Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Sala ya Idul Fitr iliyosalishwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Chapa
18/07/2015
 Taifa lililoshikamana, lenye umoja na lililoimarika kiimani la Iran, leo limetekeleza ibada ya Sala ya Idul Fitr ikiwa ni katika kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kulipa taufiki ya kutekeleza ibada za funga na kujijenga kinafsi wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani. Wananchi wa Iran katika kona zote za nchi wamefanya "Sijdatush Shukr" ili kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwapa taufiki hiyo na wametekeleza ibada ya Idul Fitr huku wakimuomba Allah aendelee kuwamiminia rehema Zake na kulipa taifa lao taufiki na saada ya duniani na Akhera. Lulu na johari ya ibada hiyo tukufu imefana katika jiji la Tehran wakati Waislamu wa mji mkuu wa Iran waliposhiriki kwa wingi mno kwenye Sala hiyo iliyosalishwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Udhma Khamenei kwenye eneo la "Musalla."
Katika khutba ya kwanza ya Sala hiyo, Ayatullah Udhma Khamenei ametoa mkono wa baraka na fanaka kwa taifa la Iran na kwa Waislamu wote duniani kwa mnasaba wa kuwadia sikukuu ya Idul Fitr na kusema kuwa, mwezi wa Ramadhani mwaka huu kwa hakika ulikuwa ni mwezi wa kumiminika baraka za Mwenyezi Mungu kwa taifa la Iran kwa maana halisi ya neno.
Ameongeza kuwa: Kufunga saumu katika siku za joto kali za kipindi cha joto, kufanyika mahafali ya kila namna ya Qur'ani Tukufu, kushiriki kwa wingi Waislamu wa Iran kwenye dua, tawassul na kunyenyekea kwa Mwenyezi Mungu, vitanga vya chakula chepesi na cha kimaskini cha futari katika misikiti, mabarabarani na kwenye maeneo ya umma na hatimaye maandamano makubwa ya Siku ya Kimataifa ya Quds, ni miongoni mwa ishara za wazi za baraka hizo za Mwenyezi Mungu.
Ameongeza kuwa: Njia sahihi ya kulitambua taifa la Iran ni kuzingatia mambo kama hayo, mambo ambayo yanayathibitishia mataifa mengine kuwa hivi ndivyo lililovyo taifa la Iran katika upande wa ibada na hivyo ndivyo lilivyo katika medani ya kupambana na uistikbari na ubeberu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia nara na kaulimbiu za "mauti kwa Israel" na "mauti kwa Marekani" zilizotolewa na wananchi wa Iran katika maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds (Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani) na kuongeza kuwa: Wale wanaotaka kujua msimamo adhimu wa harakati ya taifa la Iran waangalie kaulimbiu na nara za namna hiyo wasiangalie watu baki na mabeberu wanasema nini kuhusu taifa hili ingawa hata hivyo inasikitisha kuona kuwa hata ndani ya Iran kuna baadhi ya watu wenye welewa potofu wanakariri matamshi hayo hayo ya mabeberu.
Katika khutba ya pili ya Sala ya leo ya Idul Fitr, Ayatullah Udhma Khamenei amegusia matukio ya kusikitisha katika eneo la Mashariki ya Kati na kuongeza kuwa: Inasikitisha kuona kwamba mikono miovu isiyo na baraka yoyote imeifanya Ramadhani ya mwaka huu kuwa chungu, ngumu na nzito kwa wananchi wengi wa huko Yemen, Bahrain, Palestina na Syria na kwa hakika masuala kama hayo ni muhimu sana kwa taifa la Iran.
Ayatullah Udhma Khamenei ameihusisha sehemu kubwa ya khutba hiyo ya pili ya Sala ya Idul Fitr kwa kuzungumzia nukta kadhaa kuhusu kadhia ya nyuklia. Katika nukta ya kwanza, amewashukuru maafisa wa Iran waliondesha mazungumzo hayo marefu na magumu na kuishukuru timu ya Iran ya mazungumzo ya nyuklia kwa jitihada zake kubwa katika uwanja huo.
