Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Kiongozi Muadhamu Aonana na Mkuu na Wajumbe wa Baraza la Wanavyuoni Wataalamu Chapa
03/09/2015
 Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu leo asubuhi ameonana na mkuu na wajumbe wa Baraza la Wanavyuoni Wataalamu (linalomchagua na kusimamia kazi za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu) na kusema kuwa, baraza hilo ni dhihirisho kamili la demokrasia ya Kiislamu kwa ajili ya harakati na juhudi zilizo chini ya mfumo wa kifikra wa Kiislamu na usimamiaji wa mambo ambao unauepusha mfumo huo kufanana na msamiati wa mfumo wa kibeberu.
Amesisitiza kuwa: Jukumu kubwa la maulamaa wa kidini, wasomi wa Vyuo Vikuu na viongozi nchini ni kuwa na uchungu na kuwa na hisia kali kuhusu njama za maadui, kumjua vyema adui na kutangaza mustakbali wenye matumaini na mafanikio nchini kupitia vielelezo vilivyomo katika mfumo wa kifikra wa Kiislamu na kwa kutumia uwezo na vipaji vya vijana pamoja na uwezo mkubwa ilio nao nchi yetu.
Vile vile Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amebainisha nukta kadhaa muhimu kuhusu mwafaka wa nyuklia kati ya Iran na kundi la 5+1 na hali ya baada ya mwafaka huo.
Mwanzoni mwa hotuba yake, Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria baadhi ya aya za Qur'ani Tukufu zinazozungumzia utulivu wa Mwenyezi Mungu aliowashushia waumini baada ya Waislamu hao wa kweli kujisalimisha kikamilifu kwa Mwenyezi Mungu na kuwa na imani na nia njema kuhusu ahadi za Mwenyezi Mungu na amelitaja Baraza la Wanavyuoni Wataalamu kuwa ni muandaaji wa mazingira ya kupatikana utuvu na utulivu katika jamii.
Vile vile amebainisha sababu ya jambo hilo akisema: Baraza la Wanavyuoni Wataalamu ndilo baraza pekee ambalo ndani yake kunafanyika chaguzi mbili. Uchaguzi wa kwanza ni wa wananchi kuwachagua wajumbe wa baraza hilo na wa pili ni wa wajumbe wa baraza hilo kumchagua Kiongozi Muadhamu.
Ameongeza kuwa: Kutokana na kuwa na sifa hiyo ya kuwa na chaguzi mbili, Baraza la Wanavyuoni Wataalamu kwa upande mmoja ni dhihirisho kamili ya demokrasia ya kidini na demokrasia ya Kiislamu na katika upande mwengine ni dhihirisho la kutawala matukufu na hukumu za Kiislamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Kutokana na Baraza la Wanavyuoni Wataalamu pokuwa na sifa kama hizo za kipekee, linawawezesha wajumbe wa baraza hilo kufanya kazi zao kwa uhuru kamili na kwa muono wa mbali, na jambo hilo huandaa mazingira ya kupatikana utuvu na utulivu katika jamii.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa ni lazima katika chaguzi zote mbili, Baraza la Wanavyuoni Wataalamu lifanye kazi zake kwa uangalifu mkubwa na kwa uhuru kamili na kuongeza kuwa: Uhuru wa kifikra una maana kwamba, wajumbe wa baraza hilo wasikubali kutekwa na misamiati na pumba za mfumo wa kibeberu.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kwa kusema: Tab'an nasaha hizi haziwahusu tu wajumbe wa Baraza la Wanavyuoni Wataalamu, bali zinawahusu viongozi na taasisi zote za mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na za watu wote wenye ushawishi wa kisiasa, kijamii na kidini nchini na kwamba kila mmoja anapaswa kuwa macho ili asije akaingia katika mtego wa kulandana na kuwa na sura moja na msamiati, maneno matupu na pumba za mfumo wa kibeberu.
Aidha ameashiria propaganda kubwa na za kila upande zinazofanywa na kambi ya kiistikbari kwa lengo la kuyatishwa mataifa mengine wanafikra na watungaji wa sera wa mataifa hayo misamiati, pumba na istilahi zake za bandia.
