Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Aonana na Wahadhiri wa Vyuo Vikuu Chapa
04/07/2015
 Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Alasiri ya leo (Jumamosi) ameonana na wahadhiri elfu moja na wajumbe wa majopo ya walimu wa Vyuo Vikuu kutoka pembe zote za Iran na kuitaja nafasi ya wahadhiri wa vyuo hivyo katika kuelimisha na kulea kizazi cha watu wenye bidii, wachapa kazi, waumini wa kweli na wenye fikra za kimaendeleo kuwa haina mbadala na kusisitiza juu ya wajibu wa kuviepusha Vyuo Vikuu na michezo ya kisiasa na mambo ya pembeni pembeni yasiyo na maana akiongeza kuwa: Kasi kubwa ya kielimu iliyopo nchini Iran haipaswi kuachiwa kupungua kwa njia na sababu yoyote ile.
Katika mkutano huo uliodumu kwa zaidi ya masaa mawili, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwanza amesikiliza mitazamo na mapendekezo ya baadhi ya wahadhiri wa Vyuo Vikuu na kuzitaja taathira za kimaumbile za wahadhiri katika nyoyo na roho za wanafunzi wa Vyuo Vikuu kuwa ni fursa ya kipekee inayopaswa kutumiwa vizuri na kuwaambia wahadhiri hao kwamba: Tumieni vizuri fursa hii kubwa mno katika kulea vijana walioshikamana na dini, wenye ghera ya kitaifa, wenye shauku kubwa ya kutekeleza majukumu yao, wanamapinduzi, wachapakazi wazuri, wenye maadili mema, mashujaa, wanaojiamini na wenye matumaini na mustakbali mwema na ambao watakuwa ni sehemu muhimu yenye nguvu katika kuiletea maendeleo Iran azizi.
Vile vile amelitaja suala la kutokuwa na haja na msaada wa watu baki, kuwa na welewa sahihi kuhusu nafasi na njia ya nchi, kuwa na hisia kali na kutotetereka mbele ya jambo lolote linalotaka kutia doa uhuru wa nchi, kuwa ni sifa nyingine ya kipekee ambayo wanapaswa kuwa nayo vijana nchini.
Ameongeza kuwa: Wahadhiri wapendwa, wanapaswa kutumia mbinu na njia zao nzuri, kulea kizazi cha vijana wa namna hiyo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewataja walimu wa Vyuo Vikuu kuwa ni makamanda katika vita laini na amewakhutubu kwa kuwaambia: Waongozeni vizuri vijana wanachuo yaani ‘maafisa wa kijeshi' katika vita laini kama walivyofanya makamanda wa kijeshi wa Iran katika miaka minane ya vita vya kujihami kutakatifu (vita vilivyoanzishwa na utawala wa zamani wa Iraq dhidi ya Iran) na jitokezeni vilivyo kwenye medani ya mapambano hayo muhimu mno na yenye kina kirefu ili medani hiyo nayo iwe medani nyingine ya vita vya kujihami kutakatifu.
Aidha ameelezea kufurahishwa kwake na kuweko wajumbe 70 elfu wa majopo ya walimu wa Vyuo Vikuu nchini Iran na kuongeza kuwa: Sehemu kubwa ya wahadhiri hao ni watu waumini, walioshikamana vilivyo na dini na wenye imani thabiti na misingi ya Mapinduzi ya Kiislamu na kusisitiza kwamba, jambo hilo ni muhimu mno na ni fakhari kwa Iran.
Ayatullah Udhma Khamenei amewataka viongozi na maafisa wa Wizara ya Elimu, Utafiti na Teknolojia na wale wa Wizara ya Afya, Matibabu na Mafunzo ya Tiba kujua thamani ya kuwa na wahadhiri wa Vyuo Vikuu kama hao; waumini na wanamapinduzi na kuongeza kuwa: Watu ambao hawaogopeshwi na mashambulizi ya kuudhi na kukirihisha na wanaendelea vilivyo na kutekeleza majukumu yao muhimu bila ya kujali propaganda hizo wanapaswa kuzingatiwa na kuenziwa.
