Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Kiongozi Muadhamu Ahudhuria Sherehe za Kuhitimu Masomo Wanachuo wa Vyuo Vikuu vya Maafisa wa Jeshi Chapa
30/09/2015
 Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Atembelea Mji wa Nowshahr na Kuhudhuria Sherehe za Kuhitimu Masomo Wanachuo wa Vyuo Vikuu vya Maafisa wa Jeshi
Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ambaye pia ndiye Amirijeshi Mkuu wa vikosi vyote vya ulinzi vya Iran, leo asubuhi (Jumatano) ameshiriki katika sherehe za kuhitimu masomo na kula viapo pamoja na kupewa vyeo wanafunzi wa Vyuo Vikuu vya maafisa wa kijeshi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Chuo Kikuu cha Sayansi Bahari cha Imam Khomeini (quddisa sirruh) huko Nowshahr, kaskazini mwa Iran.
Katika sherehe hizo, Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria tukio la kusikitisha na la umwagaji damu la maafa ya Mina na kusema kuwa, maafa hayo yamekuwa ni msiba mkubwa kwa ulimwengu mzima wa Kiislamu na kwa taifa la Iran, kutokana na maelfu ya mahujaji kufariki dunia na hususan mamia ya mahujaji wa Kiirani. Vile vile amegusia wajibu wa kuundwa kamati ya kutafuta ukweli ya nchi za Kiislamu ikiwemo Iran na kuongeza kuwa: Serikali ya Saudi Arabia haitekelezi majukumu yake kuhusiana na kusafirishwa miili mitoharifu ya mahujaji waliokufa kwenye maafa ya Mina na kwamba hadi hivi sasa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikijizuia na kuchunga adabu ya Kiislamu na heshima ya udugu katika ulimwengu wa Kiislamu lakini viongozi wa Saudia watambue kuwa, kama watafanya udhalilishaji wa aina yoyote ile hata mdogo dhidi ya makumi ya mahujaji wa Kiirani huko Makka na Madina na iwapo haitotekeleza majukumu yake yanayotakiwa kuhusiana na kurejeshwa nchini Iran miili mitoharifu ya mahujaji hao, basi radiamali ya Iran itakuwa kali na nzito.
Vile vile ameashiria suala la kupoteza maisha kwa namna ya kudhulumiwa na tena wakiwa na kiu mahujaji kwenye maafa ya Mina na kutumbukia kwenye msiba familia za mahujaji hao ambazo zinasubiri kwa hamu kubwa kurejea nyumbani wapendwa wao hao na kuongeza kuwa: Hadi hivi sasa idadi kamili ya mahujaji wa Kiirani waliopoteza maisha kwenye maafa hayo haijajulikana na kuna uwezekano kukawa kuna mamia ya mahujaji wengine waliokufa kwenye tukio hilo ambao hawajajulikana. Amesema: Kwa hakika huu ni msiba mkubwa kwa taifa la Iran.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia baadhi ya ripoti zinazoonesha kwamba kuna uwezekano idadi ya mahujaji waliofariki dunia kwenye maafa ya Mina ikapindukia watu elfu tano na kusisitiza kuwa: Licha ya kwamba Qur'ani Tukufu inaihesabu Nyumba ya Mwenyezi Mungu Alkaaba kuwa ni mahala salama kwa mahujaji, lakini hivi sasa tunapaswa tujiulize, hivi ni kweli mahala hapo ni salama sasa hivi?
Ayatullah Udhma Khamene amesisitizia pia ulazima wa kuundwa kamati ya kutafuta ukweli na kushirikishwa nchi za Kiislamu ikiwemo Iran katika kuunda kamati hiyo akisisitiza kuwa: Sisi kwa hivi sasa hatuwezi kutoa hukumu ya kabla ya wakati wake kuhusiana na sababu ya tukio hilo, lakini tunaamini kwamba serikali ya Saudi Arabia haikutekeleza majukumu yake kuhusu mahujaji waliojeruhiwa bali iliwatelekeza wakiwa katika hali ya kiu na kukata tamaa.
