Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Aonana na Rais na Baraza lake la Mawaziri Chapa
14/07/2015
 Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu leo jioni (Jumanne) ameonana katika mkutano wa Kiramadhani na Rais pamoja na Baraza lake la Mawaziri na sambamba na kubainisha baadhi ya miongozo mitukufu na inayofungua njia iliyomo kwenye usia wa Amirul Muminin Imam Ali AS kwa Malik Ashtar amesisitiza kuwa: Nguvu za kiroho, kimaanawi na kifikra ndiyo njia kuu ya kuweza kutatua matatizo yanayojitokeza na kwamba kutaamali na kuzama ndani ya Nahjul Balagha ya Bwana wa wacha Mungu, kunamfanya mtu kuwa na nguvu za namna hiyo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia matamshi ya mheshimiwa Rais mwanzoni mwa mkutano huo kuhusiana na matokeo ya mazungumzo ya nyuklia na ameishukuru timu ya mazungumzo ya nyuklia ya Iran kutokana na juhudi za kweli, kujitolea na kusimama imara kwenye mazungumzo hayo.
Baada ya hapo ameashiria sifa za kipekee na shakhsia na nafasi ya aina yake aliyokuwa nayo Malik Ashtar mbele ya Amirul Munin, Imam Ali AS na kuongeza kuwa: Imam Ali bin Abi Talib Alayhis Salaam, alimwamini na kuamua kumkabidhi majukumu shakhsia huyo na hilo ni jambo muhimu na la kuzingatiwa sana.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amebainisha pia majukumu ya viongozi yaliyoainishwa kwenye amri ya kukabidhi majukumu aliyoitoa Amirul Muminin, Imam Ali AS kwa Malik Ashtar na kuongeza kuwa: Kuchukua kodi na haki za serikali kutoka kwa wananchi, kuwalinda wananchi na ardhi yao, kuiongoza jamii kwenye matendo mema na kuijenga na kuistawisha ni majukumu manne makuu ambayo Bwana wa wacha Mungu alimkabidhi Malik Ashtar katika barua aliyompa.
Ayatullah Udhma Khamenei ameyataja masuala kama kuwausia viongozi wa Kiislamu kumcha Mwenyezi Mungu katika mazingira na mahala popote walipo, kulipa uzito wa hali ya juu kabisa suala la kutekeleza mambo ya faradhi, ya sunna na mustahabu, kuamini nusra ya Mwenyezi Mungu katika moyo, katika ulimi na katika matendo na kuidhibiti nafsi mbele ya hawaa na matamanio yote ya kinafsi kuwa ni katika amri na miongozo muhimu ambayo Bwana wa wacha Mungu alimuusia Malik Ashtar katika barua yake hiyo kama njia ya kumuandalia mazingira ya kujiimarisha kiimani na kuilea nafsi katika mambo mema.
Kuwa na mtazamo wa kiinsafu na wa kiadilifu kuhusu viongozi waliotangulia ni nukta nyengine iliyotiliwa mkazo na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa kutegemea miongozo na mafundisho ya Imam Ali Alayhis Salaam.
Ameyataja matendo mema kuwa ni akiba bora kabisa katika kipindi cha uongozi kwa mtu yeyote yule na kuongeza kuwa, wananchi hawafanyi makosa katika kujua uhakika wa mambo kwa kupitia kufikiri, kutaamali na kujumuisha pamoja na mambo mbali mbali hivyo kupitia misimamo na mitazamo kama hiyo, wananchi wanaweza kuelewa kiongozi gani ni mwema na kiongozi gani si mwema.
Kuichunga kwa nguvu zote nafsi na kuizuia kupotoka na kupotea na kutanguliza majukumu ya Mwenyezi Mungu mbele ya kitu chochote kingine ni nasaha nyengine zilizotolewa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu wakati alipokuwa anatoa ufafanuzi kuhusu miongozo ya kiuendeshaji nchi ya Amirul Munin AS na kuongeza kuwa: Imam wetu mtukufu (Imam Khomeini - quddisa sirruh) alikuwa ni dhihirisho la wazi kabisa la kufanyia kazi nasaha na miongozo hiyo ya Imam Ali AS.