Vile vile amelitaja suala la kufanikiwa Iran kushika nafasi ya 16 kielimu duniani kuwa ni matunda ya jitihada zisizosita za miaka 10 hadi 15 iliyopita katika Vyuo Vikuu na vituo vya elimu nchini Iran na kuongeza kuwa: Kasi kubwa ya kielimu yenye kuleta shauku kubwa ambayo ni fakhari iliyopata Iran, leo hii imepungua, hivyo viongozi nchini wanapaswa kufanya hima kubwa zaidi kuhakikisha kasi hiyo inaendelea kama ilivyokuwa kabla na inaoana na mahitaji ya nchi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amechunguza kwa namna fulani sababu za kujitokeza mambo yanayopunguza kasi ya maendeleo hayo ya kielimu nchini na kulaumu vikali kuingizwa mambo ya pembeni na michezo ya kisiasa katika Vyuo Vikuu na kuongeza kuwa: Maeneo ya Vyuo Vikuu yanapaswa kuwa maeneo ya welewa wa kisiasa, weledi na maarifa ya kisiasa, lakini hayapaswi kujiingiza katika michezo ya kisiasa na masuala ya pembeni pembeni kwani kufanya hivyo ni kutoa pigo kwa Vyuo Vikuu katika kazi yake ya asili yaani ya maendeleo ya kielimu.
Ametoa mfano wa wazi kuhusu michezo ya kisiasa katika Vyuo Vikuu kwa kugusia suala la udhamini wa masomo akisisitiza kuwa kazi mbaya sana imefanyika katika suala hilo kwenye miaka ya hivi karibuni.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema: Utafiti wa kina uliofanyika katika suala hilo unaonesha kuwa, suala la udhamini wa masomo haukuwa kwa sura ile ambayo imetiwa chumvi na magazeti, lakini hata kama ilikuwa kama hivyo, ilibidi zitumike njia za sheria kuwapokonya nafasi hizo watu waliopata udhamini huo kinyume cha sheria na sio kuanza kupiga makelele na kulikuza kupindukia suala hilo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, michezo ya kisiasa ni sumu katika maeneo ya elimu na ameelezea kusikitishwa kwake kuona kuwa baadhi ya watu wamedhulumiwa katika suala hilo la udhamini wa masomo na kuongeza kuwa: Sumu iliyoingizwa kwenye Vyuo Vikuu kupitia maudhui hiyo inaonesha namna fikra za mchezo wa kisiasa zilivyojijenga kwenye vyuo hivyo na ameelezea kusikitishwa kwake kwa kuona kuwa jambo hilo limeruhusiwa kujitokeza licha ya kwamba ni kinyume cha sheria, ni kinyume na tadibiri bali pia ni kinyume na akhlaki na maadili mema.
Ayatullah Udhma Khamenei ameihusisha sehemu nyingine ya hotuba yake na udharura wa kufanya viongozi nchini Iran; jitihada kubwa za kuleta mapinduzi na mabadiliko makubwa katika masomo ya Sayansi ya Jamii nchini.
Ameongeza kuwa: Mapinduzi na mabadiliko hayo makubwa ni jambo la dharura, ni mahitaji yanayopaswa kuchemka yenyewe ndani ya Vyuo Vikuu na katika vituo muhimu nchini kama vile Baraza Kuu la Mapinduzi ya Kiutamaduni na Baraza la Mapinduzi ya Sayansi ya Jamii kama ambavyo pia ni jambo linalohitajia uungaji mkono kutoka nje ya Vyuo Vikuu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Alhamdulillah mwamko mkubwa wa ndani ya Vyuo Vikuu upo kwa taufiki ya Mwenyezi Mungu na kwamba vyombo husika vinapaswa kuhakikisha kuwa mwamko huo unaonekana kivitendo katika masomo ya Sayansi ya Jamii na kufanikisha kivitendo mambo yaliyopitishwa katika Baraza l a Mapinduzi ya Elimu ya Jamii.