Vile vile amezungumzia matatizo yaliyojitokeza katika suala zima la kurejeshwa nyumbani miili mitoharifu ya mahujaji waliopoteza maisha kwenye maafa ya Mina na licha ya viongozi wa Iran kulifuatilia mno suala hilo na amesisitizia wajibu wa kuendelea kulifuatilia jambo hilo kwa uzito wa hali ya juu akiongeza kuwa: Serikali ya Saudi Arabia haitekelezi majukumu yake kuhusu suala hilo na katika baadhi ya wakati pia inasumbua na kufanya maudhi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hadi hivi sasa imejizuia na inachunga adabu ya Kiislamu na heshima ya udugu katika ulimwengu wa Kiislamu, lakini viongozi wa Saudia wanapaswa wajue kuwa, mkono wa Iran ni mrefu na unafika mbali na ni bora kuliko wengi wao na kwamba Iran ina suhula na njia nyingi na kama itataka kuwajibu na kuonesha radiamali dhidi ya wanaofanya maudhi na usumbufu basi hali zao hazitakuwa nzuri na kamwe hawataweza kukabiliana na Iran katika medani yoyote ile.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kuwa, majibu na radiamali ya Iran ya Kiislamu itakuwa nzito na ngumu sana na kuongeza kuwa: Katika kipindi cha vita vya miaka minane vya kujihami kutakatifu (vilivyoanzishwa na utawala wa wakati huo wa Iraq dhidi ya Iran) madola makubwa ya Mashariki na Magharibi pamoja na nchi za eneo hili zote kwa pamoja ziliuunga mkono utawala khabithi na haribifu wa Iraq wakati huo lakini hatimaye nchi zote hizo zilipata pigo na hivi ndivyo wanavyoijua Iran na hata kama watajifanya hawaijui, basi hivi sasa wanapaswa waijue hivyo Iran.
Aidha amegusia kuweko makumi ya maelfu ya mahujaji azizi wa Iran huko Makka na Madina na kutahadharisha kuwa, uvunjiaji heshima hata mdogo wa mahujaji wa Kiirani na vile vile hatua ya serikali ya Saudi Arabia ya kutotekeleza wajibu wake kuhusu miili mitoharifu ya mahujaji itakabiliwa na majibu na radiamali kali na nzito ya Iran.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran si utawala dhalimu, lakini hakuna mtu yeyote anayekubaliana na dhulma na ukandamizaji, hivyo Tehran haiwezi kupora haki za mtu yeyote yule au taifa lolote lile, ni sawa liwe la Waislamu au lisiwe la Waislamu, lakini kama atatokezea mtu na kutaka kupora haki ya taifa na ya nchi ya Iran basi itatoa majibu makali kwake na kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu, Tehran inao uwezo uwezo huo na taifa la Iran nalo ni taifa imara lisilotetereka.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema katika sehemu nyengine ya hotuba yake kwamba, "imani thabiti," "ushujaa" na "elimu" ni mambo matatu muhimu mno katika kuunda utambulisho wa kikosi fulani cha ulinzi na kusisitiza kuwa: Kama kikosi cha ulinzi kitakosa kuwa na imani, basi ndani ya kikosi hicho hujitokeza roho ya kupenda kuua wanyonge, kama ushujaa utakosekana, kikosi hicho cha ulinzi kitashindwa kutekeleza majukumu yake wakati wa hatari na kama elimu itakosekana, zana na silaha za kikosi hicho cha ulinzi zitafanya kazi kwa kuchelewa mbele ya silaha na zana za upande wa pili.
Ametoa mfano akisema kuwa, kushambuliwa nyumba za raia, barabara, masoko na hata watu walioko kwenye sherehe za harusi huko nchini Yemen ni mfano wa wazi wa roho ya kuua watu dhaifu na kukosekana moyo wa ushujaa katika kikosi cha ulinzi. Amewataka vijana waliomo kwenye vikosi vya ulinzi nchini Iran kujiimarisha kiimani, kiushujaa, kiubunifu na kufanya utafiti na uhakiki wa kielimu. Ameongeza kuwa: Leo hii mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu unahitajia zana na vifaa vya kisasa vya kivita kama ambavyo unahitajia pia zana za kivita za kielektroniki kwani ulimwengu wa leo unadhibitiwa na madola ya kishetani na ni hatari kwa watu wacha Mungu hivyo inabidi kuwa imara na tayari wakati wote kwa ajili ya kujihami.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameitaja sababu kuu ya kuwepo uadui wa madola makubwa yenye hamaki ya dunia dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu na dhidi ya taifa shujaa na la wanamapinduzi la Iran kuwa ni kusimama imara taifa la Iran mbele ya madola hayo na kulinda utambulisho na dhati yake na kutokubali kwake kutekwa wala kuyeyushwa ndani ya mifumo wa kiistikbari.
Amesema: Kuwa imara vikosi vya ulinzi vya Iran, iwe ni jeshi, au Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) au Basiji na vikosi vingine vyote vya ulinzi nchni Iran hakuna maana ya kuwa imara kwa ajili ya kupata ushindi mbele ya adui tu, bali inabidi uimara huo uzuie uchokozi na uvamizi wa adui.