Ameongeza kuwa, katika msamiati wa mfumo wa kiistikbari, istilahi na maneno kama ugaidi na haki za binaadamu yana maana zake maalumu na kwamba katika msamiati huo, mashambulio ya mtawalia ya miezi sita sasa dhidi ya wananchi wa Yemen na kuuliwa bila huruma wananchi wasio na hatia wa Ghaza, si ugaidi; na kukandamizwa wananchi wa Bahrain kwa sababu tu ya kupigania haki zao za kupiga kura hakuhesabiwi kuwa ni uvunjaji wa haki za binadamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Katika msamiati wa mfumo wa kibeberu, haki ya kujihami na kujilinda vikosi vya muqawama huko Lebanon na Palestina inahesabiwa kuwa ni ugaidi, lakini vitendo viovu vya nchi za kidikteta zilizo karibu na Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati si uvunjaji wa haki za binadamu.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Katika msamiati wa madola ya kiistikbari, kuuliwa kigaidi wanasayansi wa nyuklia (wa Iran) ambapo Wazayuni takriban wamekiri kufanya mauaji hayo na baadhi ya nchi za Ulaya zikikiri wazi wazi kuhusika na mauaji hayo, hakuhesabiwi kuwa ni ugaidi.
Amesisitiza kuwa, kutunga istilahi hizo na kuwa na matumaini kwamba watu wote wengine wakubaliane na maana hizo ni katika mfano na ushahidi wa wazi kabisa wa ubeberu na uistikbari.
Ameongeza kuwa: Amma katika upande wa pili, mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ni mfumo wa kifikra wa Kiislamu ambao licha ya kupita miaka mingi tangu kuasisiwa kwake duniani, una mvuto, ukunjufu na haiba ya aina yake.
Ayatullah Udhma Khamenei ametolea ufafanuzi vipengee vya mfumo wa kifikra wa Kiislamu wa Iran akisema kuwa ni pamoja na kupinga dhulma, ubeberu na ukandamizaji, kupigania heshima ya kitaifa na Kiislamu pamoja na uhuru wa kifikra, kisiasa na kiuchumi, akiyataja mambo hayo kuwa ni katika mambo yanayounda mfumo huo wa kifikra.
Amma kuhusiana na umuhimu wa istikilali na nafasi ya jambo hilo katika kujiamini na kujiletea maendeleo taifa fulani amesema: Istikilali ni sehemu ya uhuru, hivyo watu wanaopinga istikilali, kwa hakika huwa wanapinga pia uhuru.
Vile vile ameitaja kaulimbiu ya "Istikilali, Uhuru na Jamhuri ya Kiislamu" kuwa ni shaari inayoonesha mfungamano mkubwa na wa kimantiki uliopo baina ya istilahi hizo tatu na kuongeza kuwa: Istikilali ya pande zote na uhuru wa kifikra na kielmu, yote mawili yamo katika mfumo wa kifikra wa Kiislamu wa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na kwamba mfumo wa namna hiyo wa kifikra huandaa uwanja wa kujiamini na kupiga hatua mbele za maendeleo kwa taifa lolote lile.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameutaja mtindo wa maisha wa Kiislamu, ubunifu, kuwa imara na kuwa na umoja wa kitaifa kwamba ni viungo vyengine vya mfumo wa kifikra wa Kiislamu na kuongeza kwamba: Katika kipindi chote cha miaka 36 iliyopita, taifa la Iran limekuwa likifanya harakati zake katika fremu ya mfumo huo wa kifikra na imefanikiwa kupiga hatua kubwa za kimaendeleo licha ya kukumbwa na vikwazo na vizuizi vingi.
Ayatullah Udhma Khamenei ameutaja upeo unaoangaliwa na taifa la Iran na malengo yanayopiganiwa kufikiwa na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu kuwa ni kuifanya Iran iwe na maendeleo makubwa ya kielimu na kiviwanda, iwe na idadi ya watu milioni 150 hadi milioni 2000 waliojengeka vizuri kiroho na kimaanawi, iwe na jamii ambayo itakuwa mbali na ushawishi wa mabeberu na ambayo itasimama kidete kukabiliana na madola ya kiistikbari yanayotumia mabavu duniani.
Amesema, wakati Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itakapofikia kwenye nafasi hiyo na kupambika kwa sifa hizo, jambo hilo litakuwa ni pigo kubwa mno kwa kambi ya kiistikbari na bila ya shaka yoyote hiyo ndiyo sababu ya kuweko njama zote hizi za mabeberu dhidi ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ili kulizuia taifa la Iran lisifikie huko.
