Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Kiongozi Muadhamu Aonana na Waziri na Maafisa wa Wizara yaa Mambo ya Nje Chapa
01/11/2015
 Ayatullah Udhma Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, leo asubuhi (Jumapili) ameonana na Waziri wa Mambo ya Nje, mabalozi pamoja na mabalozi wadogo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na huku akibainisha misingi na mikakati thabiti na isiyotetereka katika sera za kigeni kwenye Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na mambo ya lazima yanayotokana na msingi na siasa hizo, amesema kuwa, sera hizo ndizo njia za utatuzi wa kimantiki na imara wa Iran kwa masuala muhimu ya eneo la Mashariki ya Kati yakiwemo masuala ya Syria, Yemen na Bahrain na kusisitiza kuwa: Malengo ya Marekani katika eneo hili yanatofautiana kwa daraja 180 na malengo ya Iran.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema kuwa, sera za mambo ya nje za Iran ndizo hizo hizo sera za mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu katika Katiba ya Iran na kusisitiza kwamba: Sera hizo za mambo ya nje chimbuko lake ni Uislamu na zimetokana na malengo na shabaha kuu za Mapinduzi ya Kiislamu na kwamba maafisa wa Wizara ya Mambo ya Nje, mabalozi na mabalozi wadogo kwa hakika ni wawakilishi, ni wapambanaji na ni watumishi wa misingi na malengo hayo makuu matukufu.
Vile vile amesema kuhusiana na suala hilo kwamba, sera za masuala ya kigeni za Iran kama ilivyo kwa nchi zote nyengine duniani zimesimama juu ya msingi wa kulinda malengo ya muda mrefu na usuli na tunu za taifa na hazibadiliki kwa kuingia na kutoka madarakani serikali za mirengo, mielekeo na za siasa tofauti. Kitu pekee kinachofanywa na serikali hizo ni kubadilisha mbinu na kubuni njia mpya za kutekeleza mikakati na stratijia za sera za kigeni za nchi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Mbinu na njia zote za kidiplomasia za serikali tofauti zinazoingia madarakani zinapaswa zilenge katika kufanikisha usuli na misingi ya sera za kigeni zilizoainishwa kwenye Katiba na wawakilishi wa kisiasa wa Iran nje ya nchi nao wanapaswa kujua kuwa ni wawakilishi na watu imara wanaotumia mantiki katika kuzilinda na kuzihami sera na siasa za mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu.
Ayatullah Udhma Khamenei amegusia propaganda mbaya na kubwa za mabeberu wanaodai kuweko mabadiliko ya lazima au ya kutaka na kukataa katika sera za kigeni za Jamhuri ya Kiislamu na kuongeza kuwa: Madai hayo ambayo ni ndoto za kujifariji za Wamagharibi, kwa hakika zinatokana na mashinikizo ya uhakika huu kwamba, sera za kigeni za Jamhuri ya Kiislamu - kwa uchache kuhusiana na eneo la Mashariki ya Kati - ni mithili ya kigingi madhubuti kisichovuukika ambacho kinakwamisha njama za madola ya kibeberu hususan Marekani na ndio maana daima mabeberu wamekuwa na ruya na ndoto ya kuona kunatokea mabadiliko kwenye siasa hizo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, sera na siasa za Wamarekani katika eneo nyeti mno la magharibi mwa Asia ndiyo sababu kuu ya kuweko matatizo katika eneo hili na kwamba sera hizo ni sehemu ya matatizo na si utatuzi wa matatizo.
Kwa mara nyingine tena amesisitiza kuwa sera za kigeni za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran si kitu kinachotengenezwa na mtu huyu au yule bali zimesimama kwenye msingi madhubuti wa Katiba na kuongeza kwamba: Katika Katiba, Uislamu ndio msingi wa sera za kigeni (za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran), hivyo misimamo inayochukuliwa kuhusiana na nchi mbali mbali na masuala tofauti inapaswa kuwa na sifa za kidini na kuzingatia mafundisho ya Uislamu.
Ayatullah Udhma Khamenei amezungumzia usuli na misingi mengine ya sera za kigeni katika katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikiwa ni pamoja na msimamo wa kuwaona Waislamu wote dunia kuwa ni ndugu, kuwaunga mkono bila ya kusita wanyoge wote duniani, kupambana kikamilifu na ukoloni na kuzuia kujipenyeza mabeberu katika nyuga na nyanja zote, kulinda uhuru wa nchi katika mambo yote, kulinda haki za Waislamu wote, kutokuwa tayari kuburuzwa na madola ya kibeberu, kuwa na uhusiana wa amani na kuheshimiana na tawala zisizoipiga vita Jamhuri ya Kiislamu, kujiepusha kikamilifu na suala la kuingilia masuala ya ndani ya mataifa mengine, kuunga mkono mapambana ya kupigania haki ya wanyonge duniani mbele ya waistikbari katika nukta yoyote ile duniani na kuongeza kuwa: Misingi hiyo yenye mvuto wa aina yake, mipya na aali, inazivutia nyoyo za watu wa mataifa mengine hususan watu muhimu na wenye vipawa wa mataifa hayo.