Ayatullah Udhma Khamenei amegusia pia vitisho vya madola ya kibeberu duniani dhidi ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na kuongeza kuwa: Taifa la Iran katika kipindi cha miongo minne iliyopita na hususan katika kipindi cha miaka minane ya kujihami kutakatifu limethibitisha kuwa liko imara na lina nguvu na lina utambulisho wake maalumu na liko tayari wakati wote kusimama kidete kukabiliana na wanaolitakia mabaya taifa hili.
Amesisitiza kuwa, taifa la Iran liko imara na limesimama kidete kukabiliana na uistikabari likiwa macho na likiangalia mbali sambamba na kulinda utambulisho wake na kuheshimu ubinadamu akiongeza kuwa: Kusimama imara mbele ya ubeberu ni kuheshimu ubinadamu na mataifa yote duniani.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia uadui mkubwa wa maadui wa taifa la Iran na kuongeza kuwa: Daima hali imekuwa hivyo na kwamba kusimama imara waumini na kutoa pigo kubwa kwa maadui hao ndiko kunakoweza kuwafanya maadui hao warudi nyuma kwa kuona njama zao zote zinafeli.
Mwishoni mwa hotuba yake, Ayatullah Udhma Khamenei amewataka vijana walioko kwenye vikosi vya ulinzi nchini Iran kuyadurusu na kuyatalii kwa kina masuala yanayohusiana na vita vya kujihami kutakatifu na operesheni mbali mbali za vita hivyo na watembelee maeneo kulikofanyika operesheni za vita hivyo na kupata funzo katika masuala ya kijeshi na watumie uzoefu wa kizazi cha watu waliotangulia kwenye vikosi hivyo. Vile vile amewaambia: Nyinyi mnapaswa kuwa ngao madhubuti ya nchi na ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu kwa maana halisi ya neno.
Mwanzoni mwa sherehe hizo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezuru makumbusho ya mashahidi na kutoa heshima zake kwa mashahidi hao watukufu. Baada ya hapo, Amirijeshi Mkuu wa vikosi vyote vya ulinzi vya Iran amekagua vikosi mbali mbali vilivyokuwa vimepiga paredi kwenye uwanja huo.
Katika sherehe hizo, familia ya moja wa mashahidi wa jeshi la majini la Iran, mtu mmoja wa dini aliye mfano bora kwa wengine, makamanda watatu, wahadhiri watatu na watafiti, na wanafunzi watatu bora waliohitimu masomo yao kwenye Vyuo Vikuu vya maafisa wa kijeshi wamepokea zawadi zao kutoka kwa Amirijeshi Mkuu wa vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Vile vile mmoja wa wanafunzi hao aliyewawakilisha wanachuo wa Chuo Kikuu cha Sayansi Bahari cha Imam Khomeini (quddisa sirruh) naye amepata fakhari ya kupandishwa cheo na kupewa medali na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Kula kiapo cha pamoja wanachuo wapya, kupewa medali za pamoja, na kufanya maonyesho ya kivita katika medani ya Ghadir ni miongoni mwa ratiba zilizokuwepo kwenye sherehe hizo za leo.
Aidha katika sherehe hizo, vikosi mbali mbali vilivyokuwepo uwanjani katika Chuo Kikuu cha Sayansi Bahari cha Imam Khomeini huko Nowshahr, kaskazini mwa Iran, vimepita kwa gwaride mbele ya jukwaa alipokuwepo Amirijeshi Mkuu wa vikosi vyote vya ulinzi vya Iran, Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei.
Katika sherehe hizo, Meja Jenerali Ataollah Salehi, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Iran sambamba na kumkaribisha Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa: Jeshi la Iran kwa kupata ilhamu kutoka katika moyo wa kuwa tayari kujitolea kufa shahidi na kujitolea katika njia ya haki taifa la Iran, liko tayari wakati wote kukabiliana na vitisho vipya kama ambavyo liko tayari wakati wote pia kujitolea kikamilifu katika njia hiyo kwa nguvu zake zote na kwa kujiimarisha kila uchao kijeshi.
Naye "Admirali II" Hakimi, Kamanda wa Chuo Kikuu cha Sayansi Bahari cha Imam Khomeini (quddisa sirruh) cha mjini Nowshahr ametoa ripoti fupi kuhusu mchakato wa masomo na mafunzo maalumu ya kielimu ya wahachuo na maafisa wanaohitimu masomo yao katika Vyuo Vikuu vya maafisa wa kijeshi vya Iran.
Katika sherehe hizo pia, wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sayansi Bahari cha Imam Khomeini huko Nowshahr wamefanya mazoezi mbali mbali wa baharini mbele ya Amirijeshi Mkuu wa vikosi vyote vya ulinzi vya Iran, Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei.

 

 
< Nyuma   Mbele >

^