Amesema, kudhihiri nchi kama hiyo ya Kiislamu kutakuwa na maana ya kuangamia na kumalizika kabisa ubeberu na ukafiri duniani na kuongeza kuwa: Wananchi wa Iran hususan vijana, maulamaa wa kidini na wasomi wa Vyuo Vikuu kila mmoja wao anapaswa kuendesha harakati zake chini ya mwavuli wa fikra ya Kiislamu, na watu wote; wakiwemo viongozi nchini, wanapaswa kuwa macho kikamilifu mbele ya njama za adui.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Haipasi kuruhusu tabasamu la adui au baadhi ya wakati jambo maneno fulani mazuri na ya muda mfupi ya adui tena kuhusu maudhui moja maalumu, yateke fikra za watu, bali inabidi wakati wote kuzingatia adui anafanya njama na hila gani dhidi yetu na kujipanga vilivyo kukabiliana nazo.
Ayatullah Udhma Khamenei, kwa mara nyingine tena amesisitiza kuwa, adui na ubeberu wa kimataifa si suala la ndani ya ndoto, bali ni uhakika wa mambo ambao mfano wake mkubwa zaidi ni dola la Marekani na mashirika na makampuni ya kiuchumi ya Kizayuni na waitifaki wake.
Vile vile amegusia uwezo, nguvu na vipaji vya vijana waliojengeka kiimani na vile vile uwezo, utajiri na vyanzo vya maliasili vya Iran pamoja na kukita mizizi utamaduni wa Kiislamu na utamaduni wa Ahlul Bayt Alayhimus Salaam kati ya wananchi wa Iran na kuongeza kuwa: Viongozi na shakhsia wote wenye ushawishi na ambao maneno yao yana taathira katika jamii, wanapaswa kuwafahamisha na kuwafafanulia wananchi mustakbali huo ulio wazi na bora kwa kadiri wanavyoweza, na sambamba na kuwapa matumaini ya kuwa na mustakbali bora, waweze pia kuandaa uwanja wa kukita mizizi utuvu na utulivu nchini.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amebainisha nukta nyingine muhimu kuhusu mwafaka wa nyuklia uliofikiwa baina ya Iran na kundi la 5+1 na masuala ya baada ya makubaliano hayo na vile vile suala la utekelezaji wa siasa za uchumi wa kusimama kidete nchini Iran.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria mjadala wa siku za hivi karibuni kuhusu nafasi ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) katika kujadili makubaliano hayo ya nyuklia na kusema kuwa: Wataalamu wa sheria na wanafikra ndio wanaotakiwa kutoa ufafanuzi kuhusu upeo wa kisheria na kikanuni wa suala hilo na mambo yanayoambatana nalo, lakini kiujumla ni kuwa, mimi ninaamini kwamba mheshimiwa Rais naye pia amesema kuwa, si maslahi kwa nchi yetu kuitenga Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu katika kujadili mwafaka huo.
Vile vile amesisititizia ulazima wa kuingia Bunge la Iran katika kujadili mwafaka huo na wakati huo huo lakini amekumbushia jambo muhimu kwa kusema: Mimi siwezi kutoa nasaha zozote kuhusu namna ya kuujadili mwafaka huo na je Bunge liukubali au lisiukubali, bali ni wabunge wenyewe waliochaguliwa na wananchi ndio wanaopaswa kuchukua maamuzi kuhusu suala hilo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuhusiana na masuala ya baada ya mwafaka huo wa nyuklia kwamba: Mimi nimeshazungumza na ndugu zangu wapenzi serikalini kuhusiana na baadhi ya nukta zinazohusiana na suala hilo na hivi sasa napenda kubainisha nukta hizo mbele ya wajumbe wa Baraza la Wanavyuoni Wataalamu na mbele ya wananchi wote.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria nchi sita zilizofanya mazungumzo na Iran kuhusu kadhia hiyo na nafasi ya Marekani kati ya nchi hizo sita na kuongeza kuwa: Kwa hakika, nchi kuu tunayokabiliana nayo katika mazungumzo hayo ni Marekani, lakini inasikitisha kuona kuwa viongozi wa Marekani wanazungumza vibaya sana kuhusu suala hilo na inabidi ijulikane wazi kwa nini viongozi wa nchi hiyo wanatoa matamshi kama hayo na nini kifanyike kukabiliana na matamshi ya namna hiyo.
