Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Kiongozi Muadhamu Aonana na Viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu na Mabalozi wa Nchi za Kiislamu Chapa
18/07/2015
Supreme Leader's Speech in Meeting with Government Officials and Ambassadors of Islamic CountriesAyatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, leo asubuhi (Jumamosi) ameonana na majimui ya viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu, mabalozi wa nchi za Kiislamu waliopo Tehran pamoja na matabaka mbali mbali ya wananchi wa Iran na kuutaja umoja na mshikamano kuwa ni tiba ya matatizo yote ya ulimwengu wa Kiislamu na huku akisisitiza kuwa vita vya kimadhehebu na kikabila vilivyopo kwenye eneo la Mashariki ya Kati hivi sasa ni mpango wa mabeberu na ni vita walivyotwishwa wananchi wa eneo hili kwa lengo la kuyasahaulisha mataifa ya Waislamu umuhimu wa kupambana na utawala wa Kizayuni wa Israel na kuongeza kuwa: Siasa za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika eneo hili zinatofautiana kikamilifu na siasa za madola ya kibeberu na kiistrikbari yakiongozwa na Marekani na kwamba Iran haiiamini hata chembe Marekani kwani viongozi wa Marekani si wakweli hata kidogo na hawana hata punje ya isnafu.
Ametoa mkono wa baraka na fanaka kwa mnasaba wa maadhimisho ya sikukuu ya Idul Fitr na kugusia hali ya kusikitisha iliyopo katika ulimwengu wa Kiislamu na kukosekana umoja na mshikamano katika ulimwengu huo akisisitiza kuwa: Mifarakano na mizozo iliyopo hivi sasa katika eneo hili si ya kawaida, bali ni ya kutwishwa na kupandikizwa na kwamba maulamaa, wasomi, viongozi wa madola ya Kiislamu, wanasiasa, watu wenye vipaji na watu muhimu wenye ushawishi katika ulimwengu wa Kiislamu wana wajibu wa kuwatambua vyema wasaliti wa umma wa Kiislamu wanaoeneza mifarakano na mizozo hiyo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa ufafanuzi zaidi kuhusu kutokuwa kwake za kawaida na kuwa kwake za kupandikizwa hitilafu na mizozo ambayo haijawahi kushuhudiwa mfano wake katika ulimwengu wa Kiislamu ambao kwa muda mrefu Waislamu walikuwa wakiishi wote kwa usalama, kwa mapenzi na udugu bila ya kujali tofauti ndogo ndogo zilizopo baina yao Waislamu wa Kisuni na Kishia katika eneo hili na kuongeza kuwa: Lau kama umma wa Kiislamu ungelikuwa kitu kimoja na lau kama ungelishikamana na mambo mengi yanayowaunganisha, basi bila ya shaka yoyote umma huo ungelikuwa na nguvu kubwa za kisiasa duniani, lakini madola ya kibeberu yanaeneza fitna, mizozo na mifarakano katika umma wa Kiislamu ili yaweze kuulinda utawala wa Kizayuni wa Israel.
Ayatullah Udhma Khamenei amegusia namna Waislamu wanavyouchukia vibaya utawala wa Kizayuni licha ya kuweko baadhi ya tawala za nchi za Waislamu zinazoshirikiana na utawala huo pandikizi na kuongeza kuwa: Madola ya kibeberu yanashirikiana na baadhi ya watu wasio makini katika baadhi ya tawala za nchi za Waislamu ili kuwasahaulisha Waislamu hatari za utawala wa Kizayuni kupitia kupanga na kuendesha vita vya kimadhehebu na kuunda magenge yanayotenda jinai kama vile al Qaida na Daesh.
