Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Aonana na Mkuu na Maafisa wa Chombo cha Mahakama Chapa
28/06/2015
 Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, alasiri ya leo (Jumapili) ameonana na mkuu na maafisa wa Chombo cha Mahakama na sambamba na kumuenzi shahidi madhlumu Ayatullah Beheshti na shahidi Quddusi ambao ni mashahidi wenye daraja kubwa wa Chombo cha Mahakama cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameutaja uhuru na taathira kubwa cha chombo hicho kuwa ni jambo lenye umuhimu mkubwa na kusisitiza kuwa: Kuna wajibu wa kukabiliana vilivyo na mambo yote yenye lengo la kutia doa uhuru cha Mahakama kama vile vitisho, kurubuni, kuoneana muhali na kushinikiza kupitia kuharibu anga ya umma kama ambavyo amesisitiza pia kwamba inabidi kuhakikisha kuwa chombo hicho hakitoki kwenye mkondo wake sahihi.
Amezitaja nguvu na uwezo kuwa ndiyo ngao kubwa ya kuweza Chombo cha Mahakama kuwa huru na kuongeza kuwa: Juhudi za chombo cha mahakama za kuhakikisha kina nguvu si juhudi za kutaka kuwa na nguvu zilizozoeleka za kisiasa na kimirengo, bali kuna maana ya kutotereka na kusimama imara kwenye kutetea haki.
Kuheshimu sheria na kuwa salama kikamilifu katika hukumu zake ni masuala mengine mawili yaliyogusiwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusu mambo muhimu yanayoweza kuifanya Mahakama kuwa huru na yenye taathira nzuri.
Ameongeza kuwa: Kuna kazi nzuri zimefanyika za kuhakikisha chombo hicho muhimu kiko salama katika hukumu zake na inabidi kuendelea na njia hiyo kwa nguvu zote kwani ufisadi wa aina yoyote ile katika Chombo cha Mahakama huandaa uwanja wa kutokea ufisadi mkubwa zaidi katika jamii.
Ayatullah Udhma Khamenei amelitaja suala la kuzuia kutokea uhalifu kuwa ni jambo jengine nyeti na muhimu kwa ajili ya Chombo cha Mahakama. Ameongeza kwa kusema: Tab'an taasisi na vyombo vingine vyote navyo vinapaswa kuwa amilifu na kulipa uzito wa hali ya juu suala hilo, lakini kwa upande wa Chombo cha Mahakama, juhudi hizo zinapaswa zifanywe maradufu, vinginevyo vitendo vya uhalifu vitaongezeka siku hadi siku na mwishowe itashindikiana kudhibiti uhalifu wote huo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja suala la kuongezeka idadi ya wafungwa kuwa ni jambo linalosikitisha sana na kuongeza kuwa: Jambo hilo linasababisha hasara katika kila upande, hasara za kifedha, madhara katika familia pamoja na madhara ya kimaadili na kijamii na inabidi kulipa uzito wa hali ya juu suala la kutafuta njia za kila namna za kuweza kulitatua tatizo hilo.
Ayatullah Udhma Khamenei ametaja mambo kadhaa ambayo yanaweza kusaidia katika kuzuia kuongezeka idadi ya wafungwa ambayo ni pamoja na kueneza utamaduni wa kupenda amani na kuishi kwa salama watu katika jamii, kuchunguza kwa kina sababu zinazopelekea kutokea mambo hayo pamoja na kuyaimarisha mabaraza ya kutatua hitilafu zinazojitokea.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitizia umuhimu wa kufanya juhudi za kurahisisha masuala ya ndoa kwa vijana na amegusia baadhi ya matatizo ya mahakama za familia kama vile "talaka ya maafikiano" na kuongeza kuwa: Mahakimu wapendwa wana wajibu wa kupunguza mambo kama hayo kwa kushirikiana na watu wazima ndani ya familia.
"Kufanya kazi kwa mpangilio na ratiba maalumu," "kuzisafisha na kuzifanyia marekebisho sheria" na "kuwa na timu maalumu na makini za kazi" ni nukta na nasaha tatu muhimu zilizotolewa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika hotuba yake hiyo.
Ayatullah Udhma Khamenei ameanza kuzitolea ufafanuzi nasaha hizo tatu kwa kusisitiza juu ya udharua wa kuweko mipangilio na ratiba maalumu katika chombo cha mahakama na kuongeza kuwa: Kutegemea ratiba iliyo wazi na iliyoratibiwa na kupangiliwa vizuri kutakisaidia Chombo cha Mahakama kufanya kazi zake kwa umakini mkubwa katika kufanikisha malengo yake na kukipa kinga chombo hicho mbele ya misuguano ya kila siku inayotokea kila upande.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amebainisha nukta ya pili yaani kuzisafisha na kuzifanyia marekebisho sheria kwa kusema: Sheria siku zote huifungulia nchi njia ya maendeleo na inapotokezea baadhi ya sheria kuwa na dosari au kugongana na sheria nyengine, inabidi sheria hizo zirekebishwe, zisidharauliwe na kupuuzwa na kwa hakika mimi siungi mkono kitendo cha aina yoyote ile cha kukwepa kuheshimu sheria.