Aidha ameashiria matamshi ya viongozi wa Marekani wanaoshikilia msimamo wa kubakishwa fremu ya vikwazo na kusema kuwa: Kama wamekusudia kubakisha fremu ya vikwazo, basi kwa nini sisi tulifanya mazungumzo nao? Jambo hilo kwa hakika linapingana kikamilifu na sababu zilizoifanya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwenda kwenye meza ya mazungumzo hayo kwani lengo la mazungumzo hayo ni kuondolewa vikwazo vyote.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Kama kwenye mazungumzo hayo tumelegeza kamba kidogo katika baadhi ya mambo bila ya kugusa mambo muhimu zaidi na makuu, kimsingi tumefanya hivyo ili vikwazo viondolewe, vinginevyo kulikuwa na ulazima gani wa kufanya mazungumzo, bali sisi tungeliweza kuendelea na kazi zetu kama kawaida na tungeliweza kupindukia mashinepewa 19 elfu tulizo nazo na kufikisha mashinepewa elfu khamsini hadi elfu sitini na tungeliendelea na urutubishaji wetu wa urani kwa asilimia 20 na tungeliongeza kasi zaidi kwenye suala la utafiti na kutanua miradi yetu ya nyuklia.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza pia kuwa: Kama imekusudiwa kutoondolewa vikwazo, basi hakuna haja ya kuwa na muamala wowote ule, hivyo inabidi iwekwe wazi; viongozi wa Marekani wanakusudia nini wanapotoa matamshi yao kama hayo.
Aidha amewakhutubu viongozi nchini akiwaambia: Msiseme kuwa Wamarekani wametoa matamshi hayo ili kuwaridhisha wapinzani wao ndani ya Marekani, tab'an mimi ninaamini kuwa, mizozo ya ndani ya Marekani ni jambo lisilo na chembe ya shaka, naamini kuwa wana hitilafu kubwa baina yao na sababu ya hitilafu hizo ziko wazi kwetu, lakini kile ambacho kinasemwa rasmi, inabidi kitolewe ufafanuzi na kama hakitatolewa ufafanuzi basi upande wa pili utaamini kuwa hivyo ndivyo ilivyo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu vile vile amegusia matamshi ya viongozi wa Marekani yanayohusiana na kusitishwa vikwazo na kusisitiza kuwa: Tangu mwanzo suala halikuwa hilo, sisi tumekuwa tukisisitiza kuwa vikwazo viondolewe na si kusimamishwa au kusitishwa.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Tab'an tulivyotaka sisi ni kuondolewa mara moja vikwazo hivyo, lakini marafiki zetu hapa wamelifasiri vingine suala hilo na sisi hatukupingana na jambo hilo, lakini vikwazo vyote lazima viondolewe kikamilifu. Kama itakuwa ni kusitishwa tu vikwazo, basi na sisi kwa upande wake tutaishia tu kwenye kusitisha katika masuala ambayo tunatakiwa kuyafanya na si kufanya vile hasa ilivyokubaliwa.
Ameongeza kuwa: Tab'an upande wa pili unasema kuwa, baadhi ya vikwazo hivyo havimo mikononi mwa serikali ya Marekani, na sisi tunasema: hivyo hivyo vikwazo vilivyomo mikononi mwa serikali ya Marekani na mikononi serikali za Ulaya, hivyo hivyo viondolewe kikamilifu.
Ayatullah Udhma Khamenei ametaja sehemu nyingine ya maneno mabaya yanayotolewa na viongozi wa Marekani kwamba ni matamshi yao yasiyo na uhusiano hata chembe na kadhia ya nyuklia. Ameongeza kuwa, viongozi wa Marekani wanazungumza kama walivyokuwa wakizungumza Waingereza karne ya 19 kuhusiana na Iran. Inaonekana viongozi wa Marekani wako nyuma kihistoria kwa karne mbili. Hawajui kuwa dunia imebadilika na kwamba madola ya kibeberu hivi sasa hayana tena mbinde wala nguvu za kufanya yanachotaka na katika upande wa pili wanasahu kuwa kuna Jamhuri ya Kiislamu yenye uwezo na nguvu zinazotambulika na zisizotambulika ambazo huonekana tu wakati wa vitendo. Iran nayo si sawa na nchi fulani iliyobaki nyuma kimaendeleo ambayo wanaweza kuifanyia chochote wanachotaka.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa mfano wa moja ya matamshi ya kibeberu ya viongozi wa Marekani akisema: Viongozi wa Marekani wanasema wanatarajia kuwaona viongozi na serikali ya Jamhuri ya Kiislamu inafanya mambo tofauti na inayofanya sasa.