Vile vile ameashiria namna baadhi ya viongozi wa Marekani wanavyokiri jinsi serikali ya nchi hiyo ilivyohusika katika kulianzisha na kulitia nguvu kundi la Daesh, na kuyataja madai ya Marekani ya kuanzisha muungano dhidi ya Daesh kuwa ni jambo lisiloingilika akilini na ambalo halikutarajiwa kabisa na kusisitiza kwamba: Siasa za madola ya kibeberu katika eneo la Mashariki ya Kati ni za usaliti wa waziwazi na kila mmoja anapaswa kutambua vyema suala hilo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Siasa za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika eneo hili ni tofauti kikamilifu na siasa za madola ya kiistikbari na hapo hapo ameashiria kadhia ya Iraq na kusema: Siasa za mabeberu nchini Iraq ni kutaka kuipindua serikali iliyoingia madarakani kwa kura za wananchi na pia kuzusha mapigano baina ya Waislamu wa Kishia na Kisunni na hatimaye kuigawa vipande vipande Iraq, lakini siasa za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusiana na Iraq ni kuiunga mkono na kuitia nguvu serikali iliyochaguliwa na wananchi, kuisaidia serikali hiyo kupambana na mambo yote yanayosababisha vita vya ndani, kusaidia jitihada za kupambana na mizozo na pia kulindwa ardhi nzima ya Iraq.
Ayatullah Udhma Khamenei aidha amezungumzia kadhia ya Syria kwa kusema: Siasa za mabeberu nchini Syria ni za kutwisha mambo ambayo hayatakiwi na wananchi wa nchi hiyo pamoja na kutaka kuipindua serikali ya nchi hiyo ambayo imesimama kidete kupambana wazi wazi na utawala wa Kizayuni wa Israel, lakini siasa za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusiana na Syria ni kwamba serikali ambayo imesimama imara ikitekeleza kivitendo kaulimbiu ya kupambana na Wazayuni ni muhimu mno katika ulimwengu wa Kiislamu.
Vile vile amesisitiza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haipiganii maslahi yake binafasi katika masuala ya eneo hili kama vile Iraq, Syria, Yemen, Lebanon na Bahrain bali inaamini kuwa, wananchi wa nchi hizo ndio waamuzi wakuu wa mambo ya nchi zao na yeyote mwengine hana haki ya kuingilia masuala yao ya ndani.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia namna siasa za madola ya kiistikbari zinavyopingana kikamilifu na siasa za mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu kuhusiana na Lebanon na kuongeza kuwa: Mfumo wa kibeberu unaoongozwa na Marekani ulinyamazia kimya kutekwa na kukaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Kizayuni, sehemu kubwa ya ardhi ya Lebanon ikiwa ni kuonesha madola hayo kuridhishwa na jambo hilo, lakini mara baada ya kuundwa kundi la muqawama, la watu waumini na wanaojitolea kwenye njia ya haki na kuwa kundi bora kabisa la wananchi waliojitolea kulinda ardhi yao duniani mbele ya uvamizi wa Wazayuni na kufanikiwa kuwafukuza wavamizi hao katika ardhi yao ya Lebanon, madola hayo ya kibeberu yamelipachika jina la ugaidi kundi hilo na muda wote yanafanya njama ya kuliangamiza kundi hilo la muqawama.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza pia kuwa, sababu inayoifanya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iunge mkono muqawama wa Lebanon ni ushujaa, kujitolea na kusimama imara kikweli kweli wananchi wa nchi hiyo mbele ya wavamizi wa nchi yao na kuongeza kuwa: Wamarekani wanadai kuwa muqawama wa wananchi wa Lebanon ni ugaidi na wanadai kuwa Iran inaunga mkono ugaidi kutokana na kuiunga mkono Hizbullah ya Lebanon wakati ambapo magaidi wa kweli ni hao hao Wamarekani wenyewe ambao ndio walioanzisha kundi la kigaidi la Daesh na kuwaunga mkono Wazayuni makhabithi na maafiriti. Hivyo ni Wamarekani ndio wanaopaswa kulaumiwa kwa kuunga mkono kwao ugaidi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia pia suala la Yemen na namna siasa za madola ya kiistikbari zinavyokinzana kikamilifu na siasa za mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuongeza kuwa: Huko Yemen, Marekani inamuunga mkono rais ambaye aliamua kujiuzulu katika kipindi nyeti na kigumu kabisa nchini mwake ili azidishe mzozo wa kisiasa nchini humo na baadaye akkimbilia nchi nyingine na kuitaka nchi hiyo iwashambulie watu wake na kufanya mauaji ya kutisha dhidi wananchi wasio na hatia wa Yemen wakiwemo watoto wadogo na pia Marekani inashirikiana na utawala wa kidikteta kabisa ambao hauruhusu watu wake hata kutaja tu jina la uchaguzi, lakini wakati huo huo inadai Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo kuanzia kidoleni hadi utosini mwake imeundwa kwa sura ya uchaguzi, demokrasia na kura za wananchi, kuwa eti ni utawala wa kidikteta.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kuwa: Kiujumla ni kwamba wanasiasa wa Marekani hawana insafu hata chembe katika matamshi yao na wanakanusha uhakika wa wazi kabisa kwa kiburi na jeuri kubwa.
