyuga tofauti.
Vile vile amesisitiza kuwa, kusimama kidete taifa na serikali ya Iraq katika kukabiliana na magaidi ni dhamana ya kupatikana amani na usalama nchini humo na katika nchi zote za eneo hili na kuongeza kuwa: Moja ya sifa muhimu za wananchi wa Iraq na ambayo imedhihirika kwa uwazi zaidi katika mapambano ya wananchi hao na magaidi, ni ushujaa, nia ya kweli na nguvu za vikosi vya kujitolea vya wananchi na vya makabila yanayohamahama yenye ghera katika kupambana na adui.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja suala la kuwepo magaidi nchini Iraq kuwa ni jambo la muda na la kupita tu na kuongeza kuwa: Rasilimali kubwa na adhimu ya vikosi vya kujitolea vya wananchi ni chemchemu ya kuaminika na inayofaa kutegemewa katika nyuga tofauti ambazo hazihusiani tu na medani za mapigano.
Ayatullah Udhma Khamnenei amesema: Uzoefu wa wananchi wa Iraq wa siku za huko nyuma kuanzia wakati wa ukoloni wa Uingereza hadi katika kipindi cha hivi sasa cha njama za kibeberu za kupenda kujitanua Wamarekani unaonesha kuwa, madola yanayolitakia mabaya taifa la Iraq hayapendi kuona nguvu adhimu za wananchi wa nchi hiyo zimeingia katika medani ya mapambano, hivyo kuna wajibu wa kuilinda rasilimali hiyo ya wananchi, kwa nguvu zote.
Aidha amesema kwamba moja ya malengo ya mashirika ya kiusalama na kijasusi ya nchi za Magharibi huko Iraq kuwa ni kuvunja nguzo za umoja na mshikamano wa kitaifa na kisiasa nchini Iraq na kusisitiza kuwa: Kuna wajibu wa kuwa macho na kupambana vilivyo na kwa uangalifu mkubwa na njama za maadui hao za kueneza mifarakano na isiruhusiwe kutiwa doa umoja na mshikamano wa Waislamu wa Kishia na Kisuni na mshikamano wa Wakurdi na Waarabu nchini Iraq.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaunga mkono umoja na mshikamano wa makundi ya wanamapamno na wanamapinduzi wa Iraq na kwamba wananchi na viongozi wa Iraq wanapaswa kuwa macho mbele ya njama za kueneza fitna, mizozo na mifarakano zinazofanywa na maadui wa taifa lao.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza pia kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inauhesabu usalama na maendeleo ya Iraq kuwa ni sawa na usalama na maendeleo yake na kuongeza kuwa: Wanachotaka Wamarekani ni kuona kuwa kwa upande mmoja wanapora utajiri wa Iraq kama wanavyofanya katika baadhi ya nchi za Kiarabu za eneo hili na kwa upande wa pili wanataka kuwatwisha Wairaq matakwa yao kama walivyofanya huko nyuma, na inabidi kufanyike kila njia ili kutoiruhusu Marekani kufikia malengo yake hayo.
Aidha amesisitizia uungaji mkono wa pande zote wa Iran kwa serikali iliyoko madarakani kihalali nchini Iraq na kuongeza kuwa: Serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaendelea na uungaji mkono wake kwa serikali na wananchi wa Iraq.
Katika sehemu nyingine ya matamshi yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia sifa ya kupenda wageni na ukarimu ya wananchi wa Iraq katika kuwapokea wafanya ziara wa Arubaini ya Imam Husain AS na kusema kuwa hiyo ni sifa nyingine nzuri sana ya wananchi wa Iraq na kuongeza kwamba: Miamala na tabia hiyo ya mapenzi na ya kimaanawi ni muhimu mno katika ulimwengu wa leo ambao watu wanathamini zaidi mambo ya kimaada na kidunia na kwa hakika hadi hivi sasa ukubwa na kina cha tabia hizo njema za wananchi wa Iraq hakijajulikana ipasavyo.
Katika mkutano huo uliohudhuriwa pia na Bw. Eshaq Jahangiri, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Bw. Haider al Abadi, Waziri Mkuu wa Iraq ameelezea kufurahishwa kwake na kupata fursa ya kuonana na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na kusema kuwa, kuendelea kuwepo uungaji mkono wa pande zote wa Iran kwa Iraq na ushirikiano wa kidugu wa serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa ndugu zao wa Iraq ni jambo linaloonesha kuwa kuna uhusiano wa kina baina ya mataifa haya mawili ndugu na kuongeza kuwa: Maadui wa Iraq wanatumia uwezo wao wote kwa ajili ya kuzusha mifarakano na mizozo na kikaumu na kimadhehebu nchini Iraq lakini wananchi na serikali ya Iraq imesimama imara kukabiliana na njama hizo na kulinda umoja na mshikamano wao wa kitaifa.
Vile vile amesisitiza kuwa, makundi ya kigaidi na kitakfiri katika nchi za Iraq na Syria hayatofautishi hata chembe baina ya Waislamu wa Kisuni na Kishia na kuongeza kuwa: Kusimama kidete serikali na wananchi wa Iraq leo hii kimekuwa kizuizi na kinga kubwa katika kukabiliana na kupanuka wigo wa kundi la Daesh katika nchi nyingine za eneo hili, lakini hilo halitoshi bali nchi zote za eneo hili zinapaswa kuungana kwa ajili ya kupambana kikweli na kwa nguvu kubwa zaidi na mgaidi hao.
Vile vile Bw. Haider al Abadi ameishukuru sana Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutokana na misaada yake mbali mbali kwa serikali na wananchi wa Iraq katika kupambana na ugaidi.
 
< Nyuma   Mbele >

^