Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Aonana na Rais wa Austria Chapa
08/09/2015
Supreme Leader Meets with President of AustriaAyatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislalmu, leo jioni (Jumanne), ameonana na Rais Heinz Fischer wa Austria na huku akigusia uadui wa serikali ya Marekani dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu kutokana na Washington kupoteza manufaa yake nchini Iran, amelitaja suala la baadhi ya nchi za Ulaya la kufuata kibubusa siasa za kiuadui za Marekani kuhusiana na Iran kuwa si jambo la kimantiki hata kidogo. Amesisitiza kwa kusema: Tab'an Austria si miongoni mwa kundi la nchi hizo na kuna wajibu wa viongozi wa nchi mbili za Iran na Austria kupanua uhusiano wao kadiri inavyowezekana ili ziweze kushirikiana zaidi katika nyuga mbali mbali.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema katika mazungumzo hayo kuwa, lengo kuu la Mapinduzi ya Kiislamu ni kuwadhaminia wananchi wa Iran kheri na ufanisi pamoja na watu wote duniani chini ya kivuli cha kufuata njia ya Mwenyezi Mungu pamoja na kutawala akili na vitendo na kuongeza kuwa: Tab'an msimamo wetu huo wa kupenda na kupigania kheri unakabiliwa pia na maadui wa kimataifa ambao wanafanya kila njia kuzusha vita na kuyagombanisha mataifa na watu wa taifa fulani wenyewe kwa wenyewe lakini Iran ina marafiki wengi wanaolipenda sana taifa hili kati ya tawala na watu wa mataifa tofauti duniani.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia pia uadui usio na chembe ya mantiki wa baadhi ya nchi za Ulaya dhidi ya Iran baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran na kuongeza kuwa: Mapinduzi ya Kiislamu yameipokonya Marekani taifa la Iran ambalo lilikuwa mikononi mwa Marekani kikamilifu na hilo ndilo linaloifanya Marekani iifanyie uadui mkubwa Jamhuri ya Kiislamu. Ameongeza kuwa, kitendo cha baadhi ya tawala za Ulaya cha kuifuata kibubusa Marekani si cha kimantiki kabisa na wala hakistahili kufanywa na nchi hizo na tab'an Austria si miongoni mwa nchi hizo.
Vile vile amesisitizia haja ya kuwa na ratiba maalumu za kuweza kuimarisha uhusiano wa nchi mbili na amejibu swali la Rais Heinz Fischer wa Austria kuhusu mustakbali wa uhusiano wa Iran na nchi za Ulaya akisema: Hadi hivi sasa kuna masuala mbali mbali yamezungumzwa na serikali za nchi za Ulaya, hata hivyo inabidi tusubiri na kuona hatua za kivitendo za matamshi ya serikali hizo.
Katika sehemu nyingine ya matamshi yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia vitendo vya kifisadi vya magenge yaliyopotoka katika eneo la Mashariki ya Kati ambayo yanajinasibisha na dini tukufu ya Kiislamu na kuongeza kuwa: Uislamu ni tofauti kabisa na vitendo vya magenge hayo, bali Uislamu umesimama juu ya msingi wa mantiki madhubuti, imani na utumiaji mzuri wa akili.
Katika mazungumzo hayo ambayo yamehudhuriwa pia na Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Rais Heinz Fischer wa Austria ametoa shukrani zake kutokana na mapokezi mazuri sana aliyopata nchini Iran na kuongeza kwamba, amekuwa na mazungumzo mazuri na viongozi wa Iran. Amesema: Kuna wajibu wa kufanyika mazungumzo katika masuala mengine mbali mbali ili kuweze kufikiwa mwafaka na makubaliano mengi zaidi katika nyuga tofauti.
Rais wa Austria ameelezea pia kufurahishwa kwake na mtazamo mzuri wa Kiongozi Muadhamu kuhusiana na Austria na kuongeza kuwa: Mazungumzo yangu na Rais Rouhani yalikuwa mazungumzo mazuri na sisi pia tuna matumaini mazuri kuhusu mustakbali.
Ameongeza kuwa: Hivi sasa kumejitokeza fursa nzuri ya kuweko ushirikiano mpana zaidi baina ya pande mbili.
 
< Nyuma   Mbele >

^