Ameongeza kuwa: Wakati Wamarekani wanaposema wanataka kufanyike mambo tofauti wanakusudia mambo yanayokwenda kinyume na misimamo ya Jamhuri ya Kiislamu na yasiyojali matukufu ya Kiislamu na wanataka kuona kunaondolewa mfungamano wa sheria za Kiislamu, lakini wajue kuwa jambo hilo kamwe halitatoteka. Si serikali itafanya hivyo, si Bunge na si kiongozi yeyote yule wa Jamhuri ya Kiislamu, na kama atatokezea mtu akataka kufanya jambo hilo, basi wananchi wa Iran na Jamhuri ya Kiislamu kamwe hawatomruhusu kufanya hivyo.
Ayatullah Udhma Khamenei amegusia pia moja ya mambo yanayotarajiwa na Wamarekani yatokee nchini Iran akisema: Miongoni mwa siasa za Marekani katika eneo hili (la Mashariki ya Kati), ni kuvifuta na kuviangamiza kikamilifu vikosi vya muqawama na kuzidhibiti kikamilifu nchi za Syria na Iraq na wana tamaa kuwa Jamhuri ya Kiislamu nayo itaungana nao katika hilo, jambo ambalo kwa hakika kamwe haliwezi kutokea.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia matamshi mengine yanayosababisha kuzuka hisia kali na ambayo yanatolewa na viongozi wa Marekani na kusema: Wamarekani wanasema mwafaka wa nyuklia unaipatia Marekani fursa ndani ya Iran na nje ya Iran na katika eneo (zima la Mashariki ya Kati).
Amewakhutubu viongozi serikalini na katika taasisi nyinginezo akisema: Viongozi serikalini na katika taasisi nyengine mbali mbali humu nchini hawapaswi kuruhusu kwa namna yoyote kufanikiwa siasa hizo za Marekani ndani ya Iran na kuhusu nje ya Iran pia inabidi jitihada zifanyike ili kuizuia Marekani kutumia vibaya mwafaka huo kwani kadiri Wamarekani wanavyokaribia kwenye fursa wanazotaja, bila ya shaka ndivyo mataifa ya dunia yanavyozidi kudhalilishwa, kuingia katika matatizo na kuzidi kukandamizwa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia pia namna viongozi wote nchini Iran, wale wa siasa za nje na wale wa taasisi nyenginezo wanavyosisitiza kuwa, ni marufuku kikamilifu kufanya mazungumzo na Marekani isipokuwa tu katika kadhia ya nyuklia na kuongeza kuwa: Sababu inayopelekea kujitokeza upinzani huo ni misimamo ya Marekani ambayo inakinzana kikamilifu na misimamo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Ayatullah Udhma Khamenei ameendelea na hotuba yake kwa kuzungumzia kadhia muhimu ya uchumi nchini Iran na kusema: Siasa za Uchumi wa Kusimama Kidete ni majimui iliyo kamili ambayo vipengee vyake haviwezi kutenganishwa na utekelezaji wake unataka kuweko mpango madhubuti wa kiutekelezaji hivyo tumemtaka mheshimiwa Rais na serikali yake kuandaa mpango madhubuti, wenye manufaa na unaotekelezeka kwa ajili ya kufanikisha siasa hizo za uchumi wa kimuqawama na wa kusimama kidete na ni matumaini yetu kuwa hilo litatendeka.