Vile vile amesema: Hiyo ndiyo sababu inayotufanya tuseme kwa kusisitiza kuwa, Wamarekani si watu wa kuwaamini kwani si wa kweli hata kidogo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Hata katika hili jaribio na mtihani mgumu wa mazungumzo ya nyuklia, ambapo Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na wahusika wengine wote wamefanya jitihada kubwa ndani yake, tumeona mara chungu nzima namna Wamarekani wasivyo wakweli. Lakini kwa bahati nzuri viongozi wetu wamekabiliana nao vizuri na katika baadhi ya mambo wamekabiliana nao kimapinduzi na kilichobakia sasa ni kusubiri na kuona hatima ya suala hilo itakuwa vipi.
Ayatullah Udhma Khamenei vile vile amesisitiza kuwa, tiba na utatuzi wa matatizo ya ulimwengu wa Kiislamu na pia kwa kila nchi ya Kiislamu kipeke yake, ni kulinda umoja na mshikamano akisisitiza kuwa: Taifa la Iran nalo lina wajibu wa kuwa kitu kimoja na kwamba masuala ya nyuklia yasiwe sababu ya kuzuka mivutano nchini kwani kadhia ya nyuklia inaendelea kufuatiliwa na maafisa husika na wote wanapigania maslahi na manufaa ya taifa.
Vile vile ameashiria njama kubwa zinazofanywa na vyombo vya habari vya mabeberu za kujaribu kuzusha mizozo na mifarakano nchini Iran na kusisitiza kuwa: Njia pekee ya kukabiliana na njama hizo ni kudumishwa taqwa na ucha Mungu wa kitaifa na wa jamii nzima na kujiwekea kinga ya ndani kupitia kuongeza nguvu zetu za ndani ya nafsi zetu kwa kujijenga kiimani, kielimu, kimaendeleo ya viwanda na kujiimarisha kiutamaduni.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Hujjatul Islam Walmuslimin Rouhani, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa hotuba fupi na sambamba na kutoa mkono wa baraka za sikukuu ya Idul Fitr kwa Waislamu wote duniani amesema kuwa, mwezi wa Ramadhani ni mwezi wa kujaribiwa imani zetu, ni mwezi wa kusimama kidete, ni mwezi wa muqawama na ni mwezi wenye manufaa mengi mno.
Amesema: Mwezi wa Ramadhani mwaka huu ulikuwa ni mwezi wa kupendana, mwezi wa kuwa na sauti na kauli moja na ulikuwa ni mwezi wa kurejea kwenye maumbile safi ya kibinadamu.
Pia amebainisha kuwa, katika mwezi wa Ramadhani wa mwaka huu, muqawama wa miaka 12 wa taifa la Iran mbele ya madola ya kibeberu umezaa matunda kwa dua za kheri za wananchi na kuongeza kuwa: Serikali kwa kutegemea muongozo na ramani ya njia iliyochorwa na muqawama na irada ya kweli ya taifa la Iran na kwa miongozo ya hekima na busara ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na kwa uungaji mkono wa vyombo na taasisi zote za dola ya Kiislamu na vile vile kwa jitihada na bidii kubwa ya taifa katika uga wa kidiplomasia, imeweza kulinda haki za taifa kubwa la Iran mbele ya mabeberu wa dunia.
Rais Rouhani amebainisha pia kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imearifisha kwa walimwengu nguvu nyingine mpya inayojulikana kwa jina la uwezo wa kidiplomsia na nguvu za mazungumzo kama ambavyo ameashiria pia matukio ya eneo la Mashariki ya Kati na kusema kuwa, Ramadhani ya mwaka huu ilikuwa ngumu na nzito kwa majirani zetu na nchi za eneo hili kuanzia nchi za Iraq, Syria na Yemen, hadi Palestina, Lebanon, Afghanistan na Pakistan.
Amesema: Msimamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kuwaunga mkono wanyonge na watu wote wanaodhulumiwa na kusimama imara kupambana na dhulma ya aina yoyote ile.
 
< Nyuma   Mbele >

^