Ameongeza kuwa: Matini iliyoandaliwa ya mazungumzo hayo inabidi ipitie kwenye mkondo wake ulioainishwa ya kisheria lakini tab'an maafisa wa Iran walioshiriki kwenye mazungumzo hayo watalipwa malipo mema na Mwenyezi Mungu, ni sawa matini hiyo itapasishwa au haitopasishwa.
Aidha Ayatullah Udhma Khamenei ‘amewakhutubu' kwa kusisitiza maafisa wa Iran wanaohusika na kuitalii na kuidurusu matini iliyoandaliwa ya nyuklia akiwaaambia: Fanyeni kazi zenu kwa umakini na kina cha hali ya juu kwa kuzingatia maslahi ya nchi na manufaa ya taifa ili matokeo ya umakini wenu huo wa hali ya juu yaweze kuliletea ufakhari taifa na kumridhisha Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itakabiliana na njama zozote za kuitumia vibaya matini hiyo ya nyuklia na kuongeza kuwa: Kamwe hatutoruhusu kutiwa doa misingi mikuu ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, ni sawa tu, matini hiyo itakuwa imepasishwa au haikupasishwa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia anga ya vitisho iliyopo hivi sasa na namna maadui walivyoelekeza njama zao kwenye masuala ya kiulinzi ya Iran na kusema kuwa: Kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu, nguvu zetu za kiulinzi zitazidi kuimarika na mipaka ya usalama ya nchi yetu italindwa vizuri na kwamba Jamhuri ya Kiislamu kamwe haitopiga magoti mbele ya siasa za kujikumbizia upande wao kila kitu madola ya kibeberu.
Kuendelea kuwaunga mkono marafiki wa Jamhuri ya Kiislamu katika eneo hilo ni nukta nyingine iliyobainishwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu wakati alipozungumzia kadhia ya nyuklia.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema: Taifa la Iran halitaacha kuyaunga mkono mataifa madhlumu ya Palestina, Yemen, Bahrain pamoja na mataifa na serikali za Syria na Iraq wakiwemo pia mujahidina wa kweli wa Lebanon na Palestina, ni sawa tu matini hiyo ya nyuklia - baada ya kupitia mkondo wake wa kishseria nchini Iran - itapitishwa au haitopitishwa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, kwa hali yoyote ile, siasa za taifa na za mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haziwezi kubadilika kuhusiana na Marekani.
Ameongeza kuwa: Sisi hatuwezi kuwa na mazungumzo yoyote yale na Marekani kuhusu masuala ya pande mbili, ya kieneo na kimataifa, isipokuwa katika masuala ya dharura mno kama hili la nyuklia, suala ambalo tumewahi kulifanya pia huko nyuma hata kabla ya kuanza mazungumzo ya nyuklia.
Amezikosoa vikali siasa za Marekani za kuunga mkono utawala wa Kizayuni unaomwaga damu za watoto wadogo na pia siasa zake za kuwaita mujahidina wa kweli wa Hizbullah wanaojitolea kila chao kwa ajili ya ukombozi wa nchi yao kuwa eti ni magaidi na kuongeza kuwa: Siasa zetu katika eneo la Mashariki ya Kati zinatofautiana kwa daraja 180 na siasa za Marekani, hivyo ni vipi tunaweza kukaa pamoja na kuzungumzia masuala hayo?
Ayatullah Udhma Khamenei ameendelea kuzungumzia kadhia hiyo ya nyuklia kwa kugusia majigambo ya hivi karibuni ya Wamarekani na kuongeza kuwa: Siku hizi wanasiasa wa kike na wa kiume wa Marekani wanalazimika kutoa maneno ya majigambo ili kutatua matatizo yao ya ndani, na ukweli ni kuwa maneno ya hayo yanabakia kuwa majigambo tu, hayana ukweli ndani yake.
