Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Majibu ya Kiongozi Muadhamu kwa Barua ya Rais Rouhani Kuhusu Mazungumzo ya Nyuklia Chapa
15/07/2015
Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amejibu barua ya Hujjatul Islam Walmuslimin Hassan Rouhani, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu mazungumzo ya nyuklia akimshukuru kwa juhudi zake kubwa pamoja na jitihada za kupigiwa mfano za timu ya mazungumzo ya nyuklia ya Iran na kusema kuwa, kuweza kuyafikisha mwisho mazungumzo hayo ni hatua muhimu. Vile vile ameashiria namna baadhi ya wanachama wa kundi la 5+1 lililofanya mazungumzo na Iran wasivyo na mwamana na kusisitiza kuwa: Kuna wajibu wa kuhakikisha kwamba matini iliyopatikana ya nyuklia inaingizwa kikamilifu katika mkondo wake wa kisheria kama ilivyopangwa na iwapo itapasishwa kuchukuliwe hatua za kuuzuia upande wa pili usije ukakwepa kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa.
Matini kamili ya majibu ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa barua ya Rais Hassan Rouhani kuhusu mazungumzo ya nyuklia ni kama ifuatavyo:
 
Bismillahir Rahmanir Rahim
Janab Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran
Kwanza pokea salamu na shukrani zangu kutokana na juhudi zako kubwa. Awali ya yote ni wajibu kwangu kuishukuru kwa udhati wa moyo wangu timu yetu ya mazungumzo ya nyuklia kutokana na jitihada zake kubwa katika mazungumzo hayo nikimuomba Mwenyezi Mungu awalipe wote malipo mazuri. Baada ya hapo napenda kusema kuwa, suala la kufikishwa mwisho mazungumzo hayo ni hatua nzuri na muhimu, lakini pamoja na hayo kuna ulazima wa kuhakikisha kuwa, matini iliyopatikana inaingia kwenye mkondo wake wa kisheria iliopangiwa, na iwapo itapitishwa, kuchukuliwe hatua za kuhakikisha kuwa upande wa pili unaheshimu kikamilifu makubaliano hayo na kuufungia njia ya kukwepa kuyatekeleza. Mnajua vyema kuwa, baadhi ya madola hayo sita yaliyofanya mazungumzo nasi hayaaminiki.
Ni matumaini yangu wananchi wetu wataendelea kuhifadhi na kulinda umoja na mshikamano pamoja na busara zao ili tuweze kufikia kwenye manufaa yetu ya kitaifa katika anga ya utulivu na ya busara.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullah.
Sayyid Ali Khamenei,
24/4/1394
(15/07/2015)

 

Matini ya barua ya Hujjatul Islam Walmuslimin Rouhani kwa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ni kama ifuatavyo:

