Skip to content

Habari

Habari
Hifadhi

Risala na Barua

Matini
Hifadhi

Kumbukumbu na Simulizi

Kabla ya Mapinduzi
Baada ya Mapinduzi

Sauti na Taswira

Picha
Sauti
Video
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Aonana na Wanafunzi na Wanachuo Chapa
03/11/2015
 Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu leo asubuhi (Jumanne) ameonana na maelfu ya wanafunzi na wanachuo na kuyataja mapambano ya taifa la Iran dhidi ya ubeberu kuwa ni mapambano ya kimantiki, ya hekima na yaliyojaa uzoefu wa kihistoria na huku akitolea ushahidi wa matatizo na madhara liliyopata taifa kutokana na kuiamini Marekani na kutokana mitazamo finyu ya baadhi ya wanasiasa katika historia ya zama hizi ya Iran ameongeza kuwa: Marekani ya sasa hivi ndiyo ile ile Marekani ya zamani, lakini kuna baadhi ya watu wanaofanya kwa makusudi au kwa kutokana na mitazamo yao finyu, wanajaribu kumfanya adui huyo mwenye hila na njama nyingi asahauliwe katika fikra za wananchi wa Iran na kutaka waghafilike naye ili aui hiyo Mmarekani aweze kushambulia kutokea nyuma mara atakapopata nafasi ya kufanya hivyo.
Katika mkutano huo uliofanyika wakati huu wa kukaribia maadhimisho ya Aban 13 (Novemba 4) ambayo kwa nchini Iran ni Siku ya Taifa ya Kupambana na Uistikbari Duniani, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekitaja kipindi cha hivi sasa kuwa ni kipindi cha kuimarisha heshima ya taifa na kuchora ramani ya maendeleo ya Wairani na kwamba kuwa macho, kuwa makini na kuwa na busuri na muono wa mbali wananchi wa Iran hususan vijana, ni jambo muhimu mno katika kipindi hiki.
Ameongeza kuwa: Nukta ya kimsingi katika kufahamu na kuchanganua hali iliyopo hivi sasa na kuweza kubuni harakati ya baadaye ya nchi, kuuelewa vyema uhakika huu kwamba mapambano ya Jamhuri ya Kiislamu na wananchi wa Iran dhidi ya uistikbari na ubeberu, tofauti na madai wanayotoa baadhi ya watu, si harakati isiyo ya kimantiki na inayotokana na hamasa zisizo na maana, bali ni mapambano yanayoendeshwa kwa mantiki, akili, uzoefu kama ambavyo pia ni mapambano yenye msukumo wa kielimu kikamilifu.
Ayatullah Udhma Khamenei amegusia pia kwamba, kwa kuzingatia uzoefu na mafunzo yaliyopata mataifa mengine, inawezekana kuepusha kutokea makosa ya kimahesabu na kuongeza kuwa: Hata kama tutaziweka pembeni aya tukufu za Qur'ani zinazozungumzia umuhimu wa kusimama kidete na kupambana vilivyo na dhulma na uistikbari, tukio kubwa la mapinduzi ya kijeshi ya Mordad 28 1332 (Hijria Shamsia sawa na Agosti 19, 1953) linaonesha ni namna gani tunapaswa tuamiliane na Marekani.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amebainisha matukio yaliyotokea katika kipindi muhimu cha kutangazwa mafuta ya Iran kuwa ni mali ya taifa na kusema kuwa, kosa kubwa la kihistoria lililofanya na Dk Mosaddegh (Waziri Mkuu wa wakati huo wa Iran) lilikuwa ni kuiamini Marekani na kuwa na matumaini nayo. Ameongeza kuwa: Mosaddegh aliitegemea Marekani katika mapambano yake dhidi ya Uingereza na kitendo hicho cha kuwa na matumaini na Marekani na kuwa na mtazamo finyu na kukumbwa na mghafala kuhusiana na adui huyo, kuliandaa uwanja wa kufanyika mapinduzi ya kijeshi yaliyoongozwa na Marekani, mapinduzi ya kijeshi ambayo yaliharibu kikamilifu juhudi zote za wananchi wa Iran za kuhakikisha mafuta ni mali ya taifa. Mapinduzi hayo yaliufufua utawala kibaraka wa Kipahlavi, na Iran azizi ikatumbukia kwenye kipindi cha miaka 25 ya madhara makubwa na kipindi kigumu mno cha kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni.
