Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Aonana na Familia za Mashahidi wa Tir Saba Chapa
27/06/2015
Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, leo jioni (Jumamosi) ameonana na familia za mashahidi wa shambulio la Tir Saba (Juni 28, 1981) na pia majimui ya familia za mashahidi wa mkoa wa Tehran na kusema kuwa nchi na wananchi wa Iran wana deni kubwa mbele ya mashahidi na familia zao.
Vile vile ameashiria ujumbe wenye kuleta matumaini, wa kufichua mambo na uliojaa umaanawi na imani ya kweli wa mashahidi katika kila kipindi cha mashahidi hao na kusisitiza kuwa: Leo hii nchi yetu inahitajia azma na nia ya kweli na kumuelewa vyema adui na kuwa tayari kwa ajili ya kupambana na adui katika medani ya vita laini, viwe ni vile vya kiutamaduni, kisiasa au vya katika maisha ya kijamii na kwamba wale watu ambao wanafanya juhudi za kuifanya ionekane nzuri sura mbaya mno ya kuogofya na ya kizimwi ya adui afiriti kupitia kukuza mno habari zake, wajue kuwa kufanya hivyo ni kinyume na maslahi ya taifa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameitaja moja ya baraka za Mapinduzi ya Kiislamu kuwa ni kuyafufua na kuyazalisha upya mafundisho ya kimsingi ya Uislamu halisi na kuyatekelezesha kivitendo katika jamii. Ameongeza kuwa: Moja ya mafundisho hayo ya kimsingi ni majimui ya mafundisho yanayohusiana na ubora wa kufa shahidi katika njia ya haki ambapo imani hiyo hivi sasa imekita mizizi ndani ya jamii ya Iran kiasi kwamba, mashahidi wetu waliingia kwenye medani ya mapambano kwa shauku na imani thabiti na jitihada zao zilizojaa ikhlasi, zimekwenda sambamba na kupata malipo bora kutoka kwa Mwenyezi Mungu, na wamekwenda mbele ya Mola wao wakiwa hawana hofu wala huzuni yoyote. Amesema, athari nzuri za kujitolea kwao muhanga katika njia ya haki zinaonekana hadi leo hii katika jamii.
Ayatullah Udhma Khamenei amelitaja suala la kuleta hisia za heshima katika familia za mashahidi sambamba na shauku na nishati ya kimaanawi pamoja na imani ya kweli isiyotetereka kati ya watu kuwa ni baraka nyingine za kuweko katika jamii mashahidi na watu wanaojitolea damu zao kwenye njia za haki.
Amegusia pia shambulio ya Tir Saba la mwaka 1360 (mwaka wa Kiirani wa Hijria Shamsia sawa na Juni 28, 1981) na kuongeza kuwa: Tukio kubwa kama hilo la Tir Saba ambapo Ayatullah Beheshti na idadi kubwa ya mawaziri, wabunge na wanaharakati wa kisiasa na kimapinduzi waliuawa shahidi, lingeliweza kirahisi kuyafanya Mapinduzi ya Kiislamu yafeli lakini hali haikuwa hivyo, bali kwa baraka za damu ya mashahidi hao, mambo yalikuwa kinyume kabisa na alivyotarajia adui, kwani baada ya tukio hilo, wananchi wa Iran walizidi kushikamana na Mapinduzi yao ya Kiislamu na kuyafanya mapinduzi hayo yaingie kwenye mkondo wake wa kweli na sahihi.
Vile vile amesisitiza kuwa, baraka nyingine za damu ya mashahidi wa Tir Saba ni namna damu hiyo ilivyofichua sura halisi ya waliotenda jinai hiyo na kuongeza kwamba: Baada ya tukio la Tir Saba, sura halisi ya waliotenda moja kwa moja jinai hizo kubwa ambao kwa miaka mingi walikuwa wakijionesha kwa sura nyingine, ilifichuka mbele ya wananchi na hasa vijana na baada ya kupita muda si mrefu, magaidi hao waliungana na Saddam na kushirikiana naye katika kukabiliana na wananchi wa Iran na pia wananchi wa Iraq.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameitaja hatua ya tukio la Tir Saba ya kufichua sura halisi ya watu waliokuwa wakitenda jinai kwa kujificha ndani ya Iran na watenda jinai kutoka nje na pia sura ya baadhi ya watu walionyamaza kimya ikiwa ni kuonesha kuridhishwa na jinai hizo, ni baraka nyingine za damu ya mashahidi wa tukio hilo.