Aidha amesema kuhusu umuhimu wa kufanikishwa uchumi wa kusimama kidete kwamba: Kama uchumi wa kusimama kidete utafanikiwa, basi hakutakuwa na haja tena ya kusubiri kurejeshwa fedha za Iran (zinazoshikiliwa nje ya Iran) ni sawa tu fedha hizo ziwe ni dola bilioni 5 au dola bilioni 100; tab'an fedha ambazo tunadai duniani na ambazo zimezuiwa kidhulma lazima zirejeshwe na ziweze kutumika nchini, lakini uchumi wa kusimama kidete haupaswi kuegemezwa kwenye kurejeshwa fedha hizo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu vile vile ametilia mkazo ulazima wa kuundwa kamati maalumu na amilifu ya kuweza kusimamia utekelezaji wa siasa za uchumi huo wa kusimama kidete na kusema: Serikali ndiyo inayopaswa kuunda kamati hiyo na sambamba na kuainishwa mipaka ya kazi ya kila taasisi na kuandaliwa muda wa ufuatiliaji, iwezekane kuanzishwa harakati adhimu katika upande huo.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema katika sehemu ya mwisho ya hotuba yake akiikhutubu nguvu kazi ya watu wenye imani thabiti kote nchini Iran na kuiambia: Harakati kuu iliyopo nchini hivi sasa ni kwa ajili ya kuelekea kwenye ufanikishaji wa malengo makuu na shabaha tukufu za Kiislamu na kwamba nguvu kazi ya watu wenye imani thabiti, madhubuti na waumini ambapo asilimia kubwa mutlaki na wananchi wa Iran wanaunda nguvu kazi hiyo, inabidi ijiweke tayari wakati wote ikiwa na yakini ya kupata nusra ya Mwenyezi Mungu na iingie vilivyo katika medani tofauti za kiuchumi, kiutamaduni na kisiasa na kusimama imara katika kukabiliana na njama mbali mbali za adui.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Yazdi, Mkuu wa Baraza la Wanavyuoni Wataalamu ametoa hotuba fupi na kusema kuwa sababu ya kupata ushindi Mapinduzi ya Kiislamu ni uongozi imara na wa busara wa Imam Khomeini (quddisa sirruh) na ushujaa wa wananchi wa Iran kama ambavyo pia amegusia nukta kadhaa kuhusiana na kikao cha hivi karibu cha baraza hilo.
Vile vile Ayatullah Hashemi Shahroudi, Naibu wa Mkuu wa Baraza la Wanavyuoni Wataalamu ametoa ripoti kuhusiana na kikao cha kumi na nane cha baraza hilo na kusema kuwa ajenda ya kikao hicho ilikuwa ni kufanyia marekebisho kanuni na utaratibu wa idadi ya wajumbe wa baraza hilo.
Naibu wa Mkuu wa Baraza la Wanazuoni Wataalamu ameashiria pia namna kikao hicho kilivyojadili hali ilivyo katika eneo la Mashariki ya Kati hivi sasa na fitna ya makundi ya kitakfiri katika ulimwengu wa Kiislamu na kusema kuwa, kumejadiliwa pia suala la mazungumzo ya nyuklia kupitia kuita wageni mbali mbali mbele ya kikao hicho ili kutoa maelezo kuhusu mazungumzo hayo. Ameongeza kuwa: Kutolewa mapendekezo kuhusu njia za utatuzi wa masuala mbali mbali nchini, daghadagha na wasiwasi wa wajumbe wa Baraza la Wanavyuoni Wataalamu kuhusiana na masuala ya kiutamaduni, kuenziwa nafasi aali na tukufu ya mashahidi na harakati yenye thamani kubwa ya kiutamaduni ya taifa la Iran katika mazishi ya mashahidi hao, kuzingatia umuhimu wa uchaguzi ujao wa Baraza la Wanazuoni Wataalamu na jukumu zito lililo nalo Baraza la Kulinda Katiba kwa ajili ya kulinda nafasi na heshima ya baraza hilo na ulazima wa kuainishwa watu wenye sifa za kugombea kwa mujibu wa sheria pamoja na kutoa ripoti kuhusu maendeleo yaliyopatikana baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran katika mikoa iliyokuwa imebakishwa nyuma kimaendeleo na hususan maeneo ya Waislamu wa Kisuni, ni miongoni mwa mambo muhimu yaliyojadiliwa na kuzungumziwa kwenye kikao hicho cha Baraza la Wanazuoni Wataalamu.
Vile vile Ayatullah Hashemi Shahroudi ameongeza kuwa: Wajumbe wa Baraza la Wanazuini Wataalamu wamesisitiza kuwa, mwafaka wa nyuklia hauna maana ya kuwa na uhusiano wa kawaida na Marekani.
 
< Nyuma   Mbele >

^