Ameongeza kuwa: Sera za kigeni za Jamhuri ya Kiislamu ni sera za kimapinduzi kutokana na kuwa na mikakati na siasa za namna hii, na kama kutatumika njia makini na madhubuti katika kuzitekeleza, huwa na taathira za ajabu na zina uwezo wa kutatua sehemu kubwa ya matatizo ya ulimwengu wa Kiislamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia pia baadhi ya taathira chanya za utekelezaji wa mikakati ya sera za kigeni za Jamhuri ya Kiislamu na kuongeza kuwa: Utekelezaji wa siasa na sera za kigeni katika medani yoyote ile ikiwemo medani ya kidiplomasia hupelekea kuongezeka nguvu na taathira zake na kupandisha juu nafasi ya nchi na kuzidisha heshima na itibari ya Wairani kati ya watu wa mataifa mengine duniani.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitizia pia wajibu wa kuendelea bila ya kusita na ufanikishaji wa mikakati thabiti ya sera za kigeni za Iran na kuongeza kuwa: Hatuwezi kudai kuwa tumefanikiwa kufikia malengo yetu yote au hata kusema kuwa tumekaribia kwenye malengo hayo kwani utekelezaji wa sera za nje za Mapinduzi ya Kiislamu katika baadhi ya sehemu umekumbwa na mghafala, kutowajibika ipasavyo, ukosefu wa umakini na vizuizi kutoka nje ya nchi, lakini pamoja na hayo, heshima iliyo nayo Iran hivi sasa inatokana na sera na siasa hizo za busara na ni Mwenyezi Mungu tu Ndiye anayejua na hakuna mwengine anayeweza kujua - tungelikumbwa na matatizo na madhara kiasi gani ndani ya mipaka ya nchi yetu lau kama tusingelitekeleza sera hizo.
Ayatullah Udhma Khamenei ametoa muhtasari wa hotuba yake hadi kufikia hapo kwa kuwaambia maafisa wa Wizara ya Mambo ya Nje na mabalozi pamoja na mabalozi wadogo wa Iran kwamba: Endeleeni kuwa imara, endeleeni kuimarisha nguvu na kulinda heshima ya taifa, endeleeni kusimamia misingi ya kimapinduzi na mikakati thabiti ya siasa za kigeni za nchi na shikilieni misimamo hiyo hadi mabeberu na vibaraka wao wasiwe na matumaini kabisa ya kutokea mabadiliko katika siasa za nje za Jamhuri ya Kiislamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameendelea na hotuba yake kwa kuzungumzia mambo ya lazima yanayotokana na kushikamana na misingi na mikakati ya sera za kigeni za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Amezungumza kwa kusisitiza kwamba: Mnapaswa kuzingatia kuwa, mbinu zozote za utekelezaji wa sera za kigeni lazima zikubaliane na misingi ya mkakati wa siasa hizo na isije ikawa ni kwenda kinyume na misingi hiyo kwa madai ya kubadilisha mbinu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja suala la kujiamini, kuwa wazi na kutotetereka katika kukabiliana na vizuri na vikwazo mbali mbali kuwa ni miongoni mwa mambo ya lazima ya sera za kigeni na wakati huo huo amesema: Tab'an kipaji cha udiplomasia kinaonekana hapo kwamba mtu anaweza kukabiliana vilivyo na vizuizi vinavyojitokeza na kubainisha fikra zake kwa namna ambayo kazi yake hiyo itakuwa na taathira aliyokusudia.
Amesema, mantiki ya Jamhuri ya Kiislamu katika masuala ya eneo hili ni imara na ina sifa ya kukubalika duniani na ametolea ufafanuzi njia za Iran za utatuzi wa masuala hayo na kuongeza kuwa: Katika kadhia ya Paletina, sisi sambamba na kuupinga utawala ghasibu na pandikizi (wa Israel) na kulaani vikali jinai na maafa ya kila leo yanayosababishwa na utawala huo, tumependekeza kufanyike kura ya maoni itakayowashirikisha Wapalesitna wote kwa mujibu wa sheria zilizopo duniani hivi sasa na pendekezo hilo kwa hakika ni la kimantiki kikamilifu.