Ayatullah Udhma Khamenei amegusia ushawishi na nafasi kubwa ya Wamarekani nchini Iran baada ya mapinduzi ya kijeshi ya Agosti 19, 1953 na kuongeza kuwa, mataifa ambayo hayana viongozi makini na madhubuti, husalimu amri na huchukua hatua za pupa katika kukabiliana na mashaka na tabu kama hizo, lakini wananchi wa Iran kwa kutumia vizuri neema waliyopewa na Mwenyezi Mungu yaani uongozi wa Imam Khomeini, walianza kuamka pole pole na hatua kwa hatua na kwa mamko huo wa Kiislamu wakasimama imara kukabiliana vilivyo na utawala kibaraka wa Kipahlavi na muungaji mkono wake mkubwa yaani Marekani.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametolea ushahidi matamshi ya Imam Khomeini (quddisa sirruh) ya mwaka 1342 (1963) kuhusiana na namna wananchi wa Iran wanavyomchukia mno Rais wa Marekani na kuongeza kuwa: Kiongozi huyo makini na shujaa (Imam Khomeini - quddisa sirruh), alikuwa na imani kamili na ahadi za Mwenyezi Mungu na tangu wakati huo wa kuanza mwamko wa Kiislamu, aliwabainishia njia wananchi akisema kuwa shari na njama zote zinatoka kwa Marekani.
Amekumbushia pia uadui wa Marekani dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu kuanzia miezi ya mwanzoni kabisa mwa ushindi wa mapinduzi hayo na kuongeza kuwa: Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Wamarekani waliendelea kuwa na uhusiano na serikali ya Iran na walikuwa na ubalozi wao mjini Tehran, lakini hawakusita hata mara moja kufanya njama zao na kwamba uzoefu huu wa kihistoria inabidi waelezwe baadhi ya watu na watanabahishwe kwamba, kuwa na uhusiano na urafiki na Marekani hakuwezi kumaliza uadui na chuki zake dhidi ya taifa la Iran na dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.
Ayatullah Udhma Khamenei ameitaja hatua ya kutekwa ubalozi wa Marekani na kundi la wanafunzi wa vyuo vikuu vya Iran mjini Tehran kwamba yalikuwa ni majibu na radiamali yao wanachuo hao katika kukabiliana na njama za Washington na kuonesha hasira zao kwa Marekani kwa hatua yake ya kumpa hifadhi adui mkubwa wa taifa la Iran yaani Mohammad Reza Pahlavi na kuongeza kuwa: Nyaraka zilizopatikana kwenye ubalozi wa Marekani mjini Tehran zilithibitisha kuwa ubalozi huo kwa hakika lilikuwa ni pango la kijasusi na kituo kikubwa cha kufanyia njama za mtawalia dhidi ya taifa la Iran na dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu ambayo wakati huo yalikuwa ndio kwanza yamepata ushindi.
Amesema, ni jambo la dharura kuyazingatia kwa kina yaliyomo kwenye nyaraka zilizopatikana katika pango hilo la kijasusi na kupata funzo ndani yake. Amesisitiza kuwa: Nyaraka hizo zinaonesha kwa uwazi kabisa kwamba Wamarekani katika kipindi cha kuundika mwamko wa Kiislamu ilikuwa inafanya njama dhidi ya wananchi wa Iran na njama hizo ziliendelea mtawalia hata baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu kama ambavyo walikuwa wanausaidia utawala mbovu na fasidi wa kifalme kukabiliana na wananchi wa Iran, kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu.
Ayatullah Udhma Khamenei ametolea ushahidi kumbukumbu zilizoandikwa na Robert Huyser, jenerali wa Kimarekani ambaye katika msimu wa joto wa mwaka 1978 alikuja nchini Iran ili kuuokoa utawala wa kiimla na kidikteta wa mfalme wa Iran na kusisitiza kuwa: Kumbukumbu hizo zinaonesha kwa uwazi kwamba Marekani ilikuwa inawashawishi na kuwaongoza majenerali wa kijeshi wa utawala wa Kipahlavi katika kuwaua wananchi wa Iran.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, kitendo cha Wamarekani cha kuyasaidia makundi ya maadui wa Mapinduzi ya Kiislamu yaliyokuwa yanataka kujitenga, njama zake katika jaribio la mapinduzi ya kijeshi yanayojulikana kwa jina la Nojehm, kitendo chake cha kumchochea Saddam (Rais wa wakati huo wa Iraq) kuivamia na kuishambulia Iran, misaada ya kila leo ya Wamarekani kwa madikteta wasio na uungaji mkono wa watu wao katika kipindi chote cha miaka minane ya vita vya kujihami kutakatifu (vita vilivyoanzishwa na utawala wa zamani wa Iraq dhidi ya utawala mchanga wakati huo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran) ni sehemu nyengine ya silisila ya njama za Wamarekani dhidi ya taifa la Iran.