Bismillahir Rahmanir Rahim.
Kwa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu
Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei (Mwenyezi Mungu akulinde na akuhifadhi)
Pokea salamu zangu za dhati na mapenzi
Ninamshukuru Mwenyezi Mungu, Mwenye enzi na utukufu mkubwa kwa kutupa taufiki ya kutangaza rasmi kwako Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na kwa taifa lililojaa heshima la Iran kwamba tumeyakamilisha mazungumzo ya nyuklia kwa heshima na ufakhari mkubwa. Taufiki hii kutoka kwa Mwenyezi Mungu ni matunda ya istikama na kutotetereka matabaka yote ya wananchi wa taifa kubwa la Iran na ni matunda ya miongozo ya hekima na burasa ya Kiongozi mpendwa wa Mapinduzi ya Kiislamu. Ni baraka za hamasa ya kisiasa ya wananchi na ni matunda ya hatua yao ya kuchagua msimamo na fikra ya kuamiliana vizuri na dunia ambapo katika kipindi cha miezi 23 ya jitihada kubwa za matawalia katika nyuga za kiuchumi na siasa za nje, Iran ya Kiislamu imeweza kupata ushindi katika kulinda vilivyo haki yake ya nyuklia na kuandaa mazingira ya kuondolewa vikwazo vya kidhulma na kutayarisha uwanja wa kufanyika harakati yenye kasi kubwa ya nchi kuelekea kwenye ustawi na maendeleo kupitia kutekeleza vilivyo siasa za uchumi wa kusimama kidete.
Mafanikio hayo yamepatikana baada ya madola makubwa kutambua kuwa, silaha ya vikwazo haiwezi kupambana na rasilimali ya kijamii bali hata haviwezi kuzuia maendeleo ya Iran katika upande wa nyuklia. Siri ya mafanikio yetu katika medani hiyo ni umoja na mshikamano wa ndani ya nchi na jitihada na harakati zetu chini ya miongozo ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu. Uzoefu huo kwa mara nyingine tena umeonesha umuhimu na nafasi isiyo na mbadala ya Kiongozi Muadhamu akiwa ni mhimili wa umoja na mshikamano katika jamii na katika uongozi wa nchi kwenye kipindi kigumu cha tufani na kimbunga kikubwa. Kabla ya jambo lolote, suala linalopasa kupongezwa ni kujitolea kwa hali na mali wananchi wema wa Iran na hususan mashahidi madhulumu wa teknolojia ya nyuklia ambao baada ya kupita miaka mingi ya istiqama na uvumilivu, sasa wataonja utamu wa matunda ya jitihada zao.
Katika hali ambayo maadui wa nchi yetu walikuwa wanafanya njama - kupitia mpango wao wa kueneza chuki dhidi ya Iran - kuifanya nchi yetu itengwe kimataifa na kutoa pigo kwa nchi yetu, sisi si tu tumefanikiwa kufelisha mpango huo wa kueneza chuki dhidi ya Iran bali kupitia mafanikio haya tumeweza kunayanyua juu nafasi ya nchi yetu kimataifa kwa kadiri kwamba, jamii ya kimataifa leo hii ina hamu kubwa ya kufanya mazungumzo na kushirikiana na Iran katika nyuga tofauti. Makubaliano hayo ya nyuklia yanaonesha kuwa tunaweza - sambamba na kulinda heshima ya nchi yetu na kuchunga mistari yetu myekundu - kuyalazimisha madola makubwa kukubali misimamo yetu ya kimantiki. Mafanikio haya makubwa yasiyo na mfano katika historia ya mahusiano ya kimataifa ambayo yatapelekea kufutwa maazimio yote ya vitisho dhidi ya taifa letu baada ya mazungumzo hayo na kuandaa uwanja wa kufanyika ushirikiano mkubwa wa kimataifa - hata katika masuala yasiyo ya nyuklia - ni somo kubwa kwa ajili ya eneo letu hili la kwamba njia ya kutatua matatizo ya kisiasa kwenye eneo letu si kuvamia, wala kufanya kuua na wala kufanya vitendo vya kigaidi, bali ni mazungumzo na kushirikishwa vilivyo wananchi katika maamuzi ya nchi zao.
Ni wajibu kwangu kukushukuru kwa miongozo yako ya busara na kwa uungaji mkono wako wa wazi wazi kwa juhudi hizi, kama ambavyo ninaishukuru pia timu yetu ya mazungumzo ya nyuklia ambayo kutokana na kusimama kwake kidete na kwa jitihada za kupigiwa mfano, imeweza kutekeleza vilivyo siasa zote zilizowasilishwa kwa serikali pamoja na kuchunga mistari yote myekundu iliyoainishwa na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ambapo kwa jitihada zake zisizochoka timu hiyo imeweza kuwaletea fakhari kubwa wananchi wa Iran wenye subira na wanaojitolea katika njia ya haki, kupitia mazungumzo hayo.
Ni jambo lisilo na shaka kwamba mshikamano na umoja wa kweli wa ndani ya nchi bado unahitajika kwa ajili ya hatua ya baadaye ya harakati hii na utekelezaji wa hatua tofauti za makubaliano hayo hadi kufikia kwenye matakwa yote ya taifa letu na kuondolewa kikamilifu vikwazo vyote vya kidhulma dhidi yetu. Kusimama kidete, muqawama na hatua za hekima chini ya miongozo yako ya busara zinahitajika mno hivi sasa kwa ajili ya kulifanikisha hilo. Sina shaka kwamba, kwa kuwepo mwamko wa kitaifa, mshikamano, mapenzi na ushirikiano baina ya wananchi na serikali, tutaweza kushuhudia nusra ya Mwenyezi Mungu ikiwa pamoja na mfumo huu mtukufu kama tulivyoshuhudia mara zote huko nyuma na taifa hili la waungwana na la watu wenye subira litaweza kufikia kwenye malengo yake makuu matukufu.
Taufiki yote ni ya Mwenyezi Mungu na Kwake tunategemea.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.
Hassan Rouhani
23/Tir/1394
(14/Julai/2015).

 
< Nyuma   Mbele >

^