Ameongeza kuwa: Baada ya tukio la Tir Saba, Imam wetu mtukufu (Imam Khomeini) Rahimahullah, alitumia vizuri tukio hilo na kuyaokoa Mapinduzi ya Kiislamu ambayo wakati huo yalikuwa yanapelekwa kwenye mkondo usio sahihi na kuwaonesha wananchi sura halisi na sahihi ya mapinduzi hayo.
Ayatullah Udhma Khamenei amegusia pia shauku ya kimaanawi ya jamii ya Iran baada ya tukio la Tir Saba na kuongeza kwamba: Tukio hilo liliwaonesha waziwazi maadui nguvu za Mapinduzi ya Kiislamu na jinsi yalivyokita mizizi kwenye fikra za jamii ya Iran na maadui walitambua kuwa, hakuna faida ya kutumia mabavu kukabiliana na Mapinduzi ya Kiislamu ya nchini Iran.
Vile vile amekutaja kufichuka sura halisi ya madola ya kiistikbari yanayodai kutetea haki za binadamu kuwa ni baraka nyingine za damu ya mashahidi wa Tir Saba na kusisitiza kuwa: Watu wale wale waliofanya jinai ya Tir Saba ndio ambao hivi sasa wanaishi kwa uhuru kamili katika nchi za Ulaya na Marekani na wanaonana na viongozi wa nchi hizo bali hata wanapewa fursa ya kufanya makongamano na mikutano na wanapewa nafasi ya hata kuhutubia masuala ya haki za binadamu!
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa miamala ya namna hiyo inaonesha upeo wa unafiki, undumakuwili na uafiriti wa madola hayo yanayodai kutetea haki za binadamu duniani. Amesema, nchi yetu imetoa mashahidi 17 elfu ambapo wengi wa mashahidi hao ni wananchi wa kawaida wakiwemo watu waliokuwa wanatafuta riziki zao masokoni, wakulima, wafanyakazi, wahadhiri wa Vyuo Vikuu bali hata wanawake na watoto wadogo, lakini waliotenda jinai zote hizo, hivi sasa wanaishi kwa uhuru kamili katika nchi hizo zinazodai kutetea haki za binadamu.
Ayatullah Udhma Khamenei ameitaja baraka nyingine ya damu ya mashahidi kuwa ni kupuliza roho ya kusimama imara na kutotetereka katika jamii na kutia nguvu moyo na mori wa wananchi na huku akiashiria namna wananchi wa Tehran walivyojitokeza kwa hamasa na shauku kubwa hivi karibuni katika maziko ya mashahidi 270 wa Iran ameongeza kuwa: Tukio hilo adhimu, lenye harakati nyingi, linaloonesha kuwa tayari wakati wote, shauku, mapenzi makubwa na kuwa na malengo matukufu, kwa hakika ni kinyume kabisa na ugoigoi, kukosa matumaini na kutokuwa na hamu ya kutenda jambo.
Akiendelea na hotuba yake, Ayatullah Udhma Khamenei ameelezea kusikitishwa kwake na udhaifu na kutotimizwa vizuri jukumu la kuwatangaza mashahidi ikiwa na kutotangazwa mashahidi wa Tir Saba katika medani kubwa za taifa wakiwa ni dhihirisho la adhama na istikama ya taifa la Iran na kuongeza kuwa: Vijana wanaofanya harakati zao katika medani ya utamaduni wa watu waumini, utamaduni wa kimapinduzi na wa wananchi na utamaduni wa kujitolea bila ya kuhimizwa, wanapaswa kuwatumia vizuri mashahidi katika kazi zao kwa kutumia teknolojia za kisasa kuonesha kwa sura bora ya kisanii shakhsia muhimu na kubwa sana ya mashahidi hao.