Amesisitiza kuwa: Kutokana na welewa wao mbaya na kushindwa kwao kuchanganua vizuri matukio ya Iran, Wamarekani katika kipindi chote hiki cha miaka 37 iliyopita (ya kuundwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu nchini Iran) wamekuwa wakifanya njama za mtawalia za kutaka kuyapindua Mapinduzi ya Kiislamu lakini kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu njama hizo zote zimeshindwa na katika siku za usoni pia njama hizo za Marekani zitaendelea kufeli.
Ayatullah Udhma Khamenei amelitaja lengo lake la kukumbushia silisila ya njama za shetani mkubwa Marekani kuwa ni kuwafanya watu wazidi kuelewa uhakika wa dola hilo hilo la kibeberu na kuongeza kuwa: Katika miaka ya hivi karibuni, kuna baadhi ya watu wamekuwa wakifaya njama za makusudi za kujaribu kuonesha kuwa dola la Marekani ni zuri na wako ambao wanafanya hivyo kwa muono wao finyu na kwa kujisahaulisha uzoefu wa mara kwa mara wa taifa la Iran kuhusiana na njama hizo za Marekani. Watu hao wanajaribu kuonesha kuwa, kama kuna siku Wamarekani walikuwa ni maadui wa Iran, hivi sasa si maadui tena na eti wameachana na njama zao dhidi ya taifa hili.
Ameongeza kuwa: Lengo na shabaha ya njama hizo ni kufuta na kuficha sura halisi ya adui huyo katika akili za watu ili Wamarekani wapate fursa ya kuendelea na uadui wao na wapate mwanya wa kulishambulia taifa la Iran kwa kutokea nyuma.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Uhakika wa mambo ni kwamba, malengo ya Marekani kuhusiana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hayajawahi kubadilika hata mara moja na kama wangeliweza kuiangamiza Jamhuri ya Kiislamu, basi wasingelisita hata kwa sekunde moja kufanya hivyo, lakini hawawezi na kwa msaada wa Mwenyezi Mungu na chini ya kivuli cha hima ya vijana wa Iran na chini ya kivuli cha kueneza na kutia nguvu busuri na mtazamo wa mbali wa taifa na chini ya kivuli cha maendeleo na ustawi wa Iran, katika siku za usoni pia njama hizo za Marekani zitashindwa tu.
Vile vile ameashiria baadhi ya ulegezeji kamba wa kidhahihiri na kijuu juu wa viongozi wa Marekani katika mazungumzo ya nyuklia na kutahadharisha kuwa: Batini ya vitendo vya Marekani ni kuendelea na njama za kufanikisha malengo yake yale yale ya huko nyuma ya kiuadui na kwamba taifa la Iran halipaswi kuusahau uhakika huo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameendelea kulizungumzia suala hilo akisema: Kuna kiongozi mmoja wa Marekani katika mazungumzo ya nyuklia alielezea namna anavyochukizwa mno na vita na alifikia hata kulia, sasa watu wenye muono finyu wanaweza kuliamini jambo hilo, lakini uungaji mkono usioisha na misaada isiyosita ya Marekani kwa utawala wa Kizayuni unaotenda jinai, nduli na unaoua watu wasio na hatia na uungaji mkono wa Wamarekai kwa jinai zinazofanywa hivi sasa dhidi ya wananchi wa Yemen unafichua na kubainisha wazi uhakika wa madai na kilio hicho.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria suala la kuweko uhusiano wa kawaida baina ya Iran na nchi mbali mbali duniani na hata tawala ambazo hazina mtazamo mzuri na taifa la Iran na kuongeza kuwa: Licha ya wananchi wa Iran kuwa na msimamo huo, lakini hawaiangalii Marekani kuwa ni rafiki yao kutokana na dola hilo la kibeberu kutumia kila kisingizio kujaribu kuliletea madhara taifa hili na kujaribu kuiangamiza Jamhuri ya Kiislamu. Taifa hili haliwezi kuinyooshea Marekani mkono wa urafiki kwani sheria, akili, hisia za ndani ya nafsi na ubinaadamu haulipi haki taifa hili kufanya hivyo.
Ayatullah Udhma Khamenei amegusia suala la kuendelea harakati za kila upande za serikali ya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu na kuongeza kuwa: Wamarekani pole pole wameelewa kuwa, jambo linalolifanya taifa la Iran liweze kusimama kidete ni imani na itikadi zake za kidini na ni kwa sababu hiyo ndio maana leo hii Wamarekani wanatumia zana mpya kuendeshea mashambulizi yao ya kila upande dhidi ya thamani hizo lakini wanafunzi na wanachuo na vijana wetu wote wataifanya hila hiyo ya Marekani isiwe na athari yoyote.