Nukta ya nne iliyogusiwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika hotuba yake hiyo ni kuzingatiwa bajeti ya utafiti wa kielimu katika bajeti kuu ya nchi. Ameashiria sisitizo lake la mara kwa mara katika miaka ya huko nyuma kuhusu suala hilo na kuelezea kusikitishwa kwake na kushindwa kutekelezwa sisitizo lake hilo akiongeza kuwa: Katika hati ya malengo ya maendeleo, kumezingatiwa asilimia nne ya bajeti ya taifa iende kwenye masuala ya utafiti wa kielimu na ijapokuwa haiwezekani kulifanikisha hilo katika kipindi cha muda mfupi lakini kwa uchache asimilia mbili ya bajeti ya taifa inabidi itengwe kwenye kazi hiyo kama ambavyo bajeti hizo na vyanzo vya kifedha vya utafiti huo wa kielimu inabidi vitolewe kwa wakati unaofaa na kutumika kwenye sehemu zinazostahiki.
Nukta nyingine iliyozungumziwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika hotuba yake mbele ya wahadhiri wa Vyuo Vikuu vya Iran ni udharura wa kutekelezwa kivitendo ramani kuu ya kielimu nchini.
Ayatullah Udhma Khamenei amegusia namna wataalamu na weledi wa mambo wanavyoiunga mkono ramani kuu ya kielimu nchini na kuitaja hatua ya kwanza ya kutekelezwa kivitendo ramani hiyo kuwa ni kuifanya iwe ni kitu kilichokubalika katika jamii na kuongeza kuwa: Kama ambavyo suala la maendeleo ya kielimu nchini limekuwa ni jambo lililojikita na kuzoeleka katika jamii na kuwa mrengo wa kielimu nchini, hali inapaswa kuwa hivyo hivyo katika upande wa ramani kuu wa kielimu nchini na kwamba walimu wa Vyuo Vikuu na wakurugenzi na wanachuo nchini wanapaswa kuijua kiundani ramani hiyo na kuifanya ramani kuu ya kielimu nchini izoeleke na ijikite katika jamii.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameendelea na hotuba yake kwa kuzungumzia "Hati ya Mapendekezo ya Elimu ya Juu" na huku akiashiria wajibu wa kukamilishwa na kutekelezwa kivitendo hati hiyo amesema kuwa, mapendekezo hayo yana maana ya kutambua na kuchukua maamuzi kuhusu uwezo wa Vyuo Vikuu na aina za masomo za vyuo hivyo na baadaye kuainisha vipaumbele ambavyo inawezekana kuwekeza ndani yake kwa sura ya kipekee kwa ajili ya kufikiwa maendeleo ya kimsingi kuhusu vipaumbele hivyo.
Ayatullah Udhma Khamenei amelitaja suala la kuwa na mtazamo mpana kuhusu suala la kuongezeka kwa wingi wanachuo wa kozi za kukamilisha masomo yao kuwa ni fursa nzuri sana na ni katika nyuga muhimu za kazi za Wizara ya Sayansi, Utafiti na Teknolojia nchini na kuongeza kuwa, wizara hiyo inapaswa kuwa na mtazamo mpana na kuwa na mipangilio sahihi na uongozaji jumla wa mambo ili iweze kuelekeza matokeo ya kazi na juhudi za wanachuo wa kipindi hicho cha masomo, upande wa kutatua matatizo yaliyopo nchini kwani kama haitofanya hivyo basi vyanzo na suhula za nchi zitapotea bure.
Vile vile ameitaja nafasi ya wahadhiri na taasisi za kusimamia na kuendesha masuala ya kielimu nchini Iran katika kukabiliana na mipango ya maadui kuwa ni nafasi muhimu sana na kuongeza kuwa: Lengo la maadui la kuiwekea vikwazo Iran si miradi yake ya nyuklia na wala si masuala kama vile haki za binadamu na ugaidi, kwani maadui hao ndio vituo vikuu vya kulelewa magaidi na vitendo vilivyo dhidi ya haki za binadamu, bali lengo la maadui ni kulizuia taifa la Iran lisifikie kwenye daraja yake ya kiustaarabu inayostahiki kuwa nayo na kwamba kuna wajibu kwa taifa la Iran kujua kwa kina nafasi yake na kuendelea kwa ufakhari mkubwa na harakati yake; na katika hilo, nafasi ya wahadhiri wa Vyuo Vikuu na majimui za kielimu nchini, ni kubwa mno.