Ayatullah Udhma Khamenei ameyataja masuala kama kuwapenda watu kwa udhati wa moyo, na kuwapenda na kuamiliana nao kwa njia nzuri na ya huruma kuwa ni miongoni mwa miongozo mitukufu ya Imam Ali AS kwa Malik Ashtar na kuongeza kuwa: Kwa mujibu wa amri ya Amirul Munin, inatakiwa kuwasamehe watu pale wanapoteleza na wanapokosea isipokuwa katika mambo ambayo yamechupa mipaka ya Mwenyezi Mungu au inapofikia hatua ya mtu kuupiga vita Uislamu na serikali ya Kiislamu.
Mwishoni mwa hotuba yake, Ayatullah Udhma Khamenei amesma kuwa, miongozo na nasaha za Imam Ali bin Abi Talib Alayhis Salaam ni hazina kubwa sana ya kiutamaduni. Vile vile amewashukuru watumishi hao serikali kwa kazi kubwa wanazozifanya akimuomba Mwenyezi Mungu awape taufiki kwenye kazi zao hizo.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Hujjatul Islam Walmuslimin Hassan Rouhani, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amegusia matokeo ya mazungumzo ya nyuklia na kumshukuru sana Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kutokana na uungaji mkono wake na miongozo yake ya busara kwa serikali na kwa timu ya mazungumzo ya nyuklia na kuelezea matumaini yake kuwa, suala hilo litaandaa uwanja wa kumalizwa mashinikizo yote na kuondolewa tuhuma zote zisizo sahihi za maadui dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu na hatimaye kuleta harakati mpya katika njia ya maendeleo na ustawi wa Iran.
Rais Rouhani ameendelea na hotuba yake hiyo fupi kwa kutoa ripoti kuhusu kazi zilizofanywa na serikali yake hadi hivi sasa. Amegusia mafanikio pamoja na matatizo iliyokumbana nayo serikali yake katika kipindi cha miaka miwili iliyopita na kusema kwamba, kuwa na uhusiano wa karibu na majirani na kulitilia hima suala la kuendelea na mazungumzo ya nyuklia ni miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na serikali yake katika upande wa siasa za kigeni.
Ameongeza kuwa: Katika hali ambayo eneo hili limekumbwa na machafuko na vitendo vya kigaidi, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa ikiziunga mkono nchi ambazo zimekumbwa na mgogoro wa ugaidi na kwamba itandelea mbele na njia hiyo.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aidha amesema kuhusiana na masuala ya kiuchumi kwamba, kuutoa uchumi wa nchi kutoka katika hali ya kuzorota, kubadilisha uchumi hasi kuwa ustawi chanya, kudhibiti mfumuko wa bei, kupunguza kiwango cha kuagizia ngano kutoka nje pamoja na kuongeza kiwango cha kusafirisha nje bidhaa zisizo za mafuta ni katika mafanikio ya serikali yake na kuongeza kuwa, kuna haja ya kuweko uwekezaji na kupewa kipaumbele teknolojia kwa ajili ya kutatua matatizo ya nafasi za kazi na kukuza uchumi.
Amesema kuwa, deni kubwa la serikali kwa Benki Kuu na mashirika binafsi ni matatizo yanayotokana na kutolewa pesa taslimu kama ruzuku za serikali kwa wananchi, ukosefu wa kazi, kustafidi kwa kiwango cha chini na mambo mbali mbali, kuweko taasisi za kutoa itibari zisizoruhusiwa, uchache wa maji na kupungua vyanzo vya chini ya ardhi, ukame na masuala ya kimazingira pamoja na kupungua bei ya mafuta kuwa ni miongonimwa matatizo inayokabiliana nayo serikali yake.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa serikali inafanya jitihada zake zote kwa ajili ya kutatua matatizo ya wananchi na kuongeza kuwa: Kuna haja ya kuweko ushirikiano wa karibu baina ya mihimili mitatu mikuu ya dola (Serikali, Bunge na Mahakama) ili kupitia ushirikiano huo, iwezekane kupiga hatua zilizobakia kwa kasi kubwa zaidi.
 
< Nyuma   Mbele >

^