Ayatullah Udhma Khamenei amegusia pia haki na deni kubwa na lisiloweza kuelezeka la mashahidi na familia zao kwa taifa la Iran na kuongeza kuwa: Familia za mashahidi zinaionesha jamii, moyo, nia na azma yao ya hali ya juu na kwamba moyo, azma na nia hiyo ya kweli ndicho kitu ambacho tunakihitajia mno hivi sasa humu nchini.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja suala la kumtambua vizuri adui kuwa ni jambo jengine la kimsingi linalohitajiwa nchini Iran na huku akionya kuwa, kuna baadhi wanajaribu kusafisha jinai za adui kwa kutumia propaganda kubwa za vyombo vya habari na kujaribu kumuonesha adui huyo kwa sura nzuri. Ametoa mfano wa vitendo vya kigaidi vya Marekani na vibaraka wake dhidi ya taifa la Iran na kutahadharisha kuhusu njama za kuionesha Marekani kwa sura nzuri.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametaja baadhi ya jinai za Marekani na vibaraka wake dhidi ya wananchi na taifa la Iran kuwa ni pamoja na tukio la Tir Saba mwaka 1360 (Juni 28, 1981), shambulio la silaha za kemikali huko Sardasht ya Tir Saba mwaka 1366 (Juni 28, 1987), kuuawa kigaidi Shahid Saduqi hapo Tir 11 mwaka 1361 (Juni 28, 1981) na kuitungua ndege ya abiria ya Iran tarehe 12 Tir mwaka 1367 (Juni 28, 1988) na kuongeza kuwa hiyo ni mifano ya wazi kabisa ya vitendo vya kigaidi vya Marekani na vibaraka wake dhidi ya taifa la Iran. Ameongeza kuwa: Kuna baadhi ya watu wanaamini kuwa inabidi siku za mwezi wa Tir zitangazwe kuwa ni wiki ya haki binadamu za Kimarekani.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza tena kuweko udharura wa kumtambua vyema adui na kuongeza kuwa: Taifa linapaswa kuutambua kwa kina uadui wa adui ili liweze kukabiliana vilivyo na adui huyo katika vita laini kama vile katika medani za kiutamaduni, kisiasa na kijamii.
Vile vile amewalaumu watu ambao wanafanya njama za kuhalalisha vitendo viovu, vya kiuadui, vya kutisha na vya kuogofya vya Marekani na kuongeza kuwa: Wale watu ambao wanajaribu kusafisha uadui uliojaa ukhabithi na usafiri wa Marekani na baadhi ya vitimbakwiri na vibaraka wake kwa kufanya propaganda kubwa katika vyombo vya habari wajue kuwa wanaisaliti nchi na taifa.
Mwishoni mwa hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, taifa la Iran linahitajia ujumbe wenye kuleta matumaini, unaofichua ukweli wa mambo na uliojaa hamasa na shauku wa mashahidi na kuongeza kuwa: Taifa la Iran lina deni kubwa mbele ya mashahidi na familia za mashahidi na wale watu ambao wanaukana uhakika huo hawayajali maslahi ya taifa na kwa hakika ni maajnabi na ni watu baki hata kama watakuwa na utambulisho wa Kiirani.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu; Hujjatul Islam Walmuslimin Shahidi Mahallati, mwakilishi wa Fakihi Mtawala (Waliyyul Faqih) na Mkuu wa Taasisi ya Mashahidi na Masuala ya Kujitolea katika Njia ya Haki ametoa hotuba fupi na sambamba na kuwakumbuka kwa wema mashahidi wa Tir Saba amesema: Utajo na kumbukumbu za mashahidi wa Tir Saba daima ziko hai nchini Iran tofauti na wanavyotaka maadui wa Uislamu na wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Makamu wa Rais wa Iran na Mkuu wa Taasisi ya Mashahidi na Masuala ya Kujitolea katika Njia ya Haki ameongeza kuwa: Historia ya Mapinduzi ya Kiislamu imethibitisha kuwa, tukio la Tir Saba na matukio mengine mfano wake pamoja na matukio ya kuuliwa maelfu ya watu ambao ni wafuasi bora kabisa wa Mapinduzi ya Kiislamu si tu hayakusababisha kudhoofika Mapinduzi ya Kiislamu bali kumeongeza istikama, kusimama kidete, kutotetereka na kuzidi kuwa imara taifa la Iran siku baada ya siku.
 
< Nyuma   Mbele >

^