Mwanzoni mwa mkutano huo, wahadhiri saba wa Vyuo Vikuu walipata fursa ya kutoa maoni na mitazamo yao mbele ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu. Wahadhiri hao ni mabwana:
- Dk Mohammad Mehdi Nayebi - Mhadhiri kamili wa uhandisi wa umeme wa Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Sharif.
- Dk Mohammad Husain Rajabi Davani - Mkuu wa Kituo cha Utafiti wa Hadithi na Wilaya cha Chuo Kikuu cha Imam Husain Alayhis Salaam.
- Dk Mohammad Ghanadi Maragheh - Mkuu wa Kituo cha Utafiti wa Sayansi na Fani za Nyuklia na shakhsia muhimu mno katika sayansi ya nyuklia.
- Dk Husain Salimi - Mhadhiri kamili wa Chuo Kikuu cha Allama Tabatabai.
- Dk Jaafar Hezar Jaribi - Mtaalamu jamii na mhadhiri kamili wa Chuo Kikuu cha Allama Tabatabai.
- Dk Hujjatullah Abdul Maleki - Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Masomo ya Kiislamu na Uchumi.
- Pamoja na Bi Dk Sadaf Alipour - Mhadhiri msaidizi katika Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba cha Iran.
Miongoni mwa mitazamo, maoni na masuala makuu yaliyozungumzwa na wasomi hao ni pamoja na:
- Ulazima wa kutiliwa kasi ustawi wa viwanda kwa ajili ya kuzifanya kuwa na matunda kazi za utafiti wa kielimu na uzalishaji wa elimu kupitia silisila za kazi za kielimu nchini.
- Umuhimu wa kuitia nguvu sekta binafsi ya kweli.
- Udharura wa kubuniwa stratijia na mkakati wa masuala ya viwanda nchini.
- Udharura wa kutambulishwa na kuimrishwa usuli na misingi ya kifikra ya Imam Khomeini na ya Kiongozi Muadhamu na kufanywa kuwa misingi mikuu na ramani ya njia ya Mapinduzi ya Kiislamu.
- Wajibu wa kulea wataalamu waliobobea katika fikra za Imam Khomeini - rahimahullah - kwa ajili ya kukabiliana na njama za kupotoshwa fikra zake.
- Kubainishwa maendeleo muhimu ya Iran katika sekta ya nyuklia na kusisitiziwa udharura wa kufanyika utafiti na ustawi kwenye sekta hiyo.
- Udharura wa kutangazwa Uislamu wa Kishia, wa kimantiki na wenye kujenga ustaarabu na kueneza utamaduni wa kuipa umuhimu elimu katika kukabiliana na njama za kutumiwa Uislamu kwenye mambo ya kikatili na ya uharibifu.
- Udharura wa kuangaliwa upya masomo ya Sayansi ya Jamii kwa kuzingatia misingi mipya ya kila leo, kupitia kuzipa umuhimu thamani za mambo mbali mbali na kwa namna yenye kuleta faida.
- Udharura wa kuwa na mtazamo wa pamoja katika suala zima la masomo ya Sayansi ya Jamii.
- Ulazima wa kutolewa mafunzo kuhusiana na miamala ya kiutaalamu na kunyanyua ubora wa kazi ya uelimishaji nchini.
- Kusisitizia umuhimu wa mbinu mpya za matibabu kwa kutegemea teknolojia za kisasa.
- Ulazima wa kudhaminiwa nguvu kazi za watu weledi wa mambo katika utekelezaji wa mpango wa mapinduzi na mabadiliko makubwa ya usalama wa kiafya nchini.
- Kutumiwa uwezo wote mkubwa uliopo wa kiuchumi nchini kama vile sekta ya kilimo.
- Udharura wa kutumiwa vizuri na kwa njia inayofaa watu wenye vipaji nchini.
- Kutumia vizuri fursa ya vikwazo kwa ajili ya kukata kikamilifu kutegemea fedha zitokanazo na kuuza nje mafuta.
- Udharura wa kulipa mazingatio maalumu suala la utamaduni katika uchumi wa kimuqawama na wa kusimama kidete kwa kuzingatia hatua za utoaji elimu na za uelimishaji kwenye uwanja huo.

 
< Nyuma   Mbele >

^