Ameongeza kuwa: Serikali yoyote itakayochaguliwa kwa kura na kupata ridhaa ya wananchi wa Palestina, itaamua hatima ya Wazayuni na wakazi wa ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu. Tab'an wanaopinga pendekezo letu hilo la kimantiki wanasema kuwa, hilo litakuwa na maana ya kusambaratika kabisa utawala ghasibu (wa Kizayuni), nasi tunawajibu watu hao kwa kuwaambia, jambo hilo ni la kawaida kabisa na ndivyo inavyotegemewa kwani utawala huo pandikizi kuna siku lazima utasambaratika.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia pia kadhia ya Syria na kusisitiza kuwa: Tunayosema sisi kuhusu kadhia hiyo ni maneno makini kabisa. Sisi tunaamini kuwa, hakuna sababu ya nchi kadhaa za kigeni zijikusanye pamoja na kupora nafasi ya wananchi wenyewe wa Syria ya kuamua mfumo wa utawala na kuhusiana na rais wa nchi hiyo. Hii ni bid'aa hatari sana ambayo hakuna serikali yoyote duniani inayoweza kukubali itendewe jambo hilo.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Utatuzi wa kadhia ya Syria ni kufanyika uchaguzi na ili kulifanikisha hilo, kuna wajibu wa kukatwa misaada ya kijeshi na kifedha kwa wapinzani ili kwa njia hiyo iwezekane kwanza kumaliza vita na machafuko na hivyo kutoa fursa kwa wananchi wa Syria kufanya uchaguzi katika mazingira ya amani na utulivu na kumchagua mtu yeyote wanayempenda.
Aidha amepinga kabisa mpango wa kuzigawa vipande vipande nchi za mataifa mengine na kuzigeuza kuwa vijinchi vidogo vidogo na kuongeza kwamba: Suala la kulifanya moja ya makundi yenye silaha kuwa kigezo na marejeo ya kuchukulia maamuzi na marejeo ya kuunda serikali si jambo la kimantiki na halikubaliki na kwa hakika mambo kama hayo ndiyo ambayo yanapelekea kuendelea kivitendo vita na machafuko.
Vile vile Ayatullah Udhma Khamenei amesema kuhusiana na Iraq kwamba: Suala la kuigawa nchi hiyo katika maeneo ya Waarabu Mashia, Waarabu Masuni na Wakurdi linapingana kikamilifu na manufaa ya wananchi wa nchini hiyo, aidha si jambo linalotekelezeka, bali halina maana na halikubaliki kabisa.
Ameongeza kuwa: Umoja wa ardhi, kulindwa haki ya kujitawala ardhi nzima ya Iraq na kupewa kipaumbele kura za wananchi ndiyo misingi ya njia za utatuzi zinazopendekezwa na Iran kuhusiana na Iraq.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia pia kadhia ya Yemen na kusema kuwa: Jinai za Saudi Arabia zinapaswa kusimamishwa mara moja ili kutoa mwanya wa kuanza mazungumzo baina ya wananchi wenyewe wa Yemen na hilo ndilo litakaloweza kumaliza vita nchini humo.
Vile vile amesema: Vitendo vya Wasaudia huko Yemen na Syria, vimejaa undumilakuwili. Kuhusu Yemen wanasema wameingia kijeshi nchini Yemen kwa ajili ya rais aliyejiuzulu na kukimbia nchi amma kuhusu Syria hawako tayari kusikiliza matakwa ya rais aliyeko madarakani kisheria, bali wanafanya kinyume chake, wanayaunga mkono makundi yenye silaha (yanayotaka kuipindua serikali iliyochaguliwa na wananchi).
Amma kuhusiana na Bahrain, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Wananchi wa Bahrain hawataki kitu kingine chochote zaidi ya haki yao ya kupiga kura na kujichagulia wenyewe viongozi wanaowataka. Sisi tunayaona matakwa hayo ya wananchi wa Bahrain kuwa ni ya mahala pake na ni ya kimantiki.
Baada ya kubainisha njia za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran za kutatua matatizo ya aneo la Mashariki ya Kati amesema: Sababu kuu ya kuwepo ukosefu huo wa amani ni uungaji mkono wa Marekani kwa utawala wa Kizayuni na kwa makundi ya kigaidi na kwamba siasa hizo zinatofautiana kwa daraja 180 na siasa za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amepinga kufanyika mazungumzo kati ya Iran na Marekani kuhusiana na masuala yanayolihusu eneo hili na kusisitiza kuwa: Wanachotaka Wamarekani ni kuyabebesha mataifa mengine matakwa yake na si kutatua matatizo yaliyopo. Wamarekani wanataka asilimia 60, 70, ya matakwa yake katika mazungumzo yakubaliwe, na malengo mengine yaliyobakia nayo yatekelezwe kinyume cha sheria. Sasa mazungumzo ya namna hiyo yana maana gani?