Ametoa mfano mmoja wa majigambo hayo ya pale viongozi wa Marekani walipodai kuwa wameizuia Iran isizalishe silaha za nyuklia na kusema kuwa: Sisi miaka mingi nyuma tulitoa fatwa kwa msingi wa mafundisho matukufu ya Uislamu na kusema kuwa, ni haramu kuzalisha silaha za nyuklia na dini yetu tukufu inatuzuia kutengeneza silaha hizo za mauaji ya umati, lakini pamoja na yote hayo Wamarekani ijapokuwa baadhi ya wakati wanatangaza kuwa fatwa hiyo ni muhimu sana, lakini katika propaganda na majigambo yao ya uongo wanadai kuwa, wameweza kuondoa tishio lililokuwepo kwa eti kuizuia Iran kutengeneza silaha za nyuklia.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Viongozi wa sasa hivi wa Marekani wanazungumzia suala la kupigishwa magoti Iran, tab'an marais watano wa Marekani waliopita huko nyuma baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran nao pia walikuwa na ndoto hizo hizo, lakini leo hii baadhi yao wameshakufa na wengine wamepotea kwenye historia na nyinyi viongozi wa hivi sasa wa Marekani pia mtabakia katika ndoto zenu hizo hizo zisizoagulika - za kutaka kuipigisha magoti Iran.
Ayatullah Udhma Khamenei amezungumzia pia namna Rais wa hivi sasa wa Marekani anavyokiri makosa kadhaa yaliyofanywa na viongozi waliomtangulia kuhusu Iran yakiwemo mapinduzi ya kijeshi ya "Mordad 28" (Agosti 19, 1953) na uungaji mkono wa Marekani kwa Saddamu Hussein na kuongeza kuwa: Hiyo ni sehemu ndogo mno ya makosa ya Marekani na kuna makosa mengine mengi ambayo hadi hivi sasa Wamarekani wanakwepa kuyakiri.
Aidha ametoa nasaha kwa viongozi wa Marekani waachane na makosa yao ya hivi sasa ili viongozi wa siku za usoni wa nchi hiyo wasije na wao wakalazimika kukiri makosa ya viongozi wa sasa hivi wa nchi hiyo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Katika kipindi cha karibu miaka 12 nchi sita kubwa duniani zimekuwa zikijaribu kuishinikiza Iran iache kufuatilia teknolojia ya nyuklia na huku baadhi yao wakisema kuwa, lengo lao ni kuangamiza kabisa miradi ya nyuklia nchini Iran lakini leo hii zimelazimika kukubali maelfu ya mashinepewa zifanye kazi kuendeleza miradi ya nyuklia nchini Iran ikiwa ni pamoja na Iran kuendelea na utafiti na kustawisha miradi yake hiyo tena ndani ya Iran na jambo hilo halina maana nyengine isipokuwa kuonesha nguvu na uimara wa kupigiwa mfano wa taifa la Iran.
Amesema, uwezo na nguvu zinazozidi kuongezeka siku hadi siku za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zinatokana na muqawama na kusimama kidete taifa pamoja na vipaji na ubunifu wa kupigiwa mfano wa wataalamu azizi wa Iran na ameitumia fursa hiyo kuwashukuru mashahidi wa nyuklia wa Iran na kuziombea subira na uvumilivu familia za wataalamu hao. Amesema: Mwenyezi Mungu alimiminie neema Zake taifa linalosimama imara kiasi chote hiki katika kupigania haki zake.
Mwishoni mwa khutba ya pili ya Sala ya Idul Fitri, Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria matamshi ya Rais wa hivi sasa wa Marekani aliyedai kuwa ana uwezo wa kuliangamiza na kulimaliza nguvu jeshi la Iran na ‘kumkhutubu' Rais huyo akimwambia: Hata waliokutangulia nao walikuwa wakitoa matamshi hayo ya majigambo na majisifu lakini wameondoka na ndoto zao.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameendelea ‘kuwakhutubu' viongozi wa Marekani akiwaambia: Sisi hatupendi kutokea vita vyovyote vile, na kamwe hatutakuwa wa kwanza kuanzisha vita, lakini kama vita vitatokea basi atakayepata kipigo na kushindwa vibaya kwenye vita hivyo ni Marekani mchokozi na mtenda jinai.
 
< Nyuma   Mbele >

^