Ameongeza kuwa: Adui anafanya njama kubwa ya kuvirejesha Vyuo Vikuu nchini Iran katika hali viliyokuwa nayo wakati wa utawala fasidi wa Shah yaani kuwa daraja la kuelekea Magharibi, lakini kutokana na kuwa kwao macho, vijana wetu azizi wamevigeuza vyuo vikuu nchini kuwa ngazi ya kuelekea kwenye malengo matukufu ya muda mrefu ya taifa na kwamba vijana wetu hao wataendelea kuulinda uhakika huu wenye taathira nzuri.
Ayatullah Udhma Khamenei ameyataja maendeleo na nguvu za taifa la Iran kuwa ndilo jambo lililowafanya maadui walazimike kufanya mazungumzo ya nyuklia na Iran na kuongeza kuwa: Hata katika mazungumzo hayo, maadui hao wameendelea kuchukua hatua zao za kiadui kwa tamaa ya kukwamisha harakati ya Iran.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha amesema kuwa, kulitegemea suala la kuutambua vyema uadui wa Marekani dhidi ya taifa la Iran hakuna maana ya kusahau na kufumbia macho udhaifu uliopo ndani ya nchi na kuongeza kuwa: Tuna udhaifu wa kiasi fulani katika utungaji sera na utekelezaji wake, katika juhudi na katika kufanya harakati, katika utoaji vipaumbele kwa masuala tofauti na kwenye nyuga nyinginezo, na adui anautumia udhaifu huo katika mambo mengi.
Amekutaja kumsahau adui mkuu na kujishughulisha na mivutano ya ndani kuwa ni moja ya makosa makubwa na kuongeza kwamba: Kuna baadhi ya watu wanamsahau adui wa nje kutokana na udhaifu unaojitokeza hapa na pale katika masuala ya ndani.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kwamba: Tunapaswa tutofautishe baina ya adui na watu tunaotofautiana nao kimawazo. Adui ni yule mtu ambaye anatumia nguvu na uwezo wake kujaribu kuliletea madhara taifa na kujaribu kuiingiza madarakani serikali kibaraka ambayo itakuwa dhalili na itakayokuwa tayari kusalimu amri na kuzipigia magoti nchi za Magharibi na kwamba adui huyo mwenye chuki, anayejua anachokifanya na anayefanya uadui wake kwa nguvu zake zote, hatupaswi kumsahau hata kwa sekunde moja.
Vile vile Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Kukosoa palipokwenda kombo ndio msingi wa kupata maendeleo taifa na kwamba jamii iko huru na ina haki ya kukosoa lakini wakati huo huo hatupaswi kuyasahau matamshi haya ya kihistoria ya Imam (Khomeini - quddisa sirruh) ambaye alikuwa akisema mara kwa mara kwamba: "Kila ukelele mlio nao upigeni dhidi ya Marekani."
Ayatullah Udhma Khamenei vile vile amewausia vijana kulipa uzito suala la masomo na kujifunza mambo mapya kila siku, kustahabu malengo na manufaa ya umma mbele ya matakwa binafsi na kuongeza uwezo wao wa utambuzi na uwezo wao wa kuchanganua mambo na kuongeza kuwa: Sauti ya taifa la Iran ndiyo sauti pekee ya wazi ambayo inasikika kila mahali ikipinga dhulma, unyonyaji na ukoloni katika hali hii tata iliyopo duniani leo na kwamba sauti hiyo inazivutia nyoyo za watu wa mataifa mengine na hususan watu wenye vipaji miongoni mwao. Amesema: Hatupaswi kuipoteza sauti hiyo.
Akiendelea na matamshi yake hayo ambayo yamepokewa kwa nara na kaulimbiu ya mauti kwa Marekani kutoka kwa wanafunzi na wanachuo hao, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Nara na kaulimbiu ya taifa la Iran ya mauti kwa Marekani ina mzukumo wenye nguvu wa kiakili na kimantiki na chimbuko lake ni Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu na fikra za kimsingi za Iran ambazo haziko tayari kamwe kuvumilia dhulma na ukandamizaji.
Ameongeza kuwa: Maana ya nara na kaulimbiu hiyo ni mauti kwa siasa za Marekani na ni mauti kwa ubeberu na uistikbari na wakati taifa lolote lile linapofafanuliwa mantiki hiyo huikubali mara moja na bila ya kupinga.
Mwishoni mwa hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Taifa la Iran liko imara na linaendelea mbele na njia yake kwa matumaini makubwa na kwamba vijana wa leo kwa kujiimarisha kiimani na muono wao wa mbali na kwa kutegemea vielelezo vikuu, bila ya shaka yoyote watawahi kukiona kipindi ambacho mataifa ya dunia yatatoka chini ya kivuli cha mazimwi ya kutisha; na Iran yetu azizi iliyostawi kimaendeleo itatoa ilhamu kwa mataifa yote ya duniani.
 
< Nyuma   Mbele >

^