Ameendelea na hotuba yake kwa kusema kuwa, kustawisha kadiri inavyowezekana uhusiano wa Iran na majirani zake na uhusiano wake na nchi za Kiislamu pamoja na nchi za bara la Afrika ni miongoni mwa mambo ya lazima katika sera za kigeni za Jamhuri ya Kiislamu.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema kuwa, ni jambo linalofaa kabisa kuwaita maafisa na wafanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Nje kuwa ni wanamapambano na wapambanaji wa mstari wa mbele katika uga wa kimataifa. Ameongeza kuwa: Wizara ya Mambo ya Nje iko makini na amilifu kikweli kweli katika ufanikishaji wa malengo na majukumu yake na hususan katika uzoefu wa hivi karibu kwenye mazungumzo ya nyuklia. Kwa hakika Bw. Zarif na wenzake katika wizara hiyo, wamepasi vizuri mtihani wao.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amepongeza juhudi na kazi kubwa iliyofanywa na timu ya Iran katika mazungumzo ya nyuklia na kuongeza kuwa: Kupata hisia za kuwa na nguvu za kukabiliana peke yake na madola 6 yenye nguvu duniani, kulinda malengo na utambulisho wake na kuwa imara katika mazungumzo na pande kadhaa ni miongoni mwa mambo muhimu mazuri iliyokuwa nayo nchi yetu katika mazungumzo ya nyuklia.
Amelitaja suala la kuheshimu mafundisho ya dini na kujibidiisha kuyatekeleza kivitendo kuwa ni katika sifa nzuri za Bw. Zarif na kuwaambia hadhirina kwamba: Mimi wakati wote ninakuombeeni dua wapendwa wetu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Suala la kuutekeleza Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) pia, inabidi lifuatiliwe kwa kuzipa kipaumbele nukta muhimu na zinazotakiwa na kwamba ni jambo linalowezekana kabisa kufanikisha masuala hayo, kama ambavyo mheshimiwa Rais alivyowahi kuniambia kuwa, kwanza ilikuwa ni vigumu kuamini kwamba matunda yangelipatikana kwenye suala hili, lakini kutokana na kusimama kwako kidete, na sisi pia tulipata nguvu za kumesimama kidete na kulifanya jambo hilo liwezekane.
Sehemu ya tatu na ya mwisho ya hotuba ya Ayatullah Udhma Khamenei imehusiana na nasaha na ukumbusho kwa mabalozi na wawakilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nje ya nchi.
Kushikamana na kutilia mkazo vielelezo vya uwezo na nguvu za taifa ikiwa ni pamoja na kuipa uzito mkubwa nafasi kubwa na muhimu mno ya wananchi nchini, nguvu kazi kubwa ya wananchi na ambayo ni muhimu, yenye faida kubwa, ya asili na ya vijana shupavu, na maendeleo ya kustaajabisha ya kielimu na kiteknolojia, kushikamana vilivyo mabalozi na wawakilishi wa Iran nje ya nchi na mafundisho ya dini na moyo wa kimapinduzi, kutumia vizuri uwezo na nafasi ya nchi nyengine zinazounda Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande wowote (NAM) na kutoa mchango mkubwa katika suala la kuufanyia utafiti uchumi wa kimuqawama, ni miongoni mwa nasaha zilizotolewa na Ayatullah Udhma Khamenei kwa hadhirina.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Dk Mohammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amegusia hali nyeti iliyojitokeza kwenye eneo la Mashariki ya Kati hivi sasa na kusisitiza kuwa: Maagizo na mistari iliyochorwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ndio msingi wa kazi za Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran na katika kipindi cha baada ya utekelezaji wa Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) pia, barua ya hivi karibuni ya Kiongozi Muadhamu kwa Rais kuhusiana na namna ya kutekeleza makubaliano hayo ya nyuklia maarufu kwa jina la JCPOA ndiyo itakayokuwa msingi wa utekelezaji.
Dk Zarif amegusia pia namna Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran inavyolipa uzito suala la kupambana na mambo yanayopelekea kujipenyeza maadui na vile vile utekelezaji wa uchumi wa kimuqawama na wa kusimama kidete na kusema kuwa: Katika kongamano la mwaka huu la mabalozi na mabalozi wadogo, kunafanyika jitihada za kutumia vizuri hali iliyopo kwa ajili ya kufanikisha malengo ya uchumi wa kimuqawama na pia kutia nguvu mrengo wa muqawama katika eneo hili na kuyatafutia ufumbuzi matatizo ya eneo la magharibi mwa Asia kwa kuzingatia misingi na vipimo vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
 
< Nyuma   Mbele >

^