Ayatullah Udhma Khamenei ametoa ufafanuzi kuhusu nasaha yake ya tatu muhimu zaidi ambayo ni kuwa na timu makini za kazi katika Chombo cha Mahakama na kusema: Kuna timu makini na zilizo salama ndani ya Chombo cha Mahakama na inabidi kuzilea vizuri timu hizo kwa ajili ya kufaya kazi kubwa zaidi.
Mwanzoni mwa hotuba yake, Ayatullah Udhma Khamenei ametoa mkono wa baraka na fanaka kwa mnasaba wa kuanza Wiki ya Mahakama nchini Iran na kuwaenzi mashahidi Beheshti na Quddusi kutokana na mchango wao mkubwa katika chombo hicho.
Ameashiria nafasi na shakhsia ya kipekee cha shahid Ayatullah Beheshti katika kipindi cha mapambano ya Mapinduzi ya Kiislamu na pia katika jitihada za kuiendeleza nchi baada ya kupata ushindi Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran na kuongeza kuwa: Ayatullah Beheshti alikuwa miongoni mwa watu nadra na shakhsia wenye mvuto, wenye tadibiri na wenye misimamo ya kimapinduzi na kwa hakika maisha yake yalikuwa na faida na taathira kubwa kwa Mapinduzi ya Kiislamu na kwa nchi ya Iran na kuuawa kwake shahidi pia kulikuwa ni chachu ya umoja na mshikamano katika jamii na kuzidi kupata nguvu mrengo wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Vile vile amemtaja shahid Quddusi (Mwendesha Mashtaka Mkuu wa kwanza wa Mapinduzi ya Kiislamu) kwamba alikuwa shakhsia muhimu aliyekuwa na roho ya upole na wakati huo huo shujaa na mwenye ushawishi mkubwa.
Vile vile Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezisifu kazi, nia na uendeshaji wa mambo kwa kijihadi ndani ya chombo cha mahakama katika kutekeleza majukumu yake na amesema katika kubainisha umuhimu wa chombo hicho kwamba: Chombo cha Mahakama ni moja ya nguzo tatu kuu za Iran na ndicho chombo kinachotekeleza sehemu kubwa za hukumu za Kiislamu nchini hivyo ni jambo linalotegemewa kabisa kutarajia kuona watumishi katika chombo hicho wanaongeza bidii katika kazi zao wanafanya kazi kijihadi na kuvumilia mashaka na uzito wa kila namna.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Amoli Larijani, mkuu wa Chombo cha Mahakama cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa hotuba fupi na sambamba na kuwataja kwa wema na kuwaenzi mashahidi wa tukio la Tir Saba (Juni 28, 1981) hususan shahid Ayatullah Dk Beheshti, ametoa ripoti fupi kuhusu kazi na ratiba za chombo hicho.
Ayatullah Amoli Larijani amegusia pia mambo yaliyosisitizwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusu Chombo cha Mahakama na baadaye ametaja vipaumbele sita katika kazi za chombo hicho ambavyo ni kuleta mpangilio maalumu na ulio wazi kwa ajili ya kuratibu siasa za chombo hicho na ufuatiliaji wa kina wa utekelezaji wa siasa hizo; kusimamia kazi za chombo cha mahakama; kuzuia ucheleweshaji katika uchukuaji wa hatua; kuunda timu makini na kulea nguvu kazi za kushikilia nafasi maalumu; kuzuia kutokea uhalifu na kushirikiana vizuri na mihimili mingine ya dola na kuongeza kuwa: Siasa za Chombo cha Mahakama nchini Iran zinaratibiwa kwa mujibu wa miongozo ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na kwa kuzingatia malengo ya maendeleo na mpango wa miaka mitano wa maendeleo ya Iran na kwamba baada ya kukushanywa pamoja mambo yote hayo, kumeandaliwa mpango maalumu wa kazi za miaka mitano za chombo hicho.
Mkuu wa Chombo cha Mahakama cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amegusia pia kushadidishwa usimamiaji wa kazi za majaji na wafanyakazi wa chombo hicho na kuongeza kuwa: Taasisi zote za Chombo cha Mahakama nchini zimeingia kazini hivi sasa kwa lengo la kupandisha juu kiwango cha usalama wa kiidara.
Kupunguza muda wa kufuatilia kesi katika mahakama za kutoa hukumu, kuongeza kiwango cha kustafidi vizuri zaidi na muundo wa kutoa hukumu na vile vile kufanya jitihada za kuzuia kutokea uhalifu ni mambo mengine yaliyobainishwa na Ayatullah Amoli Larijani katika hotuba yake hiyo fupi.
Mwishoni mwa mkutano huo, hadhirina wamesali sala za jamaa za Magharibi na Isha zilizosalishwa na Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.
 
< Nyuma   Mbele >

^